Kipi ni marufuku kwa wanawake na wanaume katika sheria mpya kali za Taliban?

re

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Ali Hussaini
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Serikali ya Taliban imeweka sheria mpya iliyopitishwa wiki iliyopita nchini Afghanistan na wanadai inalenga ‘kukuza wema na kuondoa uovu,’ lakini Umoja wa Mataifa unasema sheria hiyo inatisha.

Vipengele katika sheria hiyo ni pamoja na kupiga marufuku wanawake kuzungumza kwa sauti kubwa hadharani na kuonyesha nyuso zao nje ya nyumba zao.

Afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa alionya siku ya Jumapili kwamba sheria hizi zinatoa "taswira yenye kutisha ya siku zijazo kwa Afghanistan."

Sheria hizo mpya tayari zimeidhinishwa na kiongozi mkuu wa nchi hiyo, Haibatullah Akhundzada.

Wizara ya Maadili, iliyokuwa ikijulikana rasmi kwa jina la Wizara ya Kueneza Wema na Kuzuia Uovu, ilisisitiza kuwa hakuna mtu yeyote ambaye anasameheka na sheria hizo.

Sheria mpya zinaruhusu mohtasabeen, au polisi wa maadili, kuingilia maisha ya umma ya Waafghanistan, kusimamia jinsi wanavyovaa hadi kile wanachokula na kunywa.

Chini ya sheria mpya, sauti za wanawake pia zinachukuliwa kuwa ni uovu zinaposikika hadharani. Sheria inasema, “wakati wowote mwanamke mtu mzima anapoondoka nyumbani kwake kwa jambo la lazima, analazimika kuficha sauti, uso na mwili wake.”

Wizara hiyo tayari ilikuwa inatekeleza sheria ya kimaadili kwa kuzingatia sharia, au sheria ya dini ya Kiislamu, na iliripoti kwamba imewaweka kizuizini maelfu ya watu kwa kushindwa kuzifuata.

Sheria hizi, kwa mujibu wa Taliban, zinaendana na tafsiri yao ya sharia na Wizara ya Maadili ndiyo yenye jukumu la kuzitekeleza.

Sheria hizo zinatokana na agizo la mwaka 2022 la kiongozi mkuu wa Taliban ambalo sasa limechapishwa rasmi kama sheria.

Sheria inasemaje kwa wanawake?

df

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sheria hiyo mpya haijafika kote Afghanistan, lakini serikali inaandaa mpango wa kupanua matumizi yake.

Sheria inaeleza jinsi wanawake wanavyopaswa kufunika kabisa miili yao, ikiwemo kuficha nyuso, ili kuepuka kuwaingiza wanaume katika majaribu na uovu. Kanuni zenyewe:

  • Sauti ya mwanamke inachukuliwa kuwa ni awrah na haifai kusikika hadharani. Neno la Kiarabu awrah linamaanisha viungo vya wanaume na wanawake ambavyo lazima vifunikwe, na havipaswi kuonekana hadharani.
  • Wanawake wasisikike wakiimba au kusoma kwa sauti, hata kutoka ndani ya nyumba zao.
  • Mavazi ya wanawake hayapaswi kuwa membamba, mafupi au ya kubana.
  • Wanawake lazima wafiche miili na nyuso zao kutoka kwa wanaume ambao hawajawaoa au kuhusiana nao kwa damu.
  • Wanaume pia wamekatazwa kutazama miili na nyuso za wanawake, na hilo pia linawahusu wanawake watu wazima kuangalia miili ya wanaume.

Kanuni mpya kwa wanaume

ed

Chanzo cha picha, Getty Images

Sheria mpya za maadili pia zinaweka kanuni fulani kwa wanaume.

  • Sasa wanatakiwa kufunika miili yao kuanzia kwenye kitovu hadi magotini wakiwa nje ya nyumba zao, kwani sehemu hizi za mwili huchukuliwa kuwa ni awrah.
  • Wanaume hawaruhusiwi kutengeneza nywele zao kwa njia ambayo ni kinyume na sharia.
  • Taliban imepiga marufuku vinyozi katika majimbo kadhaa kunyoa au kupunguza ndevu, kwa madai kwamba amri hii inaambatana na sharia.
  • Kwa mujibu wa kanuni mpya, ndevu lazima ziwe na urefu wa ngumi.
  • Sheria ya maadili pia inakataza wanaume kuvaa tai.

Mohtasabeen ni akina nani?

Mohtasabeen ni polisi wa maadili na wana jukumu la kutekeleza sheria hizi na kufanya kazi katika majimbo yote.

Kwa kupitishwa sheria hiyo mpya, nguvu zao za utendaji zimeongezeka, haswa kwa vile wanaungwa mkono kikamilifu na kiongozi wa Taliban.

Wataweza kunyamazisha sauti za wanawake au muziki unaotoka majumbani mwao, na kuwashikilia wanaume wanaonyoa ndevu au kukata nywele zao kwa mtindo usiotakiwa.

Sheria inasema, polisi wa maadili pia watakuwa na mamlaka ya kuzuia madereva wa teksi kuwasafirisha wanawake kwenye magari yao ambao hawajaandamana na jamaa wa karibu wa kiume, kama vile baba au kaka mtu mzima, au ambao hawajavaa hijabu kama ilivyoelekezwa na sharia.

Wanaume na wanawake pia hawawezi kukaa karibu kwenye gari.

Picha za viumbe hai haziruhusiwi

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Haibatullah Akhundzada, kiongozi mkuu wa nchi hiyo, aliidhinisha sheria mpya.

Sheria mpya pia inakataza kuunda, kuhifadhi au kuchapisha picha za viumbe hai, na inahusu kila kitu kuanzia kuchora ndege hadi kupiga picha ya mwanafamilia.

Kwa mujibu wa sheria mpya, ununuzi na uuzaji wa sanamu za viumbe hai pia ni marufuku.

Sheria inatoa wito kwa polisi wa maadili kuzuia matumizi yasiyofaa ya vinasa sauti na redio, kama vile kucheza muziki, ambayo inachukuliwa kuwa haramu na sharia.

Utayarishaji na utazamaji wa picha na filamu za viumbe hai pia ni marufuku.

Lakini kinyume na sheria hizo mpya, takribani maafisa wote wa serikali ya Taliban wameonekana kwenye kamera, akiwemo Mohammad Khaled Hanafi, Waziri wa Kueneza wema na Kuzuia Uovu.

Adhabu ni zipi?

Sheria inasema mtu akifanya “kitendo kilichokatazwa waziwazi, atakabiliwa na msururu wa adhabu, kuanzia “kuonywa, kutishwa na adhabu ya Mungu, faini na kifungo cha hadi siku tatu.”

Sheria hizo zimekumbana na ukosoaji mwingi.

"Baada ya miongo kadhaa ya vita na katikati ya mzozo mbaya wa kibinadamu, watu wa Afghanistan wanastahili mambo mazuri, zaidi ya kutishiwa au kufungwa ikiwa watachelewa kuswali, kuangalia mtu wa jinsia tofauti ambaye si mtu wa familia yao au picha ya mpendwa wako,” anasema Roza Otunbayeva, mkuu wa Misheni ya Usaidizi ya Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan.

Wizara ya Kueneza wema na Kuzuia uovu ni mojawapo ya mashirika ya serikali yenye nguvu zaidi nchini Afghanistan.

Mwaka jana polisi wa maadili waliripotiwa kuwashikilia kwa muda zaidi ya watu 13,000 kwa kushindwa kufuata sharia .

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah