Sokwe 'wanajitibu' kwa dawa za mitishamba-Utafiti wagundua

Chanzo cha picha, Elodie Freymann
- Author, Victoria Gill
- Nafasi, Mwandishi wa sayansi, BBC News
Sokwe mwitu hula mimea ambayo ina uwezo wa kutuliza maumivu na kuzuia bakteria kujiponya, kulingana na wanasayansi.
Walielezea "kazi yao ya upelelezi" katika misitu ya Uganda - kuangalia wanyama ambao walionekana kujeruhiwa au wagonjwa ili kujua iwapo walikuwa wanajitibu kwa mimea.
Wakati mnyama aliyejeruhiwa alipotafuta kitu maalum kutoka kwa msitu cha kula, watafiti walikusanya sampuli za mmea huo na wakafanya vipimo. Mimea mingi iliyopimwa ilipatikana kuwa na nguvu za kupambana na bakteria.
Wanasayansi, ambao walichapisha matokeo yao katika jarida PLOS One, wanafikiri sokwe wanaweza kusaidia katika kutafuta dawa mpya za mitishamba .

Chanzo cha picha, Elodie Freymann
"Hatuwezi kupima kila kitu katika misitu hii kwa sifa zake za dawa, mtafiti mkuu Dk Elodie Freymann, kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, alisema. "Kwa hivyo kwa nini tusifanyie vipimo mimea ambayo tuna habari hii - mimea ambayo sokwe wanatafuta?"
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Dk Freymann ametumia miezi kadhaa kufuata na kutazama kwa makini jamii mbili za sokwe-mwitu katika Hifadhi ya Msitu Mkuu wa Budongo.
Pamoja na kutafuta dalili za maumivu - mnyama akichechemea au kuushika mwili wake kwa njia isiyo ya kawaida - yeye na wenzake walikusanya sampuli za kinyesi na mkojo ili kuangalia ugonjwa na maambukizi.
Walizidisha umakinifu wao wakati sokwe aliyejeruhiwa au mgonjwa alipotafuta kitu ambacho hawali kwa kawaida - kama vile magome ya mti au ngozi ya matunda.
"Tulikuwa tunatafuta dalili hizi za kitabia kwamba mimea inaweza kuwa dawa," Dk Freymann alielezea.
Alielezea sokwe mmoja - dume - ambaye alikuwa na mkono uliojeruhiwa vibaya.

Chanzo cha picha, Austen Deery
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Hakuwa akitumia mikono kutembea, alikuwa akichechemea," alikumbuka. Wakati wengine walikuwa wameketi kula, sokwe aliyejeruhiwa alijikongoja akitafuta feri(mmea). "Alikuwa sokwe pekee aliyetafuta na kula feri hizi."
Watafiti walikusanya na kuchambua mma huo (fern) - mmea unaoitwa Christella parasitica, ambao uliibuka kuwa sifa za kuzuia mlipuko wa maambukizi ya bakteria.
Kwa jumla, watafiti walikusanya sampuli 17 kutoka kwa aina 13 tofauti za mimea na kuzipeleka kufanyiwa majaribio na Dk Fabien Schultz, katika Chuo Kikuu cha Neubrandenburg cha Sayansi nchini Ujerumani.
Hiyo ilifichua kuwa karibu 90% ya mimea hiyo ilizuia ukuaji wa bakteria, na theluthi moja ilikuwa na sifa za asili za kuzuia ongezeko la maambukizi, ikimaanisha kuwa zinaweza kupunguza maumivu na kukuza uponyaji.
Sokwe wote waliojeruhiwa na wagonjwa walioripotiwa katika utafiti huu walipona kabisa, Dk Freymann alifurahi kuripoti. "Aliyekula feri alikuwa akitumia mkono wake tena ndani ya siku chache zilizofuata," alieleza.
"Bila shaka, hatuwezi kwa 100% kuthibitisha kwamba kesi yoyote kati ya hizi ni matokeo ya moja kwa moja ya kula rasilimali hizi," aliiambia BBC News.
"Lakini inatilia mkazo ujuzi wa kitiba unaoweza kupatikana kwa kuchunguza viumbe vingine porini na kusisitiza uhitaji wa haraka wa kuhifadhi misitu ambayo ni kama 'maduka ya dawa' kwa ajili ya vizazi vijavyo."

Chanzo cha picha, Austen Deery
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












