Marekani yafanya shambulizi Nigeria, dhidi ya nani na kwa nini?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Rais Donald Trump amesema Marekani imefanya "shambulio kali na hatari" dhidi ya kundi la Islamic State (IS) kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Kiongozi huyo wa Marekani amesema IS ni "magaidi wakubwa," na kulishutumu kundi hilo kwa "kuwalenga na kuwaua kikatili, Wakristo wasio na hatia."
Trump amesema jeshi la Marekani "limefanya mashambulizi hayo,” huku Kamandi ya Marekani ya Afrika (Africom) ikiripoti kwamba shambulio la Alhamisi lilifanywa kwa ushirikiano na Nigeria katika jimbo la Sokoto.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Yusuf Maitama Tuggar ameiambia BBC ni "operesheni ya pamoja" inayolenga "magaidi," na "haina uhusiano wowote na dini fulani."
Tuggar hakuondoa uwezekano wa kutokea mashambulizi mengi zaidi, akisema hilo litategemea "maamuzi yatakayochukuliwa na uongozi wa nchi hizo mbili."
Katika chapisho lake kwenye Truth Social Alhamisi jioni, Trump alisema "chini ya uongozi wangu, nchi yetu haitaruhusu ugaidi wa misimamo mikali wa Kiislamu kustawi."
Mwezi Novemba, Trump aliliamuru jeshi la Marekani kujiandaa kuchukua hatua nchini Nigeria kukabiliana na makundi ya wanamgambo wa Kiislamu.
Madai ya Trump
Madai ya mauaji ya halaiki dhidi ya Wakristo wa Nigeria yamekuwa yakisambaa katika miezi ya hivi karibuni katika baadhi ya majukwaa ya wafuasi wa mrengo wa kulia Marekani.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth alisema siku ya Alhamisi kwamba "nashukuru kwa msaada na ushirikiano wa serikali ya Nigeria."
"Krismasi Njema!" aliongeza kwenye X.
Makundi yanayofuatilia vurugu yanasema hakuna ushahidi unaoonyesha kwamba Wakristo wanauawa zaidi kuliko Waislamu nchini Nigeria, nchi ambayo imegawanyika sawa kati ya wafuasi wa dini hizo mbili.
Mshauri wa Rais wa Nigeria Bola Tinubu aliiambia BBC siku za nyuma kwamba hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya makundi ya jihadi inapaswa kufanywa kwa pamoja.
Daniel Bwala alisema Nigeria itakaribisha msaada wa Marekani katika kukabiliana na waasi wa Kiislamu lakini akabainisha kuwa Nigeria ni nchi "huru."
Pia alisema wanajihadi hawawalengi wafuasi wa dini fulani pekee na wamewaua watu wa dini zote.
Rais Tinubu amesisitiza kwamba kuna uvumilivu wa kidini Nigeria na kusema changamoto za usalama zinawaathiri watu "wa dini na maeneo yote."
Siku za nyuma Trump alitangaza kwamba Nigeria ni "nchi ya kutia Wasiwasi" kwa sababu ya "tishio" linalowakabili Wakristo. Alisema "maelfu" wameuawa, bila kutoa ushahidi wowote.
Nchi ya kutia Wasiwasi ni msemo unaotumiwa na Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ambao unaruhusu kuwekwa vikwazo nchi "zinazohusika katika ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa kidini."
Kufuatia tangazo hili, Tinubu alisema serikali yake imejitolea kufanya kazi na Marekani na jumuiya ya kimataifa kulinda imani zote.
Wengi ni Waislamu

Makundi ya Jihadi kama vile Boko Haram na Dola la Kiislamu Afrika Magharibi yamesababisha uharibifu kaskazini mashariki mwa Nigeria kwa zaidi ya muongo mmoja, na kuua maelfu ya watu.
Hata hivyo, wengi wa waliouawa ni Waislamu, kulingana na Acled, kundi linalofuatilia vurugu za kisiasa kote ulimwenguni.
Katikati mwa Nigeria, pia kuna mapigano ya mara kwa mara kati ya wafugaji wengi wao wakiwa Waislamu na vikundi vya wakulima, ambao mara nyingi ni Wakristo, kuhusu upatikanaji wa maji na malisho.
Mashambulizi ya mara kwa mara ya kulipiza kisasi pia yamesababisha maelfu ya watu kuuawa – na ukatili huo umefanywa na pande zote mbili.
Makundi ya kutetea haki za binadamu yanasema hakuna ushahidi kwamba Wakristo wamekuwa wakilengwa zaidi.
Wiki iliyopita, Marekani ilifanya "shambulio kubwa" dhidi ya IS nchini Syria.
Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) ilisema ndege za kivita, helikopta za mashambulizi na makombora "zilishambulia zaidi ya maeneo 70 katika maeneo kadhaa katikati ya Syria."
Ndege kutoka Jordan pia zilihusika.















