Watu wa kujitolea wanaingia shimoni Afrika Kusini kuwasaidia wachimba madini

er

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Nomsa Maseko & Danai Nesta Kupemba
    • Nafasi, BBC News World
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Makumi ya watu wa kujitolea wameingia katika mgodi wa dhahabu uliotelekezwa nchini Afrika Kusini ili kuwasaidia maelfu ya wachimbaji haramu ambao wamekuwa chini ya ardhi kwa mwezi mmoja.

Kwa sababu wachimbaji hao waliingia katika shimo hilo huko Stilfontein kwa makusudi, wakijaribu kuchimba madini, serikali imechukua hatua kali, ya kuzuia chakula na maji.

Mapema wiki hii, waziri mmoja wa serikali alisema: "tutawalazimisha watoke."

Wachimbaji hao wamekataa kutoa ushirikiano kwa serikali kwa kuwa baadhi yao ni wahamiaji wasio na vibali na wanahofia kufukuzwa au kukamatwa.

Kuna taarifa kuwa wachimbaji hao wamekuwa wakila siki na dawa ya meno ili kuishi wakiwa chini ya ardhi. Inahofiwa kuwa afya zao zinaweza kudhoofika, na wasiweze kutoka katika mgodi huo wenyewe.

Pia unaweza kusoma

Uchimbaji haramu

OI

Watu waliojitolea ambao wamepangwa katika vikundi vitatu vya watu 50, wanasema inachukua kama saa moja kumtoa mtu mmoja nje.

Lebogang Maiyane amekuwa akijitolea tangu mwanzo mwa wiki.

"Serikali haijali kuhusu haki ya kuishi ya wachimbaji haramu ambao wako chini ya ardhi - hii ni sawa na mauaji" anasema.

Wachimbaji haramu wanafanya kazi katika migodi iliyotelekezwa katika nchi hiyo yenye utajiri wa madini. Uchimbaji madini haramu hugharimu serikali ya Afrika Kusini mamilioni ya dola katika mauzo kila mwaka.

Migodi mingi ya madini ya Afrika Kusini imefungwa katika miaka ya hivi karibuni na wafanyakazi wengi wamefutwa kazi.

Ili kuishi, wachimbaji madini na wahamiaji wasio na vibali hushuka chini ya ardhi kuchimba dhahabu na kuziuza kwenye soko la biashara haramu.

Wengine hutumia miezi wakiwa chini ya ardhi - kuna hata biashara ndogo ndogo za kuuza chakula na sigara kwa wachimbaji.

Serikali yagoma

DF
Maelezo ya picha, Thandeka Tom anasema kaka yake ni mmoja wa maelfu ya wachimbaji walio chini ya ardhi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakazi wa eneo hilo wameiomba serikali kuwasaidia wachimbaji hao, lakini imekataa.

"Tutawatoa kwa nguvu. Watatoka. Hatupeleki msaada kwa wahalifu. Wahalifu hawapaswi kusaidiwa," Waziri katika Ofisi ya Rais Khumbudzo Ntshavheni alisema siku ya Jumatano.

Jamaa wa wachimbaji hao wamekuwa wakiandamana karibu na eneo la mgodi, wakiwa wameshikilia mabango yenye maneno ya kuikosoa serikali.

Waziri wa usalama, Senzo Mchunu alitembelea eneo hilo siku ya Ijumaa, lakini alipojaribu kuzungumza na wanajamii waliokuwa wakisubiri kusikia habari za wapendwa wao shimoni, alifukuzwa.

Thandeka Tom ambaye kaka yake yuko mgodini, anawakosoa polisi kwa kutopeleka msaada.

"Kuna tatizo la ukosefu wa ajira nchini na watu wanavunja sheria wanapojaribu kutafuta chakula" aliiambia BBC.

Polisi wanasitasita kuingia mgodini kwani baadhi ya walio chini ya ardhi wanaweza kuwa na silaha.

“Baadhi ni sehemu ya makundi ya wahalifu,” Busi Thabane, kutoka Benchmarks Foundation, shirika la hisani nchini Afrika Kusini, aliiambia BBC.

Bila kupeleka mahitaji, hali ya chini ya ardhi inaweza kuwa mbaya.

Hali inaweza kuwa mbaya

SD

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha, Baadhi ya wachimbaji katika mgodi huo uliotelekezwa wako chini kwa takribani mwezi mmoja

"Haihusiani tena wachimbaji haramu - hili ni janga la kibinadamu," anasema Bi Thabane.

Siku ya Alhamisi, kiongozi wa kijamii Thembile Botman aliambia BBC kwamba watu waliojitolea walitumia kamba na mikanda ya usalama kuvuta mwili kutoka mgodini.

"Harufu mbaya ya miili inayooza imewaacha wanaojitolea wakiwa na kiwewe," alisema.

Haijulikani chanzo cha kifo cha mtu huyo.

Ingawa serikali imekuwa ikizuia chakula na maji, lakini wameruhusu wakaazi wa eneo hilo kutuma mahitaji kwa kamba.

Bw Botman anasema wamekuwa wakiwasiliana na wachimba migodi hao kwa maelezo yaliyoandikwa kwenye vipande vya karatasi.

Polisi wameziba maeneo ya kuingilia na kutokea, katika juhudi za kuwalazimisha wachimba hao kutoka nje. Hii ni sehemu operesheni ya kuzuia uchimbaji madini haramu.

Wachimbaji watano walitolewa nje siku ya Jumatano kwa kamba, lakini walikuwa dhaifu na wamechoka. Wahudumu wa afya waliwahudumia, kisha wakawekwa chini ya ulinzi wa polisi.

Wiki iliyopita, wachimba madini 1,000 walitoka na kukamatwa.

Polisi na jeshi wapo eneo la tukio wakisubiri kuwashikilia wale wasiohitaji huduma ya matibabu baada ya kutoka.

Wachimba madini wengi hutumia miezi mingi chini ya ardhi katika mazingira yasiyo salama ili kutunza familia zao.

"Kwa wengi wao ndiyo njia pekee wanayoijua ya kupata chakula mezani," anasema Bi Thabane.

Wakazi wa eneo hilo pia wamejaribu kuwashawishi wachimba madini kutoka nje ya shimo hilo.

"Ni lazima watoke nje kwa sababu tuna kaka huko, tuna wana huko, baba wa watoto wetu wako, watoto wetu wanataabika," mkazi wa eneo hilo Emily Photsoa aliiambia AFP.

Tume ya Haki za Kibinadamu ya Afrika Kusini inasema itawachunguza polisi kwa kuwanyima wachimba madini hao chakula na maji.

Inasema kuna wasiwasi kwamba operesheni ya serikali inaweza kuwa na athari kwa haki ya kuishi.

Matamshi ya Waziri Ntshavheni yameibua hisia tofauti kutoka kwa raia wa Afrika Kusini, huku baadhi wakipongeza msimamo wa serikali.

Huku wengine wakihisi msimamo huo sio wa kibinadamu.

"Kwa maoni yangu, aina hii ya maneno kutoka kwa Waziri katika Ofisi ya Rais ni ya fedheha na chuki ya hatari," mtumiaji mmoja wa X aliandika.

Mwingine aliandika: "Hao ni wahalifu lakini wana haki pia."

Uchimbaji madini haramu ni biashara yenye faida kubwa katika miji mingi yenye migodi Afrika Kusini.

Tangu mwezi Desemba mwaka jana, karibu bunduki 400, maelfu ya risasi, almasi ambazo hazijakatwa na pesa vimeshikiliwa kutoka kwa wachimbaji haramu.

Hii ni sehemu ya operesheni kali ya polisi na jeshi kukomesha tabia hiyo ambayo ina athari kubwa kwa mazingira.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi