Nchi 10 zenye nguvu kubwa zaidi za kijeshi Afrika 2025

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Ripoti ya hivi majuzi iliofanywa na mtandao wa Marekani wa Global firepower {GFP} ilitathmini nguvu za kijeshi za nchi 145 ulimwenguni, kwa kuzingatia ukubwa wa vifaa, Idadi ya wanajeshi , uwezo wake, fedha, jiografia na rasilimali.
Uwezo huo wa kijeshi unashawishiwa na miungano, uhusiano wa kidiplomasia na hatua zilizopigwa katika teknolojia.
Hapa barani Afrika, Mataifa ya Misri, Algeria, na Nigeria ndio yaliyoorodheshwa katika mstari wa mbele kama yanayoongoza kwa uwezo wa kijeshi yakionesha uwekezaji mkubwa katika bajeti za ulinzi ili kuboresha miundombinu na kupata silaha za hali ya juu.
Mataifa yaliyostawi kiuchumi kama vile Misri na Afrika Kusini yametanguliza matumizi ya ulinzi katika bajeti zake ili kudumisha usalama, huku mataifa mengine yakikabiliwa na changamoto za migogoro ya ndani, vikosi vya kijeshi, na vikosi visivyo na ufadhili wa kutosha kukabiliana na waasi.
Licha ya uwezo wa kikanda, wanajeshi wa Afrika wamesalia nyuma ikilinganishwa na mataifa yaliyoendelea kwa sababu ya tofauti katika ugawaji wa bajeti, teknolojia, mafunzo na ufikiaji wa kimkakati.
Kulingana na Global Firepower, hizi hapa ni nchi 10 za Afrika zenye nguvu kubwa zaidi za kijeshi mwaka 2025.
10. Libya

Chanzo cha picha, Getty Images
Libya inakamilisha orodha ya kumi bora barani Afrika ikiwa katika nafasi ya 76 ulimwenguni. Nguvu za kijeshi za nchi hiyo zimeathiriwa na miaka mingi ya migogoro ya wenyewe kwa wenyewe lakini inabakia na umuhimu wa kimkakati kutokana na eneo lake na maliasili
9. Sudan

Chanzo cha picha, AFP/Getty
Sudan imeorodheshwa ya tisa barani Afrika na inashikilia nafasi ya 73 ulimwenguni. Jeshi lake linakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na kukosekana kwa utulivu wa kisiasa lakini bado linalenga kudumisha uadilifu wa kieneo.
Nguvu ya jeshi la Sudan imekadiriwa kuwa wanajeshi 109,300 mwaka 2011 (kulingana na IISS), wanajeshi 200,000 kabla ya vita vya sasa vya Sudan kuzuka mwaka 2023 (kulingana na CIA), na wanajeshi 300,000 mwaka 2024 (kulingana na shirika la habari Al Jazeera} kwa mujibu Wikipedia.
8. DR Congo

DRC inashika nafasi ya nane barani Afrika na inashikilia nafasi ya 66 duniani. Licha ya migogoro ya ndani, nchi hiyo imekuwa ikifanya kazi ya kuleta utulivu. Imepata uwezo wake wa kijeshi kupitia ushirikiano wa kimataifa na kuongeza uwekezaji katika jeshi lake.
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) lenye wanajeshi wanaokadiriwa kufikia 135,000, ni jeshi kubwa lakini linakabiliwa na changamoto za mafunzo, vifaa na mawasiliano, hali ambayo imesababisha mapambano dhidi ya wanamgambo wadogo walio na vifaa vya kutosha kama vile M23.
Jeshi la DRC FARDC, linalojumuisha Jeshi la Wanamaji, na Jeshi la Wanahewa, linakadiriwa kuwa na karibu wanajeshi 135,000.
Wengi wa wanajeshi wa FARDC wako katika vikosi vya nchi kavu.
Pia lina kikosi kidogo cha angani na kikosi kidogo zaidi cha wanamaji, pamoja na kikosi cha rais kiitwacho Walinzi wa Republican.
7. Morocco

Chanzo cha picha, FMSO - Foreign Millitary Study Office
Morocco imeorodheshwa ya saba barani Afrika na ya 59 duniani kote.
Nchi hiyo imejikita katika kuboresha vifaa vyake vya kijeshi, haswa kwa usalama wa mpaka na operesheni za kukabiliana na ugaidi.
Morocco inadumisha uhusiano mkubwa wa kidiplomasia na mataifa ya Magharibi kwa ushirikiano wa kiulinzi.
6. Angola
Angola inashikilia nafasi ya sita barani Afrika na nafasi ya 56 duniani. Nguvu yake ya kijeshi inaimarishwa na mapato ya mafuta ambayo yanafadhili sekta yake ya ulinzi.
Angola imewekeza katika kuboresha vikosi vyake vya kijeshi ili kukabiliana na changamoto za usalama wa ndani
5. Ethiopia

Chanzo cha picha, Getty Images
Ethiopia ipo katika nafasi ya tano barani Afrika na ya 52 duniani. Licha ya changamoto za kiuchumi, Ethiopia inadumisha jeshi kubwa linalozingatia masuala ya usalama wa kikanda, hasa migogoro katika Pembe ya Afrika.
Taifa hilo limewekeza pakubwa katika miundombinu, kupanua upatikanaji wa huduma na kuboresha hali ya maisha.
Vilevile nchi hiyo ni mwanachama hai wa muungano wa Umoja wa Afrika.
Wanajeshi wa Ethiopia wamepewa mafunzo nchini Urusi, na nchi hiyo ina historia ya ushiriki wa kijeshi katika migogoro ya kikanda.
Ethiopia ni mchangiaji mkubwa katika misheni ya kimataifa ya kulinda amani, ikiwa na kikosi kilichofunzwa na uzoefu mkubwa.
4. Afrika Kusini
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Afrika Kusini imeorodheshwa ya nne barani Afrika na ya 40 kote duniani.
Ikijulikana kwa tasnia ya hali ya juu ya ulinzi, Afrika Kusini inazalisha vifaa vyake vingi vya kijeshi.
Hata hivyo, vikwazo vya bajeti vimepunguza maendeleo zaidi ya vikosi vyake vya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni.
Wanajeshi waliopo na wale wa akiba: Jeshi la SANDF lina maafisa 71,235 walio hai na 29,350 wa akiba.
Nguvu ya Nchi Kavu: Afrika Kusini ina kikosi chenye nguvu cha nchi kavu, kikijumuisha vifaru 195, magari ya kivita 12,140, mifumo mbalimbali ya mizinga na roketi.
Nguvu ya angani: Jeshi la Anga la Afrika Kusini lina jumla ya ndege 194, zikiwemo ndege za kivita, ndege maalum, ndege za usafiri, ndege za mafunzo na helikopta.
Nguvu ya Wanamaji: Jeshi la Wanamaji la Afrika Kusini lina jumla ya meli 47, ikiwa ni pamoja na zile za kivita na nyambizi, lakini halina meli za kubeba ndege za kivita.
Bajeti ya Ulinzi: Inakadiriwa bajeti ya ulinzi ni karibu $2.7 bilioni.
3. Nigeria

Chanzo cha picha, Getty Images
Nigeria imeorodheshwa ya tatu barani Afrika na ya 31 ulimwenguni. Imefanya uwekezaji mkubwa katika vikosi vyake vya kijeshi ili kupambana na uasi na ugaidi ndani ya mipaka yake.
Vikosi vya Wanajeshi vya Nigeria vinajumuisha idadi kubwa ya maafisa pamoja na magari ya kivita na ndege.
Mwaka 2024, jeshi la anga la Nigeria liliripotiwa kuwa na maafisa 18,000, Silaha za kukabiliana na mashambulizi ya angani 179, zikiwemo ndege 117, helikopta 55 na ndege saba zisizo na rubani (UAVs).
2. Algeria
Algeria inashika nafasi ya pili barani Afrika na ya 26 duniani.
Nguvu yake ya kijeshi inasaidiwa na mapato makubwa ya mafuta, kuiwezesha kupata silaha za hali ya juu na kudumisha nguvu iliyofunzwa vizuri.
Algeria inaangazia usalama wa mipakani na oparesheni za kukabiliana na ugaidi huku ikidumisha vikosi vikali vya anga na nchi kavu.
1.Misri

Chanzo cha picha, Reuters
Misri inatambulika kuwa nchi yenye nguvu zaidi kijeshi barani Afrika na inashika nafasi ya 19 duniani.
Vikosi vya Wanajeshi wa Misri vinajumuisha matawi makuu manne: Jeshi la Wanamaji, Jeshi la Wanahewa, na Vikosi vya Ulinzi wa Angani.
Nchi hiyo imewekeza sana katika kuboresha vifaa vyake vya kijeshi na miundombinu, vifaru vingi, ndege na meli za wanamaji. Misri pia inafaidika na msaada mkubwa wa kijeshi wa kigeni, ikiwa ni pamoja na dola bilioni 1.85 kila mwaka kutoka Marekani.
Vikosi vya Misri vinapitia juhudi za uboreshaji wa haraka wa kisasa, kupata silaha za kisasa na teknolojia za dharura za ardhini, baharini na angani.
Jeshi la Misri lina jukumu kubwa katika kudumisha utulivu katika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.
Marekani imeipatia Misri msaada mkubwa wa kijeshi - uwekezaji katika utulivu wa kikanda.
Misri ina jeshi kubwa, jeshi la wanamaji, na la angani, lenye historia ya kuhusika katika migogoro, ikiwa ni pamoja na Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Yemeni Kaskazini na Vita vya Misri na Libya.
Misri ni moja wapo ya nchi chache katika Mashariki ya Kati kuwa na satelaiti za kijasusi, ilizindua EgyptSat 1 mnamo 2007, ikifuatiwa na EgyptSat 2 mwaka 2014, MisrSat-2 mwaka 2023, na Horus-1 mwaka 2025.
Jeshi la Wanamaji la Misri lina kundi kubwa la meli za mashambulizi ya haraka, nyingi zikiwa na mifumo ya makombora, na linahusika katika uzalishaji wa ulinzi wa majini, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa frigates, corvettes, na boti za doria.
Jeshi la Wanahewa la Misri limekuwa likifanya meli zake kuwa za kisasa na lina historia ya utengenezaji wa ndege.














