Aliwahi kuwakosoa viongozi wa Afrika wanaong'ang'ania madaraka. Sasa anataka muhula wa saba

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Yoweri Museveni
Muda wa kusoma: Dakika 6

Raia wa Uganda walio na umri wa chini ya miaka 40 - na ambao ni zaidi ya robo tatu ya watu - wamemfahamu rais mmoja tu.

Yoweri Museveni alinyakua wadhifa huo wa juu mwaka 1986 kufuatia uasi wa kutumia silaha na akiwa na umri wa miaka 81, haonyeshi dalili za kuwachia.

Wakati wake wa uongozi umeambatana na kipindi kirefu cha amani na maendeleo makubwa, ambayo wengi wanashukuru. Lakini wakosoaji wake wanasema anang'ang'ania madaraka kupitia mchanganyiko wa kuwatenga wapinzani na kuzitumia vibaya taasisi huru.

"Hatuamini katika ukomo wa mihula [ya urais]," aliwahi kuiambia BBC, akiutetea wadhfa wake baada kushinda uchaguzi wa tano.

Mwaka mmoja baadaye, ukomo wa umri wa mgombea urais uliondolewa - na kufungua njia, kwa Museveni kuwa rais wa maisha.

Safari ya Museveni ilianza mwaka wa 1944, alipozaliwa katika familia ya wafugaji wa ng'ombe huko Ankole, magharibi mwa Uganda.

Alikua wakati Uganda ikipigania uhuru kutoka kwa Uingereza, ambayo ilifuatiwa na kipindi cha ukatili na misukosuko chini ya Milton Obote na Idi Amin.

Kwa miaka mingi, Museveni hakujua tarehe yake ya kuzaliwa, akiandika katika kumbukumbu yake: "Tulikuwa na changamoto za kutishia maisha kama vile mauaji ya nje ya mahakama na uporaji ... hatukuwa na wakati wa kuwa na maelezo kama vile tarehe za kuzaliwa."

Mnamo 1967, Museveni aliondoka Uganda kwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika nchi jirani ya Tanzania. Huko, alisomea sayansi ya uchumi na siasa na akaanzisha ushirikiano na wanafunzi wanaofanya siasa kutoka eneo lote.

Jina la Museveni lilipata umaarufu katika miaka ya 1970, baada ya mapinduzi ya Amin.

Museveni alisaidia kuunda Front for National Salvation - moja ya makundi ya waasi ambayo, kwa msaada wa Tanzania, yalimuondoa Amin.

Amin alikuwa maarufu kwa kukandamiza upinzani na kuwafukuza watu wa jamii ya Asia nchini humo. Chini ya utawala wake wa miaka minane inakadiriwa watu 400,000 waliuawa.

Museveni alisaidia kuunda Front for National Salvation - moja ya makundi ya waasi ambayo, kwa msaada wa Tanzania, yalimuondoa Amin.

Amin alikuwa maarufu kwa kukandamiza upinzani na kuwafukuza jumuiya ya Asia ya nchi hiyo. Chini ya utawala wake wa miaka minane inakadiriwa watu 400,000 waliuawa.

..

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Museveni akiwa na Nelson Mandela mwaka 1998
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Alikuwa sehemu ya mfumo wa kikoloni," Museveni aliuambia Mtandao wa Global Indian katika mahojiano ya hivi karibuni. "Idi Amin alikuwa mjinga... .

Kufuatia kuanguka kwa Amin, Rais wa zamani Milton Obote alirejea mamlakani kupitia uchaguzi mkuu. Hata hivyo, Museveni alikataa kukubali uongozi wa Obote, akidai kura ziliibiwa.

Alianzisha mapambano ya msituni mwaka 1981 na miaka mitano baadaye, kundi lake la waasi, National Resistance Movement (NRM), lilichukua mamlaka na Museveni akawa kiongozi.

Uchumi wa Uganda ulianza kukua kwa kasi na zaidi ya miaka 10, nchi hiyo iliona ukuaji wa wastani wa zaidi ya 6%. Usajili wa wanafunzi katika shule za msingi uliongezeka maradufu na viwango vya VVU vilishuka kwa sababu ya kampeni ya kupambana na Ukimwi iliyoongozwa na rais.

Museveni alikua kipenzi cha nchi za Magharibi, lakini sifa yake ilipata pigo mwaka 1998, wakati Uganda na Rwanda zilipovamia nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuunga mkono waasi wanaopigana kupindua serikali.

Wakati huo, wakosoaji pia walilalamika kwamba rais alikuwa akizidi kuvumilia maoni yanayopingana. Pia ilionekana wazi hakuwa na mpango wa kuachia madaraka.

Museveni alikuwa amesema, katika mkusanyiko wa maandishi wa 1986: "Tatizo la Afrika kwa ujumla, na hasa Uganda, si watu bali ni viongozi wanaotaka kuzidi kukaa madarakani."

Lakini kufikia mwaka 2005 maoni yake yalionekana kubadilika na katiba ya Uganda ikafanyiwa marekebisho, na kuondoa ukomo wa mihula mingapi ambayo rais anaweza kuhudumu.

Mnamo 2017, ukomo wa umri wa wagombea urais pia uliondolewa - hatua iliyosababisha wabunge kurusha viti katika rabsha bungeni.

Museveni pia amekabiliwa na madai kwamba amedhoofisha uhuru wa taasisi muhimu.

Hasa, mahakama ya Uganda imeshutumiwa kwa kuajiri wale wanaoitwa "majaji wa kada" ambao uaminifu wao upo kwa serikali.

Majaji wanapokwenda kinyume na serikali, wakati fulani wamejikuta wakizozana na mamlaka.

Kwa mfano, mwezi Desemba 2005, maafisa wa usalama waliokuwa na silaha walivamia Mahakama Kuu katika mji mkuu, Kampala, na kuwakamata tena washukiwa wa kundi la waasi, ambao walikuwa wametoka kuachiliwa kwa mashtaka ya uhaini.

Vyombo vya habari pia vimetishiwa uhuru wake. Kwa juu juu, Uganda ina tasnia ya habari iliyochangamka, lakini vyombo vingi vimevamiwa na wanahabari kuzuiliwa.

Pengine jambo muhimu zaidi katika maisha marefu ya Museveni ni kupunguzwa kwa nguvu za upinzani.

Ilipodhihirika kuwa Museveni hakukusudia kuondoka madarakani, baadhi ya washirika wake wa zamani walianza kujitenga. Walipofanya hivyo, vyombo vya usalama vilielekeza macho yao kwao.

Kwa mfano, Kizza Besigye wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change, ambaye wakati mmoja alikuwa daktari wa Museveni, aligombea kwa mara ya kwanza dhidi ya rais mwaka 2001.

Tangu wakati huo, amekamatwa na kufunguliwa mashtaka mara kadhaa. Mnamo 2024, alitoweka kwa njia isiyoeleweka jijini Nairobi, na kufikishwa siku nne baadaye katika mahakama ya kijeshi ya Uganda. Anasalia gerezani kwa mashtaka ya uhaini, ambayo anakanusha.

Mwanamuziki wa Pop aliyegeuka kuwa mwanasiasa Bobi Wine ndiye mkosoaji wa hivi punde zaidi wa Museveni kukabiliana na ghadhabu za serikali.

Kiongozi huyo wa upinzani mwenye umri wa miaka 43, ambaye nguvu zake zinavutia umati mkubwa wa vijana, amekamatwa, kufungwa jela na kushtakiwa kwa uhalifu ikiwa ni pamoja na uhaini. Haya yote yametupiliwa mbali baadaye.

Mnamo 2021 polisi walimfyatulia mabomu ya machozi na hata kumpiga risasi Bobi Wine na wafuasi wake, wakisema walikuwa wamekaidi vizuizi vya coronavirus kwenye mikusanyiko mikubwa.

Katika kipindi cha sasa cha kampeni, vikosi vya usalama vimetumia "silaha na risasi za moto kutawanya mikutano ya amani" na kuwateka nyara wanachama wa vyama vya upinzani kwenye magari yenye namnbari za kiraia ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema.

Katikati ya mazingira haya, Museveni aliuambia umma kwamba "askari mmoja anabeba risasi 120". Hata hivyo, pia aliwaamuru polisi kutowapiga wafuasi wa upinzani na badala yake watumie mabomu ya machozi.

Wafuasi wa Museveni wanaashiria utulivu wa kiasi ambao Uganda imekuwa ikifurahia katika miongo kadhaa ambayo amekuwa madarakani.

Emmanuel Lumala Dombo, msemaji wa NRM, anaeleza kuwa zaidi ya watu milioni 1.7 wamehamia Uganda baada ya kukimbia mapigano katika nchi zao.

"Miaka 40 iliyopita, tulikuwa miongoni mwa wasafirishaji wakubwa wa wakimbizi miongoni mwa mataifa jirani yanayotuzunguka," Dombo aliambia BBC. "Kwa sasa Uganda ndiyo mwenyeji mkubwa zaidi wa wakimbizi barani Afrika."

Serikali ya Museveni hivi karibuni pia imekuwa ikihimiza uwekezaji wa kigeni, ikiingia mikataba na mataifa kama China, Uingereza na Umoja wa Falme za Kiarabu. Anasema anataka Uganda iwe nchi ya kipato cha kati ifikapo 2040.

Museveni anajiona sio tu kama mtu dhabiti na mwenye tamaa, lakini pia kama mtu anayelea vijana wa Uganda. Anawaita wafuasi wake vijana Bazukulu (maana yake wajukuu katika lugha ya Kiganda) na wanamtaja kwa lakabu za M7 au Sevo.

Lakini kwa jicho la Bobi Wine, ambaye ni takriban nusu ya umri wa Museveni, rais amekuwa akionyesha kutochoka.

Mnamo 2020, ili kuhimiza mazoezi wakati wa kuenea kwa virusi vya corona alirekodiwa akifanya mazoezi mbele ya vyombo vya habari, na kisha akarudia ujanja huo mara kadhaa mwaka huo, pamoja na mbele ya wanafunzi wakishangilia.

Amezungumzia afya yake mara nyingi, akisema mwishoni mwa mwaka jana: "Nimekuwa hapa na wewe kwa miaka 40 sasa. Je, umewahi kusikia kwamba nimekuwa hospitalini? Isipokuwa nilipokuwa na [coronavirus] kwa siku 21."

Kadiri Museveni anavyozeeka, wakosoaji wana wasiwasi kuwa anaigeuza nchi kuwa miliki ya familia yake.

Wanabainisha kuwa mke wa rais, Janet, ni waziri wa elimu na mwanawe, Jenerali Muhoozi Kainerugaba ni mkuu wa jeshi. Mjukuu wa Museveni pia alijiandikisha katika jeshi mwezi Julai, hatua inayoonekana kuwa na uwezekano wa kuendeleza nasaba ya familia.

Chama cha NRM kimesema machache kuhusu jinsi kitakavyosimamia urithi wa Museveni, lakini uvumi kwamba Jenerali Kainerugaba mwenye umri wa miaka 51 atajitokeza ni mwingi.

Iwapo hili litatokea, linaweza kuhatarisha urithi wa Museveni kwa utulivu. Jenerali Kainerugaba anajulikana kwa kutotabirika na uchochezi, haswa kwenye mitandao ya kijamii. Ametumia X kutania kuhusu kuivamia Kenya, akaighairi Ethiopia kwa kuunga mkono Misri wakati wa mzozo kati ya nchi hizo mbili na kukubali kumzuilia mlinzi wa Bobi Wine katika chumba chake cha chini cha ardhi.

Kwa sasa, hata hivyo, akiwa na tajriba ya takriban miongo minne, Museveni ana imani atapata ushindi wa saba.

"Uganda iko salama. Tokeni nje na kupiga kura," aliuambia umma wakati wa hotuba ya mkesha wa Mwaka Mpya. "NRM ya Uganda haiwezi kuzuilika."