'Ninafanya kazi katika mgodi ulio kilomita 2 chini ya ardhi ulio na makaburi na biashara ya ukahaba'

Chanzo cha picha, Getty Images
Sambamba na wanaume wengine wapatao 600, Ndumiso anaishi na kufanya kazi katika "mji" mdogo unaodhibitiwa na genge la kihalifu,ukizungukwa na masoko na wilaya yenye idadi kubwa ya wafanya biashara wa ukahaba - ambao umekua chini ya ardhi katika mgodi wa dhahabu ambao hautumiki nchini Afrika Kusini.
Ndumiso aliiambia BBC kwamba baada ya kuachishwa kazi na kampuni kubwa ya uchimbaji madini, aliamua kujiunga na genge hilo katika ulimwengu wake wa chini ya ardhi na kuwa kile kinachojulikana kama "zama zama", mchimbaji haramu wa madini.
Yeye huchimba madini hayo ya thamani na hutoka kila baada ya miezi mitatu au zaidi ili kuuzwa sokoni kwa faida kubwa, akipata zaidi ya alivyowahi kufanya hapo awali - ingawa hatari sasa ni kubwa zaidi.
"Maisha ya chini ya ardhi hayana huruma. Wengi hawafanikiwi kuwa hai," alisema kijana huyo mwenye umri wa miaka 52, ambaye alizungumza na BBC kwa sharti kwamba jina lake halisi lisitumike kwani alihofia kulipiziwa kisasi.
"Katika ngazi moja ya shimoni kuna miili na mifupa. Tunaita hayo makaburi ya zama-zama," alisema.
Lakini kwa wale ambao wamenusurika,kama Ndumiso, kazi inaweza kuwa yenye manufaa.
Huku akilala juu ya mifuko ya mchanga baada ya siku ngumu za kufanya kazi chini ya ardhi, familia yake inaishi katika nyumba ambayo amenunua katika kitongoji cha jiji kuu, Johannesburg.
Alifanya malipo ya pesa taslimu ya randi 130,000 (kama dola 7,000; pauni 5,600) kwa nyumba hiyo ya chumba kimoja, ambayo sasa ameipanua kujumuisha vyumba vingine vitatu, alisema.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mchimbaji huyu haramu wa madini kwa takriban miaka minane, Ndumiso ameweza kuwapeleka watoto wake watatu katika shule za kulipia - mmoja wao sasa yuko chuo kikuu.
"Lazima nimtimizie mke na watoto wangu mahitaji na hii ndiyo njia pekee ninayoijua," alisema na kuongeza kuwa alipendelea kufanya kazi chini ya ardhi badala ya kuongeza kiwango cha uhalifu kwa kuwa mtekaji nyara au majambazi, baada ya miaka mingi ya kutafuta kazi halali.
Kazi yake ya sasa ni katika mgodi ulioko katika mji mdogo wa Stilfontein, karibu maili 90 (145km) kusini-magharibi mwa Johannesburg, ambako ni katikati ya kituo kilichotolewa tahadhari ya kimataifa baada ya waziri wa serikali, Khumbudzo Ntshavheni, kuahidi "kuwatoa" mamia ya wachimbaji madini waliokuwa chini ya ardhi huko, huku vyombo vya usalama vikizuia chakula na maji kuteremshwa.
"Wahalifu hawatakiwi kusaidiwa. Wahalifu wanapaswa kuteswa," Ntshavheni alisema.
Kikundi cha wanaharakati kinachofahamika kama The Society for the Protection of Our Constitution, kimeanzisha kesi mahakamani kudai kufikiwa kwa shimo la kuchimba madini, ambalo polisi wanasema lina kina cha kilomita 2 (maili 1.2).
Mahakama imetoa uamuzi wa muda, ikisema kuwa chakula na vitu vingine muhimu vinaweza kuwasilishwa kwa wachimbaji hao.

Chanzo cha picha, Reuters
Ndumiso anafanya kazi kwenye shimo tofauti la mgodi huo, na alijitokeza mwezi uliopita, kabla ya kusitishwa kwa sasa.
Sasa anasubiri kuona jinsi hali inavyoendelea, kabla ya kuamua kurejea au la.
Mgogoro huo unafuatia uamuzi wa serikali wa kukabiliana na tasnia ambayo imedorora, huku magenge kama mafia yakiendesha.
"Nchi imekuwa ikikabiliwa na janga la uchimbaji haramu kwa miaka mingi, na jamii za wachimbaji zilibeba mzigo wa vitendo vya uhalifu kama ubakaji, wizi na uharibifu wa miundombinu ya umma," alisema Mikateko Mahlaule, mwenyekiti wa kamati ya Bunge inayoshughulikia rasilimali za madini.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alisema mgodi huo ulikuwa "eneo la uhalifu", lakini polisi walikuwa wakijadiliana na wachimba migodi hao ili kumaliza mzozo huo, badala ya kwenda chini kuwakamata.
"Mamlaka za kutekeleza sheria zina taarifa kwamba baadhi ya wachimbaji madini wanaweza kuwa na silaha nzito. Imethibitishwa wazi kwamba wachimbaji haramu wanaajiriwa na magenge ya wahalifu na kuwa sehemu ya makundi makubwa yanayopanga njama za kihalifu," aliongeza.
Ndumiso alikuwa miongoni mwa mamia ya maelfu ya wafanyakazi - wenyeji na raia wa mataifa jirani kama Lesotho - ambao wameachishwa kazi huku sekta ya madini nchini Afrika Kusini ikidorora katika miongo mitatu iliyopita. Wengi wa hawa wameendelea kuwa "zama zama" kwenye migodi iliyotelekezwa.
Mtafiti wa Benchmark Foundation yenye makao yake makuu Afrika Kusini David van Wyk, ambaye amefanyia utafiti sekta hiyo, alisema kuna takriban migodi 6,000 iliyotelekezwa nchini humo.
"Wakati hainufaishi uchimbaji madini wa viwanda vikubwa, wana faida kwa uchimbaji mdogo," aliiambia podikasti ya BBC Focus on Africa.
Ndumiso alisema alikuwa akifanya kazi ya kuchimba visima, akipata chini ya $220 (£175) kwa mwezi, kwa kampuni ya uchimbaji dhahabu hadi alipoachishwa kazi mwaka 1996.

Baada ya kuhangaika kwa miaka 20 iliyopita kusaka ajira kwa sababu ya kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira nchini Afrika Kusini, alisema aliamua kuwa mchimbaji madini haramu.
Kuna makumi ya maelfu ya wachimba migodi haramu nchini Afrika Kusini, huku Bw Van Wyk akisema wanafikia takriban 36,000 pekee katika jimbo la Gauteng –kitovu cha uchumi wa nchi hiyo ambapo dhahabu iligunduliwa kwa mara ya kwanza katika Karne ya 19.
"Zama zama mara nyingi itatumia miezi kadhaa chini ya ardhi bila kujitokeza na kutegemea sana msaada kutoka nje wa chakula na mahitaji mengine. Ni kazi ngumu na ya hatari," ilisema ripoti ya kikundi cha wanaharakati wa Global Initiative Against Transnational Organised Crime.
"Wengine hubeba bastola, bunduki na silaha kali ili kujilinda na magenge hasimu ya wachimba migodi," iliongeza.
Ndumiso aliambia BBC kwamba alimiliki bastola, lakini pia alilipa genge lake "ada ya ulinzi" ya kila mwezi ya takriban $8.
Walinzi wake wenye silaha nzito huepuka vitisho, hasa kutoka kwa magenge ya Lesotho yanayosifika kuwa na uwezo mkubwa wa kisilaha, alisema.
Chini ya ulinzi wa saa 24 wa genge hilo, Ndumiso alisema alitumia baruti kulipua mwamba na zana zisizo za kawaida kama vile shoka, jembe na patasi kutafuta dhahabu.
Sehemu kubwa ya kile anachopata humpa kiongozi wa genge, ambaye humlipa kima cha chini cha $1,100 kila baada ya wiki mbili. Alisema aliweza kuweka dhahabu, ambayo anaiuza sokoni ili kuongeza mapato yake.
Alikuwa miongoni mwa wachimba migodi waliobahatika kuwa na mpangilio kama huo, akieleza kuwa wengine walitekwa nyara na kupelekwa shimoni kufanya kazi kama vibarua, bila kupokea malipo yoyote au dhahabu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ndumiso alisema kwa kawaida hukaa chini ya ardhi kwa takriban miezi mitatu kwa wakati mmoja, kisha hurejea kwa wiki mbili hadi nne ili kuwa na wakati na familia yake na kuuza dhahabu yake, kabla ya kurejea kwenye shimo refu.
"Ninatarajia kulala juu ya kitanda changu na kula vyakula vilivyopikwa nyumbani. Kuvuta hewa safi ni hisia yenye nguvu ya ajabu."
Ndumiso hatoki mara nyingi, ikiwa atapoteza eneo lake la kuchimba, baada ya miezi mitatu inakuwa siku nyingi sana kusalia chini ya ardhi.
Alikumbuka kwamba mara moja alipofika juu ya uso: "Nilipofushwa na mwanga wa jua hivi kwamba nilifikiri kuwa nilikuwa kipofu."
Ngozi yake pia ilikuwa imebadilika rangi sana hivi kwamba mke wake alimpeleka kufanya uchunguzi wa kimatibabu: "Nilikuwa mkweli kwa daktari kuhusu mahali nilipoishi. Hakusema chochote, na alinitibu tu. Alinipa vitamini."
Awapo Juu ya ardhi Ndumiso hapumziki tu. Pia hufanya kazi na wachimbaji haramu wengine kwani miamba yenye madini inayoletwa kutoka chini inalipuliwa na kusagwa kuwa unga laini.
Hii basi "huoshwa" na kikundi chake kwenye kiwanda cha dharura ili kutenganisha dhahabu kwa kutumia kemikali hatari kama zebaki na sodium cyanide.
Ndumiso alisema kisha anauza sehemu yake ya dhahabu - gramu moja kwa $55, pungufu ya bei rasmi ya takriban $77.
Alisema ana mnunuzi aliye tayari, ambaye huwasiliana naye kupitia WhatsApp.
“Mara ya kwanza nilipokutana naye sikuwa na imani naye hivyo nilimwambia tukutane kwenye maegesho ya magari ya kituo cha polisi nilijua nitakuwa salama pale.
"Sasa tunakutana sehemu yoyote ya kuegesha magari tuna mzani, tunapima dhahabu hapohapo, kisha namkabidhi na yeye ananilipa pesa taslimu," alisema huku akionyesha kuwa anatembea na kati ya $3,800 na $5,500.
Anapata kiasi hiki kila baada ya miezi mitatu, ikimaanisha wastani wa mapato yake kwa mwaka ni kati ya $15,500 na $22,000 - zaidi ya $2,700 alizopata kama mchimbaji madini aliyeajiriwa kihalali.
Ndumiso alisema viongozi wa genge hilo walipata pesa nyingi zaidi, lakini hakujua ni kiasi gani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa upande wa mnunuzi wa dhahabu yake Ndumiso alisema hajui lolote kumuhusu,isipokuwa ni mzungu katika sekta haramu inayohusisha watu wa rangi na matabaka tofauti.
Hii inafanya kuwa vigumu kukabiliana na mitandao ya uhalifu, na Bw Van Wyk akisema serikali ilikuwa inalenga wachimba migodi - lakini sio "wakuu wanaoishi katika vitongoji vya Johannesburg na Cape Town".
Bw Ramaphosa alisema uchimbaji haramu wa madini unagharimu "uchumi wetu mabilioni ya fedha katika kupoteza mapato ya nje, mirabaha na kodi", na serikali itaendelea kushirikiana na makampuni ya madini "kuhakikisha yanachukua jukumu la kukarabati au kufunga migodi ambayo haifanyi kazi tena. ".
Bw Van Wyk aliambia podikasti ya BBC Focus on Africa kwamba serikali itazidisha mgogoro wa kiuchumi wa Afrika Kusini ikiwa italibana "zama zama".
“Kuwe na sera ya kuharamisha shughuli zao, kuzipanga vyema na kuzidhibiti,” aliongeza.
Wakati Ndumiso anarudi chini kazini, anachukua ziada ya chakula cha makopo ili kuepuka gharama kubwa ya vyakula vinavyopatikana huko.
Mbali na chakula, vitu vya msingi - kama sigara, tochi, betri - na zana za uchimbaji madini viliuzwa huko, alisema.
Hii inabainisha kwamba jumuiya - au mji mdogo huo - ulikuwa umeendelea chini ya ardhi kwa miaka mingi, huku Ndumiso akisema hata kulikuwa na eneo la bishara haramu, na wafanyabiashara ya ngono waliletwa chini ya ardhi na magenge hayo.
Ndumiso alisema mgodi aliofanyia kazi ulikuwa na viwango kadhaa, na miundo mbinu ya barabara zilivyounganishwa.
"Ni kama barabara kuu, zenye mabango yaliyopakwa rangi yakitoa maelekezo ya maeneo na viwango tofauti - kama choo, au kiwango ambacho tunakiita makaburi ya zama-zama," alisema.
"Wengine wanauawa na wanachama wa genge pinzani; wengine wanakufa wakati wa maporomoko ya mawe na kusagwa na mawe makubwa. Nilipoteza rafiki baada ya kuporwa dhahabu yake na kupigwa risasi kichwani."
Ingawa maisha ya chinichini ni hatari, ni hatari ambayo maelfu kama Ndumiso wako tayari kuikabili, kwa kile wanachosema kuwa njia mbadala ni kuishi na kufa maskini katika taifa ambalo kiwango cha ukosefu wa ajira kinazidi 30%.
Imetafsiriwa na Martha Saranga












