Rais Trump ana lengo gani hasa na Iran?

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
- Author, Paul Adams
- Nafasi, Mwandishi wa habari za kidiplomasia, Washington
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kwa Rais Trump, huu ni wakati wa kufanya uamuzi.
Siku kumi zilizopita, alisema Marekani ilikuwa tayari kwenda kuwaokoa waandamanaji wa Iran endapo serikali yao ingetumia nguvu dhidi yao.
Marekani, rais alisema, ilikuwa "imejiandaa kikamilifu na iko tayari kuchukua hatua."
Hayo yalikuwa kabla ya ukandamizaji nchini Iran kuanza kwa kiwango kikubwa. Sasa, kadiri ukubwa wake wa kutisha unavyozidi kufichuliwa, dunia inasubiri kuona Trump atachukua hatua gani.
"Hakuna anayejua Rais Trump atafanya nini isipokuwa Rais Trump mwenyewe," alisema Katibu wa Habari wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt. "Dunia inaweza kuendelea kusubiri na kukisia."
Lakini kwa muda gani?
Maafisa wakuu wanatarajiwa kumuarifu rais siku ya Jumanne kuhusu njia mbalimbali zinazowezekana za kuchukua hatua. Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ndege ya Air Force One siku ya Jumapili, Trump alisema alikuwa akiangalia "baadhi ya hatua kali sana."
Akiwa na hali ya kujiamini baada ya kile alichokiita mafanikio makubwa nchini Venezuela, ambapo rais alielezea kukamatwa kwa Nicolas Maduro kuwa mojawapo ya operesheni zilizofanikiwa zaidi katika historia ya Marekani, kishawishi cha kutumia jeshi lazima kiwe kikubwa.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kama matukio ya majira ya kiangazi mwaka jana yalivyoonesha, Marekani ina uwezo wa kushambulia kutoka mbali. Mabomu ya B-2 yaliruka safari za saa 30 za kwenda na kurudi kutoka Kituo cha Jeshi la Anga cha Whiteman huko Missouri, na kudondosha mabomu ya kupenya ngome (bunker-busting bombs) kwenye maeneo mawili muhimu zaidi ya nyuklia ya Iran.
Iwapo Marekani itaamua kurudia mbinu hizo hizo, au kuchagua mashambulizi ya kulenga kwa usahihi maeneo ya utawala yanayohusika na ukandamizaji wa sasa, ni jambo la msingi kudhani kuwa Washington ina orodha ndefu ya kuchagua.
Maafisa wa Pentagon, walionukuliwa na mshirika wa BBC nchini Marekani, CBS News, wanasema mwitikio huo unaweza kujumuisha mbinu nyingine mbalimbali za siri zaidi, zikiwemo operesheni za mtandaoni (cyber) na kampeni za kisaikolojia za siri zinazolenga kuvuruga na kuchanganya miundo ya uongozi wa Iran.
Serikali ya Marekani inaweza kuchukua hatua, lakini si kwa mtindo uleule au kwa aina ile ile ya tukio lililotokea Caracas tarehe 3 Januari.
Hata katika hali yake dhaifu, na licha ya kupigwa na mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani na Israel, Iran si Venezuela. Jamhuri ya Kiislamu ni utawala uliokomaa katika mapambano. Kuondolewa kwa mtu mmoja pekee hakutalazimisha nchi nzima kuifuata Washington.
Rejea ya hivi karibuni ya Trump kuhusu jaribio la maafa la mwaka 1980 la Rais Jimmy Carter la kuwaokoa mateka wa Kimarekani waliokuwa wakishikiliwa Iran pia inaonesha kuwa anatambua hatari zinazoweza kuandamana na jaribio lolote la kupeleka wanajeshi wa Marekani.
Wanajeshi wanane wa Marekani walifariki wakati helikopta moja ilipogongana na ndege ya usafiri ya EC-130 ikiwa ardhini katika jangwa la mashariki mwa Iran.
Operesheni hiyo iliyofeli, pamoja na aibu iliyohisiwa kutokana na picha za mateka wa Kimarekani wakiwa wamefunikwa vichwa na kuoneshwa mbele ya kamera mjini Tehran, ilikuwa sababu kubwa iliyochangia kushindwa kwa Carter katika uchaguzi baadaye mwaka huo.
"Sijui kama angeweza kushinda uchaguzi," Trump aliwaambia waandishi wa habari wa New York Times wiki iliyopita, "lakini bila shaka hakuwa na nafasi yoyote baada ya janga hilo."
Lakini miaka 46 baadaye, kuna swali kubwa zaidi linaloongoza mahesabu ya kijeshi ya Washington: utawala wa Trump unajaribu hasa kupata nini nchini Iran?
"Ni vigumu kusema kwa uhakika ni hatua gani Trump anaweza kuchukua," alisema Will Todman, mtafiti mwandamizi katika mpango wa Mashariki ya Kati wa Kituo cha Mafunzo ya Mkakati na Kimataifa (CSIS), "kwa kuwa hatujui lengo lake hapa."
Todman alisema Rais Trump huenda anajaribu kuathiri mwenendo wa utawala wa Iran, badala ya kuuangusha.
"Nadhani hatari za kubadilisha utawala ni kubwa sana kiasi kwamba bado sijaamini hilo ndilo lengo lake kuu kwa sasa," alisema. "Inaweza kuwa ni kupata masharti zaidi katika mazungumzo ya nyuklia. Inaweza kuwa ni kusimamisha ukandamizaji. Pia inaweza kuwa ni kujaribu kutekeleza mageuzi yatakayofungua njia ya… aina fulani ya afueni ya vikwazo."
Trump amesema baadhi ya watu wa utawala wa Iran wamewasiliana, wakiwa na wasiwasi na tayari kujadiliana, huenda ili kuendeleza mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa nchi hiyo.
"Kile unachosikia hadharani kutoka kwa utawala wa Iran ni tofauti kabisa na ujumbe ambao utawala wetu unapokea kwa faragha," Leavitt alisema Jumatatu, akiongeza kuwa diplomasia ilikuwa "chaguo la kwanza kila wakati."

Chanzo cha picha, Andrew Caballero-Reynolds/ AFP via Getty Images
Maafisa ambao hawajatajwa majina yao wameliambia jarida la Wall Street kwamba Makamu wa Rais JD Vance ni miongoni mwa wasaidizi wachache wa ngazi ya juu wanaomsihi Trump atangulize diplomasia.
"Kitu cha busara zaidi ambacho wangefanya," Vance aliwaambia waandishi wa habari Alhamisi iliyopita, "ni kuingia katika mazungumzo ya kweli na Marekani kuhusu kile tunachohitaji kuona kuhusiana na mpango wao wa nyuklia."
Hata hivyo, endapo ukandamizaji wa damu utaendelea kote Iran, diplomasia iko katika hatari ya kuonekana kama ishara ya udhaifu.
"Iwapo haitoshi, inawavunja moyo waandamanaji," Todman alisema.
Labda akizingatia hilo, na huku simulizi za kutisha zikiendelea kutoka Iran licha ya kuzimwa kwa mtandao, rais amesema huenda akahisi kulazimika kuchukua hatua hata kabla njia za kidiplomasia kuchunguzwa kikamilifu.

Baadhi wanaamini kuwa shambulio dogo la kijeshi linaweza kuwapa waandamanaji moyo, huku likiipa pia serikali onyo kwamba huenda kukawa na hatua kali zaidi baadaye.
"Kile Trump anachohitaji kufanya ni kusababisha hofu ndani ya utawala," alisema Bilal Saab, mtafiti mshirika katika Mpango wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wa Chatham House.
"Shambulio la Marekani litaweza kuwapa ujasiri waandamanaji na kuuvuruga umakini wa utawala," aliongeza.
Hata hivyo, Saab alisema hatua ya kijeshi pia inaweza kuleta matokeo kinyume.
"Inaweza kuimarisha azma ya utawala na msingi wake mkubwa wa uungwaji mkono kote nchini. Kuungana chini ya bendera ya taifa kusingeshangaza," alisema. "Hilo lina uwezekano mkubwa zaidi… ikiwa shambulio litakuwa la mfano tu au la mara moja."
Haya yote ni mahesabu magumu kwa rais, yanayozidishwa na ukweli kwamba Iran imetishia kujibu shambulio lolote la Marekani.
Na licha ya uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Israel na Marekani, Iran bado ina akiba kubwa ya makombora ya balistiki.
Kote Mashariki ya Kati, washirika na vikundi vinavyoiunga mkono Iran huenda wameondoka, kama aliyekuwa rais wa Syria, Bashar al-Assad au kudhoofika, kama ilivyo kwa Hezbollah nchini Lebanon, lakini kile kinachoitwa "Muhimili wa Upinzani" bado haujakwisha nguvu.
Wahouthi nchini Yemen na wanamgambo wa Kishia nchini Iraq bado wana uwezo wa kuchukua hatua.
Miongoni mwa sauti zinazomsukuma Rais Trump kuchukua hatua kali ni mtu anayejitolea kuongoza Iran kwa mpito kutoka katika utawala wa viongozi wa kidini.
"Rais ana uamuzi wa kufanya hivi karibuni," Reza Pahlavi, mwana wa mfalme wa mwisho wa Iran,akiwa uhamishoni aliiambia CBS News.
"Njia bora ya kuhakikisha kuwa watu wachache zaidi wanauawa Iran ni kuingilia mapema," alisema. "Ili hatimaye utawala huu uanguke na kumaliza matatizo yote tunayokabiliana nayo."
Inaonekana kuwa rahisi. Katika Ikulu ya White House, maafisa watajua kwamba si rahisi hata kidogo.















