Pablo Escobar hadi "El Mencho": Je, enzi ya viongozi wa magenge ya dawa za kulevya imekwisha?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka za Mexico zimetangaza kifo cha Nemesio Oseguera Cervantes, anayejulikana kama "El Mencho," mmoja wa viongozi mashuhuri zaidi wa magenge ya dawa za kulevya nchini humo.
Kuuawa kwake kulizua ghasia na vurugu nchini Mexico, kuanzia shambulio la risasi katika uwanja wa ndege wa Guadalajara hadi vizuizi vya barabarani na moto uliowashwa na wafuasi wake.
Hii si mara ya kwanza kutangazwa kukamatwa au kuuawa kwa mtu mashuhuri katika ulimwengu wa biashara ya dawa za kulevya anayesakwa kimataifa, tangu Pablo Escobar maarufu wa Colombia alipopata umaarufu, kabla ya hadithi yake kumalizika kwa kifo chake mwaka 1993.
Kwa miongo kadhaa, Amerika Kusini imeshuhudia mapambano kati ya mamlaka za ndani na viongozi wa magenge ya biashara ya dawa za kulevya, viongozi wa magenge ambao wamejulikana kwa majina na sura zao na wamekuwa wakikimbia kwa miaka mingi.
Uhalifu huu haukuishia kwenye biashara ya dawa za kulevya pekee; pia ulihusisha mashambulizi ya risasi, mauaji, na ufyatuaji wa risasi kati ya magenge hasimu au kati ya magenge na vikosi vya usalama.
Vita dhidi ya dawa za kulevya au vita vya magenge ya madawa, katika nchi za Amerika Kusini vimesababisha vifo vya raia wengi.
Watu hawa waliokuwa wakisakwa wamekuwa chanzo cha msukumo kwa waandishi na watengenezaji wa filamu, ambao wameandika maisha yao katika filamu na makala zilizovutia watazamaji wengi, kama vile filamu Blow iliyowashirikisha Johnny Depp na Penélope Cruz, mfululizo wa Narcos kuhusu Escobar kwenye Netflix, pamoja na makala The Two Escobars, iliyozungumzia mapambano ya Colombia dhidi ya ulimwengu wa dawa za kulevya.
Amerika Kusini ni moja ya maeneo duniani yaliyoathiriwa zaidi na biashara ya dawa za kulevya na athari zake, hasa kutokana na biashara ya kokeini, ambayo hulimwa katika Bolivia, Colombia na Peru, huku Mexico ikiwa njia kuu ya kupitisha dawa za kulevya kuelekea Marekani, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayopambana na dawa za kulevya na uhalifu wa kimataifa.
Je, hali ya kuwepo kwa viongozi wa magenge ya dawa za kulevya itaisha baada ya kuuawa kwa Nemesio Oseguera Cervantes maarufu kama "El Mencho," mmoja wa viongozi wa mwisho mashuhuri wa magenge ya dawa za kulevya nchini Mexico, kufuatia kufungwa jela kwa Joaquín Guzmán anayejulikana kama "El Chapo," na Ismael Zambada García maarufu kama "El Mayo" nchini Marekani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pablo Escobar, jina linalotajwa mara nyingi zaidi katika filamu
Pablo Escobar anachukuliwa kuwa mtu maarufu zaidi katika ulimwengu wa biashara ya kokeini. Alizaliwa nchini Colombia mwaka 1949 na alianza shughuli zake zinazohusiana na dawa za kulevya katikati ya miaka ya 1970.
Encyclopaedia Britannica inaeleza kwamba alikuwa mmoja wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya wenye nguvu zaidi duniani katika miaka ya 1980.
Alianzisha na baadaye kuongoza Medellín Cartel, iliyopewa jina la mji wa Medellín nchini Colombia. Genge hilo lilidhibiti sehemu kubwa ya biashara ya kokeini nchini humo, jambo lililomwezesha Escobar kujilimbikizia utajiri mkubwa na kupata ushawishi ndani ya vyombo vya usalama na duru za kisiasa.
Ensaiklopidia hiyo pia inaeleza kwamba alionekana kama "Robin Hood" kwa sababu ya msaada wake kwa baadhi ya maskini katika maeneo aliyokuwa akifanya shughuli zake, licha ya shughuli zake za uhalifu wa umwagaji damu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Encyclopaedia Britannica inaeleza kuwa miongoni mwa waathirika wake walikuwa maafisa wa kisiasa na polisi, pamoja na raia waliouawa katika mlipuko wa bomu kwenye ndege ya abiria, ambapo genge la Pablo Escobar lilituhumiwa kuweka bomu ndani ya ndege hiyo ili kumlenga mtoa taarifa.
Escobar alikuwa akisakwa na kufuatiliwa na Marekani tangu mwishoni mwa miaka ya 1980. Alifungwa jela kwa mara ya kwanza mwaka 1974 kwa kosa la wizi.
Baadaye, mwaka 1991, alijisalimisha kwa masharti ya makubaliano maalum na kuingia gerezani, ambako aliweza kuendelea kuendesha biashara yake ya usafirishaji wa kokeini.
Mamlaka zilipoamua kumhamisha kwenda gereza jingine, alipanga kutoroka kabla ya uamuzi huo kutekelezwa.
Mapambano kati yake na genge pinzani kwa upande mmoja, na mamlaka kwa upande mwingine, yaliongezeka, na idadi kubwa ya watu waliangamia katika vita kati ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Mwaka 1993, siku moja baada ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, mamlaka za Colombia ziligundua maficho yake katika eneo la Medellín, zikavamia nyumba hiyo na kumuua Escobar pamoja na walinzi wake kadhaa katika operesheni hiyo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Joaquín Guzmán - El Chapo
Joaquín Guzmán, anayejulikana zaidi kama "El Chapo," alizaliwa katikati ya miaka ya 1950 katika jimbo la Sinaloa kaskazini mwa Mexico.
Shughuli zake za uhalifu zilianza katikati ya miaka ya 1980 ndani ya genge la Guadalajara, iliyoongozwa na Miguel Ángel Félix Gallardo.
Baadaye, El Chapo aliongoza genge la Sinaloa , ambalo likawa moja ya mashirika makubwa na yenye nguvu zaidi ya uhalifu mwishoni mwa karne ya 20, kulingana na Encyclopaedia Britannica.
Alisimamia uundaji wa mbinu za kisasa za usafirishaji wa dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na kuchimba visima kando ya mpaka wa Mexico na Marekani na kuficha dawa ndani ya mikebe ya pilipili au vifaa vya kuzima moto. Genge lake lilisafirisha kokeini, heroine, bangi, na methamphetamine.
Wizara ya sheria ya Marekani ilieleza kwamba genge aliloliongoza lilikuwa mojawapo ya magenge yanayofanya kazi zaidi, zenye vurugu nyingi, na zenye ushawishi mkubwa duniani.
Genge lake lilidhibiti kati ya asilimia 40 hadi 60 ya biashara ya dawa nchini Mexico, na faida zikiwa takribani dola bilioni tatu kwa mwaka.
Kadiri muda ulivyopita, "El Chapo" alikua mmoja wa wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya kuelekea Marekani, na alikuwa kwenye orodha ya watu matajiri duniani ya Forbes, akiwa nafasi ya 701 na utajiri wa takribani dola bilioni 1.
El Chapo alishtakiwa kwa kusafirisha mamia ya tani za kokeini kwenda Marekani.
Anasemekana kutumia wauaji wa kitaalamu kutekeleza mamia ya mauaji, utekaji nyara, na matukio ya mateso dhidi ya wapinzani wake. Wengi wa washirika wake wa karibu pia walishuhudia dhidi ya kiongozi wao wa zamani wakati wa kesi yake.
Alikamatwa kwa mara ya kwanza mwaka 1993, na kutoroka gerezani zaidi ya mara moja.
Mwaka 2016, mamlaka za Mexico walimkamata na kumhamisha kwendMarekani mwaka 2017.
Mwaka 2019, alihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kuhukumiwa kwa mashtaka dhidi yake akiwa na umri wa miaka 62.
Miguel Ángel Félix Gallardo - The Godfather
Akipewa jina la utani "The Boss of Bosses" au "The Godfather" (El Padrino), Miguel Ángel Félix Gallardo ni mmoja wa wafanyabiashara hatari zaidi wa dawa za kulevya nchini Mexico.
Mnamo miaka ya 1980, alianzisha na kuendesha shirika la kwanza kubwa la biashara ya dawa za kulevya nchini humo, Guadalajara Cartel, ambalo lililenga zaidi kwenye usambazaji kuliko uzalishaji.
Gallardo aliboresha mbinu za kisasa za usafirishaji wa dawa, akitengeneza njia za kusafirisha kokeini kutoka Amerika Kusini, kupitia Mexico hadi Marekani na Ulaya.
Alikuwa afisa wa kikosi cha polisi na alihudumu kama mlinzi wa Gavana wa Sinaloa, Leopoldo Sánchez, akitumia ushawishi wake, kulingana na taarifa ya The Guardian.
Alijulikana kwa kuepuka vitendo vya vurugu, lakini yeye na wanachama wa genge lake walituhumiwa kuwaua maafisa wa US Drug Enforcement Administration baada ya afisa mmoja kuingia kwa siri katika genge.
Alikamatwa mwaka 1989 na kupewa kifungo cha miaka arobaini gerezani. Kutoka ndani ya gereza, alijaribu kuendelea kuendesha biashara zake kwa utulivu, lakini baadaye Guadalajara iligawanyika katika matawi kadhaa.
Mnamo 2017, mfumo wa haki nchini Mexico uliamuru kifungo cha ziada dhidi yake, kuongeza miaka 25 kwenye kifungo chake gerezani baada ya kuhukumiwa kwa uhalifu mwingine kutoka wakati aliokuwa akiongoza genge.
Mnamo 2022, mahakama iliridhia uhamisho wake kwenda gereza lenye hatua za usalama zilizopunguzwa, kutokana na matatizo yake ya kiafya.
Amado Carrillo Fuentes - "Lord of the Heavens"
Amado Carrillo Fuentes alikuwa mmoja wa viongozi wa magenge wa dawa za kulevya wenye nguvu zaidi nchini Mexico katika miaka ya 1980 na 1990.
Amado alizaliwa katika jimbo la kaskazini la Sinaloa. Alikuwa mpwa wa mmoja wa waanzilishi wa genge Guadalajara, ambalo alijiunga nalo baada ya muda mfupi.
Carrillo Fuentes alijifunza kurusha ndege, na baadaye alitumia ujuzi wake wa ndege na njia za ndege kupanua shughuli zake za usafirishaji wa dawa kwa njia ya anga, jambo lililompatia jina lake la utani maarufu "God of the Heavens".
Alianza kwa kusafirisha bangi, lakini baadaye alihamia kusafirisha kokeini hasa kutoka Colombia kupitia Mexico hadi Marekani.
Alichukua udhibiti wa genge la Juárez baada ya kiongozi wake kuuuliwa. Alijitahidi kuepuka kuonekana mbele ya umma na mara chache alipigwa picha.
Mwaka 1997, alijiingiza katika hospitali nchini Mexico kwa jina bandia ili kufanyiwa upasuaji wa mapambo katika jaribio la kubadilisha sura yake na kuepuka kukamatwa.
Alifariki kutokana na operesheni iliyoshindikana ambayo pia ilihusisha upasuaji wa kuondoa mafuta mwilini (liposuction).
Mamlaka zilitoa picha za mwili wake kuharakisha uvumi kwamba bado alikuwa hai, lakini picha ya kutisha ya mwili wake ilichochea zaidi uvumi huo.
Miezi michache baadaye, miili ya madaktari waliotekeleza operesheni hiyo ilipatikana ikiwa na alama za mateso.
Ndugu yake alichukua uongozi wa wa genge baada ya kifo chake, lakini mamlaka za Mexico zilimkamata mwaka 2014.

Chanzo cha picha, Alamy
Griselda Blanco: The Godmother
Wanawake mashuhuri zaidi ambao majina yao yamejitokeza katika ulimwengu wa biashara ya kokeini kama viongozi au kama watu wa umaarufu ni wachache, lakini mmoja wa maarufu zaidi ni Griselda Blanco.
Blanco alizaliwa nchini Colombia mwaka 1943. Hadithi yake ilianza alipohamia Marekani mwaka 1964 akiwa na mwanawe mmoja tu na bila pesa. Ndipo ambapo uhusiano wake na ulimwengu wa dawa za kulevya ulianza, alipoweka kilo moja ya kokeini kwenye mizigo yake.
Blanco anachukuliwa kuwa mmoja wa waliokuwa na jukumu la kusafirisha kokeini kwenda Colombia katika miaka ya 1970 na 1980.
Alitumia wanawake kusafirisha na kusambaza kokeini kwa sababu walichukuliwa kuwa hawataamsha shaka.
Mfululizo wa filamu ya Netflix kuhusu maisha yake ulionesha jinsi wanawake walivyokuwa wanaweka pakiti za kokeini kwenye nguo zao za ndani kabla ya kusambazwa.
Alioana na muuzaji wa dawa za kulevya na kuishi naye New York, ambapo yeye na mume wake walianza biashara kubwa ya kokeini nchini Marekani. Baadaye alirudi Colombia ili kuepuka mashtaka ya biashara ya dawa za kulevya.
Alirudi Miami mwishoni mwa miaka ya 1970, na katika kipindi hiki ndipo alipojenga himaya yake na kujulikana kama "The Godmother".
Alikabiliwa na mashtaka kadhaa ya mauaji kwa kutumia wauaji wawili waliokuwa na silaha kwenye pikipiki. Alihama California mwaka 1984, ambapo alikamatwa na kupewa kifungo cha miaka 15 gerezani mwaka 1985.
Pia aliweza kuendelea na shughuli zake akiwa gerezani. Aliachwa huru mwaka 2004 na kurejeshwa nchini Colombia.
Mnamo 2012, alipokuwa akitoka dukani Medellín, Colombia, alipigwa risasi na kuuwawa na mtu aliyekuwa kwenye pikipiki.














