Matetemeko ya ardhi yameifundisha nini Japan?

Tetemeko kubwa la ardhi katika Siku ya Mwaka Mpya 2024 liliangusha nyumba katikati mwa Japani

Chanzo cha picha, Reuters

Imepita takribani miaka 13 tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi na tsunami iliyosababisha ajali katika kinu cha nyuklia huko Fukushima.

Lakini kumbukumbu huko Japan bado ni mpya. Na siku ya Jumatatu, wote watakuwa wamerejeshwa ili kuangazia tetemeko hilo lilipoanza huko Ishikawa na kengele za tsunami kuanza kusikika.

Maonyo hayo si ya kawaida kabisa nchini Japan. Nilipohamia huko mara ya kwanza, niliruka kutoka kitandani wakati jengo letu lilipokuwa likipata mtikisiko hata mdogo tu.

Lakini baada ya miezi kadhaa, nilikuwa nikipata usingizi pamoja na matetemeko hayo. Na huko Japan, matetemeko kwa haraka yamekuwa sehemu ya maisha.Unafikia hatua ya kuzoea.

Bado kuna hisia hiyo ya kusumbua kwenye akili yako. Lini tetemeko lijalo litapiga? Je, jengo letu ni imara vya kutosha?

Kwa kizazi hiki hofu hizo zote zilitimizwa tarehe 11 Machi, 2011. Kwa dakika mbili dunia ilitetemeka kwa njia ambayo hakuna mtu aliyepata uzoefu wa hilo.

Iliendelea, na kuendelea. Yeyote aliyeishi kupitia hilo anaweza kusimulia mahali ambapo walikuwa na jinsi walivyohisi uoga.

Ndani ya dakika 40, tsunami za kwanza zilikuwa zinakuja ufuoni, zikigonga kuta za bahari na kufagia miji na vijiji kwa mamia ya kilomita kando ya pwani ya kaskazini-mashariki ya Japai, zote zikioneshwa moja kwa moja kwenye televisheni na helikopta ya habari iliyokuwa ikiruka juu ya jiji la Sendai.

Tetemeko la ardhi la Mashariki ya Japani la 2011 liliacha maeneo makubwa ya nchi kuwa magofu

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Siku iliyofuata ilileta habari mbaya zaidi, kinu cha nguvu za nyuklia kilikuwa katika shida. Kuyeyushwa kwa Fukushima kulikuwa kumeanza. Mamia ya maelfu ya watu walikuwa wakiamriwa kuondoka katika nyumba zao. Hata Tokyo hawakujihisi kuwa salama.

Tukio la siku hiyo liliacha kiwewe kikubwa cha pamoja. Katika miezi iliyofuata, nilikuwa nikitafuta eneo jipya la kuishi Tokyo. Mke wangu alisoma ramani za kijiolojia ili kuona mahali palipo na mwamba wenye nguvu zaidi, kwenye ardhi ya juu mbali na mito. Yeye alikuwa makini akizingatia umri wa majengo.

Alikuwa wazi: "Hatuangalii chochote kilichojengwa kabla ya 1981."

Mara tulipohamia katika jengo letu la 1985, tulianza kuhifadhi chakula na maji. Chini ya sinki la bafuni kulikuwa na masanduku ya katoni zilizopakiwa awali ambazo zingeweza kutumika kwa miaka mitano.

Hofu ya 2011 ingerudi Jumatatu.

Na bado tetemeko hili la hivi karibuni pia ni hadithi ya ajabu ya Japan.

Japan hairipoti tetemeko la ardhi kwa ukubwa. Inaripoti ni kiasi gani ardhi inatikisika. Kiwango kinatoka 1 hadi 7. Na siku ya Jumatatu huko Ishikawa mtikiso ulifikia kiwango cha juu zaidi, 7.

Kumekuwa na uharibifu mkubwa wa barabara na madaraja. Ilisababisha maporomoko makubwa ya ardhi. Lakini idadi kubwa ya majengo bado yamesimama.

Katika miji mikubwa ya Toyama na Kanazawa, maisha tayari yanarudi kwa hali ya kawaida.

Nilizungumza na rafiki yangu katika jiji la karibu la Kashiwazaki. "Ilikuwa ya kutisha sana," alisema. "Kwa kiasi kikubwa zaidi nimewahi kushuhudia hapa. Na tulilazimika kuhama kutoka pwani. Lakini tumerejea nyumbani sasa na kila kitu kiko sawa."

Ni hadithi ya ajabu ya ushindi wa uhandisi ulioanza karne moja iliyopita mwaka wa 1923, wakati tetemeko kubwa lilipopiga Tokyo.

Mamlaka imechukua hatua haraka kurejesha mitandao ya usafiri baada ya tetemeko la ardhi siku ya Jumatatu

Chanzo cha picha, reuters

Tetemeko Kubwa la Kanto, kama linavyojulikana, liliharibu maeneo makubwa ya jiji. Majengo ya kisasa yalianguka.

Matokeo yalisababisha kutayarishwa kwa kanuni ya kwanza ya ujenzi ya Japan inayostahimili tetemeko. Kuanzia hapo majengo mapya yalihitaji kuimarishwa kwa chuma na zege. Majengo ya mbao yalikuwa na mihimili minene zaidi.

Kila wakati nchi imekumbwa na tetemeko kubwa, uharibifu umechunguzwa na kanuni kusasishwa. Hatua kubwa zaidi ilifanyika mnamo 1981, baada ya hapo majengo yote mapya yalihitaji hatua za kulindwa dhidi ya athari za mitetemo. Tena, baada ya tetemeko la Kobe katika 1995, mafunzo zaidi yalipatikana.

Kipimo cha mafanikio ni kwamba wakati tetemeko kubwa la 9.0 lilipopiga mwaka wa 2011, kiwango cha kutikisika huko Tokyo kilifikia 5. Hiyo ni sawa na mtetemo ambao mji mkuu wa Japan ulikumbwa mwaka wa 1923.

Mnamo mwaka wa 1923 jiji hilo liliboreshwa, watu 140,000 walikufa. Mnamo 2011, majumba makubwa makubwa yaliyumba, madirisha yalivunjika, lakini hakuna majengo makubwa yaliyoanguka. Ilikuwa ni tsunami iliyoua maelfu ya watu, sio tetemeko la ardhi.

Kuna picha kutoka Ishikawa za nyumba za zamani za mbao zilizoharibiwa na tetemeko hilo. Jengo moja la kisasa limeporomoka, ingawa vituo vya habari vimekuwa na haraka kueleza kwamba lilijengwa mwaka wa 1971. Watu wachache wanaripotiwa kufariki. Wengi wamejeruhiwa.

Lakini ni vigumu kufikiria nchi nyingine yoyote duniani ambayo ingeweza kukumbwa na tetemeko kama hilo bila kuathirika vibaya zaidi.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi