Wanawake wakosekana katika kinyang'anyiro cha urais Uganda

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
- Author, Swaibu Ibrahim
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Mnamo Agosti mwaka jana, wakili na mwanaharakati wa Uganda , Yvonne Mpambara, 34, alichukua hatua ya kujaza fomu za uteuzi kwa nia ya kuwania urais wa nchi yake. Kampeni yake ilijikita katika ajenda ya uongozi jumuishi, uboreshaji wa utoaji wa huduma za umma, pamoja na mageuzi ya mfumo wa kisheria.
Hata hivyo, tarehe 24 Septemba 2025, Mpambara alipata taarifa kuwa hakuwa miongoni mwa wagombea walioidhinishwa na Tume ya Uchaguzi kushiriki katika uchaguzi wa urais. Hatua hiyo ilimfanya kuikosoa vikali tume hiyo, akiishutumu kwa kuwatenga wanawake katika mchakato wa uteuzi wa wagombea.
"Ninailaumu mifumo iliyopo," alisema Mpambara.
"Kulikuwa na wanawake watatu wenye uwezo na sifa stahiki ambao wangeweza kufika katika orodha ya mwisho ya wagombea, lakini mfumo uliwakwamisha wote. Aidha, tunaamini kuwa Tume ya Uchaguzi haikuwa na utaratibu wa wazi, wa haki na unaoeleweka wa uhakiki wa wagombea."
Uganda inapojitayarisha kuelekea kwenye uchaguzi wa urais Alhamisi hii, wapiga kura watashuhudia orodha ya wagombea wote wa kiume. Rais wa sasa, Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81, anawania muhula wa saba mfululizo baada ya kukaa madarakani kwa zaidi ya miongo minne.
Mpinzani wake mkuu ni Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu Bobi Wine, mwanamuziki aliyebadilika na kuwa mwanasiasa, mwenye umri wa miaka 43.
Wagombea wengine sita, Frank Bulira, Robert Kasibante, Joseph Mabirizi, Nandala Mafabi, Mugisha Muntu na Mubarak Munyagwa wote ni wanaume.
Akijibu tuhuma zilizotolewa na Mpambara, msemaji wa Tume ya Uchaguzi, Julius Mucunguzi, alisisitiza kuwa tume ilifuata kikamilifu taratibu na miongozo iliyowekwa kisheria wakati wa zoezi la uteuzi na uhakiki wa wagombea.
"Endapo hakuna mgombea mwanamke anayekidhi masharti yaliyoainishwa, tume haiwezi kuvunja sheria zake. Kikatiba, uchaguzi unaweza kuwa wa wanaume pekee, wanawake pekee au mchanganyiko wa wote," alisema.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, mgombea wa urais lazima awe raia wa Uganda kwa kuzaliwa, awe na umri wa angalau miaka 18, awe mpiga kura aliyesajiliwa, na alipe ada ya uteuzi ya shilingi milioni 20 za Uganda yaani paundi 4,200. Aidha, anatakiwa kuwasilisha angalau saini 100 za waungaji mkono kutoka angalau theluthi mbili ya wilaya 146 za nchi hiyo.
Mpambara, hata hivyo, anasema hakupewa maelezo ya kuridhisha kuhusu sababu za kukataliwa kwa nyaraka zake. Anadai kuwa fomu zake za waungaji mkono zilidaiwa kuwa bandia bila kuwekwa wazi vigezo vilivyotumika kuthibitisha madai hayo.
Tangu Uganda ilipoanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 2005, kufuatia kura ya maoni iliyoungwa mkono na zaidi ya asilimia 90 ya wapiga kura, kila uchaguzi wa urais umehusisha angalau mgombea mmoja mwanamke. Miongoni mwao ni Miria Kalule Obote (2006), Beti Kamya (2011), Maureen Kyalya (2016) na Nancy Kalembe Linda, aliyekuwa mgombea pekee mwanamke mwaka 2021.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kukosekana kwa mgombea mwanamke katika uchaguzi wa sasa ni hatua ya kurudi nyuma katika juhudi za kukuza ushiriki wa wanawake katika uongozi wa kisiasa na uimarishaji wa demokrasia.
Hata hivyo, kwa ujumla, Uganda bado inatajwa kuwa miongoni mwa nchi za Afrika zenye uwakilishi mzuri wa wanawake katika nyadhifa za juu za uongozi. Spika wa Bunge, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wote ni wanawake, huku takribani asilimia 45 ya baraza la mawaziri likiwa na wanawake. Aidha, viti 146 vya Bunge vimetengwa mahsusi kwa ajili ya wawakilishi wa wanawake wa wilaya.
Kura ya vijana na mustakabali wa uongozi Uganda
Si wanawake pekee wanaohisi kutengwa katika mchakato huu wa uchaguzi. Uchaguzi huu unafanyika wakati Uganda ikikabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi na kupungua kwa imani ya wananchi kwa taasisi za umma.
Kwa vijana wengi, uchaguzi huu ni zaidi ya mchakato wa kisiasa; ni kipimo cha iwapo mfumo wa sasa unaweza kutoa fursa za kiuchumi, ushirikishwaji na matumaini ya maisha bora. Zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wa Uganda wana umri wa chini ya miaka 30, jambo linalowafanya vijana kuwa nguvu kubwa ya kisiasa na kijamii.
Gloria Nawanyanga, mwenye umri wa miaka 28, anawania nafasi ya ubunge kwa lengo la kuwakilisha maslahi ya vijana wa eneo la Uganda ya Kati. Kwa mtazamo wake, uwezeshaji wa kiuchumi wa vijana ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.
"Ikiwa vijana watawezeshwa ipasavyo, Uganda inaweza kufikia hadhi ya taifa la kipato cha kati au hata kuingia katika kundi la nchi zilizoendelea kwa muda mfupi, kwa kuwa sisi ndio wengi," alisema.
Hata hivyo, gharama kubwa za siasa zimeibua wasiwasi mkubwa. Wakosoaji wanasema biashara ya siasa imekuwa kikwazo kikubwa kwa vijana na makundi yaliyo pembezoni. Mpambara anaonya kuwa gharama za kugombea zinafunga milango ya uongozi kwa walio wengi.
"Siasa zimekuwa ghali kupita kiasi. Huu ni ubaguzi unaoanzia mwanzo kabisa. Ni nani anaweza kumudu zaidi ya shilingi bilioni tatu za Uganda kugombea ubunge?" aliuliza bila kusubiri ajibiwe akionyesha ni ghali mno hasa kwa kijana kuthubutu kuingia katika siasa.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Katika muktadha wa kimataifa, ushiriki wa vijana katika siasa umechukua sura mpya. Kizazi cha Gen Z kimeibuka kama nguvu ya mabadiliko, kikiongoza maandamano na kudai uwajibikaji, utawala bora na ajira katika nchi mbalimbali zikiwemo Kenya, Bangladesh, Madagascar, Nepal na Morocco.
Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2024, kiwango cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana nchini Uganda bado ni kikubwa. Kati ya watu milioni 25.1 walio katika umri wa kufanya kazi, ni takribani milioni 9.4 pekee waliokuwa wameajiriwa.
Katika kampeni zake, Rais Museveni amewahimiza vijana kutumia fursa ya amani na utulivu uliopo, na kushiriki katika programu za serikali za kujikimu kiuchumi. Amewataka pia waache kutegemea ajira za serikali pekee na badala yake wajikite katika ubunifu na uzalishaji mali.
Kwa upande wa upinzani, chama cha National Unity Platform kinachoongozwa na Bobi Wine kimeahidi, kupitia ilani yake Uganda Mpya Sasa, kuunda ajira milioni kumi ifikapo mwaka 2032, kupambana na rushwa na kuibadilisha Uganda kuwa taifa linaloendeshwa na teknolojia.
Kwa viongozi vijana kama Gloria Nawanyanga, wakati wa mabadiliko umefika.
"Huu ni wakati sahihi kwa vijana kuchukua dhamana ya uongozi wa nchi hii, kwa kuwa sisi ndio wengi," alisema.
Uganda inapokwenda kupiga kura, kura ya vijana inatarajiwa kuwa na uzito mkubwa katika kuamua mwelekeo wa uongozi wa taifa. Maoni kutoka kwa wananchi yanaonyesha matarajio makubwa kwa viongozi watakaoteuliwa.
Atuhire Vandah, mfanyabiashara wa samaki mwenye umri wa miaka 24 kutoka Luzira pembezoni mwa Kampala, anataka kuona hatua madhubuti dhidi ya rushwa.
"Ninaomba fedha za uwezeshaji wa vijana ziwafikie walengwa. Tulisikia zilitolewa, lakini wengi wetu hatukuzipata kwa sababu ya udanganyifu," alisema.
Kwa upande wake, Halimah Mutesi, muuza bidhaa sokoni mwenye umri wa miaka 38, anahimiza uongozi kuendelea kuweka mkazo katika kuwawezesha wanawake.
"Wanawake ni nguzo ya jamii. Ni muhimu kuendelea kutupa nafasi hadi ngazi za juu zaidi za uongozi, kwa kuwa mara nyingi sisi ndio tunaathirika zaidi," alisema.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












