Waandamanaji wakaidi ukandamizaji huku Iran ikionya kuwa italipiza kisasi iwapo Marekani itashambulia

Waandamanaji nchini Iran walikaidi msako mkali wa serikali Jumamosi usiku, wakiingia mitaani licha ya ripoti kusema mamia ya watu wameuawa au kujeruhiwa na vikosi vya usalama katika siku tatu zilizopita.

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu

  1. Trump aiambia Cuba 'ifanye makubaliano, kabla haijachelewa'

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Donald Trump ameitaka Cuba "kufanya makubaliano" au ikabiliane na matokeo, akionya kwamba mtiririko wa mafuta na pesa za Venezuela sasa utasitishwa.

    Rais wa Marekani amekuwa akielekeza mawazo yake kwa Cuba tangu majeshi ya Marekani yalipomkamata kiongozi wa Venezuela Nicolás Maduro katika shambulio la Januari 3 katika mji mkuu wake.

    Venezuela, mshirika wa muda mrefu wa Cuba, inaaminika kutuma takriban mapipa 35,000 ya mafuta kwa siku katika kisiwa hicho, lakini Trump amesema hilo litaisha.

    "Cuba iliishi, kwa miaka mingi, kwa kiasi kikubwa cha MAFUTA na FEDHA kutoka Venezuela.

    Kwa upande wake, Cuba ilitoa 'Huduma za Usalama' kwa madikteta wawili wa mwisho wa Venezuela, LAKINI HILO HALITAFANYIKA TENA!" alichapisha kwenye Truth Social on Sunday.

    "HAKUTAKUWA NA MAFUTA WALA PESA KWENDA CUBA - SIFURI! Ninashauri sana wafanye mkubaliano, KABLA HAIJACHELEWA." Trump hakutaja masharti ya makubaliano au matokeo ambayo Cuba inaweza kukabiliana nayo.

  2. Israel yautaka Umoja wa Ulaya kuorodhesha Walinzi wa Mapinduzi nchini Iran kama "shirika la kigaidi"

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel alitoa wito kwa Umoja wa Ulaya kulitambua Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi nchini Iran IGRC kama "shirika la kigaidi." Gideon Saar aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X:

    "Nilijadili hili na Alexander Dobrindt, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, ambaye alikuwa amesafiri kwenda Israel, kwamba sasa ni wakati wa Walinzi wa Mapinduzi kutambuliwa kama shirika la kigaidi katika Umoja wa Ulaya."

    "Ujerumani imekuwa na msimamo huu kwa muda mrefu, na leo umuhimu wa suala hili uko wazi kwa kila mtu," alisema.

    Nchi kadhaa, zikiwemo Marekani na Canada, zimeorodhesha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi kama "shirika la kigaidi."

  3. Habari za hivi punde, Shirika la Haki za Kibinadamu la Iran: Takriban watu 192 wameuawa

    Shirika la Haki za Kibinadamu la Irani lenye makao yake makuu nchini Norway lilitangaza Jumapili kwamba watu wasiopungua 192 wameuawa katika wiki mbili za maandamano, ongezeko kubwa kutoka kwa idadi ya awali ya vifo 51.

    Shirika hilo lilisema "limethibitisha vifo vya waandamanaji wasiopungua 192," na kuonya kwamba idadi ya waandamanaji inaweza kuwa kubwa zaidi kwa sababu siku kadhaa za kukatika kwa mtandao kumezuia uthibitishaji na uthibitisho wa takwimu hizo.

    Shirika la Haki za Kibinadamu la Irani pia linasema, likinukuu makadirio kutoka kwa vyanzo vingine, kwamba idadi ya vifo inaweza kuwa mamia na labda zaidi ya 2,000.

    Shirika la Haki za Kibinadamu la Iran limeelezea wasiwasi wake kuhusu kushadidi na kuendelea mauaji ya waandamanaji na hatari ya kunyongwa kwa kiasi kikubwa wafungwa, na limetoa wito wa jibu la haraka kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

  4. Papa awaombea waathiriwa wa maandamano ya Iran

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Papa Leo

    Kiongozi wa Wakatoliki duniani, amewaombea waliouawa katika maandamano nchini Iran na mizozo nchini Syria katika sala yake ya kila wiki siku ya Jumapili, akitaka mazungumzo na amani.

    Kiongozi wa Wakatoliki duniani alisema huko Vatican: "Nia yangu inaangazia kile kinachotokea siku hizi katika Mashariki ya Kati, haswa Iran na Syria, ambapo mvutano unaoendelea unaua watu wengi."

    Alisema aliomba kwa matumaini kwamba mazungumzo na amani viweze kukua katika jamii kwa uvumilivu na busara kwa manufaa ya wote.

    Papa pia aliwaombea watu wa Ukraine, akisema: "Mashambulizi haya yanaathiri raia hata zaidi huku kukiwa na hali ya hewa inayozidi kuwa baridi."

    Kiongozi wa Wakatoliki duniani aliongeza: "Ninawaombea wale wanaoteseka na kwa mara nyingine tena kuunga mkono kukomeshwa kwa ghasia na ongezeko la juhudi za kufikia amani."

  5. Khamenei: Mungu akipenda, hivi karibuni ataeneza hisia za ushindi katika nyoyo za watu wote wa Iran

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Ali Khamenei

    Simulizi ya Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mtandao wa kijamii wa X, jioni ya Jumamosi, Januari 10, iliweka picha yake na kuandika: Mwenyezi Mungu akipenda, karibuni ataeneze hisia za ushindi katika nyoyo za watu wote wa Iran.

    Chapisho hilo liliibua hisia tofauti kwenye mitandao ya kijamii, huku wengine wakiandika kwa kejeli kwamba "Bwana Khamenei mwenyewe ametambua kuwa waandamanaji watashinda hivi karibuni."

    Wengine pia wameandika kwamba katika nyakati hizo hatari, hotuba ya Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ni kwa waungaji mkono na "waungaji mkono wa utawala" ili wasiwe na shaka yoyote juu ya mustakbali na uhai wa serikali.

    Wakati huo huo, wengine wamekisia kwamba kwa kukata kabisa mtandao, lengo la serikali ni "kukandamiza kwa nguvu waandamanaji," kama katika vipindi vilivyotangulia, na kauli hii kwenye Mtandao wa X ni "kukubali kwa Khamenei kuamuru mauaji."

  6. Maafisa wa Ulaya waunga mkono maandamano ya raia wa Iran

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maafisa wa Ulaya na Uingereza walitangaza kuunga mkono waandamanaji nchini Iran.

    Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, na Kansela wa Ujerumani Friedrich Mertz walitoa taarifa ya pamoja siku ya Ijumaa wakiwataka viongozi wa Iran kujizuia kujibu maandamano hayo.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Yvette Cooper aliwasifu waandamanaji wa Iran siku ya Jumamosi: "Kuzungumza katika mfumo wa kimabavu, hasa kwa wanawake vijana, kunahitaji ujasiri wa kweli.

    Kuomba kusikilizwa haipaswi kuwa hatari sana." "Hizi ni haki za kimsingi: uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani, na utekelezaji wa haki hizi kamwe usiambatane na vitisho vya vurugu au kulipiza kisasi," alisema.

    Kiongozi wa Chama cha Conservative cha Uingereza pia alisema "hatakuwa na tatizo" na mabadiliko ya utawala nchini Iran.

    "Utawala wa Iran ungefurahia kuiangamiza Uingereza ikiwa ingehisi inaweza kuepuka matokeo," Kamy Badenoch aliambia BBC.

    "Utawala huu umejaribu kuua watu katika ardhi yetu. Ni adui yetu na unatuita shetani mdogo."

    Alipoulizwa kuhusu ushiriki wa Marekani na washirika wake katika mabadiliko ya utawala nchini Iran, Bi Badenoch alisema: "Kutokana na tishio tunaloona kwa watu [wa Iran], nadhani ni jambo sahihi kufanya."

  7. Qalibaf: Iran ikishambuliwa, kambi za kijeshi za Israel na Marekani zitakuwa shabaha ya kwanza

    .

    Chanzo cha picha, Tasnim News Agency via Reuters

    Maelezo ya picha, Spika wa Iran Mohammad Baqer Qalibaf

    Kufuatia onyo la Donald Trump kuhusu ukandamizaji mkali dhidi ya waandamanaji, Spika wa bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf amesema katika kikao cha leo cha bunge:

    "Iwapo Marekani itaanzisha mashambulizi ya kijeshi, maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu na vituo vya kijeshi na meli za Marekani zitakuwa shabaha halali kwetu."

    Spika wa Bunge alisema: "Ndani ya mfumo wa utetezi halali, hatujifikirii kuwa na kikomo cha kujibu baada ya hatua, na tutachukua hatua kwa kuzingatia dalili za vitisho, na tunamwambia Trump na washirika wake katika eneo hilo wasifanye makosa."

    Vile vile amesema: "Leo tunapigana na adui Mzayuni na Marekani katika nyanja nne: kiuchumi, kiakili, kijeshi na kigaidi."

    Siku ya Jumamosi, Bw.Trump alisema kwenye mitandao ya kijamii kwamba Iran inatafuta uhuru na kwamba Marekani iko tayari kusaidia.

    Vyombo vya habari vya Marekani pia vimeripoti kuwa Donald Trump amezingatia chaguzi mpya za kufanya mashambulizi ya kijeshi kujibu mauaji ya waandamanaji, lakini bado hajatoa uamuzi wa mwisho.

  8. New York Times: Trump apewa ushauri kuhusu chaguzi mpya za kijeshi dhidi ya Iran

    .

    Chanzo cha picha, Reuters/Getty Images

    Ripoti za vyombo vya habari vya Marekani zinaonyesha kuwa Rais Donald Trump amefahamishwa kuhusu chaguzi mpya za mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran ili kukabiliana na mauaji ya waandamanaji.

    Maafisa wameliambia gazeti la The New York Times kwamba anatafakari kwa dhati hatua hiyo, lakini bado hajafanya uamuzi wa mwisho.

    Siku ya Jumamosi, Bw.Trump alisema kwenye mitandao ya kijamii kwamba Iran inatafuta uhuru na kwamba Marekani iko tayari kusaidia.

    Juni mwaka jana, Marekani ilishambulia kwa mabomu maeneo ya nyuklia ya Iran wakati wa vita vya Israel na Jamhuri ya Kiislamu.

  9. Salah asisimua Misri wakiwashinda Ivory Coast

    .

    Mohamed Salah kwa mara nyingine tena alifunga bao wakati Misri wakiwafunga mabingwa Ivory Coast katika mchezo wa robo fainali uliojaa mbwembwe katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025.

    Baada ya Omar Marmoush kuwaweka mbele Mafarao baada ya dakika nne pekee, Waafrika hao wa Kaskazini hawakurudi nyuma katika mchezo huo.

    Lakini Tembo wa Emerse Fae wanajulikana kwa uimara wao na walikataa kuwaruhusu wapinzani wao kuendelea kungara licha ya bao la kichwa la Ramy Rabia kuwapa Misri uongozi wa 2-0 baada tu ya nusu saa.

    Bao la kujifunga la Ahmed Fatouh liliwapa Wana Ivory Coast matumaini kabla ya kipindi cha kwanza kwenda mapumziko, lakini Salah haraka alirejesha uimara wa mabao mawili kwa washindi hao mara saba.

    Matokeo hayo yanamaanisha kwamba ombi la Salah kuwania taji la kwanza la bara na nchi yake bado liko mbioni.

    Sasa ataipeleka timu yake Tangier kumenyana na Senegal, ambao waliifunga Misri katika fainali ya 2021, siku ya Jumatano

  10. Jeshi la Marekani lashambulia kundi la Islamic State nchini Syria - maafisa

    .

    Chanzo cha picha, US Central Command

    Marekani na vikosi washirika wamefanya mashambulizi makubwa dhidi ya kundi la Islamic State (IS) nchini Syria, kamandi kuu ya Marekani (Centcom) imetangaza.

    Rais wa Marekani Donald Trump aliamuru mashambulizi Jumamosi, ambayo ni sehemu ya Operesheni ya Hawkeye, kulipiza kisasi shambulio baya la IS dhidi ya vikosi vya Marekani huko Syria mnamo Disemba 13, Centcom iliandika kwenye X.

    Mashambulizi hayo yalifanywa katika juhudi za kupambana na ugaidi na kulinda vikosi vya Marekani na washirika katika eneo hilo, kulingana na Centcom.

    "Ujumbe wetu unabaki kuwa mkali: ikiwa utawadhuru wapiganaji wetu, tutakutafuta na kukuua popote duniani, bila kujali jinsi unavyojaribu kukwepa " Centcom alisema.

  11. Waandamanaji wa Iran wakaidi ukandamizaji huku video zikionyesha makabiliano makali

    .

    Chanzo cha picha, EPA - EFE

    Waandamanaji nchini Iran walikaidi msako mkali wa serikali Jumamosi usiku, wakiingia mitaani licha ya madaktari katika hospitali mbili kuiambia BBC kuwa miili zaidi ya 100 imeletwa kwa muda wa siku mbili.

    Video zilizothibitishwa na BBC na akaunti za mashahidi zilionekana kuonyesha serikali ilikuwa ikiimarisha usalama ili kukabiliana na waandamanaji.

    Mwanasheria mkuu wa Iran alisema yeyote atakayeandamana atachukuliwa kuwa "adui wa Mungu" - kosa ambalo lina adhabu ya kifo.

    Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuipiga Iran "vibaya sana" ikiwa "wataanza kuua watu".

    Spika wa bunge la Iran alionya kuwa iwapo Marekani itashambulia Iran, Israel na kambi zote za kijeshi za Marekani na meli katika eneo hilo zitakuwa shabaha halali.

  12. Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja