Je, unaweza kumzuia mtoto wako kutumia mitandao ya kijamii?

Chanzo cha picha, BBC/Jessica Hromas
- Author, Tiffany Turnbull
- Nafasi, BBC Sydney
- Muda wa kusoma: Dakika 9
Ilimchukua msichana anayeitwa Isobel, 13, chini ya dakika tano tu kukwepa kanuni za marufuku mpya ambayo Australia inapanga kuziweka ili kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto.
Msichana huyo alikuwa amepokea arifa kwenye simu yake kutoka kwa Snapchat, mojawapo ya majukwaa ambayo yamepigwa marufuku, ikimuonya kwamba akaunti yake itafutwa kutoka kwa huduma hiyo itakapoanza kutumika wiki hii, isipokuwa kama athibitishe kuwa ana umri wa zaidi ya miaka kumi na sita.
Isobel anasema: "Nilileta picha ya mama yangu na kuiweka mbele ya kamera, na mfumo huo uliniruhusu kuendelea na shughuli yangu, ukisema: 'Asante kwa kuthibitisha umri wako.'
Anaongeza: "Nilisikia kwamba mtu fulani alitumia uso wa Beyoncé (mwimbaji) ."
Isobel anaendelea: "Nilimtumia ujumbe mama yangu, Mel, na kusema: 'Hujambo Mama, nimekwepa marufuku ya mitandao ya kijamii,' na mama yangu akajibu: 'Wewe ni mtukutu.'
Mama Mill anasema ilimchekesha, na kuongeza: "Hivi ndivyo nilivyotarajia kutokea."
Ingawa alimruhusu Isobel kutumia TikTok na Snapchat chini ya uangalizi mkali akipendelea zaidi binti yake kutumia programu hizo kwa siri mama huyo alitumaini kwamba marufuku hiyo, kama wazazi walivyoambiwa, ingesaidia kuwalinda watoto dhidi ya hatari za mtandao ya kijamii.
Hata hivyo, matumaini hayo yalififia baada ya wataalamu kadhaa, pamoja na watoto wenyewe kuanza kutilia shaka ufanisi na usalama wa sheria hii, ambayo inafuatiliwa kwa karibu duniani kote na kusababisha wasiwasi miongoni mwa baadhi ya makampuni yenye ushawishi mkubwa.
Kuna wasiwasi kuhusu kutegemewa kwa teknolojia itakayotumika kutekeleza marufuku hiyo, pamoja na wasiwasi kwamba utekelezaji wa sheria unaweza kuwatenga watoto walio hatarini zaidi na kuwasukuma wengine katika maeneo hatari na yasiyodhibitiwa sana kwenye mtandao.
Swali linaloulizwa kwa wasiwasi bungeni, miongoni mwa raia kote nchini Australia, na katika mabaraza ya makampuni ya teknolojia duniani kote ni:
Je, kweli sheria hii itafanikiwa?
"Wazazi wanajali sana usalama wa watoto mtandaoni."

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika Australia, ni wachache wanaoamini kuwa makampuni ya mitandao ya kijamii yanachukua hatua za kutosha kuwalinda watumiaji, hasa watoto. Kauli zao za kujitetea huonekana kutokuwa na uzito.
Danny Elachi, baba wa watoto watano na mtetezi wa kudhibiti matumizi ya simu janja, aliambia BBC: "Hatuna imani kwamba makampuni ya teknolojia yanafanya chochote zaidi ya kutetea faida zao."
Anaongeza kuwa kampuni zimepewa nafasi nyingi kuthibitisha kujali usalama wa watoto, lakini "zimeshindwa katika kila jaribio."
Emma Mason, wakili na mama ambaye binti yake wa miaka 15 alijiua kutokana na unyanyasaji mtandaoni, alilihoji suala hili katika Umoja wa Mataifa: "Wasichana wangapi zaidi kama Tilly watajitoa uhai?"
Danny na Emma na wazazi wengine waliongoza kampeni kubwa ya kitaifa kutaka kuwekwa umri wa chini wa kutumia mitandao ya kijamii.
Ingawa wataalamu kadhaa, akiwemo Mkuu wa Usalama Mtandaoni nchini Australia, walisema marufuku si suluhisho bora, shinikizo la wazazi na mazingira ya kisiasa yaliipa sheria hiyo nguvu.
Mnamo Novemba 2024, Waziri Mkuu Anthony Albanese alitangaza sheria hiyo mpya akisema hakuna mzazi wala mtoto atakayeadhibiwa endapo atakiuka masharti.
Kwa mujibu wa sheria, majukwaa ya mitandao yatatakiwa kuchukua "hatua zinazofaa" kuhakikisha watumiaji wana umri wa angalau miaka 16, vinginevyo yakabiliwe na faini kubwa inayoweza kufikia dola milioni 49.5 za Australia.
Albanese alisema: "Hatua hiyo inalenga mama na baba, ambao, kama mimi, wanajali sana usalama wa watoto wetu kwenye mtandao."
Wanaounga mkono sheria hiyo , ambayo baadhi ya mamlaka nyingine duniani kote zimetaka kutekeleza katika matoleo machache na yenye ufanisi mdogo, itasaidia kuwalinda watoto dhidi ya kanuni zinazowasukuma kutazama maudhui hatari kama vile vurugu, ponografia na habari zisizo sahihi.
Pia itafanya kazi ili kupunguza unyanyasaji wa mtandaoni na unyanyasaji wa watoto kwenye mtandao, na itawahimiza kutumia muda nje ya nyumba, na pia kuboresha usingizi wao na kutunza afya zao za kimwili na kiakili.
Lakini kilichokuwa kinakosekana katika tangazo la Albanese ni mpango wa kina unaoeleza jinsi serikali ingetekeleza sheria hii, kwani ilijipa mwaka mmoja kuweka maelezo muhimu.
Serikali ya Australia ilipitisha muswada kwa haraka, ikitoa chini ya saa 48 kwa umma kuwasilisha maoni yao kuhusu sheria hiyo.
Je, serikali ya Australia inataekeleza vipi sheria hiyo?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka mmoja baadaye, siku chache kabla ya sheria kuanza kufanya kazi rasmi, maswali muhimu bado hayajajibiwa.
Jaribio lililofanywa na serikali chini ya sekta ya tasnia lilionyesha kuwa mbinu za kuthibitisha umri zinawezekana kiteknolojia, lakini hakuna yenye uhakika kamili.
Uthibitishaji kwa kutumia nyaraka rasmi kutambua umri wa mtumiaji wa mtandao ndio mbinu sahihi zaidi, lakini inawataka watumiaji kutoa taarifa nyeti jambo ambalo wengi hawalikubali kutokana na kutokuamini makampuni ya mitandao.
Teknolojia ya utambuzi wa sura na uchanganuzi wa mienendo mtandaoni pia haikuwa sahihi vya kutosha, hasa kwa vijana walioko karibu na umri wa miaka 16.
Hata makampuni kama Meta na Snapchat, ambayo tayari hutumia teknolojia hizi, yamekiri kuwa kuna changamoto kubwa.
Tony Allen, mkuu wa Mpango wa Uidhinishaji wa Umri wa Uingereza na mkurugenzi wa kesi hiyo, alisema: "Unapoingia kwenye duka la pombe na wakakutazama juu na chini na kusema, 'Um, hatuna uhakika kabisa,' na kukuuliza uonyeshe kitambulisho chako, ni sawa."
Lakini jaribio hilo nalo limekosolewa kwa upendeleo na kupuuzia mbinu ambazo vijana hutumia kukwepa vizingiti.
Matokeo ya jaribio hilo hayakuwa na utata, kwani wajumbe wawili wa zamani wa bodi ya ushauri waliikosoa kwa upendeleo na kile walichokiita "uchafuzi wa faragha." Ingawa jaribio lilizingatia mbinu ambazo vijana wanaweza kutumia kukwepa vizuizi, halikujaribu mbinu hizi.
Ushauri ulienea katika mitandao ya kijamii, kuanzia kujiandikisha kwa kutumia anwani ya barua pepe ya mzazi na kubadili mifumo ambayo haijatajwa waziwazi kwenye orodha ya serikali, hadi kutumia mitandao pepe ya faragha (VPNs) inayoweza kuficha eneo la mtumiaji.
Ongezeko la muda la matumizi ya mitandao ya kibinafsi pia ilirekodiwa nchini Uingereza baada ya hatua kali za uthibitishaji wa umri kutekelezwa kabla ya kutazama maudhui ya ponografia mapema mwaka huu, na wataalam wanatarajia jambo kama hilo kutokea hapa.
Kura ya maoni ya serikali mwezi Mei ilionyesha kwamba thuluthi moja ya wazazi wananuia kuwasaidia watoto wao kuepuka marufuku, na jaribio la Chuo Kikuu cha Melbourne lilionyesha kuwa barakoa ya Halloween yenye thamani ya $22 ilitosha kupita teknolojia ya utambuzi wa uso katika baadhi ya matukio.
Watetezi wa teknolojia za uthibitishaji wa umri wanasema kwamba teknolojia inayohitajika kuzuia kukwepa marufuku inapatikana, na kwamba kutumia picha ya mtu mwingine, kama Isobel alivyofanya, hakufai kudanganya mifumo hii.
BBC iliwasiliana na Snapchat ili kuuliza kuhusu suala hilo, na msemaji wa kampuni hiyo alieleza kuwa mara kwa mara wameelezea wasiwasi wao kuhusu "changamoto za kiufundi" zinazohusiana na kutekeleza marufuku hiyo, akibainisha kuwa "hii ni mojawapo ya changamoto hizo."
Luke Delaney, mkurugenzi mtendaji wa K-ID, ambayo inahusika na uthibitishaji wa umri, aliongeza kwa niaba ya Snapchat: "Ni vita vya mara kwa mara kuhakikisha kwamba hatua za kuzuia zinatengenezwa, halisi kila siku."

Chanzo cha picha, BBC/Jessica Hromas
Isobel, anayejivunia uzoefu wake a kukwepa marufuku ya kutumia mitandao miongoni mwa watoto, anasema ana uhakika karibu kwamba marufuku hiyo haitafanikiwa.
Aliongeza: "Mimi si mraibu wa skrini, lakini nadhani wazo la Anthony Albanese kuhusu kupata watoto nje haliwezekani," akirejelea maoni ya Waziri Mkuu kuhusu shughuli za kucheza nje za watoto.
Aliendelea: "Ikiwa nitapigwa marufuku, nitapata programu nyingine ya kutumia."
Mama yake, Mel, anaeleza kuwa suala hili linajadiliwa, lakini anawaunga mkono wengine wanaohofia kwamba majukwaa na chombo cha udhibiti kitakuwa kwenye mzozo wa mara kwa mara wa "paka na panya", kubaini mianya na kuziba moja baada ya nyingine, na kuorodhesha majukwaa yanayoibuka ili watoto wahamie majukwaa mengine.
Wataalamu wanasema kampuni za mitandao huenda zikapunguza kwa makusudi nguvu za sheria ili nchi nyingine zisifuate mkondo huo.
"Watajaribu kudukua," anasema Steven Schiller, mkurugenzi wa Facebook wa Australia na New Zealand kati ya 2013 na 2017.
Aliongeza: "Ni kama kuwauliza watoto wako kufanya kazi kama kupakia mashine ya kuosha vyombo. Wataifanya, lakini si kwa ufanisi, na hawataifanya kwa tabasamu."
Zaidi ya hapo, vigawanyo vya sheria kama "hatua zinazofaa" vinaacha mianya ya kufasiriwa upya.
Steven Schiller, aliyewahi kuwa mkurugenzi wa Facebook Australia na New Zealand, anasema kuwa kutoza faini sio kichocheo kikubwa cha kufuata sheria, kwani Facebook, kwa mfano, inapata kiasi hiki kimataifa kwa chini ya saa mbili: " faini ni "kama tiketi ya maegesho".
Wakati huohuo, vijana wawili tayari wamefikisha kesi mahakamani wakidai sheria hiyo inakiuka katiba, huku Alphabet (Google/YouTube) ikionekana kufikiria kufungua kesi yake.
Licha ya msisitizo wa serikali kwamba kampuni za mitandao ya kijamii zina rasilimali za kifedha na kiufundi kutekeleza marufuku hiyo, wakati huo huo imejaribu kupunguza matarajio ya umma.
Waziri wa Mawasiliano Annika Wells alisema: "Inaweza kuonekana kuwa na fujo kidogo wakati wa utekelezaji; mageuzi makubwa huwa hivyo."
Allen anasema swali la msingi sio kama watoto wataweza kukwepa marufuku hiyo, jibu la hilo ni ndiyo - lakini kama inatosha wao itafanya juhudi kufanya hivyo.
Anaongeza: "Ili sheria ifanikiwe, si lazima kuwazuia watoto wote kutumia mitandao ya kijamii, lakini inatosha kuwajumuisha takriban asilimia 80, na wengine watawafuata moja kwa moja."
Baadhi ya wazazi waliovunjika moyo wangependa kutangaza kuwa ni kinyume cha sheria, kwa kuwa hawataki watoto wao wahisi kuwa wana haki, au kushinikizwa, kutumia mitandao ya kijamii.
Elachi anasema: "Siku zote tumesisitiza, iwe sheria inaweza kutekelezeka au la, kwamba lengo kuu la haya yote ni kuanzisha kanuni.
Je, sheria ya kupiga marufuku utumizi wa mitandao kwa watoto itapunguza madhara?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kando na swali la iwapo sheria hiyo inatumika au la, wengi bado wanajiuliza: Je, inafaa kutumika?
Kwanza, kuna wasiwasi kwamba sheria hii inaweza kuwasukuma watoto kutafuta tovuti hatari zaidi kwenye mtandao.
Je, hii itakuwa katika vyumba vya gumzo vya tovuti za michezo ya kubahatisha, ambazo Polisi wa Shirikisho la Australia wameonya kuwa ni misingi ya itikadi kali, lakini ambazo haziruhusiwi kupigwa marufuku?
Na je, itapitia tovuti kama "Omegle," ambazo vizazi vilivyotangulia vilikimbilia walipoambiwa walikuwa wachanga sana kutumia mitandao ya kijamii ya kawaida? Tovuti iliruhusu watumiaji kupiga gumzo la video na watu wasiowajua, kisha ikafungwa miaka miwili iliyopita kwa kushindwa kuwalinda watoto kutoka kwa watu waliokuwa wakiwanyanyasa, na tovuti kama hizo zilichukua nafasi yake haraka.
Wengine wanaonya kuwa watoto wanaweza kuendelea kutumia majukwaa kama YouTube na TikTok bila kuunda akaunti, ambako udhibiti ni mdogo zaidi.
Kampuni moja ilisema wiki hii:
"Sheria hii haitawasaidia watoto, bali itawaweka katika mazingira hatarishi zaidi kwenye YouTube."
Wakati makampuni makubwa yanakosolewa kwa udhaifu wa kudhibiti maudhui, bado yamepandikiza mifumo bora kuliko majukwaa madogo yasiyodhibitiwa.
Tim Levy, rais wa kampuni ya usalama mtandaoni ya Qoria na mmoja wa washauri wa majaribio ambaye alijiuzulu, anasema: "Huzuii tabia hiyo, unaihamishia kwenye majukwaa mengine, na kuwaambia wazazi wa Australia wanaojali kwamba kila kitu kiko sawa sasa ni ujumbe hatari sana."
Mjadala wa kitaaluma na kijamii

Chanzo cha picha, Getty Images
Tafiti zinaonyesha picha mchanganyiko: mitandao ya kijamii inaweza kuwa chanzo cha madhara, lakini pia ni msaada muhimu kwa baadhi ya watoto hasa wale wa LGBTQ+, wenye changamoto za neva au wanaoishi mbali na huduma za kijamii.
Anne Hollonds, aliyekuwa Kamishna wa Watoto, anasema juhudi za serikali hazikuangazia mahitaji ya watoto walio hatarini zaidi, ambao hutafuta mitandaoni msaada na hisia ya kustawi.
Wataalamu zaidi ya 140 walitia saini barua ya wazi wakionya kuwa kuweka umri pekee kama miaka 16 hakutatua tatizo.
Kabla kuwa msimamizi wa sheria hiyo, Mkuu wa Usalama Mtandaoni Julie Inman-Grant alisema:
"Hatuzui watoto kuogelea baharini; tunaunda maeneo salama ya kuogelea."
Waziri Annika Wells alijibu kwa ukali:
"Tunaweza kufuatilia papa."
Akaongeza kuwa hii ni hatua ya kwanza tu, na kwamba "uwajibikaji wa kidijitali" kuwalazimisha makampuni kuzuia madhara yanayotabirika ndicho kitafuata.
Mwisho, anasema:
"Huu si mwisho wa tatizo, bali ni mwanzo wa mpango wa kulitatua. Na ni hatua inayostahili kuchukuliwa kwa ajili ya kizazi kijacho."















