Nigeria yashuhudia utekaji nyara mbaya zaidi huku 315 wakithibitishwa kutekwa kutoka shuleni

Chama cha Kikristo cha Nigeria kilisema wanafunzi 303 na walimu 12 walichukuliwa kutoka Shule ya St Mary's huko Papiri, jimbo la Niger - zaidi ya ilivyokadiriwa hapo awali.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Washirika wa Ukraine kuzungumzia mpango wa amani wa Marekani kwenye mkutano wa G20

    .

    Chanzo cha picha, PA Media

    Washirika wa Ukraine watajitahidi "kuimarisha" mpango wa Marekani wa kumaliza vita na Urusi watakapokutana katika mkutano wa G20 nchini Afrika Kusini, Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer amesema.

    Mkutano huo unaanza siku moja baada ya Rais Volodymyr Zelensky kuonya Ukraine inakabiliwa na "moja ya nyakati ngumu zaidi katika historia yetu" juu ya shinikizo la kukubali mpango huo - maelezo yaliyofichuliwa ambayo yameonekana kupendelea Moscow.

    Zelensky alizungumza kwa njia ya simu na Sir Keir na viongozi wa Ufaransa na Ujerumani siku ya Ijumaa. Baadaye, Waziri Mkuu alisema "marafiki na washirika" wa Ukraine walisalia kujitolea kupata "amani ya kudumu milele".

    Si Rais wa Marekani Donald Trump au Rais wa Urusi Vladimir Putin wanaohudhuria mkutano wa G20.

    Soma zaidi:

  2. Nigeria yashuhudia utekaji nyara mbaya zaidi huku 315 wakichukuliwa kutoka shuleni

    .

    Zaidi ya watoto 300 na wafanyakazi sasa wanachukuliwa kutekwa nyara na watu wenye silaha kutoka shule ya Kikatoliki katikati mwa Nigeria, na kuifanya kuwa mojawapo ya matukio mabaya zaidi ya utekaji nyara nchini humo.

    Chama cha Kikristo cha Nigeria kilisema wanafunzi 303 na walimu 12 walichukuliwa kutoka Shule ya St Mary's huko Papiri, jimbo la Niger - zaidi ya ilivyokadiriwa hapo awali.

    Ilisema takwimu hizo zimerekebishwa "baada ya zoezi la uhakiki" kukamilika.

    Utekaji nyara huo unafayika huku kukiwa na ongezeko la mashambulizi ya makundi yenye silaha. Idadi ya watu waliotekwa nyara inazidi 276, ikiwa ni ile ya waliotekwa nyara katika shule ya Chibok wa 2014.

  3. Marjorie Greene, mbunge wa Republican kujiuzulu baada ya kutofautiana na Trump

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Maelezo ya picha, Greene na Trump kwenye kampeni za uchaguzi mnamo mwaka 2024

    Marjorie Taylor Greene ametangaza kujiuzulu kama mbunge jambo ambalo halikutarajiwa kutoka na kuwa mshirika wa ngazi ya juu wa chama cha Republican.

    Greene, mbunge aliyekuwa na ukuruba wa karibu na Donald Trump na mtetezi shupavu katika eneo bunge la Georgia amekuwa akitoa wito wa kutolewa kwa faili zinazohusiana na mnyanyasaji wa kingono marehemu Jeffrey Epstein na ukosoaji wa hivi karibuni wa baadhi ya sera zake kulisababisha hasira kali kwa umma.

    Baada ya rais wa Marekani kumwita "msaliti", alisema kwenye video akitangaza kuondoka kwake: "Ninakataa kuwa 'mke aliyepigwa' akitumai kwamba yote yatapita na kuwa vizuri."

    Katika video ya dakika 10 iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii, Greene alisema alichochewa kujiuzulu kutokana na kutarajia kukubaliana na mpinzani wakati wa mchujo wa chama cha Republican anayeungwa mkono na Trump na uwezekano wa kiti cha Ubunge eneo hilo kunyakuliwa na Democrats katika uchaguzi wa katikati ya muhula wa mwaka ujao.

    Pia alilalamika kwamba Bunge kwa kiasi kikubwa "limetengwa" tangu Trump arudi kwenye kiti cha urais mnamo Januari.

    Alisema katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, kwamba ataondoka kwenye Bunge la Marekani tarehe 5 Januari 2026.

    Akihojiwa na ABC News, Trump alisema kujiuzulu kwa Greene, ni "habari njema kwa nchi. Ni jambo zuri."

    Greene alilalamikia hali ya siasa za Marekani, akidai kuwa si Warepublican wala wabunge wa Democratic, hakuna mwenye nafasi ya kutatua matatizo ya taifa hilo, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa gharama ya maisha.

    Soma zaidi:

  4. Trump asitisha kinga iliyolinda Wasomali wasifukuzwe Minnesota

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Ijumaa amesema anakatisha mara moja ulinzi wa muda wa kufukuzwa kwa Wasomali wanaoishi Minnesota, na kuharakisha mwisho wa mpango ulioanza mwaka wa 1991 chini ya rais mwingine wa Republican.

    "Magenge ya Kisomali yanawatia hofu watu wa Jimbo hilo kuu, na MABILIONI ya Dola yanapotea," Trump alisema katika chapisho la usiku wa manane kwenye mtandao wa Truth Social, bila kutoa maelezo zaidi au

    "Mimi, kama Rais wa Marekani, ninakatisha mara moja, Hali ya Kulindwa kwa Muda (Mpango wa TPS) kwa Wasomali huko Minnesota," alisema.

    Trump aliita Minnesota "kitovu cha shughuli za utakatishaji fedha" chini ya Gavana wa Democratic Tim Walz, jibu kwa ripoti za vyombo vya habari ambazo hazijathibitishwa, zilizoshirikiwa na wabunge kadhaa wa Republican, zilisema kwamba kikundi cha wanamgambo wa Al-Shabaab nchini Somalia kilinufaika kutokana na ulaghai uliofanywa huko Minnesota.

    Walz alijibu kwenye ntandao wa X, "Sio jambo la kushangaza kwamba Rais amechagua kulenga jumuiya nzima. Hiki ndicho anachofanya kubadilisha mada."

    Mpango wa TPS kwa Wasomali ulizinduliwa na Rais wa wakati huo George HW Bush mnamo Septemba 1991. Unatoa ulinzi wa serikali kwa wazaliwa wa kigeni wanaostahiki ambao hawawezi kurejea nyumbani salama kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe au majanga ya asili.

    Soma zaidi:

  5. Ndege ya kivita ya India yaanguka wakati wa onyesho la anga Dubai

    .

    Chanzo cha picha, Dubai Media Office

    Ndege ya kivita ya India ilianguka ilipokuwa ikifanya maonyesho katika anga la Dubai na rubani mmoja akapoteza maisha, maafisa wamesema.

    Jeshi la Wanahewa la India lilisema katika taarifa: "IAF inajutia sana kupoteza maisha na inasimama pamoja na familia iliyofiwa katika wakati huu wa huzuni.

    "Mahakama ya uchunguzi inaundwa, ili kubaini chanzo cha ajali."

    Ndege ya Hindustan Aeronautics Ltds Tejas ilianguka takriban 14:10 saa za eneo (10:10 GMT), kulingana na Associated Press.

    Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Dubai na Wizara ya Ulinzi ya UAE zimesema wazima moto na huduma za dharura "walijibu haraka" tukio hilo.

    Picha za video za ajali hiyo zinaonyesha moshi mweusi ukipanda angani.

    Tovuti ya Dubai Airshow 2025 inasema hafla hiyo imevutia zaidi ya wahudhuriaji na waonyeshaji 148,000 kutoka kampuni 1,500.

    Ajali hiyo mbaya ilitokea siku ya mwisho ya onyesho la anga lililoanza Jumatatu, lililoandaliwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Al Maktoum.

  6. Japan inakaribia kuanzisha tena kinu kikubwa zaidi cha nishati ya nyuklia duniani

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Japan inakaribia kuidhinisha kuanzishwa upya kwa kinu kikubwa zaidi cha nishati ya nyuklia duniani – itakuwa mara ya kwanza kuendeshwa tangu janga la Fukushima la 2011.

    Hideyo Hanazumi, gavana wa eneo la Niigata ambako kituo cha kuzalisha umeme cha Kashiwazaki-Kariwa kinapatikana, alisema ametoa ruhusa ya kuanzishwa tena hatua kwa hatua.

    Mpango wa kuanza tena shughuli ya kuzalisha nishati ya nyuklia katika kituo hicho, kinachoendeshwa na kampuni ya kuzalisha umeme ya Tepco, bado unahitaji idhini kutoka kwa bunge la serikali ya wilaya hiyo na mdhibiti wa nyuklia wa Japan kabla ya kuanza.

    Iwapo utaidhinishwa, itakuwa mara ya kwanza kwa Tepco kuruhusiwa kuanza tena shughuli za kinu cha nyuklia nchini Japan tangu kiwanda chake cha Fukushima kilipoharibika.

    Kurejeshwa kwa shughuli katika kituo hicho ni sehemu ya mpango wa uimarishaji biashara wa Tepco kufuatia mlipuko wa nyuklia wa Fukushima uliochochewa na tetemeko kubwa la ardhi la ukubwa wa 9.0 na tsunami mnamo Machi 2011.

    Wakati vinu vya mtambo huo vilipolipuka kutokana na tsunami hiyo, ilisababisha mionzi kuvuja na kuwalazimu watu 150,000 kuhamishwa kutoka eneo hilo.

    Japan iliamuru vinu vyake vyote vya nyuklia kufungwa mnamo 2011 kufuatia maafa hayo. Tangu wakati huo, mitambo 14 imeruhusiwa kuanza kufanya kazi tena.

    Soma zaidi:

  7. Mjumbe wa bodi ya BBC ajiuzulu

    .

    Mjumbe wa bodi ya BBC amejiuzulu kwa kile anachosema ni "maswala ya utawala" katika ngazi ya juu ya shirika hilo.

    Shumeet Banerji pia alisema katika barua kwamba "hakushauriwa" kuhusu matukio yaliyosababisha kuondoka kwa mkurugenzi mkuu, Tim Davie, na mtendaji mkuu wa BBC News, Deborah Turness.

    Banerji alithibitisha kujiuzulu kwake siku ya Ijumaa, BBC ilisema katika taarifa yake.

    BBC News imemtafuta Banerji kwa maoni yake.

    Watendaji wakuu wawili wa BBC walijiuzulu mapema mwezi wa Novemba kutokana na mzozo kuhusu kipindi cha Panorama ambacho kilihariri sehemu za hotuba ya 2021 ya Rais wa Marekani Donald Trump.

    Tangu wakati huo, wasiwasi umeibuka kuhusu jinsi bodi ya BBC inavyofanya kazi. Bodi inawajibika kwa usimamizi na mkakati wa shirika.

    Katika kulaumu masuala ya utawala, Banerji anaonekana kumkosoa moja kwa moja mwenyekiti Samir Shah na wanachama wengine wa bodi.

    Kujiuzulu kwa Banerji kunatokea wakati mgumu kwa BBC, huku Shah na wajumbe wa bodi Sir Robbie Gibb na Caroline Thomson wakitakiwa kutoa ushahidi kwa Kamati ya Utamaduni na Michezo ya Wabunge Jumatatu mchana.

    Maswali tayari yameulizwa Bungeni kuhusu wateule wa kisiasa kwenye bodi ya BBC (kuna watano akiwemo Shah na Gibb).

    Kuna uwezekano mkubwa wakaulizwa kuhusu madai, yaliyotolewa kwanza katika hati iliyovuja, kwamba BBC ina "matatizo ya kimfumo" yanayohusiana na utoaji taarifa za maeneo, kwa mfano, mzozo wa Israeli na Gaza na jinsia. Hilo lilikataliwa na Turness na Davie.

    Soma zaidi:

  8. Ukraine iko njia panda "ama kupoteze utu, au mshirika mkuu"

    .

    Chanzo cha picha, Zelensky/Telegram

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameonya kuwa Kyiv iko hatarini kupoteza uungwaji mkono na Marekani kutokana na mpango wa Ikulu ya Marekani kuhusu jinsi ya kumaliza vita na Urusi.

    Akihutubia taifa siku ya Ijumaa, Zelensky alisema Ukraine "huenda ikakabiliwa na chaguo gumu sana: ama kupoteza utu, au hatari ya kupoteza mshirika mkuu", akiongeza kuwa "leo ni moja ya nyakati ngumu zaidi katika historia yetu".

    Mpango wa amani wa Marekani uliovujishwa sana ni pamoja na mapendekezo ambayo Kyiv ilikuwa imefuta hapo awali: kuacha maeneo ya mashariki ambayo inadhibiti sasa, kupunguza kwa kiasi kikubwa ukubwa wa jeshi lake, na kuahidi kutojiunga na Nato.

    Masharti haya yanaonekana kuwa yameelekezwa sana kwenye matakwa ya Urusi, ambayo Rais Vladimir Putin alisema mpango huo unaweza kuwa "msingi" wa suluhu ya amani.

    Katika mkutano wa Ijumaa na baraza lake la mawaziri la usalama, Putin alisema Moscow imepokea mpango huo, ambao haujajadiliwa kwa kina na Kremlin. Alisema Urusi ilikuwa tayari "kuonyesha kubadilika" lakini pia iko tayari kupambana.

    Baadaye mchana, Rais wa Marekani Donald Trump alisema Zelensky "hana budi kukubali" mpango huo, na kuongeza kuwa vinginevyo Ukraine na Urusi zitaendelea kupigana.

    Ukraine inategemea sana uwasilishaji wa silaha za hali ya juu zilizotengenezwa na Marekani, ikiwa ni pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga ili kukomesha mashambulizi mabaya ya anga ya Urusi, pamoja na taarifa za kijasusi zinazotolewa na Washington.

    Urusi ilianzisha uvamizi wa Ukraine mnamo 2022.

    Soma zaidi:

  9. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara ya Tarehe 22/11/2025. Mimi ni Asha Juma.