Je, usingizi unaweza kuhifadhiwa kwa matumizi ya baadaye?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Katie Wright
- Nafasi, BBC Future
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Wikendi huwapa watu wengi fursa adimu ya kuzima alamu, kujinyoosha kitandani, na kulala kwa saa chache za ziada. Wenye bahati ya kufanya hivyo hujaribu kufidia usingizi walioukosa siku za kazi.
Lakini vipi kama mfumo ungeweza kufanya kazi kinyume chake? Je, kulala vya kutosha mapema na hivyo "kuhifadhi" usingizi kunaweza kumsaidia mtu kustahimili vipindi vya kukosa usingizi baadaye?
Kwa mujibu wa baadhi ya watafiti, kuhifadhi usingizi kabla ya vipindi vigumu vya kukosa usingizi huenda ikawa mbinu yenye ufanisi.
Ubongo wa binadamu una uwezo wa kukusanya rasilimali fulani muhimu kwa matumizi ya baadaye, jambo linaloweza kusaidia kudumisha uwezo wa juu wa kiakili wakati wa upungufu wa usingizi.
Lakini wazo hili lina ufanisi kwa kiwango gani, hasa ikizingatiwa kuwa limepata umaarufu mkubwa katika akaunti za afya kwenye mtandao wa TikTok?
Asili ya dhana ya "akiba ya usingizi"
Kama ilivyo kuweka fedha benki kwa matumizi ya baadaye, dhana ya kuhifadhi usingizi ilianza kuchunguzwa na watafiti wa usingizi nchini Marekani mwaka 2009.
Utafiti huo uliongozwa na Tracy Rupp, aliyekuwa mtafiti wa kijeshi na sasa profesa katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Utah. Timu yake iliwagawanya askari 24 katika makundi mawili: kundi moja lililala saa saba kwa siku kwa wiki moja, huku kundi jingine likilala saa kumi kwa siku.
Wiki iliyofuata, askari wote waliruhusiwa kulala saa tatu tu kwa siku. Wiki ya tatu, walibadilishiwa ratiba na kuruhusiwa kulala saa nane kwa siku.
Matokeo yalishangaza: wale waliopata "akiba" ya saa tatu za ziada za usingizi katika wiki ya kwanza walionyesha umakini na utendaji bora zaidi katika wiki ya pili. Aidha, walirejea katika viwango vyao vya kawaida vya kikazi haraka zaidi katika wiki ya tatu.
Tafiti zilizofuata zimeendelea kufafanua athari za kimwili na kiakili za kuhifadhi usingizi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Utafiti mmoja uliofanyika katika hospitali moja nchini Marekani mwaka 2023 ulibaini kuwa watu waliolala kwa dakika 90 za ziada kwa siku, kwa siku tatu kabla ya kuanza zamu za usiku za wiki mbili, walifanya kazi vizuri zaidi wakati wa zamu hizo.
Matokeo yanayofanana yameonekana pia katika michezo.
Wanariadha wa mashindano ya baharini hutumia mbinu hii mara kwa mara. Imeonekana kupunguza makosa na kuchelewa kwa majibu kunakosababishwa na kukosa usingizi.
Utafiti mmoja uligundua kuwa wachezaji wa raga wa kulipwa walipunguza msongo wa mwili kwa kulala saa kumi kwa usiku kwa wiki tatu.
Utafiti mwingine ulionyesha wachezaji wa tenisi kuboresha usahihi wa mipira yao ya kuanzisha mchezo au ukipenda "serve" walipoongeza usingizi hadi saa tisa kwa usiku.
Kwa wachezaji wa mpira wa kikapu, kuongeza muda wa usingizi kwa kipindi cha wiki tano hadi saba kulihusishwa na maboresho katika usahihi wa kurusha mpira na kasi ya mbio fupi.
Akiba ya benki au kadi ya mkopo?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hata hivyo, si wanasayansi wote wanaokubaliana na wazo hili.
Baadhi wanaamini kuwa haiwezekani kuhifadhi usingizi kwa matumizi ya baadaye.
Kwa mtazamo wao, miili yetu haiwezi kutofautisha kati ya kuhifadhi usingizi na kulipa deni la usingizi tulilokusanya awali.
Tathmini ya tafiti kadhaa yalionyesha kuwa maboresho ya utendaji hayakuwa yanahusiana moja kwa moja na dhana ya kuhifadhi usingizi.
Kwa nini mwili unahitaji usingizi?
Swali la msingi katika mjadala huu ni: kwa nini usingizi ni muhimu?
"Kuna nadharia nyingi kuhusu kwa nini tunalala," anasema Peter Polos, mtafiti wa usingizi katika Chuo cha Tiba cha Hackensack Meridian. Anaongeza:
"Wakati wa usingizi, michakato mingi ya kimetaboliki, homoni, neva, na kiakili hutokea. Ubongo pia huimarisha kumbukumbu na kuweka kipaumbele kwa taarifa muhimu."
Michael Howell, profesa wa neva katika Chuo Kikuu cha Minnesota, anaeleza kuwa usingizi ni hitaji la kifizikia kwa trilioni za seli katika miili yetu.
"Kila seli inahitaji usingizi mzuri ili ijirekebishe na kupata 'nishati'," anasema.
"Taka mbalimbali hukusanyika mwilini na ubongoni mchana kutwa. Ubongo huzisafisha tunapolala."
Madhara ya kukosa usingizi
Watu wazima wengi hufanya kazi kwa ufanisi zaidi wanapolala kati ya saa saba na tisa kwa usiku. Howell anasisitiza kuwa watu wanaoweza kuishi kwa saa nne au tano za usingizi ni nadra sana.
Athari za kukosa usingizi kwa muda mrefu zinaweza kuwa mbaya.
"Wengi wetu tunaweza kuvumilia kupungukiwa usingizi kwa saa moja au mbili bila madhara makubwa," anasema Polos.
"Tatizo huanza pale hali hii inapokuwa ya kudumu."
Athari hizo hujikusanya taratibu na kuathiri utendaji kazini, mahusiano ya kijamii, motisha, na kasi ya kufikiri.
Bila mapumziko ya kutosha, ubongo hushindwa kuchakata taka ipasavyo, na hivyo kufanya iwe vigumu kujifunza au kuzingatia mambo muhimu.
"Ikiwa unajifunza lugha mpya, chombo cha muziki, au mbinu mpya ya michezo, itakuwa vigumu sana," anasema Howell.
"Utapata shida kujifunza taarifa mpya na kuzihifadhi kwenye kumbukumbu ya muda mrefu."
Kwa nini kuhifadhi usingizi kunaweza kusaidia
Rupp na timu yake wanaamini kuwa kuhifadhi usingizi huupa ubongo muda wa ziada wa kusafisha taka za neva na kujaza akiba ya glycogen chanzo muhimu cha nishati kwa ubongo wakati sukari ya damu inaposhuka. Hili, wanasema, huupa mwili faida wakati wa vipindi vya kukosa usingizi.
Kulala zaidi: jioni au asubuhi?
Watafiti wanasema mbinu hii hufanya kazi, na yeyote anayejiongezea usingizi kabla ya safari ndefu, mitihani, au vipindi vya masomo mazito ataona tofauti.
Howell anashauri ''kuongeza usingizi kwa dakika 30 hadi 60 kwa siku, kwa wiki moja au mbili kabla ya kipindi cha kukosa usingizi''.
Anasema watu wengi hupata urahisi wa kuamka kuchelewa kuliko kulala mapema, ingawa si kwa kila mtu.
Polos anaongeza kuwa kwa wengine, kulala mapema kunaweza kuwa na manufaa zaidi.
"Ikiwa mwili wako umezoea kuamka saa 6 asubuhi, unaweza kuamka mwenyewe saa 6 asubuhi hata ikiwa utaweka kengele saa 7 asubuhi."
Howell pia anaeleza kuwa ''usingizi wa mchana ni njia yenye ufanisi mkubwa ya kusaidia mahitaji ya usingizi ilimradi hauharibu usingizi wa usiku''.

Chanzo cha picha, Getty Images
Vipi kama tayari una 'deni kubwa la usingizi'?
Kuna mvutano wa maoni kuhusu kama kuhifadhi usingizi kunaweza kusaidia pale mtu tayari ana deni kubwa la usingizi.
Rupp anaamini inawezekana, lakini anasisitiza kuwa deni hilo linapaswa kulipwa haraka iwezekanavyo.
Elizabeth Klerman, profesa wa neva katika Shule ya Tiba ya Harvard, anakataa hoja hiyo.
"Ili kuthibitisha kuwa usingizi unahifadhiwa, lazima mtu aweze kulala hata bila kuwa na usingizi na hakuna ushahidi wa hilo," anasema.
Katika hatua hii, anataja majaribio ambapo washiriki waliopewa muda zaidi kitandani hawakuweza kulala kwa muda mrefu zaidi.
Kwa mtazamo wake, usingizi ni kama kadi ya mkopo, si kama akiba ya benki: unaweza kukusanya deni, lakini huwezi kukusanya ziada.
Anaonya kuwa kuamini kupita kiasi dhana ya kuhifadhi usingizi kunaweza kuwafanya watu wapuuze umuhimu wa usingizi wa mara kwa mara.
"Hii inamaanisha wanajinyima kitu muhimu kwa afya zao," anasema.
Hata hivyo, watafiti wengi wanakubaliana kwamba kufidia usingizi uliokosekana kuna faida ingawa usingizi wa mchana unaozidi dakika 45 unaweza kusababisha sleep inertia, hali ya kutoamka vizuri, au wasiwasi unaohisi unapoamka baada ya usingizi mzito.
Iwe tunatayarisha usingizi kwa ajili ya siku zijazo au 'tunalipa deni', kupata usingizi wa nusu saa kila usiku kunaonekana kuwa na manufaa.
Lakini kama Howell asemavyo, ikiwa hauitaji kulala zaidi ya saa 12 kila usiku, tabia hii inaweza kuashiria tatizo la msingi.
Polos anasema kwamba wakati mkusanyiko wa usingizi unaweza kuwa mzuri, haupaswi kuonekana kama suluhisho la muda mrefu.
"Usione hili kama jibu kwa matatizo yako yote ya usingizi, au kwa madai yote ambayo kazi yako au jamii inaweka juu yako," anasema.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












