Trump kuiwekea vikwazo na ushuru mpya Urusi
Donald Trump amesema anafikiria kuweka vikwazo na ushuru mpya dhidi ya Urusi, kufuatia mashambulizi makali ya usiku dhidi ya Ukraine.
Muhtasari
- Trump kuiwekea vikwazo na ushuru mpya Urusi
- GMO yagonga mwamba Kenya
- Usafiri wa treni wasitishwa baada ya kugunduliwa bomu la vita vya pili vya dunia Paris
- Maelfu ya Wapalestina wafanya swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Al-Aqsa
- WHO kupeleka dawa za ukoma Nigeria
- Rais Zelensky, ashutumu Urusi kwa kushambulia 'miundombinu muhimu kwa maisha'
- Rais wa Kenya William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga watia saini mkataba wa kisiasa
- Kesi ya uhaini dhidi ya Dr Besigye yaahirishwa
- Asasi za kiraia nchini Tanzania zapendekeza kuondolewa adhabu ya viboko shuleni
- Visa vingine vipya vya Ebola vyaripotiwa Uganda
- Urusi yashambulia vituo vya gesi vya Ukraine, watoto wanusurika
- Jinsi maisha ya Wanawake yalivyobadilika chini ya Utawala wa Taliban
- Makumi wauawa jeshi la Syria likipambana na wafuasi wa Assad
- Kenya yachukua hatua dhidi ya TikTok kuhusiana na unyanyasaji wa watoto
- Sudan yaishtaki UAE katika mahakama ya kimataifa kwa 'kuchochea vita'
- Papa Francis atuma ujumbe wa sauti kwa mara ya kwanza tangu alazwe hospitalini
- Marekani, Ukraine kukutana tena wiki ijayo, Zelensky aomba msamaha
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid
Trump kuiwekea vikwazo na ushuru mpya Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Donald Trump amesema anafikiria kuweka vikwazo na ushuru mpya dhidi ya Urusi, kufuatia mashambulizi makali ya usiku dhidi ya Ukraine.
Trump aliandika: "Kutokana na ukweli kwamba Urusi inashambulia kwa nguvu Ukraine hivi sasa, nazingatia kwa nguvu vikwazo vikubwa vya kibenki na ushuru dhidi ya Urusi hadi mapatano ya kusitisha vita na makubaliano ya mwisho ya amani yatakapofikiwa
"Kwa Urusi na Ukraine, nendeni kwenye meza ya majadiliano sasa, kabla hamjachelewa!!Asanteni"
Ujumbe wa hivi karibuni kutoka kwa Donald Trump kwenye mtandao wa kijamii Truth Social unazungumzia "shambulio kubwa" ambalo limelenga Ukraine, akimzungumzia Urusi baada ya mashambulizi ya usiku yaliyoathiri maeneo ya makazi na miundombinu muhimu ya nishati.
Katika mji wa bandari wa Odesa, serikali ya mkoa imesema kwamba kulikuwa na milipuko kadhaa ya moto, huku wafanyakazi wa zimamoto wakikimbilia kwenye eneo la tukio.
Kabla ya Rais wa Marekani kuitahadharisha Urusi kuhusu vikwazo zaidi ili kulazimisha makubaliano ya amani, alikuwa akielekeza shinikizo kwa Ukraine.
Mwanzo wa juma hili, Ikulu ya White House ilisema kuwa Marekani itasitisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine kwa muda huku ikiangalia kama msaada huo unachangia kwenye suluhisho la mgogoro.
Mnamo tarehe 4 Machi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema kwamba rais alikuwa akishughulikia "kuwaleta Warusi kwenye meza ya majadiliano".
Siku moja baadaye, Marekani ilitangaza kuwa itasitisha kushirikiana kwa taarifa za kijasusi na Ukraine.
Mshauri wa Usalama wa Marekani, Mike Waltz, alisema wakati huo kuwa utawala wa Trump ulikuwa ukisitisha na kupitia "vipengele vyote vya uhusiano huu."
Soma pia;
GMO yagonga mwamba Kenya

Mahakama ya Kenya imezuia kwa muda mpango wa serikali kuingiza mazao na vyakula vilivyokuzwa kijenetiki (GMO).
Uamuzi huo unasubiri kusikilizwa kwa rufaa iliyowasilishwa na wakulima wa vijijini na watumiaji, ambao wanadai kwamba kuondoa marufuku ya GMOs kunakiuka haki zao.
Mahakama ya rufaa imesema kwamba ikiwa mazao hayo yatakubaliwa na kupandwa au kuuzwa kabla ya kumalizika kwa mujibu wa sheria, inaweza kuwa vigumu kurudia hali ya awali.
Shirika linalowakilisha wakulima wa vijijini na watumiaji wa chakula nchini Kenya lilikata rufaa dhidi ya uamuzi wa awali wa Mahakama ya Juu ulioondoa marufuku ya GMOs, wakidai kwamba jamii haikushirikishwa.
Mahakama ya Juu ilikataa kesi hiyo, ikisema serikali ya Kenya imeweka hatua za usalama wa kutosha.
Soma pia;
Usafiri wa treni wasitishwa baada ya kugunduliwa bomu la vita vya pili vya dunia Paris

Chanzo cha picha, Reuters
Huduma za treni kutoka na kuingia Paris zimesitishwa kwa siku nzima baada ya kugundulika kwa bomu la Vita vya Pili vya Dunia karibu na kituo cha Gare du Nord.
Wataalamu wa kutengeneza mabomu wanachunguza ili kuhakikisha kifaa hicho ni salama baada ya kuripotiwa kugundulika "katikati ya reli" katika eneo la Saint-Denis wakati wa usiku.
Si jambo la ajabu kugunduliwa mabomu ya enzi ya vita katika maeneo kama haya, anaripoti Hugh Schofield kutoka Paris.
Awali kulikuwa na umati mkubwa wa wasafiri waliokasirika wakiwa wanazunguka ndani ya kituo, lakini abiria wengi wametoka sasa, wakiwa wamesikitishwa wengine wakifurahia kubaki siku moja zaidi.
Maeneo ya reli jirani na jiji la Paris yalikuwa maeneo lengwa na Waingereza na Wamarekani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, na hii si mara ya kwanza kugundulika kwa mabomu.
Eneo la usalama limetengwa, na sehemu ya barabara kuu ya kuingia Paris imefungwa.
Soma pia;
Maelfu ya Wapalestina wafanya swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Al-Aqsa

Chanzo cha picha, Reuters
Serikali ya Israeli iliweka vizuizi kwa Wapalestina wanaotoka Ukingo wa Magharibi kufanya swala ya Ijumaa ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani katika Msikiti wa Al-Aqsa huko Yerusalemu.
Idara ya Kiislamu huko Yerusalemu ilisema, "takriban waumini 90,000 walifanya swala ya Ijumaa ya kwanza ya Ramadhani katika viwanja vya Msikiti wa Al-Aqsa."
Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC mjini Yerusalemu Mahmoud Addama Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israeli ilitangaza vizuizi kwa Wapalestina kutoka Ukingo wa magharibi kutoingia viwanja vya Msikiti wa Al-Aqsa Ijumaa, ambapo ni wanaume wenye umri wa miaka 55 na zaidi, wanawake kuanzia umri wa miaka 50 na watoto chini ya miaka 12 pekee ndio walioruhusiwa kuingia.
Wote walioafikiana na vigezo iliwapasa kupata "idhini ya kiusalama kabla ya kuingia."
Hatua hizi zinakuja wakati ambapo Ukanda wa Gaza unashuhudia makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na Israeli, baada ya vita vilivyodumu kutoka Oktoba 2023 hadi Januari 2025.
Soma pia;
Mchezaji wa zamani wa Olimpiki asakwa na FBI

Chanzo cha picha, Getty Images
Mchezaji wa zamani wa Olimpiki na raia wa Canada, Ryan Wedding, mwenye umri wa miaka 43, ametajwa kwenye orodha ya wahalifu 10 wanaotafutwa sana na FBI kwa tuhuma za kuendesha mtandao wa kimataifa wa biashara haramu ya dawa za kulevya.
Wedding anatafutwa kwa tuhuma za kusafirisha mamia ya kilogramu za cocaine kutoka Colombia, kupitia Mexico na kusini mwa California, hadi Canada na maeneo mbalimbali ya Marekani, na kwa kupanga mauaji kadhaa ili kutekeleza uhalifu huu wa dawa za kulevya.
Marekani imetangaza kitita cha hadi dola milioni 10 (paundi milioni 7.7) kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa itakayofanikisha kukamatwa kwa Wedding.
Wachunguzi wanaamini kwamba anaishi Mexico, lakini hawajakata tamaa kumfuatilia nchini Marekani, Canada, na nchi nyingine za Latini Amerika au maeneo mengine.
Haifahamiki kama ana wakili.
Wedding aliwakilisha Canada katika michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya mwaka 2002 huko Salt Lake City.
Majina anayotumia ni pamoja na "El Jefe," "Giant," "Public Enemy," "James Conrad King," na "Jesse King," kwa mujibu wa FBI.
Mnamo Juni 2024, Wedding na msaidizi wake Andrew Clark, mwenye umri wa miaka 34, pia raia wa Canada, walikabiliwa na mashtaka huko California kwa kujihusisha na bishara hiyo haramu, mauaji na makosa mengine yanayohusiana na dawa za kulevya, na kuhusika katika njama za kumiliki, kusambaza, na kusafirisha cocaine.
Soma pia;
WHO kupeleka dawa za ukoma Nigeria

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema litapeleka dawa za ukoma nchini Nigeria Jumamosi baada ya kushughulikia ucheleweshaji ambao ulisababisha maelfu ya wagonjwa kukosa dawa kwa mwaka mzima.
Nigeria ambayo inaripoti zaidi ya watu elfu moja wapya kupata ukoma kila mwaka - ilikosa mgao wa dawa kwa sehemu kutokana na ucheleweshaji baada ya kuanzishwa kwa kanuni mpya za upimaji.
Ukoma unaweza kutibika kwa kutumia mchanganyiko wa antibiotiki mbalimbali.
Lakini kwa sababu Nigeria imeshindwa kupata dawa tangu mwanzoni mwa mwaka jana, hali ya baadhi ya wagonjwa imekuwa mbaya, na wakiwa na vidonda na uharibifu wa neva za fahamu unaosababisha mikono kupinda.
Wagonjwa wengine walirudishwa nyumbani, jambo ambalo linaongeza hatari ya kueneza ugonjwa huu.
Shirika la Afya Duniani limesema lililiomba Nigeria kuimarisha kwa muda sera yake mpya ya upimaji na linatarajia dawa kutoka India zitawasili nchini humo Jumamosi.
Katika miongo minne iliyopita, maambukizi ya ukoma yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Lakini Nigeria bado inaripoti zaidi ya watu elfu moja wapya kila mwaka.
Aidha zaidi ya elfu kumi kwa mwaka huripotiwa katika maeneo mengine kama Brazil, India, na Indonesia.
Soma pia;
Rais Zelensky, ashutumu Urusi kwa kushambulia 'miundombinu muhimu kwa maisha'

Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ameshutumu Urusi kutekeleza mashambulizi dhidi ya "miundombinu inayohakikisha usaidizi wa maisha ya kila siku."
Zelensky amesema kwamba karibu makombora 70 na ndege zisizokuwa na rubani 200 zilitumika katika mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati na gesi.
Alisema kupitia telegram kwamba majengo ya makazi pia yalishambuliwa, na kombora la Urusi lililenga makazi ya watu huko Kharkiv, na kusababisha majeruhi.
Aidha Zelensky ameshukuru Ufaransa kwa kutoa ndege za kivita za F-16 na Mirage-2000, akisema zimekuwa na ufanisi mkubwa dhidi ya makombora ya Urusi.
Amesema kwamba Ukraine iko tayari kutafuta amani, lakini hatua ya kwanza lazima iwe "kukilazimisha chanzo kimoja cha vita hiki, ambacho ni Urusi, kusitisha mashambulizi kama haya dhidi ya Maisha ya watu."
Soma pia;
Habari za hivi punde, Rais wa Kenya William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga watia saini mkataba wa kisiasa

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Rais William Ruto na Raila Odinga walitia saini mkataba wa kisiasa katika KICC mnamo Machi 7, 2025. Rais William Ruto na kiongozi wa upinzan aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, wametia saini rasmi mkataba wa kisiasa unaoashiria juhudi za mpya za kufanya kazi pamoja katika serikali moja.
Mkataba kati ya chama tawala cha Ruto cha United Democratic Alliance (UDA) na Orange Democratic Movement (ODM) cha Raila metiwa saini Ijumaa rasmi katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta (KICC).
Akizungumza baada ya kutiwa saini, Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga alipongeza ushirikiano huo mpya, na kuutaja kuwa ishara ya kuweka maslahi ya taifa mbele kibinafsi.
“Umoja na utulivu na ustawi wa nchi hii si jukumu la watu wachache; ni jukumu letu sote kama taifa. Na ingawa tunaweza kuwa na ushawishi tofauti wa kisiasa, na kutoka sehemu mbalimbali za nchi na kujifunza kutokana na fikra mbalimbali , hakuna mtu anayeweza kukosea umoja. Hakuna mtu anayeweza kukosea usawa," alisema.
“Umoja huu mliouweka pamoja leo hauwahusu ninyi wawili, maana 'Baba' ameona yote; kwa kweli anatosha kwa vizazi vyote. Rais amekaa kwenye nyadhifa zote. Kwa hivyo, kwa mawazo yangu, umoja huu ni wa vijana, wanawake, waliotengwa...ni kwa Wakenya wote ambao wamehisi kama hawajawahi kuwa sehemu ya Kenya.”
Mwenzake wa UDA na bosi wa Kaunti ya Embu Cecily Mbarire aliunga mkono matamshi hayo, na kupongeza zaidi uwazi wa mchakato huo na yaliyomo katika MoU.
Mbarire aliendelea kuwapongeza Rais Ruto na Raila kwa kuweka kando tofauti zao na misimamo mikali kwa ajili ya kuboresha taifa.
Tunaendelea kukupa maelezo zaidi kuhusu taarifa hii...
Unaweza pia kusoma:
Kesi ya uhaini dhidi ya Dr Besigye yaahirishwa

Kesi ya uhaini inayomkabili mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Dkt. Kizza Besigye, na wenzake Hajji Obeid Lutale na Kapteni Dennis Ola imesogezwa mbele hadi Machi 25.
Mwendesha mashtaka wa serikali aliambia mahakama kuwa bado wanaendelea na uchunguzi.
Mahakama pia imeahirisha hadi Machi 14 kusikiliza ombi la serikali kutaka amri ya mahakama kuruhusiwa kupata historia ya mawasiliano ya simu za Dkt. Kizza Besigye na Hajji Obeid Lutale.
Mwendesha mashtaka alitaka kesi iendelee kusikilizwa, lakini upande wa utetezi ulipinga akisema kuwa walitumiwa taarifa katika kipindi cha muda mfupi (jana).
Soma pia;
Asasi za kiraia nchini Tanzania zapendekeza kuondolewa adhabu ya viboko shuleni

Maelezo ya picha, Adhabu ya viboko itakoma lini Tanzania Kufuatia kifo cha mwanafunzi wa kidato cha pili Mhoja Maduhu anayedaiwa kuadhibiwa na mwalimu wake, baadhi ya asasi za kiraia zimepinga vikali adhabu za viboko kwa watoto wa shule nchini Tanzania,kwa mujibu wa gazeti la The Citizen.
Asasi hizo sasa zimetaka serikali kubatilisha mwongozo wa elimu wa 2002 ambao unaruhusu adhabu ya viboko shuleni.
Zimetaka kubuniwa kwa adhabu mbadala ambazo zitanuia kurekebisha mienendo ya wanafunzi na sio kuwaumiza.
Kamishna wa elimu Dkt Lyabwene Mutahabwa ameliambia gazeti hilo kwamba kuondolewa kabisa adhabu kwa wanafunzi ni suala ambalo haliwezekani bali wataweka mifumo ya kutathmini na kuhakikisha adhabu hizo hazivuki mipaka.
Tukio hilo lilitokea tarehe 26 mwezi Februari katika shule ya upili ya Mwasamba iliyoko mkoa wa Busega eneo la Simiyu.
Inadaiwa mwanafunzi huyo alifariki baada yakuchapwa viboko 10 na kukanyagwa kichwani na mwalimu wake baada ya kushindwa kumaliza kazi.
Mwanafunzi ambaye alishuhudia kisa hicho anadai Maduhu alichapwa kichwani na mgongoni kabla yakupigwa teke.
Licha ya Tanzania kuridhia mikataba ya kimataifa ya haki za watoto ,Tanzania bado inatumia adhabu ya viboko.
Ananastazia Rugaba ,meneja utetezi wa asasi ya TWAWEZA anasema wao wanapingana na adhabu ya viboko lakini wanaamini kwamba kuna adhabu mbadala ya viboko.
Meneja wa programu kutoka mtandao wa elimu Tanzania(TEN/MET) Nichodemous Shauri aliongeza kwa kubainisha kuwa ni shule za umma ndio zimekubuhu katika adhabu hii tofauti na shule za binafsi.
Soma pia:
Visa vingine vipya vya Ebola vyaripotiwa Uganda

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka ya Uganda iko mbioni kudhibiti maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ebila baada ya visa 12 kuripotiwa nchini humo.
Wasimamizi wa Afya kutoka kwa shirika la Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika CDC wamethibitisha ongezeko la visa vya Ebola.
Watu wawili- msichana wa miaka minne na muuguzi wamefariki tangu mlipuko wa ugonjwa huo kuanza mwezi Januari katika mji mkuu wa Kampala.
Madaktari sasa wanafanya shughuli za ufuatilitaji wa watu waliotangamana na waathiriwa wa ugonjwa hatari wa Ebola.
Afisa wa shirika la CDC Ngashi Ngongo amezungumza na wanahabari na kutaja watu watatu wamethibitishwa kuwa na Ebola huku wawili wakionyesha dalili ya ugonjwa huo.
Visa hivi vipya vimeripotiwa katika mikoa miwili tofauti baada ya vingine vitatu kuripotiwa kuwa na waathiriwa wa Ebola.
Kwa jumla, Uganda imerekodi visa 14 na vifo 2 tangu mlipuko wa Ebola, haya ni kwa mujibu wa shirika la CDC,
‘’Kuzuka kwa ugonjwa Ebola nchini Uganda ni changamoto kwani visa zaidi vinaendelea kuripotiwa. Hata hivyo nina imani mamlaka husika inafanya kila iwezalo kufuatilia waliotangamana na wagonjwa hao’’ anasema Ngongo.
Sio mara ya kwanza Uganda kuwa na mlipuko wa Ebola mwaka wa 2022 watu 55 kati ya 143 waliougua ugonjwa huo walifariki.
Maambukizi ya ugonjwa huo yalitangazwa kuisha mwaka wa 2023.
Taifa Jirani la Tanzania hivi majuzi liliripoti ugonjwa wa Marburg na mataifa yaliyo mipakani mwa Uganda kama vile Rwanda pia walishuhudia visa vya Marburg.
Ebola ni nini?
Ni virusi hatari vyenye dalili za awali ambazo zinaweza kujumuisha homa ya ghafla, udhaifu mkubwa, maumivu ya misuli na koo.
Dalili zinazofuata zinaweza kujumuisha kutapika, kuhara na katika hali nyingine kutokwa na damu ndani na nje, inayojulikana kama haemorrhaging.
Pia unaweza kusoma:
Urusi yashambulia vituo vya gesi vya Ukraine, watoto wanusurika

Chanzo cha picha, Getty Images
Angalau watu 18, wakiwemo watoto wanne, wamejeruhiwa katika shambulio la Urusi lililotokea usiku, mamlaka za maeneo mbalimbali nchini Ukraine zinaripoti. Hadi sasa, hakuna taarifa za vifo.
Hili lilikuwa shambulio kubwa zaidi la Urusi kwa kutumia meli zilizoko katika Bahari Nyeusi tangu mwanzo wa mwaka, msemaji wa jeshi la majini la Ukraine, Dmytro Pletenchuk, amesema.
Ameeleza kwenye televisheni ya Ukraine kwamba walirusha hadi makombora 20 usiku kucha.
Ijumaa iliyopita, Rais Zelensky wa Ukraine na Donald Trump wa Marekani walizozana hadharani katika Ikulu ya White House - ambapo Trump alisema Zelensky hakuwa tayari kumaliza mapigano.
Ameomba radhi na tayari kikao kijacho cha kutafuta suluhu kwa kuanzia na kusaini mkataba wa madini na Marekani, utafanyika wiki ijayo.
Hili pia lilikuwa shambulio la kwanza tangu kusitishwa kwa msaada wa kijeshi kutoka Marekani. Waziri wa Nishati amesema kuwa shambulio hilo lililenga miundombinu ya nishati ya Ukraine na vituo vya uzalishaji wa gesi.
Jinsi maisha ya wanawake yalivyobadilika chini ya utawala wa Taliban

Chanzo cha picha, BBC News: Nava Jamshid
Maelezo ya picha, Zeenat ambaye ni muokaji mikate Afghanistan Kabla ya Taliban kurejea madarakani Afghanistan mwaka 2021, wanawake na wasichana walikuwa na uhuru wa kusoma na kufanya kazi, ingawa walikumbana na changamoto za kijamii na unyanyapaa katika shughuli zao.
Hata hivyo, tangu utawala huo urejee, maisha ya wanawake yamebadilika kwa kiasi kikubwa.
Wanawake wamezuiliwa kupata elimu ya kimsingi pindi wanapofikisha umri wa miaka 12, na fursa zao za ajira zimepunguzwa.
Kwa sasa, sauti za wanawake hazipaswi kusikika hadharani au kuonekana bila kujistiri, na wanahitaji kuandamana na mwanamume kila wanapotoka nyumbani.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa asilimia 18 ya wanawake Afghan wamesema hawajatangamana na wanawake wenzao kwa miezi mitatu.

Chanzo cha picha, AFP
Zenat, mwenye umri wa miaka 55, alikua na duka la kuoka mikate kabla ya Taliban kurudi madarakani, lakini sasa anafanya biashara yake nyumbani.
Anasema biashara yake imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na hali ngumu ya maisha.
“Nikioka mikate yangu nyumbani nauza mafungu manne hadi sita, na kila mkate ni peni tano, ikiwa ni idadi kidogo ukilinganisha nilipokuwa nikiuza mjini,” anasema Zenat.

Maelezo ya picha, Freshta ni mkunga nchini Afghanistan Freshta, ambaye ni mkunga, alikatiziwa masomo yake wakati Taliban walipoingia madarakani.
Sasa anasema mapumziko yake ya kazi, ambayo yalikuwa ya furaha zamani, sasa ni kikwazo cha upweke.
“Tulipokuwa katika mapumziko, tungetembea sehemu mbalimbali kujiburudisha, lakini sasa hatuna mahali pa kuzuru. Hatuwezi kutoka nje hata siku moja. Tunachokubaliwa ni kwenda duka la jumla na kujisitiri hadi uso huku chapa nyingi za nguo tulizozipenda zikipigwa marufuku,” anasema Freshta.
Taliban walichukua tena udhibiti wa Afghanistan mwaka 2021, miongo miwili baada ya kuondolewa madarakani na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani.
Waliteka mkoa baada ya mkoa, hadi walipochukua mji mkuu, Kabul, mnamo Agosti 15, 2021, wakati jeshi la Afghanistan lilipoanguka.
Vikosi vya kigeni na baadhi ya wakaazi walikimbia kwa hofu ya utawala wa Taliban.
Soma pia:
Makumi wauawa jeshi la Syria likipambana na wafuasi wa Assad

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Vikosi vya Syria vinaelekea Latakia baada ya mapigano makali kuripotiwa Takriban miezi minne tangu utawala wa Bashir al- Assad kuangushwa mwishoni mwaka jana, wafuasi wake wameonekana kujibu kwa kushambulia wanajeshi wa serikali mpya.
Haya yamejiri baada ya wanajeshi wa utawala mpya wa Syria kushambuliana vikali na wapiganaji wa Rais aliyetimuliwa mamlakani Bashar al- Assad katika ukanda wa Gaza.
Ikiwa ni vita vikali kuwahi kutokea tangu wanamgambo wamvue madaraka Assad mwezi Disemba na kuweka serikali ya mpito ya Waislamu.
Kikundi kinachotathmini vita cha Uingereza kilichoko Syria kimesema takriban watu zaidi ya 70 wameuawa, hata hivyo BBC haijahakiki idadi kamili.
Ili kurejesha utulivu, amri ya kutotoka nje imetangazwa katika miji ya Latakia na Tartous ambapo mashambulizi hayo yamefanyika.
Mashambulizi hayo ya kushtukizia yalianza wakati wanajeshi wa Syria walipokuwa wakishika doria katika eneo la Latakia.
Msaada wa kijeshi wa ziada umetumwa katika eneo hilo huku video za mitandao ambazo hazijahakikiwa na BBC zikionyesha ufyatuliaji wa risasi katika baadhi ya maeneo.
Eneo hilo ambalo liko pwani ya nchi limehifadhi jamii ya walio wachache ya Alawite ambayo ni ngome ya familia ya Assad.
Pia kumekuwa na ripoti ya mapigano katika miji ya Homs na Aleppo huku ufyatuaji wa risasi ukisikika katika makazi kwa mujibu ya video ambayo bado haijahakikiwa.
Msemaji wa wizara ya Ulinzi ya Syria kanali Hassan Abdul Ghani ametoa onyo kwa watiifu wa Assad wanaozua rabsha katika eneo la Latakia.
‘’Maelfu wamechagua kusalimisha silaha zao nakurejea kwa familia zao huku wengine wakisisitiza kuendelea kupigana kwa niaba ya wahaliFu na wauaji. Chaguo liko wazi, salimisha silaha ama tukuangamize,’’ anasema.
Eneo hilo limekuwa tishio kwa Rais wa Muda Ahmed al-Sharaa.
Huku wanaharakati wa jamii ya Alawite wakisema jamii yao imekuwa ikihangaishwa tangu utawala wa Assad uanguke.
Mapema wiki hii, Waziri wa mambo ya Kigeni wa Syria aliambia idara ya uangalizi wa silaha za kemikali kuwa serikali mpya imejitolea kuharibu mirundiko ya silaha za kemikali zilizotengenezwa wakati wa utawala wa Assad.
Haya yanajiri hata baada ya serikali ya Assad kukataa vikali kutumia silaha za kemikali katika vita vya kiraia vya miaka 14, lakini wanaharakati waliwalaumu kufanya mashambulizi ya kemikali.
Soma pia:
Kenya yachukua hatua dhidi ya TikTok kuhusiana na unyanyasaji wa watoto

Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA) imetangaza wasiwasi wake kufuatia ripoti tulioichapisha (BBC) tarehe 3 mwezi Machi 2025, inayodai kuwa TikTok imekuwa ikifaidi kutokana na unyanyasaji wa watoto katika matangazo ya moja kwa moja nchini Kenya.
Huku Kenya ikiapa kubuni jopo kazi la kuchunguza unyanyasaji huo katika mtandao huo wa kijamii imeielekeza TikTok kuondoa mara moja maudhui yote ya ngono yanayohusisha watoto.
Vile vile, Mamlaka ya Tiktok imetakiwa pia kuboresha mifumo yake ya udhibiti ili kuepuka unyanyasaji wa watoto.
Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya pia imesisitiza kujitolea kwake katika kuunda mazingira salama na yenye maadili mtandaoni na inatoa wito kwa watoa huduma za mtandao wote wanaofanya kazi nchini Kenya kutii sheria na masharti ya ulinzi wa watoto na kuzuia usambazaji wa maudhui hatarishi.
Kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Mawasiliano David Mugonyi kwa kunukuu ''Kenya ina sheria madhubuti za kulinda watoto dhidi ya unyanyasaji mtandaoni, ikiwa ni pamoja na Sheria ya Utumiaji Mbaya wa Kompyuta na Uhalifu wa Mtandao ya mwaka 2018, Sheria ya Filamu na Michezo ya Jukwaani, inayohitaji Kamati ya Uainishaji ya Filamu ya Kenya (KFCB) kudhibiti maudhui ya vyombo vya habari, na Sheria ya Watoto, inayohakikisha ulinzi wa haki za watoto'' inaeleza.
Shirika la ChildFund Kenya likitaja taifa la Kenya kama kitovu cha unyanyasaji huu, mamlaka ya mawasiliano imewataka wazazi kuchukua hatua madhubuti kulinda watoto wao dhidi ya hatari mtandaoni kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Kulingana na uchunguzi uliofanywa na BBC ulibaini kuwa watoto wanahusika katika kuuza maudhui ya ngono, huku TikTok ikichukua ada ya asilimia 70% kutoka kwa maudhui hayo.
Kampuni hiyo ilikana kuchukua ada kubwa kiasi hicho baada ya BBC kuthibitisha ada hiyo katika uchunguzi wa 2022.
TikTok imekuwa ikifahamu kuhusu unyanyasaji wa watoto katika matangazo ya moja kwa moja tangu mwaka 2022, lakini ilipuuzilia mbali suala hilo kwa sababu "ilifaidi sana" kutokana na hali hiyo, kulingana na madai ya kesi iliyoletwa na jimbo la Utah, Marekani, mwaka jana.
TikTok inataka kujiimarisha katika masoko ya Afrika, lakini haijaajiri wafanyakazi wa kutosha ili kudhibiti maudhui ipasavyo, walisema wasimamizi wa maudhui Kenya.
Soma zaidi:
Sudan yaishtaki UAE katika mahakama ya kimataifa kwa 'kuchochea vita'

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, RSF imeshutumiwa kwa kufanya mauaji ya kimbari huko Darfur - dhidi ya makundi yasiyo ya Kiarabu katika eneo hilo Sudan imeamua kuchukua hatua kali dhidi Umoja wa falme za kiarabu kwa madai inaunga mkono wanamgambo wa RSF katika vita vya wenyewe kwa vinavyoendelea nchini humo.
Ikitafuta haki katika Mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa ICJ imeshutumu falme hizo kuwa inahusika katika mauaji ya kimbari ya makundi yasiyo ya Kiarabu katika jimbo la Darfur.
Aidha Sudan imelalamika kuwa UAE inatoa msaada wa kijeshi na kifedha kwa waasi wa RSF.
Kwa upande wa UAE, imepinga vikali madai ya Sudan ikieleza kesi hiyo kama "jambo lisilo na msingi kwa umma’’ na kuapa kukata rufaa itupiliwe mbali.
Hata hivyo, Wataalam wa Umoja wa Mataifa UN wanaofuatilia zana za vita zilizopigwa marufuku Darfur wameelezea madai ya UAE kufanya magendo ya silaha kwa RSF kupitia Chad ni ya kuaminika.
Ombi la Sudan la kutaka ushauri kutoka mahakama ya ICJ si la kisheria, ila linaweza kuwa na athari za kisiasa.
Vita hivyo vilivyodumu kwa miaka miwili vimeathiri Sudan huku maelfu wakiuawa na zaidi ya milioni 12 wakiachwa bila makaazi na kusababisha janga la kibinadamu.
Mapema wiki hii, shambulizi lilitekelezwa katika kambi ya wakimbizi kaskazini mwa Darfur na kusababisha watu kadhaa kufariki.
Vile vile,soko lililokuwa limejaa watu wengi eneo la Abu Shouk, kambi iliyo karibu na jiji la El- Fasher ilishambuliwa kwa takriban saa mbili siku ya Jumanne jioni , ofisa mmoja aiambia BBC.
Tangu vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vianze mwezi Aprili 2023, RSF na jeshi la Sudan wamelaumiwa kwa kutekeleza uhalifu wa kivita.
Soma pia:
Papa Francis atuma ujumbe wa sauti kwa mara ya kwanza tangu alazwe hospitalini

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika ujumbe wake wa kwanza kupitia kutuma sauti tangu alipolazwa hospitalini tarehe 14 mwezi Februari, Papa Francis wa kanisa la katoliki amewashukuru wale ambao wamekuwa wakimuombea afueni ya haraka.
Papa Francis mwenye umri wa miaka 88 amekuwa hospitalini kwa takriban wiki tatu baada ya kuugua homa ya mapafu.
Katika ujumbe mfupi wa sentensi mbili kutoka hospitali ya Gemeli alikolazwa, Papa amesikika kupumua kwa taabu wakati akiwashukuru wasamaria wema kwa dhati.
Ujumbe huo ulichezwa wakati wa ibada ya usiku ya kumuombea Papa katika kanisa la St Peter's Square iliyoko Vatican.
Hata hivyo, Vatican imesema ujumbe huo ulirekodiwa jana Alhamisi.
Hivi karibuni, Vatican ilitangaza kuwa Papa alikuwa katika hali ya utulivu baada ya kushuhudia matukio mawili ya kushindwa kupumua, na alikuwa akitumia msaada wa “mashine ya kupumua,” lakini sasa amerejea kutumia maski ya oksijeni.
Papa amekuwa akilazimika kutohudhuria shughuli kadhaa tangu kupelekwa hospitalini, ikiwa ni pamoja na ibada ya Jumatano ya Majivu, ambayo inaashiria mwanzo wa kipindi cha majuma sita kuelekea Pasaka.
Pia unaweza kusoma:
Marekani, Ukraine kukutana tena wiki ijayo, Zelensky aomba msamaha

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais Volodymyr Zelensky amesema mazungumzo kati ya Marekani na Ukraine yatafanyika Saudi Arabia wiki ijayo, akieleza matumaini kwamba utakuwa "mkutano wenye maana". Kiongozi huyo wa Ukraine, ambaye atakuwa katika ufalme huo wa Ghuba lakini hatashiriki katika mazungumzo, alisema Kyiv inapambana kufikia amani "ya haraka na ya kudumu".
Mjumbe maalum wa Rais wa Marekani, Donald Trump, Steve Witkoff, alisema timu ya Marekani ilitaka kujadili "mfumo" wa amani kujaribu kumaliza vita vya Urusi na Ukraine. Ijumaa iliyopita, Zelensky na Trump walizozana hadharani katika Ikulu ya White House - ambapo Trump alisema Zelensky hakuwa tayari kumaliza mapigano.
Marekani baadaye ikatangaza kusitisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine na kusimamisha kushirikiana kwenye taarifa za kijasusi. Rais wa Ukraine ameonyesha majuto kuhusu tukio hilo na kujaribu kurekebisha uhusiano na Marekani – ambayo ndiyo inayotoa msaada mkubwa wa kijeshi wa nchi hiyo.
Witkoff alisema Alhamisi, Trump alipokea barua kutoka kwa Zelensky iliyojumuisha "kuomba msamaha" na kuonyesha" hisia ya shukrani". "Tunatumai, tutarejesha mambo kwenye mstari na Waukraine, na kila kitu kitaanza tena," Witkoff alisema.
Zelensky amekuwa chini ya shinikizo kubwa la Marekani kufanya makubaliano kabla ya mazungumzo yoyote ya amani, wakati rais wa Ukraine amekuwa akishinikiza dhamana thabiti za usalama kwa Kyiv.
Zelensky alitangaza mazungumzo ya Marekani na Ukraine nchini Saudi Arabia katika mfululizo wa machapisho yake kwenye mitandao ya kijamii, baada ya kuhudhuria mkutano wa dharura wa Alhamisi mjini Brussels ambapo viongozi wa Umoja wa Ulaya waliidhinisha mipango ya kuongeza matumizi ya ulinzi.
"Timu za Ukraine na Marekani zimeanza tena kazi, na tunatumai kwamba wiki ijayo tutakuwa na mkutano wenye maana," aliandika kwenye X.
"Ukraine imekuwa ikitafuta amani tangu wakati wa kwanza wa vita, na tumekuwa tukisema kila wakati kwamba vita vinaendelea tu kwa sababu ya Urusi." Zelensky alihimiza jumuiya ya kimataifa kuweka shinikizo zaidi kwa Moscow ili "ikubali hitaji la kumaliza" vita. Urusi ilianzisha uvamizi kamili wa Ukraine mnamo Februari 2022, na sasa inadhibiti takriban 20% ya eneo la Ukraine.

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Kikao cha Trump na Zelensky kilivunjika wiki iliyopita baada ya kuzozana hadharani Pia unaweza kusoma:
