Kutoka Noriega hadi Maduro fahamu viongozi waliowahi kukamatwa au kuangushwa na Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Historia ya kisiasa ya Marekani imejaa visa vingi vya kuvamia nchi za kigeni ili kukamata viongozi. Operesheni hizi mara nyingi zimeibua mjadala mkubwa kimataifa, huku baadhi ya mataifa zikionyesha hasira na hofu, na wengine kushangaa jinsi hatua hizo zinavyotekelezwa.
Kwa Marekani, hatua za kukamata viongozi wa kigeni mara nyingi zimechukuliwa kama njia ya kulinda usalama wake, kukomesha uhalifu au kudhibiti vurugu. Hata hivyo, operesheni hizi pia zimekasirishwa na mashirika ya kimataifa na baadhi ya wadau, wakihoji kuhusu uhuru wa taifa na msingi wa kisheria wa hatua hizo.
Kukamatwa kwa viongozi mara nyingi hufuata shinikizo la kisiasa au mashtaka ya kisheria, ikiwemo ufisadi, ukiukaji wa haki za binadamu au uhalifu wa kivita. Historia inaonyesha kuwa Marekani imekuwa ikitumia njia mbalimbali, kuanzia operesheni za kijeshi, mashambulizi ya anga, hadi hatua za kisheria, kuhakikisha viongozi hawa wanakabiliwa na matokeo.
Tukio la sasa la kukamatwa kwa Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, linadhihirisha mtindo huu. Operesheni ya Marekani ililenga biashara haramu na kudhibiti rasilimali za taifa hilo na kuondoa kiongozi anayeshutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu.
Tukio hili linaonyesha kuwa historia ya kukamata viongozi wa kigeni inazidi kuendelea. Ilihusika moja kwa moja kwa tukio la Panama, lakini kwa viongozi na mataifa mengine, ushawishi wa taifa hilo ulionekana dhahiri.
Manuel Noriega – Panama

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 1989, Marekani ilivamia Panama na kumkamata kiongozi wake, Manuel Noriega, akishutumiwa kwa biashara ya dawa za kulevya na ufisadi.
Operesheni hiyo ya kijeshi, inayoitwa "Operation Just Cause", ilihusisha majeshi ya Marekani kuingia Panama City, na baadaye kumpeleka Noriega Marekani kwa mashtaka ya jinai.
Tukio hili linachukuliwa kama mfano wa kwanza wa moja kwa moja wa Marekani kukamata kiongozi wa nchi jirani.
Slobodan Milošević – Serbia
Slobodan Milošević, rais wa zamani wa Serbia na Shirikisho la Yugoslavia, alikamatwa mwaka 2001 na mamlaka ya Serbia na kupelekwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Vita (ICTY) The Hague.
Marekani haikuwa nyuma katika harakati za kutiwa kwakwe nguvuni, haikumtia nguvuni yenyewe bali ilishirikiana na vyombo vya kimataifa kuhakikisha Milošević anakabiliana na mashtaka ya uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika mizozo ya Balkan.
Saddam Hussein - Iraq

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Saddam Hussein alikuwa Rais wa Iraq kuanzia mwaka 1979 hadi kuangushwa kwake mnamo 2003. Alijulikana kwa utawala wake wa kiimla, ukandamizaji wa wapinzani, na vita vya kikanda, ikiwa ni pamoja na vita vya Iran-Iraq na uvamizi wa Kuwait. Hussein aliongoza nchi yake kwa mkono wa chuma, akitumia mashambulizi makali dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa na makundi ya kabila.
Mnamo Machi 2003, Marekani iliongoza uvamizi wa Iraq, ikiunganisha majeshi ya Anglo-Amerika, baada ya kudai Hussein alikuwa akihifadhi silaha za maangamizi ya wingi. Ingawa hakukamatwa moja kwa moja ndani ya Iraq, operesheni ya kijeshi iliingilia moja kwa moja mamlaka yake. Baada ya miezi michache ya mapambano, Saddam alikamatwa mnamo Desemba 13, 2003, na majeshi ya Marekani na walinzi wa Iraq walioshirikiana.
Kamatwa kwake kulikamilisha hatua ya Marekani kuondoa utawala wake, na kumfikisha Saddam kwneye mikono ya sheria. Baada ya kesi iliyokuwa chini ya mahakama ya Iraq, alihukumiwa kifo mnamo Novemba 2006 kwa uhalifu dhidi ya binadamu, hususan kuhusiana na mauaji ya wapinzani wa kisiasa wa Ki-Kurdi na Ki-Shiia.
Saddam Hussein ni mfano wa kiongozi aliyeangushwa na ushawishi na operesheni za Marekani, tofauti na wale waliokamatwa moja kwa moja ndani ya nchi zao. Kisa chake kinaonyesha jinsi Marekani ilivyoweza kuingilia ndani ya taifa la kigeni kuathiri utawala na kuamua hatma ya viongozi wa kikanda.
Muammar Gaddafi – Libya

Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa Rais huyo wa Libya, Gaddafi hakukamatwa moja kwa moja na Marekani, mashambulizi ya anga yalioungwa mkono na Washington mwaka 2011 yalichochea kuangushwa kwake na hatimaye kukamatwa na kuuawa.
Tukio hili linaonyesha ushirikiano wa Marekani na wadau wengine wa kimataifa ili kuondoa viongozi wanaoshutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu.
Omar al-Bashir – Sudan
Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, aliyehukumiwa na Mahakama ya Kimataifa kwa uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari, alikamatwa mwaka 2019. Hata hivyo, Marekani ilichukua jukumu la kisiasa na kisheria, ikilazimisha hatua za kimataifa kumfanya alikabiliwe na mashtaka, ikionyesha ushawishi wa Washington bila kufanya uvamizi wa moja kwa moja.
Ilionyesha tu uhsawishi wake, lakini haikuhusika kumkamata moja kwa moja.
Nicolás Maduro – Venezuela

Chanzo cha picha, Getty Images
Tukio la hivi sasa la kukamatwa kwa Nicolás Maduro na mkewe kwa mashambulizi ya kijeshi ya Marekani linaongeza sura mpya katika historia hii. Marekani inadai kumkamata Maduro na mkewe kupitia operesheni ya kiwango kikubwa, ikilenga kudhibiti biashara haramu ya dawa za kulivya na rasilimali za mafuta na kuondoa viongozi wanaoshutumiwa kwa ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu.
Tukio hili linaonyesha jinsi Marekani inavyoweza kutumia nguvu za kijeshi na mbinu za kisiasa kukamata viongozi wa kigeni.
Historia ya Marekani inaonyesha kuwa kukamata viongozi wa kigeni ni sehemu ya mtindo wake wa kisiasa na kijeshi unaoendelea, jambo linaloibua mjadala juu ya uhuru wa taifa, ushawishi wa kigeni na nafasi ya Washington katika masuala ya dunia.












