Afghanistan: 'Taliban wataniua wakiuteka mji wangu'

Chanzo cha picha, BBC
"Katika ndoto zangu mara kwa mara naona wanamgambo wa Taliban wakichukua udhibiti wa mji wangu,"anasema Habib.
Habib ni mwandishi wa habari wa Afghanistan na kwa miaka minane iliyopita amekuwa akifanyia kazi kituo cha habari kinachofadhiliwa na majeshi ya Ujerumani. Ajira yake ilikomeshwa mwishoni mwa Juni wakati wanajeshi wa kimataifa walipoanza kuondoka nchini.
Kutokana na sababu za kiusalama, ametuomba tusitumie jina lake halisi.
"Taliban wataniua ikiwa watauteka mji wangu," baba huyo wa watoto watatu aliiambia BBC katika mahojiano ya simu.
Wanamgambo wa Taliban wanakaribia kuingia mji wa Habib' uliopo kaskazini mwa nchi, na anasema barabara mara nyingi hazina magari hali inayoashiria hatari inayowakodolea macho.

"Nusu ya wilaya [mkoa wangu] tayari iko mikononi mwa Taliban. Siku chache zilizopita waliingia karibu kilomita 10 hadi 12 ndani ya mji kabla warudishwe nyuma," anasema.
Raia wa Afghanistan wamekabiliwa na miongo kadhaa ya mzozo, lakini baadhi yao wanahofia hali inaweza kuwa mbaya zaidi baada ya Rais Biden kutangaza kuondoa wanajeshi wote wa Marekani kufikia mwezi Agosti.
Vikosi vinavyoongozwa Marekani vilifanikiwa pakubwa kudumisha utulivu, lakini kuna wasiwasi ikiwa majeshi ya Afghan wanaweza kufanya hivyo. Wakiwa wameingiwa na woga, wengi wanahangaika kupata pasipoti.
Hofu ya kulipiza kisasi
Wakati wa utawala wao wa muda mfupi mwishoni mwa 1990, Taliban uliwaua watu hadharani na kuwazuia wanawake kupata elimu na ajira.
Taliban wanasema wamebadilika na kwamba hawatarejelea kufanya ghasia kama hizo.
Katika taarifa, walisema watu kama Habib waliofanyia kazi majeshi ya kigeni hawatalengwa,lakini kwa masharti: "Wanapaswa kuonyesha kuwa wanajutia vitendo vyao vya zamani na hawapaswi kushiriki katika shughuli kama hizo ambazo ni uhaini dhidi ya Uislamu na nchi.
Habib ana mashaka na licha ya shirika la kutetea haki la Human Rights Watch, kuorodhesha visa vya mashambulio ya kisasi vinavyotekelezwa na wanamgambo dhidi ya raia waliodhaniwa kuunga mkono serikali.

Chanzo cha picha, BBC
Habib hana shaka kuwa atabandikwa jina la msaliti na amekusanya virago vyake tayari kuondoka.
"Jamii yetu inabadilika haraka sana. Watu sasa wananiambia wazi wazi, 'lifanyia kazi wageni'. Hali inayonifanya kuwa na uwoga sana."
Hana uhakika ikiwa jamaa zake aua marafiki wanaweza kumficha hali ya dharura ikitokea wakifahamu fika hatari inayohusiana na hatua hiyo.
"Tulifanya kazi na Wajerumani. Tulichapisha taarifa zilizokuwa na umuhimu kwa wanamgambo wa Taliban. Kwetu, tishio kubwa linatoka kwao."
Habib na wenzake hukutana mara kwa mara kupeana taarifa.
"Nimesoma kwamba Ujerumani itawapatia hifadhi wale wote waliofanyia kazi wanajeshi wao. Lakini hatujui lolote kuhusu mchakato huo na utachukua muda gani," anasema.
Baadhi yao wametoa maombi ya visa ya usafiri - Habib pia anajaribu bahati yake katika ubalozi wa India.
"Ni hatari kwenda kinyume cha sheria. Tunaweza kuibiwa au hata kuuawa. Kuna tofauti gani kati ya kufariki hapa na kufariki ukiwa njiani kwenda Ulaya?"
Vitisho
Tofauti na Habib, wengine wengi wanatathmini njia zote za kutoroka, kisheria au vinginevyo.
"Najaribu kupata visa ya kwenda Uingereza. Ikiwa sitapata, Nitaenda Ulaya kupitia njia njia za kiharamu," daktari mmoja kutoka mashariki mwa Afghanistan aliiambia BBC.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Katika kipindi cha miezi mitatu, wafanyakazi tisa wameuawa na wengine wanne kujeruhiwa," alisema.
Daktari huyo alifanyia kazi kampeni ya afya ya umma katika mikoa minne ya kusini. Kampeni hiyoilisitishwa katika mkoa wa - Nangarhar - baaada ya wafanyakazi watano kuua wa Juni 15. Kundi la Islamic State linashukiwa pakubwa kuhusika na mauaji hayo.
Daktari huyo anasema amepokea vitosho kadhaa kutoka kwa makundi yaliyojihami yanayohudumu katika eneo hilo na ambayo yanayopinga. Hana imani kwamba serikali inaweza kumhakikishaia usalama wake.
Baba huyo wa watoto watanoanataka kuuza alicho nacho na kuondoka nchini humo haraka iwezekanavyo.
Uhitaji mkubwa
Ni raia wachache sana wa Afghanistan wanaweza kupata visa hali inayowafanya wengi wao kutafuta msaaada wa mtandao wa wahalifu.
"Mahitaji yako juu, kwa hivyo gharama iko juu sana," anasema Sami (sio jina lake halisi - alisisitiza utambulisho wake usitolewe), ambaye ni mlanguzi wa watu aliye na makao yake mjini Kabul.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Nilikuwa nikitoza hadi dola elfu 8,000 kumpeleka mtu Italia. Sasa ni dola milioni 10,000."
Hizi ni pesa nyingi katika nchi ambayo mapato ya wastani ni karibu dola 500 kwa mwaka.
Tangu Marekani ilipoondoka kabi kubwa ya anga ya Bagram, Sami anasema biashara yake imeshamiri.
"Katika wiki mbili zilizopita, Nimewapeleka karibu watu 195. Natarajia kupeleka makumi ya wengine zaidi hivi karibuni."
Safari hatari
Sami anasema yeye huwaambia wateja wake kuhusu hatari inayohusika, lakini hamzuilii mtu yeyote. Baadhi yao wamewahiukamatwa na kurejeshwa nyumbani.
"Ikiwa Taliban watachukua uongozi, watu zaidi huenda wakauawa, kwa hivyo wengi wako tayari kuhatarisha maisha yao ili kujinusuru," anasema.

Chanzo cha picha, BBC
Watu wanasafirishwa kiharamu kupitia Iran hadi Uturuki na kupelekwa Ugiriki kwa kutumia maboti.
"Karibu watu 900 wameangamia wakati wa safari ya kuvuka bahari na kuingia Ulaya mwaka huu," anasema Babar Baloch ambaye ni msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Wakimbizi (UNHCR) .
"Kuna karibu waomba hifadhi 9,000 katika visiwa vya Ugiriki. Raia wa Afghanistan wanakadiria hadi asilimia 48 ya watu hao," anasem.
Kulingana na ripoti ya UNHCR ya Mwelekeo wa Ulimwenguni 2020, karibu watu miilioni tatu wa walifurushwa makwao ndani ya Afghanistan kufikia mwisho wa mwaka jana, milioni 2.6 wakiwa ughaibuni.
Ndani ya miezi sita ya kwanza ya mwaka huu, Waafghan wengine 200,000 walitoroka makwao na Umoja wa Mataifa unahofia "wengine wengi watafurushwa makwao ndani ya nchi na nje ya mipaka yake''.
Kuhofia mabaya zaidi
Mmoja wa wahamiaji aliymlipa Sami ni Asad( sio jina laki sahihi) aliye na umri wa miaka 17, kutoka mkoa wa Nangarhar. Alivuka Iran na kuzungumza na BBC -kwa masharti ya kutotambulishwa - kupitia mji wa mpakani wa Van nchini Uturuki.

Chanzo cha picha, BBC
"Katika wiki chache zijazo watakuwa wakitembea kutoka mtaa moja hadi mwingine wakipigana,"anasema Asad.
Makundi mengi yaliyojihami yanahudumu nchini. Baadhi yao ni sehemu ya serikali na ni maadui wakubwa wa Taliban na makundi mengine ya wanamgambo kama vile Islamic State.
"Hatujui ni nini kitafanyika Afghanistan siku zijazo. Nataka kwenda mahali palipo na amani," Asad anasema.
Hawezi kuongea Kiingereza au lugha nyingine ya Ulaya. anasafiri na wanaume wengine 30 wa Afghanistan - wenigi wao sawa na yeye walimaliza shule lakini hawana ujuzi wa kiufundi.
"Nikishikwa nitajaribu tena. Sitaki kuishi nchini Afghanistan," anasema.
Asad - ambaye familia yake angalau inajiweza - anasema anatazamia omba hifadhi nchini Ufaransa.
Kati ya matumaini na kukata tamaa
Nyumbani Afghanistan, kadri muda unavyosonga ndivyo Habib anaingiwa na wasiwasi.

Chanzo cha picha, BBC
Mji wake bado uko chini ya udhibiti wa majeshi ya Afghan, lakini wanamgambo wa hawako mbali na hapo kwani anasikia milipuko ya vilipuzi na makabiliano ya risasi nyakati za usiku.
Ana wasiwasi huenda asifanikiwe kuondoka endapo uwanja wa ndege utatekwa. Kwa sasa kila anachomiliki kinaendelea kupoteza thamani kwa haraka.
"Hakuna anayetaka kununua gari au nyumba. Watu wanataka kuuza kila kitu na kutoroka,"anasema.
Habib anaendelea kusubiri ujumbe muhimu utakao okoa maisha yake.
"Tunaishi kati ya matumaini na kukata tamaa. Nasubiri ujumbe wa barua pepe ambayo unasema 'unaweza kuja Ujerumani',"aliiambia BBC.













