Wachimba mgodi 955 waliokwama Afrika Kusini waokolewa

A rescued South African miner gestures out a bus window, 2 February 2018

Chanzo cha picha, AFP / Getty Images

Maelezo ya picha, Mchimba mgodi aliyeokolewa akiondolewa eneo hilo kwa basi

Wachimba mgodi wote 955 waliokuwa wamekwama katika mgodi mmoja wa dhahabu ulioko mkoa wa Free State nchini Afrika Kusini wameokolewa wakiwa salama.

Walikuwa wamekwama ndani ya mgodi huo baada ya umeme kukatika Jumatano usiku.

"Kila mtu ametolewa," James Wellsted, msemaji wa kampuni inayosimamia shughuli kwenye mgodi huo ya Sibanye-Stillwater amesema.

Ameeleza kuwa kuna visa kadha vya "watu kupungukiwa na maji mwilini na shinikizo la damu, lakini hakuna aliye na tatizo kubwa."

Mgodi huo wa dhahabu wa Beatrix unapatikana kilomita 300 Kusini Magharibi mwa Johannesburg na una ngazi 23 ambapo hufika hadi mita 1,000 chini ya ardhi.

Chanzo cha wachimba migodi hao kukwama ilitokana na mvua kubwa iliyonyesha nyakati za usiku wakati wachimba migodi hao walipokua chini ya mgodi huo na kuangusha nguzo ya umme iliyosababisha umeme kukatika

Afrika Kusini inaongoza kwa uchimbaji wa madini lakini usalama katika migodi umekuwa wa kutiliwa shaka.

Lakini Ijumaa subuhi, umeme ulirejeshwa na kuwezesha wafanyakazi hao kuokolewa.

"Ilikuwa hali ya kutisha, hakukuwa na hewa ya kutosha," mmoja wa wachimbaji mgodi hao Mike Khonto amesema.

"Twashukuru wasimamizi kwamba waliweza kututumia chakula na maji."

Wafanyakazi hao wamepelekwa kula chakula na kuoga kabla ya kufanyiwa uchunguzi wa kiafya na kisha kuruhusiwa kuondoka.

Photograph taken in the dark shows the mineshaft of the mine where men are trapped

Chanzo cha picha, AFP/getty

Maelezo ya picha, Umeme umerejeshwa eneo hilo

Jamaa za wachimba mgodi hao walikuwa wamekusanyika barabara ya kuelekea kwenye mgodi huo lakini wakadhibitiwa na vikosi vya usalama.

Maafisa wa vyama vya wachimba mgodi awali walikuwa wamelalamika kwamba maisha ya wafanyakazi hao yalikuwa hatarini.

Watu zaidi ya 80 walifariki kwenye migodi Afrika Kusini mwaka 2017.

Map of South Africa with Welkom, where mine is, and Johannesburg marked