Kusitisha mapigano kwa muda kunaweza kumaliza vita?

Chanzo cha picha, Reuters
Iran na Marekani wamekubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa wiki mbili, na kuruhusu meli kupita katika mlango bahari wa Hormuz.
Hatua hii imeafikiwa baada ya mwezi mmoja wa Israel na Marekani kuanzisha mfululizo wa mashambulizi dhidi ya Iran.
Saa chache tu baada ya Rais Trump kutishia kuwa "ataiangamiza Iran" kama hawatafungua mlango bahari wa Hormuz na kuruhusu meli kupita, makubaliano ya kusitisha vita yalitangazwa.
Trump kupitia mtandao wake wa Truth Social alisema alikubali kusitisha mashambulizi "kwasababu tuko karibu kuafikia makubaliano ya kudumu ya amani Mashariki ya Kati"
"Karibu vipengele vyote vimekubaliwa na Marekani na Iran, tumetoa muda wa wiki mbili ili tuhitimishe kila kitu" alisema Trump.
Trump aliliambia shirika la habari la AFP kuwa bila shaka Marekani imepata "ushindi kamili".
Ila Baraza Kuu la Usalama nchini Iran limesema kuwa Marekani "amepata pigo la kihistoria."
Mazungumzo hayo yatafanyika nchini Pakistan chini ya siku 15 ili kukubaliana na vipengele vya makubaliano hayo.

Chanzo cha picha, Reuters
Waziri mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, alisema "pande zote mbili zimeonyesha kuwa na busara na uelewa na wanashiriki kikamilifu katika juhudi ya kupata amani"
"Tunatumai kuwa mazungumzo yatakayofanyika Islamabad yatafaulu na kuleta amani ya kudumu, tunatarajia kuwa na habari njema siku zijazo"
Kusitishwa kwa vita kwa muda kunamaanisha nini?
Kulingana na Umoja wa mataifa, hakuna ufafanuzi wa kipekee wa kusitisha mapigano. Jina hili hutumika kijeshi la kutoa amri ya kuacha "kufyatua" silaha baada ya "kuanzisha makabiliano"
Jina hilo hutafsiriwa tofauti na pande zote zinazo zozana na kuanza kufanya mazungumzo.
Jina kusitisha mapigano na kujiondoa katika vita hutumika mara kwa mara kumaanisha kitu kimoja. Ila Umoja wa Mataifa unasema kuwa kuna tofauti kati ya istilahi hizo.
Kusitisha mapigano inaweza kueleweka kama makubaliano yasiyo rasmi, kwani usitishwaji rasmi wa mapigano huwa na makubaliano yalioandikwa na yanayobainisha:
- Madhumuni ya kusitisha mapigano
- Mwelekeo utakaofuata kisiasa
- Ni lini utaanza kutekelezwa
- Eneo la jiografia husika
Makubaliano hayo pia hufafanua mienendo ya kijeshi inayoruhusiwa na ambayo hairuhusiwi na jinsi usitishaji makubaliano utafuatiliwa na kutekelezwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mfano, katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia vilivyomalizika mwaka wa 1993, na serikali ya Transnational Unity kutia Saini mkataba na Liberian Patriotic Front pamoja na Liberian Democratic liberation movement, pande zote zilikubaliana kuacha kutumia silaha, kutolenga kituo chochote cha kijeshi, kutochochea vita vingine na kutoweka mabomu ya ardhini ambayo yanaweza kuchochea vita.
Kusitisha mapigano ni hatua ya kudumu au ni ya muda tu?
Inaweza kuwa yote, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Pande zinazo zozana hukubaliana kusitisha mapigano kwa muda au kwa njia ya kudumu.
Hii hufanyika ili kupunguza mateso na madhila wanayopitia raia wakati wa vita.
Wakati Israel na Hamas walipokubaliana kusitisha vita kwa muda kati ya tarehe 24 mwezi Novemba na tarehe 30 mwaka wa 2023, Hamas iliwaachilia mateka 105, na Israel kuwaachilia wafungwa 240.
Usitishaji wa mapigano pia huafikiwa ili kutoa mazingira mazuri ya mazungumzo kufanyika yatakayosaidia kupata suluhu ya kudumu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwezi juni mwaka wa 2000, Ethiopia na Eritrea walisitisha vita kwa muda ili kutoa fursa kwa mazungumzo rasmi kufanyika. Baada ya kukubaliana rasmi, walitia saini mkataba wa kumaliza vita hivyo baadaye mwezi Disemba mwaka huo, maarufu kama Algiers Agreement.
Licha ya kuwepo na makubaliano, vita vinaweza kuendelea baada ya vipengele vilivyokubaliwa kudhoofishwa.
Wakati mwingine upande mmoja unaozozana unaweza kutumia usitishaji wa mapigano kuimarisha nafasi yao ardhini kwa vita zaidi.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula












