Je, Panenka huwa chaguo sahihi kwa penalti?

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika iliyojaa utata, Brahim Diaz wa Morocco alikosa penalti, baada ya dakika 17 za kusimama kwa mpira kuelekea kipenga cha mwisho.
Mshambuliaji huyo wa Real Madrid alipunguza mwendo alipokaribia mpira na kuupiga katikati ya goli lakini kipa Edouard Mendy wa Senegal hakuruka pembeni, aliudaka mpira na mchezo ukaendelea hadi muda wa ziada na Senegal ikaibuka na ushindi.
Ilikuwa siku mbaya kwa Diaz, aliyeonekana na huzuni alipokabidhiwa kiatu cha dhahabu kama mfungaji bora wa mashindano hayo na rais wa Fifa, Gianni Infantino mwishoni mwa mchezo.
Sio mara ya kwanza kwa mchezaji kukosa goli kwa kupiga penalti katikati ya goli, penalti inayoitwa Panenka.
Penalti kama hiyo ya Enzo le Fee wa Sunderland ilinaswa na Caoimhin Kelleher katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Brentford mapema Januari.
Je, kupiga penalti katikati ya goli ndio chaguo baya zaidi kwa mkwaju wa penalti?
Penalti ya Panenka ilitoka wapi?
Panenka ni jina kutoka kwa Antonin Panenka, ambaye alipiga penalti katikati ya goli na kushinda Mashindano ya Ulaya ya 1976 kwa timu yake Czechoslovakia.
Mchezo dhidi ya mabingwa watetezi Ujerumani Magharibi ulimalizika kwa sare ya 2-2 baada ya muda wa ziada huko Yugoslavia, huku mikwaju ya penalti ikiamua mshindi.
Haikuwa mara ya kwanza Panenka kujaribu penalti kama hiyo. Aliifungia timu yake ya Bohemians bao dhidi ya mpinzani wao wa ndani Dukla Prague kwa njia kama hiyo mwezi mmoja uliopita.
Lakini kushinda Ulaya, ndio uliipa umaarufu mbinu hiyo ya upigaji penalti na jina Panenka likazaliwa.
Wachezaji maarufu

Chanzo cha picha, GettyImages
Miaka 50 tangu Panenka alipoleta penalti ya aina hiyo, umaarufu wake umeongezeka.
Wachezaji kadhaa, wakiwemo Lionel Messi, Thierry Henry na Francesco Totti, wamefanikiwa kutumia mbinu hiyo kushinda penalti zao.
Gwiji wa Ufaransa Zinedine Zidane anaaminika ndiye mpigaji wa penalti ya aina hiyo ikiwa na kasi ndogo sana, katika fainali ya Kombe la Dunia ya 2006 kwani penalti yake ilivuka tu mstari.
Lakini licha ya mafanikio yote, Diaz si mchezaji wa kwanza maarufu kukosa.
Mwaka 1992, Gary Lineker alipata nafasi ya kufikia mabao 49 ya Sir Bobby Charlton wa England katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Brazil lakini alishindwa kufunga bao lake la Panenka na kuishia kuwa chini ya rekodi ya wakati huo.
Mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero, kwa kawaida alikuwa hodari kwenye penalti lakini alikosa alipojaribu kufunga Panenka Mei 2021 huku Chelsea ikishinda 2-1 baada ya penalti kuokolewa na Edouard Mendy.
Takwimu zinasemaje?
Hakuna shaka kwamba mchezaji akikosa Panenka, ukosoaji unaonekana kuwa mkali zaidi kuliko kama angepiga kwa nguvu zaidi kuelekea kwenye kona ya goli.
"Utawafanya watu walalamike kwa sababu wanaona ni kitu tofauti," mshambuliaji wa zamani wa Bristol City na Swansea, Lee Trundle, aliambia BBC Sport.
"Mawazo yangu ni kwamba panenka ni njia pia ya kufunga penalti," anasema.
"Kama ukipiga kushoto au kulia na kipa akapiga mbizi na na akaiokoa, ndivyo hutokea pia kwa Panenka na akabaki katikati na kuiokoa."
"Ikiwa utashinda basi kila mtu atasema jinsi ilivyo nzuri."
Takwimu zinaonyesha 84% ya penalti kama hizo kwenye Kombe la Dunia (tangu 1966) na Euro (tangu 1980) zimeingia kwenye wavu. Ukilinganisha na 78% zinazokwenda kushoto na 74% zinazokwenda kulia.
Mawazo ya Diaz alidhani Mendy angepiga mbizi. Hata hivyo, Mendy aliomuona Diaz na akabaki pale alipo.















