'Bado tuko vitani': Wakurdi wa Syria wanapigana na Uturuki baada ya kupinduliwa Assad

- Author, Jiyar Gol
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Ili kufika kaskazini-mashariki mwa Siria, tunavuka daraja linaloelea juu ya Mto Tigri na basi dogo kutoka Kurdistan ya Iraq kupitia maeneo ya mafuta ya Syria.
Sehemu hii ya Syria inadhibitiwa na Wakurdi, wanaiita Rojava - maana yake Kurdistan ya magharibi. Tangu 2012, baada ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe, eneo hili lilijitangazia uhuru, na linalindwa na vikosi vinavyoongozwa na Wakurdi.
Lakini utawala wa Bashar al-Assad haukuwahi kuutambua uhuru huo. Hata baada ya utawala wake kuanguka kutoka madarakani, mustakabali wa eneo hili bado haujulikani.
Baada ya zaidi ya muongo mmoja wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, Wakurdi wa Syria wanakabiliwa na mzozo wa miaka mingi na jirani yake wa kaskazini, Uturuki - vita bado vinaendelea.
Mapambano dhidi ya IS

Chanzo cha picha, Getty Images
Muongo mmoja uliopita, kundi la Islamic State (IS) liliingia eneo hili, na kuteka miji na vijiji - hadi likafika katika jiji la Kobane, karibu na mpaka wa Uturuki, Septemba 2014.
Wanamgambo wa IS hawakufanikiwa kuingia katika jiji hilo, lakini waliweka mzingiro uliodumu kwa miezi kadhaa.
Makundi yanayoongozwa na Wakurdi, yakiungwa mkono na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani, yalivunja mzingiro huo mapema mwaka 2015. Mwezi Januari niliungana na wana mji, wakiadhimisha miaka kumi tangu kuvunja mzingiro huo.
Katika lango la kuingia Kobane, wanawake wenye umri wa miaka 50, wakiwa na bunduki za kivita aina ya AK-47, wanalinda vituo vya ukaguzi. Wanawake walihusika katika vita dhidi ya IS - walijitolea katika Vitengo vya Ulinzi vya Wanawake (YPJ).
Tunapoendesha gari kuzunguka jiji, makovu ya vita bado yanaonekana, kuna mabango ya picha za vijana wa kiume na wa kike waliopoteza maisha yao.
Lakini katika bustani kuu - wasichana na wavulana, waliovalia mavazi ya Kikurdi wanacheza wakiwa wameshikana mikono, wakiimba huku wakisherehekea.
Ingawa kwa watu wazima, ni wakati wa huzuni. "Jana usiku niliwasha mishumaa kwa ajili ya kaka yangu aliyeuawa shahidi na wengine waliouawa huko Kobane," anasema Newrouz Ahmad, mama wa watoto wanne mwenye umri wa miaka 45. "Ni siku ya furaha, lakini pia ni huzuni. Natamani angekuwa hapa kushuhudia."
Mgogoro na Uturuki

Jeshi la Syrian Democratic Forces (SDF) linaloongozwa na Wakurdi lilitangaza ushindi dhidi ya IS kaskazini-mashariki mwa Syria mwaka wa 2019. Lakini ushindi dhidi IS haujaleta amani ya kudumu.
Uturuki na muungano wa waasi wanaoungwa mkono na Uturuki wanaojulikana kama Jeshi la Kitaifa la Syria (SNA) wamefanya operesheni kadhaa za kijeshi dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na SDF tangu 2016, na kuteka eneo kubwa.
Uturuki inakihesabu kitengo kikubwa zaidi cha SDF - kiitwacho Kitengo cha Ulinzi wa Watu (YPG) – ambacho ni sehemu ya Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK), ambacho kinapigania uhuru wa Wakurdi nchini Uturuki kwa miongo kadhaa kuwa ni shirika la kigaidi. Nchi hiyo inataka kuwarudisha nyuma SDF mbali na mpaka wake.
Utawala wa Assad ulipoporomoka mwishoni mwa 2024, SNA inayoungwa mkono na Uturuki ilianzisha mashambulizi mapya ya kuteka eneo la magharibi mwa Mto Euphrates kutoka SDF.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sasa vita vimefika maeneo ya karibu na Kobane. Kamanda wa Kikurdi katika mji huo ananiambia: "Usichukue video hapa, tumejenga mahandaki chini ya jiji ili kujiandaa kwa mzingiro mwingine."
Katika jiji hili, harufu ya petroli imejaa hewani, na sauti za majenereta zinasikika kila mahali. Wenyeji wananiambia vituo vingi vya umeme, mitambo ya kusafisha mafuta na hata antena za mawasiliano – vimeharibiwa na mashambulizi ya anga ya Uturuki katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Newrouz Ahmad anasema "kwa kuwashinda IS huko Kobane ... hatutaruhusu Uturuki na washirika wake kuchukua mji wetu, tutawashinda pia."
Katika mkahawa, watu walipogundua kuwa sisi sio wenyeji, wanaamua kuja tulipo. Namuuliza mzee mwenye mvi na fimbo mikononi, ana umri gani. Namdhania kuwa ana miaka 80 hivi, lakini jibu alilonipa linanishangaza. "Nina miaka 60," anasema.
Ni wazi kwamba watu hapa wamechoshwa na vita, wameshuhudia vifo vingi na umwagaji damu. Na sasa tishio la vita vingine linakaribia.
Mashambulizi dhidi ya raia

Ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa Uturuki na ndege za kivita za Uturuki zimeshambulia maeneo ya SDF kuzunguka jiji hilo. Hata raia wanaoandamana wameshambuliwa.
Katika hospitali ya eneo hili, ninampata mmoja wa waliojeruhiwa - Lea Bunse, mwanaharakati wa amani kutoka Ujerumani mwenye umri wa miaka 28 ambaye amekuwa akijitolea katika makazi ya wanawake huko Rojava kwa zaidi ya miaka miwili.
Ananionyesha video ya shambulio kwenye maandamano ambayo anasema alishiriki mwezi Januari. Kanda hiyo inaonyesha makombora mawili yakidondoka kutoka angani na kugonga umati wa watu wanaocheza.
Maandamano hayo yalifanyika karibu na bwawa la Tishreen, ambapo mapigano yamekuwa yakiendelea. SDF inasema raia sita waliuawa, na makumi kujeruhiwa.
Pia kuna ripoti kuwa gari la wagonjwa lilishambuliwa. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limelaani shambulizi dhidi ya gari la wagonjwa la Hilali Nyekundu na kusema ni "uhalifu wa kivita" unaofanywa na Uturuki na SNA.
Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki iliiambia BBC kwamba "ripoti zinazodai kuwa Uturuki ilihusika katika mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu muhimu haziakisi ukweli" na kuongeza kuwa SDF huwapeleka raia katika "eneo lenye vita kwa makusudi" ili kuwatumia kama "ngao... ili wasipoteze udhibiti wa bwawa hilo."
Uturuki inaishutumu SDF kwa kutumia "vurugu na ugaidi" kutekeleza "ajenda yake ya kujitenga," kukiuka usitishaji mapigano na kuzuia timu za kiufundi kufika katika bwawa kwa ajili ya matengenezo.
Mtanziko wa Damascus

Kiongozi mpya wa Syria, Ahmad al-Sharaa yuko kwenye mtanziko. Rais huyo wa mpito - ambaye kundi lake la Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham (HTS), liliongoza mashambulizi ya waasi na kumpindua Assad - ameahidi kuunda serikali shirikishi huko Damascus, na ametaka makundi yote yenye silaha kuweka chini silaha zao. Mazungumzo na SDF yanaripotiwa kufanywa ili kutafuta suluhu kwa upande wa kaskazini-mashariki.
Lakini mazungumzo hayo na vikundi vya Wakurdi yanamweka Sharaa, katika hali ngumu na mshirika wake Uturuki.
Sharaa alipofungua mkutano wa mazungumzo ya kitaifa kuhusu mustakabali wa Syria siku ya Jumanne, eneo linalojitawala la Wakurdi halikushiriki – na limesema halijaalikwa.
Akizungumza na nami kutoka eneo la siri karibu na kambi ya Marekani katika mkoa wa Hassakeh kaskazini-mashariki mwa Syria, kamanda wa SDF Jenerali Mazloum Abdi ananiambia aliwahi kukutana na Sharaa huko Damascus.
Lakini pande hizo mbili bado hazijafikia makubaliano.
"Kwa kweli, bado tuko kwenye vita na Uturuki na washirika wake. Ndege za Uturuki na ndege zisizo na rubani zinaendelea kushambulia," anasema na kuongeza: "Huko Damascus, bado haijafahamika ni hatua gani serikali mpya itazichukua. Kauli zao ni nzuri, lakini wako chini ya shinikizo kutoka Uturuki kuchukua hatua dhidi ya maeneo ambayo tunayadhibiti.
"Lakini Marekani, Ufaransa, na baadhi ya mataifa ya Kiarabu yanaisukuma serikali mpya ya Syria kutambua haki za Wakurdi," anasema.
Kwa Marekani, wapiganaji wa SDF wamekuwa washirika wa kutegemewa katika vita dhidi ya IS. Mamia ya wanajeshi wa Marekani wamesalia katika maeneo yanayodhibitiwa na Wakurdi, kukabiliana na makundi ya IS.
Lakini Wakurdi wanahofia kwamba Rais Donald Trump anaweza kuwaondoa wanajeshi hao, na kuacha eneo hilo kuwa hatarini kwa operesheni ya kijeshi ya Uturuki, na uwezekano wa kuibuka tena IS.
Inakadiriwa kuwa bado kuna familia 40,000 za IS na wapiganaji 10,000 wa IS katika kambi na magereza yanayodhibitiwa na SDF kaskazini-mashariki, anasema Jenerali Abdi.
"Iwapo Uturuki itashambulia, hatutakuwa na budi ila kupeleka vikosi vyetu navyo kushambulia," anaonya. "Hilo litawapa IS fursa ya kushambulia magereza na kuwaachilia wapiganaji wake."
Mustakabali wenye mashaka

Kuna mashaka zaidi kwa wanawake ambao walipigana dhidi ya IS katika kikosi cha wanawake watupu cha YPJ.
Kuta za ofisi ya msemaji wa YPJ, Roksana Mohamed mwenye umri wa miaka 29 zimefunikwa na picha za makamanda wenzake wa kike waliouawa vitani.
"Hadi sasa, hatujaona majukumu yoyote yanayotolewa kwa wanawake katika uongozi mpya wa Damascus," anasema. "Kwanini mwanamke asiwe waziri wa ulinzi?"
Bi Mohamed anasema wanawake walipigania haki zao katika eneo hili. Wameshiriki kikamilifu katika kila nyanja ya maisha ya kisiasa, kijamii, na kijeshi.
"Ikiwa haki zetu haziheshimiwi, tunawezaje kutarajiwa kuweka chini silaha zetu?" anauliza.
Wakati wengine wakiamini kuwa utulivu nchini Syria uko karibu, kwa Wakurdi, mustakabali bado haueleweki. Je, watatambuliwa kama washirika katika Syria mpya, au watakabiliana na vita vingine?
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












