Wapiganaji wa Kikurdi: Kifahamu kikosi cha siri cha jeshi la wanawake pekee

Chanzo cha picha, Valentina Sinis
- Author, Kawoon Khamoosh
- Nafasi, BBC World Service
- Akiripoti kutoka, Erbil, Iraq
- Muda wa kusoma: Dakika 7
BBC imetembelea kundi moja la wapiganaji wa Kikurdi - kikosi cha wanawake pekee.
Ilichukua siku za kadhaa za kujadiliana ili kuingia kwenye mapango marefu na handaki za chini ya ardhi ambazo hutumika kama kambi ya wapiganaji wa Kikurdi wa Iran kaskazini mwa Iraq.
Wanaendesha mtandao wa mawasiliano ya siri na hawajulikani sana katika eneo hili lenye uhuru wa ndani la la Kurdistan.
Ni mpiga picha mwanamke pekee aliyeruhusiwa kuingia katika eneo hilo na kutumia siku kumi na Wakurdi.
Katika miongo ya hivi karibuni, makundi kadhaa ya waasi wa Kikurdi kutoka Iran yamehamia katika milimani iliopo kaitika mpaka na Iraq.
Wanajificha dhidi ya intelejensia ya Iran, makundi ya kiShia nchini Iraq na vikosi vya Uturuki.
Hivi majuzi, makundi makubwa ya Kikurdi ya Iran kaskazini mwa Iraq yaliunda muungano na kumekuwa na uvumi kwamba Rais wa Marekani Donald Trump aliwasiliana moja kwa moja na viongozi hao na kuwaomba wajiunge na vita hivyo.
Katika mahojiano ya simu na Reuters Machi 5, Trump alisema ataunga mkono mashambulizi ya Wakurdi dhidi ya Iran, akisema, "Nadhani ni vizuri kama wanataka kufanya hivyo."
Hata hivyo, Rais wa Marekani aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumamosi kwamba hataki wapiganaji wa Kikurdi katika ardhi ya Iran.
"Hatutaki kuvifanya vita kuwa vigumu zaidi kuliko ilivyo sasa," alisema.
Huku mashambulizi ya mabomu ya Marekani na Israel yakiendelea, Iran ilianzisha mashambulizi dhidi ya makundi kadhaa ya Kikurdi, ikiwemo shambulio la kombora la masafa marefu ambalo liliua mpiganaji mmoja.
Mojawapo ya vikundi maarufu zaidi ni Free Life Party of Kurdistan (PJAK), ambacho kinasema kimekuwa kikijiandaa kwa miaka mingi kurejea nchini Iran.
"Ninapigania familia yangu na watu wa Kikurdi ambao wamekandamizwa kwa muda mrefu," anasema Aryen mwenye umri wa miaka 21.
Yeye ni mwanachama wa kitengo cha Jeshi la Ulinzi la Wanawake katika PJAK.
Akiwa Mkurd, Aryen anasema ameishi katika ukosefu wa haki na ubaguzi nchini Iran, na hakuachwa na chaguo ila kuchukua silaha. Alijiunga na PJAK miaka miwili iliyopita.
Ndani ya kambi za siri

Chanzo cha picha, Valentina Sinis
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mahandaki hayo ni mahali salama pa kuhifadhia chakula, pesa taslimu na maghala ya silaha.
PJAK huficha idadi ya wapiganaji wake, lakini takriban wapiganaji 60 - wengi wao wakiwa wanawake - wamekuwa wakifanya mazoezi katika kambi hii kabla ya vita vya Marekani na Israeli na Iran kuanza.
Wapiganaji hupitia mazoezi ya kijeshi, mafunzo ya kiitikadi na kufanya mazoezi ya ujuzi mbalimbali, kama vile mbinu za udunguaji na ndege zisizo na rubani.
Pia walifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu wakijiandaa kupelekwa mpakani huku mvutano kati ya Marekani na Iran ukiongezeka.
"Vita hivi vilitarajiwa sana," Gelawej Ewrin mwenye umri wa miaka 40 aliiambia BBC.
Akiwa na umri wa miaka 20, Ewrin aliacha masomo yake ya jiografia katika jiji la Urmia nchini Iran, na kujiunga na PJAK kama askari wa miguu. Baadaye akawa msemaji.
Akizungumza kutoka kwenye moja ya mapango ya siri, Ewrin anasema ametumia nusu ya maisha yake katika milima hii na hajaiona familia yake tangu alipoondoka.
Anasema ingawa Khamenei huenda amekufa katika mashambulizi ya sasa, mfululizo wa maandamano yanayoongozwa na wanawake kote Iran kuanzia mwaka 2022 tayari yalikuwa yameidhoofisha Jamhuri ya Kiislamu.
Anazungumzia machafuko baada ya kifo cha Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22, mwanamke Mkurdi ambaye alikamatwa na polisi wa Iran kwa kutofuata sheria zinazowataka wanawake kuvaa hijabu.
Chaguo pekee

Chanzo cha picha, Valentina Sinis
Iran ilijibu maandamano hayo - ambayo yalibadilika na kuwa harakati inayoitwa 'Wanawake, Maisha, Uhuru' - kwa msako mkali, lakini msako huo ulitoa msukumo kwa baadhi ya wanawake kujiunga na PJAK.
Kabla ya kujiunga na PJAK, Bigen mwenye umri wa miaka 18 alishiriki katika maandamano makubwa na alikataa kuvaa hijabu shuleni.
"Wanawake hawana machaguo mengi," Bigen anasema huku akisuka nywele za mpiganaji mwenzake.
"Ama tunapaswa kuvumilia vurugu za majumbani na vikwazo vya kijamii, au kujilinda kupitia mapinduzi."
Makundi ya waasi wa Kikurdi mara nyingi hushutumiwa kwa kuajiri watoto kama wanajeshi, na Bigen alikuwa bado msichana wa shule nchini Iran alipojiunga na kundi la waasi miaka mitatu iliyopita. Wapiganaji wengi hapa wanasema, upinzani wa silaha ndio njia pekee ya suluhisho.
"Mapambano yangu ni kupata mustakabali huru kwa kizazi kijacho cha Wakurdi," anasema daktari wa meno Delal, ambaye alianza kuwa mpiganaji wa msituni akiwa na umri wa miaka 23.
"Kwa watu wa Kikurdi ... miaka mia mbili iliyopita imekuwa na ukandamizaji na vurugu," anaongeza.
Kundi la PJAK lilianzishwa mwaka 2004 na linahusishwa na Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK), chama kinachotaka kujitenga nchini Uturuki ambacho kiliweka chini silaha zake mwaka jana baada ya miongo minne ya mgogoro na taifa hilo la Uturuki.
PJAK inasema inaheshimu uamuzi huo, lakini Wakurdi wa Iran wataendelea na upinzani wao wa kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Uturuki na Iran zote zinalitambua kundi hili kama shirika la kigaidi.
Wizara ya ulinzi ya Uturuki inasema inafuatilia shughuli za "kundi la kigaidi la PJAK" ambalo inalishutumu kwa kuchochea utengano wa kikabila na kutishia amani na utulivu katika eneo hilo.
Hofu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe

Chanzo cha picha, Valentina Sinis
Wapiganaji wa Kikurdi wanafahamu ukubwa wa changamoto iliyo mbele yao - na uwezekano wa mgogoro wa moja kwa moja na vikosi vyenye silaha vya Jamhuri ya Kiislamu.
"Vita vya wenyewe kwa wenyewe ni kitu ambacho hatutaki kitokee," Ewrin aliambia BBC.
"Tunapaswa kufanya kila tuwezalo kuongoza vita kuangusha kwa utawala, ili vita visielekezwe kwetu na kutulazimisha kupigana sisi kwa sisi katika siku zijazo," anaongeza.
Makundi ya upinzani ya Iran yanatumai Iran itamaliza vita hivi kwa kupata demokrasia, lakini yanaogopa kushindwa ikiwa nguvu za vikosi vya kizalendo zitashinda.
Wakurdi ni 10% ya idadi ya watu milioni 90 nchini Iran, na kwa miongo kadhaa wamehisi kutengwa na kuteswa na Jamhuri ya Kiislamu.
Tangu wakati huo, Tehran imezidisha mashambulizi dhidi ya makundi ya Kikurdi ya Iran katika eneo la Kurdistan la Iraq.
BBC ilizungumza na viongozi wa muungano mpya na kuwauliza kuhusu mazungumzo yao na Trump, lakini walikataa kutoa maoni, na kukataa ripoti kwamba vikosi vyao vimevuka mpaka na kuingia Iran.
Hata hivyo, PJAK inadai kuwa na vikosi "vikubwa" vya kijeshi tayari katika ardhi ya Iran, ambavyo vinasubiri wakati mwafaka kuchukua hatua.
"Kuhusika kwetu kijeshi kunategemea jinsi mambo yanavyoendelea katika siku chache zijazo," kiongozi mmoja alituambia.
Njia panda

Chanzo cha picha, Valentina Sinis
Makundi mengine ya upinzani ya Kikurdi ya Iran yanasema yanafuatilia hali hiyo na kutathmini chaguzi mbalimbali.
Mustafa Hijri, kiongozi wa Chama cha Kidemokrasia cha Kurdistan ya Iran (KDPI), anasema jukumu lao ni "kusimamia Kurdistan ya Iran wakati wa kipindi cha mpito" na aliwataka wafuasi wake kujiepusha na mambo ambayo yanaweza kudhoofisha usalama.
Wakati huo huo, baadhi ya wapiganaji wa Kikurdi wanaelezea mashaka kuhusu usaidizi wa Marekani, ikiwa unaweza kutegemewa katika vita vyovyote vilivyo mbele yao.
Chanzo kinachowafahamu wapiganaji wa Kikurdi wa Iran kiliambia BBC, makundi ya upinzani yatapeleka vikosi vya ardhini ikiwa tu kuna uhakika wa kuungwa mkono na jeshi la anga la Marekani.
Anaamini jeshi la Iran linasalia kuwa imara na wapiganaji wa Kikurdi wanaweza kukabiliwa na matokeo "mabaya" ikiwa wataanzisha mashambulizi ya ardhini.
Kwa wapiganaji wanawake wa Kikosi cha Ulinzi cha Wanawake, wakati walioutamani kwa muda mrefu unakaribia.
Delal sasa ameondoka kwenye maeneo ya mafunzo na amejipanga karibu na mpaka. Ikiwa Wakurdi watajiunga na vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, hakuna njia ya kujua ni muda gani mapigano yanaweza kudumu, au matokeo yake yanaweza kuwa nini.















