Kwanini watu mashuhuri wanakumbatia kudungwa manii ya samaki usoni?

.
Muda wa kusoma: Dakika 4

Katika miaka yangu mingi kama mwandishi wa habari, sikuwahi kufikiria ningekuwa nikiuliza mtu jinsi inavyohisi kudungwa manii ya samaki usoni mwake.

Abby Warnes amelazwa juu ya kiti kikubwa cheusi kilicho na matakia katika kliniki ndogo ya urembo kusini mwa Manchester.

Anasisimka huku sindano iliyopo kwenye bomba dogo ikiingizwa kwenye shavu lake kwa ustadi.

"Ouch. Lo," anasema akiashiria maumivu.

Ninapaswa kueleza wazi kwamba Abby mwenye umri wa miaka 29 hapati dozi kamili ya manii.

Sehemu ya chini ya uso wake inadungwa vipande vidogo vya DNA, vinavyojulikana kama polynucleotides, ambavyo vimetolewa kwenye samaki au mbegu za samaki Salmoni.

Kwa nini? cha kushangaza ni kwamba DNA yetu ni sawa na ile ya samaki.

Kwa hivyo tumaini ni kwamba mwili wa Abby hautakaribisha tu nyuzi hizi ndogo za chembechembe ya samaki, seli za ngozi yake zitachochewa kufanya kazi, na kutoa kolagini zaidi na elastini, protini mbili ambazo ni muhimu kwa kudumisha uadilifu wa muundo wa ngozi yetu.

Kwa Abby, lengo ni kufanya ngozi yake kuwa nzuri, kuifanya iwe na muonekano wa kuvutia, na tunatumaini la kutibu chunusi ambazo ameishi nazo kwa miaka mingi, kupunguza makovu na uwekundu.

"Nataka tu kutatua matatizo hayo ya ngozi niliyonayo," Abby anaeleza.

.
Maelezo ya picha, Abby anachomwa sindano kwenye sehemu ya chini ya uso wake ili kumsaidia ngozi yake kukabiliana na "matatizo" ya chunusi aliyonayo.

Matibabu ya 'polynucleotides', tiba ya ngozi kwa kutumia vipande vya DNA ndiyo yaliokwenye gumzo kwa sasa kama "muujiza" na inaendelea kupata umaarufu baada ya watu mashuhuri kuzungumza waziwazi juu ya wao "kudungwa manii ya salmoni".

Mapema mwaka huu, Charli XCX aliwaambia wafuasi wake milioni tisa wa Instagram kwamba anahisi tiba ya kutiwa "vichuji imepitwa na wakati kwa sasa", na kueleza kuwa amehamia kwenye polynucleotides, ambayo "ni kama vitamini za ndani kabisa".

Kim na Khloe Kardashian pia wanaripotiwa kuwa mashabiki wa hili. Na alipoulizwa kuhusu utaratibu wake wa kutunza ngozi kwenye kipindi cha hivi majuzi cha Jimmy Kimmel Live, Jennifer Aniston alijibu: "Jamani, kwani sina ngozi inayovutia ya salmoni?"

,

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock

Maelezo ya picha, Charli XCX anasema anatumia tiba ya 'polynucleotides' ambayo ni "vitamini vinavyoingizwa kwenye ngozi kwa kudungwa sindano.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Swali ni je, licha ya mwanzo wao wenye mashaka, je, tiba ya 'polynucleotides' ni kweli hubadilisha utunzaji wa ngozi?

Suzanne Mansfield, ambaye anafanya kazi katika kampuni ya urembo ya Dermafocus, anasema.

Hayo ni marejeleo ya filamu ya 2008 ya 'The Curious Case of Benjamin Button', ambapo Brad Pitt anaigiza kama mwanamume anayerudi nyuma kiumri. Alipofikia umri wake wa baadaye, alikuwa na ngozi kama ya mtoto.

Ingawa matokeo kama hayo huenda yasipatikane kwa kiasi kikubwa na linaweza kuwa suala la kutatanisha mno, Bi Mansfield anasema 'polynucleotides' inatengeneza njia linapokuja suala la utunzaji wa ngozi na kuifanya kuwa ya kuvutia.

Kikundi kidogo lakini kinachoendelea kufanya utafiti na majaribio ya kimatibabu kinapendekeza kuwa matibabu ya 'polynucleotidi' yanaweza kufanya ngozi kung'aa, sio tu kuifanya kuwa na afya njema lakini pia kunaweza kupunguza muonekano wa mishipa midogo midogo, mikunjo na makovu.

"Yote tunayofanya, kwa kutumia mbinu hii katika tasnia ya urembo," anasema, "ni kuimarisha kitu ambacho mwili tayari unafanya. Ndio maana matibabu haya ni ya kipekee."

Lakini pia urembo huu unafanyika kwa kugharamika kidogo.

Kipindi kimoja cha sindano za 'polynucleotide' kinaweza kugharimu popote pale duniani kutoka £200 hadi £500 - na inashauriwa upate angalau sindano tatu kwa wiki kadhaa.

Baada ya kupata tiba ya kwanza, kliniki huwa inakushauri kupata sindano kila baada ya miezi sita hadi tisa ili kudumisha mwonekano.

Lakini tukirudi kwenye kliniki, matibabu ya Abby karibu yanamalizika.

"Imebaki hatua moja tu," Helena Dunk, muuguzi wa urembo anayemiliki kliniki, Skin HD, anamhakikishia.

Anasema matibabu ya 'polynucleotides' yameongezeka kwa kiasi kikubwa hasa katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.

"Nusu ya wateja wangu wanaona tofauti kubwa - ngozi yao inahisi kuwa na maji zaidi, yenye afya zaidi na imekuwa changa - wakati nusu nyingine haioni mabadiliko makubwa kama hayo. Lakini ngozi zao huwa na hisia za kuwa imara na mpya."

Abby tayari amedungwa eneo la chini ya macho yake kama sehemu ya matibabu ya awamu tatu katika kliniki - na amefurahishwa sana na matokeo.

Alidungwa sindano nyingi ndogo za 'polynucleotides', ambayo ilikuwa "utaratibu wenye uchungu sana", lakini anasema ilisaidia kupunguza weusi chini ya macho yake.

.

Chanzo cha picha, Charlotte Bickley

Ingawa idadi inayoongezeka ya tafiti inaichukulia kama matibabu salama na yenye ufanisi, bado ni mpya na baadhi ya wataalam wanaonya kwamba kuendelea kwake huenda kukawa kwa kasi zaidi kuliko sayansi.

Mtaalamu mshauri wa magonjwa ya ngozi Dk John Pagliaro, aliyeko Brisbane, Australia, anasema kwamba ingawa tunajua kuwa nyukleotidi zina jukumu muhimu katika miili yetu - ndizo nyenzo za ujenzi wa DNA yetu kwa mwanzo - anahoji ikiwa "kudunga sindano zenye DNA ya salmoni iliyokatwa vipande vidogo vidogo" kwenye nyuso zetu kutafanya kazi pamoja na nyukleotidi zetu wenyewe.

"Hatuna data nzuri, yenye nguvu," anasema. "Kama mtaalamu wa matibabu, ningetaka kufuatilia angalau miaka michache zaidi ya tafiti kubwa, za kuaminika zinazoonyesha usalama na ufanisi kabla sijaanza kuitumia katika kazi yangu. Ukweli ni kwamba bado hatujafikia hitimisho."

Charlotte Bickley anaelezea ujio wake katika ulimwengu wa 'polynucleotides' kama "mwanzo mbaya" kwake.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 31 kutoka New York alifanyiwa matibabu hayo mwaka jana muda mfupi kabla ya "harusi yake".

Lakini Charlotte aliishia na maambukizi ya ngozi, kuvimba na weusi kwenye sehemu za chini ya macho yake kuliko kabla ya kupata matibabu.

"Nilipata kinyume kabisa cha kile nilichotaka," anasema. "Nilimwamini daktari huyo, lakini ameniacha na kovu."

Charlotte anaamini kuwa alidungwa kwa undani sana chini ya macho yake, na kusababisha matokeo hasi. Kunaweza kuwa na madhara - kama vile uwekundu, uvimbe na michubuko lakini haya huwa ni ya muda.

Katika baadhi ya matukio, watu wanaweza kuwa na athari ya mzio, au, ikiwa 'polynucleotidi' haijadungwa vizuri, kuna hatari za muda mrefu, kama vile rangi ya ngozi na maambukizi.

"Ninaendelea kufikiria, 'Kwa nini nilifanyiwa matibabu haya?'" Charlotte anasema. "Wakati kitu kitaenda vibaya usoni mwangu mimi hujua tiba hii ndio chanzo."

Amelipa maelfu ya pesa za matibabu ili kujaribu kurekebisha hali hiyo, lakini miezi 10 baadaye, bado kuna makovu chini ya macho yake.

"Sina sababu ya kudungwa DNA ya salmoni kwenye uso wangu tena," Charlotte anasema, "milele."