Trump anataka mafuta ya Venezuela, Je, mpango wake utafanikiwa?

.

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images

Maelezo ya picha, Venezuela ina akiba kubwa zaidi ya mafuta ulimwenguni, ingawa uzalishaji wa nchi hiyo ni mdogo kwa sababu ya vikwazo (picha ya faili)
Muda wa kusoma: Dakika 5

Donald Trump ameapa kuingia katika hifadhi ya mafuta ya Venezuela baada ya kumkamata Rais Nicolás Maduro na kusema Marekani "itaendesha" nchi hiyo hadi kipindi "salama" cha mpito.

Rais wa Marekani anataka makampuni ya mafuta ya Marekani kukusanya mabilioni ya dola katika nchi hiyo ya Amerika Kusini, ambayo ina akiba kubwa zaidi ya mafuta ghafi duniani, ili kukusanya rasilimali ambayo haijatumiwa kwa kiasi kikubwa.

Alisema makampuni ya Marekani yatarekebisha miundombinu ya mafuta "iliyoharibika vibaya" ya Venezuela na "kuanza kutengeneza pesa kwa ajili ya nchi hiyo".

Lakini wataalam walionya juu ya changamoto kubwa na mpango huo wa Trump, wakisema kuwa ungegharimu mabilioni na kuchukua hadi muongo mmoja kuimarisha pato la mafuta.

Je, kweli Marekani inaweza kuchukua udhibiti wa akiba ya mafuta ya Venezuela? Na je mpango wa Trump utafanikiwa?

Ikiwa na wastani wa mapipa bilioni 303, Venezuela ina hifadhi kubwa zaidi ya mafuta iliyothibitishwa duniani.

Lakini kiasi cha mafuta ambacho nchi hiyo hutoa ni kidogo mno ikilinganishwa na hifadhi hiyo..

Pato lake limeshuka sana tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, kwani Rais wa zamani Hugo Chavez na kisha utawala wa Maduro waliimarisha udhibiti wa kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali, PDVSA, na kusababisha kuondoka kwa wafanyikazi wenye uzoefu zaidi.

Ingawa baadhi ya makampuni ya mafuta ya nchi za Magharibi, ikiwa ni pamoja na kampuni ya Marekani ya Chevron, zinafanya kazi nchini humo, shughuli zao zimepungua kwa kiasi kikubwa kwani Marekani imeongeza vikwazo na kulenga mauzo ya nje ya mafuta, ikumzuia Maduro kufikia njia kuu ya kiuchumi.

Pia unaweza kusoma
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Vikwazo - ambavyo Marekani iliweka kwa mara ya kwanza mwaka 2015 wakati wa utawala wa Rais Barack Obama kutokana na madai ya ukiukaji wa haki za binadamu - umeliwacha taifa hilo kushindwa kujiimarisha kutokana na kukatwa kwa uwekezaji na sehemu inazohitaji.

"Changamoto ya kweli waliyo nayo ni miundombinu yao," Callum Macpherson, mkuu wa bidhaa katika Investec alisema.

Bill Farren Price, mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Oxford ya Mafunzo ya Nishati, aliiambia BBC kwamba sekta ya mafuta ya Venezuela "ilikuwa na mafanikio ya miongo kadhaa iliyopita" na imekuwa ikidorora katika miaka 20 iliyopita.

"Njia nyingi za ugavi na miundombinu zimeporwa kugawanywa na kuuzwa," aliongeza.

Mnamo Novemba, Venezuela ilizalisha wastani wa mapipa 860,000 kwa siku, kulingana na ripoti ya hivi punde ya soko la mafuta kutoka Shirika la Nishati la Kimataifa.

Hiyo ni karibu theluthi moja ya ilivyokuwa miaka 10 iliyopita na chini ya 1% ya matumizi ya mafuta duniani.

Akiba ya mafuta nchini humo inashirikisha mafuta "mazito, machungu". Ni ngumu zaidi kusafisha, lakini ni muhimu kwa kutengeneza dizeli na lami. Kwa kawaida Marekani huzalisha mafuta "myepesi, matamu" yanayotumika kutengenezea petroli.

Katika kuelekea mashambulizi na kukamatwa kwa Maduro, Marekani pia ilikamata meli mbili za mafuta katika pwani ya Venezuela, pamoja na kuamuru kuzuiwa kwa meli zilizoidhinishwa kuingia na kutoka nchini humo.

Homayoun Falakshahi, mchambuzi mkuu wa bidhaa katika jukwaa la data la Kpler, anasema vikwazo muhimu kwa makampuni ya mafuta yanayotarajia kunyonya hifadhi za Venezuela ni za kisheria na kisiasa.

Akizungumza na BBC, alisema wanaotarajiwa kuchimba visima nchini Venezuela watahitaji makubaliano na serikali, jambo ambalo halitawezekana hadi mrithi wa Maduro atakapokuwapo.

Kampuni zitaachwa zikichezea kamari mabilioni ya uwekezaji katika uthabiti wa serikali ya baadaye ya Venezuela, Bw Falakshahi aliongeza.

"Hata ikiwa hali ya kisiasa ni shwari, ni mchakato unaochukua miezi," alisema. Kampuni zinazotarajiwa kuchukua fursa ya mpango huo wa Trump zitahitaji kutia saini kandarasi na serikali mpya itakapokuwa tayari, kabla ya kuanza mchakato wa kuongeza uwekezaji katika miundombinu nchini Venezuela.

Wachambuzi pia wameonya kuwa itachukua makumi ya mabilioni ya dola - na uwezekano wa miaka kumi - kurejesha pato la zamani la Venezuela.

Neil Shearing, mchumi mkuu wa kikundi cha Capital Economics, alisema mipango ya Trump itakuwa na athari ndogo kwa usambazaji wa kimataifa, na kwa bei, ya mafuta.

Anasema kuna "idadi kubwa ya vikwazo kukabiliana navyo huku muda wa kile kitakachofanyika ukiwa mrefu sana" na kwamba bei ya mafuta mwaka 2026 inaweza kuwa na mabadiliko madogo.

Bw Shearing anasema makampuni hayatawekeza hadi serikali imara itakapowekwa nchini Venezuela, na miradi hiyo haitatekelezwa kwa "miaka mingi".

"Suala daima limekuwa miongo kadhaa ya uwekezaji duni, usimamizi mbaya huku ikiwa ni ghali kuchimba mafuta," alisema.

Aliongeza kuwa hata iwapo nchi inaweza kurejea viwango vya awali vya uzalishaji wa takriban mapipa milioni tatu kwa siku, bado itakuwa nje ya wazalishaji 10 bora duniani.

Naye Bw Shearing ametaja uzalishaji mkubwa miongoni mwa nchi za Opec+, akisema dunia kwa sasa "haikumbwi na uhaba wa mafuta".

Mkurugenzi mkuu wa zamani wa BP, Lord Browne, ameiambia BBC kwamba kufufua sekta ya mafuta ya Venezuela ni "mradi wa muda mrefu sana".

"Watu hudharau muda unaochukuliwa kufanya mambo. Kuweka rasilimali zote, nyenzo na watu pamoja, huchukua muda mrefu sana."

Ingawa kunaweza kuwa na "kuimarika kwa haraka" kwa uzalishaji fulani, aliongeza, kwamba matokeo yanaweza kuanguka wakati tasnia inajipanga upya.

.

Chevron ndiye mzalishaji pekee wa mafuta wa Marekani ambaye bado anafanya kazi nchini Venezuela, baada ya kupokea leseni chini ya Rais wa zamani Joe Biden mnamo 2022 kufanya kazi, licha ya vikwazo vya Marekani.

Kampuni hiyo, ambayo kwa sasa inahusika na takriban humusi ya uchimbaji wa mafuta ya Venezuela, ilisema inazingatia usalama wa wafanyikazi wake na inafuata "sheria na kanuni zote zinazofaa".

Mashirika mengine makubwa ya mafuta yamekuwa kimya juu ya mipango hiyo hadi sasa, huku Chevron pekee ikiangazia suala hilo .

Lakini Bw Falakshahi anasema wakuu wa mafuta watafanya mazungumzo ya ndani kuhusu iwapo watafaidika na fursa hiyo.

Aliongeza: "Hamu ya kwenda mahali fulani inahusishwa na mambo mawili makuu, hali ya kisiasa na rasilimali zilizopo."

Kampuni za mafuta zinaweza kusita kurejea Venezuela kutokana na uzoefu wao wa hapo awali. ExxonMobil na ConocoPhilips bado wanatafuta mabilioni ya fidia kutoka Venezuela baada ya mali zao kunyakuliwa katika miaka ya 2000.

Hata hivyo, licha ya hali ya kutokuwa na uhakika wa kisiasa, Bw Falakshahi anasema "gharama yake inaweza kuonekana kuwa kubwa sana kuepukwa".

Lord Browne anasema makampuni yangetaka kujihusisha kwa sababu "kuwa na chaguzi za biashara katika sehemu mbalimbali za dunia ni jambo zuri".

"Kama kipande cha biashara, ikiwa ulikuwa unaendesha kampuni ... ungependa kujihusisha haraka sana".