Ajali 7 kubwa za migodini zilizotikisa Afrika

G

Chanzo cha picha, AP

    • Author, Mariam Mjahid
    • Nafasi, Mwandishi BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Ajali ya hivi karibuni ya mgodi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) iliyoua zaidi ya watu 200 imeibua tena maswali kuhusu usalama wa migodi barani Afrika.

Migodi imekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa nchi nyingi za Afrika.

Dhahabu, almasi, platinamu, kobalti na shaba zimejenga miji, zimeongeza mapato ya serikali na kuifanya Afrika kuwa mhimili wa rasilimali za dunia.

Lakini chini ya ardhi, mbali na takwimu za mauzo na faida, kuna simulizi nyingine ya jasho, hatari na mara nyingi vifo.

Hizi ni ajali saba zilizoacha alama isiyofutika.

Mgodi wa Coalbrook – Afrika Kusini (1960)

f

Ajali ya mgodi wa makaa ya mawe wa Coalbrook bado inachukuliwa kuwa janga kubwa zaidi la migodini barani Afrika. Wachimbaji 437 walifukiwa hai baada ya nguzo za chini ya ardhi kuporomoka.

Coalbrook haikuwa tu ajali; ilikuwa funzo la kikatiba. Vifo hivyo vilisababisha mageuzi makubwa ya sheria za usalama migodini Afrika Kusini.Kusini.

Ajali ya Mgodi wa Marikana – Afrika Kusini (2012)

Maombolezo wakati wa mazishi ya wachimba madini waliouawa

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Maombolezo wakati wa mazishi ya wachimba madini waliouawa

Ingawa tukio hili linajulikana zaidi kama mauaji ya Marikana, lilihusisha moja kwa moja wachimbaji wa madini ya platinamu au ukipenda dhahabu nyeupe.

Zaidi ya wachimbaji 34 waliuawa na polisi wakati wa mgomo, wakidai malipo zaidi, tukio lililotikisa Afrika Kusini na dunia nzima, na kufichua hali mbaya ya maisha na usalama wa wachimbaji migodini.

Mauaji hayo yaliyofanyika tarehe 16 mwezi Agosti, yanasemekana kuwa mabaya zaidi kuwahi kufanyika tangu kumalizika kwa enzi ya ubaguzi wa rangi mwaka 1994.

Marikana ilionyesha kuwa hatari migodini si ardhi pekee, bali pia siasa, ukosefu wa haki na matumizi ya nguvu. Ilikuwa kielelezo cha mgodi kama uwanja wa mapambano ya kijamii, si tu kiuchumi.

Ajali ya mgodi wa Kamoto – Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (2019)

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maporomoko ya ardhi katika mgodi wa shaba na kobalti wa Kamoto uliua zaidi ya wachimbaji 40, wengi wao wakiwa wachimbaji wadogo wasio rasmi.

Ajali ya mgodi wa dhahabu – Siaya, Kenya (Julai 2024)

Katika Kaunti ya Siaya, Kenya, mgodi wa dhahabu uliporomoka na kusababisha vifo vya wachimbaji 7, huku wengine wakijeruhiwa na kupelekwa hospitalini. Hii ilionyesha hatari inayowakumba wachimbaji wadogo bila usalama wa kutosha.

Wataalam wa masuala ya usalama na uchimbaji wa madini wamezungumzia jinsi wachimbaji wadogo wanavyofanya kazi katika mazingira hatarishi bila usalama wa kutosha.

Mgodi wa dhahabu ulioporomoka, Mkoa wa Simiyu (Januari 2024)

Wafanya kazi wa migodini hukumbwa na matatizo ya vifaa
Maelezo ya picha, Wafanya kazi wa migodini hukumbwa na matatizo ya vifaa

Mgodi mdogo wa dhahabu usio na leseni ulipoporomoka kufuatia mvua kubwa uliwaua angalau wafanyakazi 22 kaskazini mwa Tanzania.

Wengi waliojeruhiwa walihitajika uokoaji mzito kutoka chini ya matope, wakiwa ni wa umri wa miaka 24 hadi 32.

Ajali hii ilitokea wakati wachimbaji walianza kazi bila kusubiri taratibu za kiusalama.

"Awali tuliambiwa kulikuwa na watu 19 hadi 20 waliokuwa wamenasa migodini lakini kwa bahati mbaya tuliishia kuopoa miili 22," Simon Simalenga, aliliambia shirika la habari la Reuters.

Maendeleo yanagharimu nani?

Ajali za migodi zimeibua hisia miongoni mwa wachambuzi wakitafakari kuwa maendeleo ya Afrika yamejengwa juu ya wachimbaji madini wasio na sauti na vifaa vya kuchimba.

Kadiri mahitaji ya kimataifa ya madini ya Afrika yanavyozidi kuongezeka, kuna msukumo mpya kutoka kwa serikali kujifunza kutokana na makosa yaliyopita na kuhakikisha utajiri ulio chini ya ardhi unainua maisha ya walio juu yake.

''Wachimbaji wengi barani Afrika hufanya kazi katika mazingira hatarishi bila ulinzi wa kutosha, hali inayogeuza migodi kuwa maeneo ya vifo vinavyoepukika'', lasema Shirika la haki za binadamu la Amnesty.