'Nataka kuuonyesha ulimwengu Afrika: Nyota wa YouTube aleta furaha na machozi kwenye ziara yake

Chanzo cha picha, Wizara ya Utalii Eswatini
Mmoja wa waundaji wa maudhui maarufu zaidi duniani amekuwa akivutia umati mkubwa, wengi wao wakiwa mashabiki wake wachanga, katika ziara yake katika mataifa 20 barani Afrika, bara ambalo anasema "limejaa mambo ya kustaajabisha."
Wavulana wa umri wa chini ya miaka 19 nchini Rwanda na Ethiopia walilia kwa furaha walipokuwa wakimkumbatia shujaa wao wa mtandaoni katika maisha halisi.
IShowSpeed au Speed , kwa sasa ana wanachama milioni 48 YouTube. Anajulikana kwa matangazo yake ya moja yasiyo na maandalizi maalumu ambayo hudumu kuanzia saa tatu hadi 11.
Wamarekani wenye asili ya Afrika pia wameguswa kuona upendo na heshima ikionyeshwa kwa mwenzao, ambaye atatimiza miaka 21 wakati wa ziara yake ya "Speed Does Africa."
Speed, ambaye jina lake halisi ni Darren Watkins Jr, alifurahishwa na mwitikio wa watu nchini Angola.
"Kaka, sitasema uongo," alisema kuwaambia watazamani wake mubashara. "Napenda upendo wa barani Afrika. Shauku hapa ni ya ajabu."
Katika kipindi cha siku 28, yeye na timu yake ya watu wa kurekodi, usalama na usafirishaji wanapanga kutembelea nchi 20 barani Afrika, ikiwa ni pamoja na Nigeria, Ivory Coast, Liberia na Ghana.
Anapanga kuona mandhari, kujifunza historia, kuchunguza maisha ya kila siku, utamaduni na chakula, kufanya michezo, kukutana na mashabiki na, kukutana na baadhi ya mawaziri wa utalii - na kwa ujumla kuzungumza na yeyote anayekutana naye njiani.
"Nataka kuonyesha ulimwengu jinsi Afrika ilivyo," Speed alisema wakati akiwa Afrika Kusini - ambapo alijifunza baadhi ya miondoko ya densi ya amapiano, kucheza na gari na kumuona duma.
Mashabiki wake

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Speed alianza kama mchezaji wa gemu, na akawa maarufu sana mwaka 2022, kabla ya kuhamia kwenye maudhui halisi na ya mpira wa miguu.
Kuinuka kwake hakukuwa bila utata.
Amepigwa marufuku kabisa kushiriki mashindano yote ya mtandaoni ya Riot Games baada ya kumkashifu mchezaji wa kike. Aliomba msamaha na kukubali kwamba alikuwa amekosea.
Pia aliwahi kupigwa marufuku YouTube kwa wiki moja kwa kumruhusu mhusika wake wa mchezo wagemu kushiriki katika shughuli za ngono mbele ya watazamaji.
Speed amejenga chapa yake na utu wake mtandaoni kwa kutumia video za moja kwa moja, kelele na wakati mwingine ukali.
Mbali na kubweka, sarakasi, riadha, vituko - kama vile kuruka juu ya magari yanayotembea – na mapenzi yake kwa shujaa wa mpira wa miguu Cristiano Ronaldo.
Vijana wanapenda maudhui yake ya moja kwa moja.
"Ninafurahia sana aina ya shauku aliyonayo na mambo anayofanya," shabiki wa Zambia Chinyama Yonga aliambia BBC.
"Hata mayowe anayopiga," anacheka kijana huyo wa miaka 16, ambaye alipigwa na mvua kubwa ili kumshuhudia Speed.
Nchini Zambia, Speed aliingia kwenye Dimbwi la Devil's kwenye ukingo wa Mosi-oa-Tunya, au maporomoko ya Victoria, na akaimba muziki wa mwanzilishi wa muziki wa hip-hop kutoka Zambia, Slapdee.
Pia alinyoa nywele kwa kinyozi mmoja katika mji mkuu, Lusaka - jambo lililowafurahisha maelfu ya watu waliomiminika hapo huku habari zikienea kwenye mitandao ya kijamii.
"Ni mcheshi sana; ni mzuri sana katika kupiga ngema na ni mkarimu sana. Anatoa pesa na anajitahidi kuwasaidia watu walio katika matatizo," anasema Henry Dale, ambaye ana umri wa miaka 11, na anasoma Uingereza.
Nilitazama kipindi cha moja kwa moja cha takriban saa nne huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, na nilivutiwa zaidi na mikutano na shughuli ambazo wakati mwingine zilikuwa na watu wengi.
Huko Ethiopia Speed, akiwa amevalia kaptura na shati lake alikwenda Merkato, soko kuu la jiji, kisha alikwenda hadi Jumba la Makumbusho la Sayansi la Ethiopia, hadi kwenye Ukumbusho wa Ushindi wa Adwa, ambapo alitembea bila viatu kuwaenzi wapiganaji wa Ethiopia walioshinda vikosi vya Italia mwaka 1896.
Alipogundua kwamba nchi inatumia kalenda yake ya Ge'ez, alisema kwa mshangao: "Subiri! Ni... 2018. Nina umri wa miaka 13? Ronaldo bado yuko Real Madrid?"
Speed pia alicheza na wachezaji wa dansi wa kitamaduni, wanaojulikana kwa "eskista" ambao huchezesha mabega.
Hakuna bila changamoto

Chanzo cha picha, Getty Images
Matembezi makubwa ya Speed hayajakosa ajali, kama ilivyo katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare.
Wakati Miss Universe Zimbabwe alipotoka kumlaki, malkia huyo wa urembo alikosa kumuona kwa bahati mbaya katika vurugu la watu.
Baadhi ya mashabiki walikimbilia kukumbatiana na kupiga picha na timu ya ulinzi ya Speed iliwazuia.
Na Speed alikatiza wakati wa pekee wa kusherehekea huko Addis Ababa alipokuwa akitembelea kaburi la Mfalme Haile Selassie - kwa sababu ya muunganisho wa intaneti kuchelewa.
Je, ziara kama hiyo inaweza kubadilisha mitazamo ya watu na kuchochea masimulizi ya kimataifa juu ya bara la Afrika?
Ni mwanzo, alisema Samba Yonga, mama wa kijana wa Zambia Chinyama.
"Speed ameamsha dira ya ndani kwa vijana wengi - kote ughaibuni na barani - ambao wamekuwa wakitafuta kimya fahari na utambulisho wao."















