Mzozo wa DRC: Kuuawa kwa Willy Ngoma kunaashiria nini?

Willy Ngoma katika uwanja wa mji wa Goma, muda mfupi baada ya wao kuudhibiti mji huo mwaka uliopita.

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Samba Cyuzuzo
    • Nafasi, BBC Gahuzamiryango
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

"Napigana ili Congo iwe bora", haya ni majibu aliyotoa Willy Ngoma mwezi Novemba mwaka uliopita alipoulizwa na mwandishi wa BBC mbona anajihusisha na vita vinavyoendelea mashariki mwa DRC.

Jeshi la DR Congo, FARDC limedhibitisha kuwa limetekeleza mashambulizi katikati mwa mji wa Rubaya, mashariki mwa taifa hilo siku ya Jumanne, na kumuua Willy Ngoma, msemaji wa kundi la AFC/M23.

Mwezi Novemba mwaka wa 2021, baada ya miaka minane ya kimya kutoka kwa M23, kundi hilo lilianza mapigano tena katika milima ya Chanzu na Runyoni karibu na mlima Sabyinyo.

Wakati huu, M23 ilikuwa imejipanga na kujiandaa vyema kukabiliana na FARDC.

Wakati huu vita vikianza tena watu wengi hawakuwa wanamjua Willy Ngoma.

Kuanzia mwaka wa 2022, jina la "Meja" Willy Ngoma msemaji wa kundi la waasi la M23, lilianza kupata umaarufu katika vyombo vya habari.

Willy Ngoma alichukua nafasi ya kanali Jean Marie Vianney Kazarama, ambaye alikuwa msemaji wa M23 wa awali kabla ya kundi hilo kutokomezwa na kugawanyika mwaka wa 2013.

Willy Ngoma awali alisema amekuwa mwanachama wa M23 kuanzia mwaka wa 2012 baada ya kuondoka katika chama cha UDPS kilichoanzishwa na babake rais Felix Tsishekedi, Étienne Tshisekedi.

Msemaji huyo aliuawa kupitia shambulio la angani lililotekelezwa na FARDC eneo la Rubaya Jumanne usiku, shambulio ambalo liliwaacha viongozi kadhaa wa M23 na majeruhi.

Tukio hili linajiri wiki chache tu baada ya taifa la DRC kuipa kampuni za Marekani leseni za kuchimba madini.

"Droni" silaha mpya za kivita

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Shambulio hili lilitotekelezwa kutumia ndege zisizo na rubani na kumuua Willy Ngoma ambaye alikuwa amepanda cheo katika kundi hilo na kuwa Luteni Kanali, inasemekana kuwa ilifanywa kwa uangalifu na kwa kutumia ujasusi wa hali ya juu.

Ndege zisizo na rubani au droni za kijeshi ziko na kamera ambazo humwonyesha mtu anayeziendesha picha za mtu au kitu wanachokilenga kabla ya shambulio kutekelezwa.

Mapema mwezi huu, msemaji wa M23 Lawrence Kanyuka alisema kundi hilo "liliharibu" jengo moja lililokuwa katika uwanja wa ndege wa Kisangani ambalo lilikuwa na droni ambazo zilikuwa zinatarajiwa kutumika kuwashambulia.

Corneille Nangaa, kiongozi wa AFC/M23 alisema watashambulia viwanja vya ndege, na kuwa watadungua droni zote zitakazowalenga.

FARDC imeweza kutekeleza shambulio kwa kutumia ndege zisizo na rubani huku mapigano makali yakiripotiwa eneo la Minembwe kusini mwa Kivu, pamoja na maeneo mengine kama Walikale,Masisi,Rutshuru Kivu Kaskazini.

Kutumika kwa droni hizi kuwalenga viongozi wa M23 kunaonekana kama mwamko mpya wa vita hivi.

Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakiwa na droni ya kivita angani huku moto ukiwaka nyuma yao.

Chanzo cha picha, VPMDefenseRdc

Kuuawa kwa Willy Ngoma kwa shambulio la angani, linaonyesha nguvu ambayo imeanza kutumika katika vita vya kudhibiti kundi la waasi wa M23.

Kando na kifo cha Willy Ngoma, inahofiwa kuwa wapiganaji wa M23 na viongozi wa kundi hilo ni miongoni mwa waliofariki katika shambulio hilo.

Matumizi ya ndege zisizo na rubani na FARDC yameripotiwa kuongezeka siku za hivi karibuni, kuonyesha nguvu ya ziada jeshi hilo ikonayo ikija katika kutekeleza mashambulizi ya angani.

Juma lililopita, FARDC iliilaumu M23 kwa kushambulia vituo vya kijeshi.

Pande zote mbili zinapozidi kulaumiana kuhusu nani anaanzisha mashambulizi, na kukiuka makubaliano ya kusitisha vita, kifo cha Willy Ngoma, kinaweka makubaliano hayo yaliyoafikiwa katika njia panda.

Willy Ngoma alikuwa nani haswa?

Willy Ngoma (kushoto) akikutana na Brigedia Jenerali Emmanuel Kaputa (kulia) wa wanajeshi wa FARDC.

Chanzo cha picha, Getty Images

Alijulikana kama mkosoaji mkubwa wa Rais Felix Tshisekedi, na alipenda kusema kuwa anajua mifumo yote ya chama cha UDPS kwani aliwahi kuwa mwanachama wa chama hicho.

Umoja wa Mataifa ulikuwa umemuekea vikwazo Ngoma mwaka wa 2023 kwa kusema "Anaendelea kushiriki katika vurugu inayotekelezwa na M23" ikiwemo mauaji, utekaji nyara, wizi, kuwasajili Watoto kupigana,biashara haramu ya madini na mengineyo."

Umoja wa Mataifa, pia ulimkashifu kwa "kutetea na kutangaza mashambulizi yaliyotekelezwa na M23" mashariki mwa DRC.

Akijibu tuhuma za umoja wa mataifa na vikwazo alivyowekewa, Ngoma katika mahojiano ya awali na BBC alisema kuwa " haituhusu sisi, sisi ni jeshi la raia, tunapigana ili raia wa Congo wapate maisha bora."

Vyanzo kadhaa vinasema kuwa Ngoma alizaliwa kaskazini mwa Rwanda ila alikuwa na ukoo kutokea Wilaya ya Congo ya Kati (Kongo-Central), ambako alisomea shule ya msingi na kulelewa eneo la Mbanza-Ngungu, kijiji kilichoko kilomita 150 kusini magharibi mwa mji wa Kinshasa.

Vyanzo kadhaa ikiwemo umoja wa mataifa vinasema alikuwa na umri wa miaka zaidi ya 50.

Hakuwahi kuzungumzia maisha yake binafsi, ila waliomjua, wanasema alikuwa na watoto wanne.

Baada ya kuudhibiti mji wa Goma mwezi Januari mwaka uliopita, Ngoma alionekana katika video moja iliyosambaa mitandaoni iliyoonyesha kundi la M23 lilivyokuwa limewakamata mamluki wakizungu.

Ngoma alionekana tena mwezi Machi katika video nyingine akipiga gumzo na wanajeshi wa Afrika Kusini waliokuja kudumisha amani kupitia muungano wa SADC, na walikuwa wamezuiliwa kwa muda katika uwanja wa ndege wa Goma, kabla ya kurejea nchini mwao.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula na kuhaririwa na Samba Cyuzuzo