Iran kutuma nusu ya hifadhi yake ya Urani nje ya taifa hilo na kuyeyusha iliyosalia- Reuters

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa Iran imetoa "ridhaa mpya" kuhusu mpango wake wa nyuklia katika mazungumzo yake ya kuafikia makubaliano na Marekani, mradi tu waondolowe vikwazo vya kiuchumi na watambue haki ya Tehran ya "kumiliki silaha za nyuklia kwa amani."
Ila shirika hilo lilisema kuwa afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Iran, alisema kuwa pande hizo mbili bado zinatofautiana kwa kiasi kikubwa baada ya duru mbili za mazungumzo kumalizika.
Hii inajiri baada ya Oman, ambaye ndiye mpatanishi mkuu wa mataifa hayo mawili, kusema kuwa mfululizo mwingine wa mazungumzo utafanyika mjini Geneva kuanzia Alhamisi.
Afisa huyo wa Iran aliyezungumza na Reuters alisema kuwa Iran "Imeanza kuzingatia wazo la kutuma nusu ya hifadhi yake ya Urani nje ya nchi, na kuyeyusha kiwango kilichosalia, na kuunda muungano wa kikanda wa kumiliki urani," wazo ambalo limeibuliwa mara kwa mara katika miaka ya hapo nyuma.
Afisa huyo alisema Iran itafanya hivyo ili Marekani ikubali kuwa wanahaki "ya kumiliki nyuklia" katika maafikiano yao yatakayohusisha pia wao kuondolewa vikwazo vya uchumi.
Aliendelea kusema kuwa "Katika mazungumzo kuhusu uchumi yanayoendelea, Marekani pia ilisema inataka fursa ya kuwekeza kiuchumi katika sekta ya mafuta ya Iran."
Kando na hayo, rais wa Iran Masoud Pezeshkian alisema kuwa mazungumzo kati ya Iran na Marekani yaliyokamilika hivi karibuni yalikuwa yenye tija, ila akaongezea kuwa Tehran iko tayari kwa lolote.
Kupitia mtandao wa X, Pezeshkian aliandika kuwa "Iran imejitolea kudumisha amani na utulivu katika kanda hii. Katika mazungumzo ya hivi karibuni tumebadilishana mapendekezo. Hata hivyo, tunaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo ya Marekani, na tumeweka maandalizi yote muhimu kwa chochote kitakachotokea."
Ingawa Iran inasema wamepiga hatua katika mazungumzo, Marekani imekuwa ikiongeza nguvu zake za kijeshi Mashariki ya kati kwa kutuma meli na ndege za kivita.
Siku ya Ijumaa, rais wa Marekani Donald Trump alionya kuwa anazingatia "kufanya shambulio la wastan" dhidi ya Iran iwapo hawaatafikia makubaliano. Tehran ilijibu kwa kusema watazingatia shambulio lolote kutoka Marekani kama "uchokozi."

Chanzo cha picha, Getty Images
Duru mpya ya mazungumzo
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Waziri wa mambo ya kigeni wa Oman, Badr al-Busaidi, alitangaza kuwa Iran na Marekani watajumuika mjini Geneva siku ya Alhamisi katika duru ya tatu ya mazungumzo.
Mtandao wa habari wa Axios ulisema kuwa afisa mmoja mkuu wa Marekani alisema kuwa wanatarajia pendekezo la Iran ifikiapo siku ya Jumanne na kuwa juhudi hizi za kidiplomasia "huenda ikakuwa nafasi ya mwisho Trump ataipa Marekani" kabla ya shambulio litakalo mlenga kiongozi wa kidini Ali Khamenei.
Washauri wa Trump wanasema kuwa Rais huyo anaweza kubadili mawazo yake wakati wowote na kuishambulia Iran, ila wamemshauri kuwa na subira kwa sasa.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Abbas Araqchi, kupitia mtandao wa X aliandika kuwa "nashangaa mbona hatujisalimisha? Kwasababu sisi ni wa Iran"
Hii ni baada ya mjumbe maalum wa Marekani mashariki ya kati Steve Witkoff kuhoji mbona Iran hawajajisalimisha kufikia sasa.
Hayo yakijiri, Waziri wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas ametaka "suluhu ya kidiplomasia" kutumika katika kusuluhisha suala la Iran. "Hatutaki vita vingine, tayari tunavita vingi vinavyoendelea" Alisema Kallas.

Chanzo cha picha, Reuters
Siku ya Jumapili, shirika za habari nchini Iran, ziliripoti kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu waliandamana na kukabiliana na maafisa wa polisi.
Maandamano hayo yanakuja baada ya kukamilika kwa maandamano ya kupinga serikali yaliyoshuhudiwa mwezi uliopita, ambapo maelfu ya watu waliuawa.
Silaha za Urusi kwa Iran
Shirika la habari la Financial Times, limesema kutokana na nyaraka zilizovuja, wamebaini kuna makubaliano kati ya Urusi na Iran, ambapo Iran ilikuwa inataka kununua silaha za ulinzi wa angani kutoka kwa Urusi zenye dhamana ya dola millioni 545 mwezi Julai mwaka wa 2025, baada ya kumalizika kwa vita vya siku 12 vilivyoshuhudiwa wakati huo.
Kulingana na ripoti hiyo, mkataba huo ulitiwa saini mjini Moscow mwezi Disemba mwaka wa 2025.
Katika mkataba huo, Tehran itapokea vifaa 500 vya kurusha makombora na makombora 2500 kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Khamenei kuwataja warithi wake
Gazeti la The New York Times, limeripoti kuwa kiongozi wa kidini wa Iran, Ali Khamenei, katika miezi ya hivi karibuni alimpa majukumu mengi kiongozi mmoja wa uslama Ali Larijani, wakati ambapo kumekuwa na wasiwasi wa kushambuliwa na Marekani.
Kulingana na ripoti hizo Khamenei, alimpa majukumu Larijani mwenye umri ya miaka 67, mwanasiasa wa amani na kamanda wa awali wa jeshi la Revolutionary Guard ambaye kwa sasa anaongoza baraza kuu la usalama wa taifa hilo, kusimamia sekta muhimu za serikali hiyo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ushawishi wa Larijani umeongezeka kutokana na vile alikabiliana na waandamanaji ,kudhibiti habari na mawasiliano, kushirikiana na Urusi na Oman na kufuatilia mazungumzo yanayoendelea na Washington.
Larijani pia ametwikwa jukumu la kusimamia taifa hilo iwapo taifa hilo litaingia vitani na Marekani na viongozi wakuu kuuawa ikiwemo kiongozi wa kidini Ali Khamenei.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliauala











