Jinsi mitandao ya kijamii inavyotumika kupinga ‘sheria kandamizi’ Tanzania

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mitandao ya kijamii
    • Author, Sammy Awami
    • Nafasi, Mwandishi
    • Akiripoti kutoka, Tanzania

Shedrack Chaula, ni mtu huru sasa. Siku chache zilizopita, alichungulia miaka miwili gerezani baada ya Mahakama ya wilaya ya Rungwe mkoa wa Mbeya kusini magharibi mwa Tanzania kumtia hatiani kwa kosa la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa TikTok, kinyume na Sheria ya Makosa ya Mtandao, kifungu cha 16.

Chaula, kijana mwenye umri wa miaka 24 tu alikwepapa kifungo jela si kwa kwa hamasa ya jamaa au ndugu zake wa damu. Wala haikuwa kupitia akiba ya fedha aliyokuwa ameitunza benki au kwenye kibubu. Mamia ya watu kupitia mtandao wa kijamii, wengi wao asiowafahamu wala hakuwahi kukutana nao, ndiyo walimtoa jela kupitia michango iliyoratibiwa katika mitandao ya kijamii.

Wanasheria na wapigania haki za watu wanasema michango hiyo si bahati mbaya bali ni ujumbe kwa mamlaka unaopinga sheria zinazoonekana kandamizi kwa wananchi.

“Unajua mtu anapopewa adhabu anapewa ile adhabu ili imuumize yeye kama aliyefanya hicho kitendo. Lakini sasa tunaona Watanzania wanajitokeza kwa wingi na kuiambia serikali kwamba haya maumivu ni yetu sote” Fulgence Massawe, Mkurugenzi wa Uchechemuzi, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Tanzania.

Massawe, ambaye ni mtetezi wa haki za binadamu, anasema Watanzania wanajitokeza kuchangia kupitia mitandao ya kijamii ili pia kuziambia mamlaka kwamba tutaendelea kufanya haya makosa na tutashiriki katika hicho kikombe cha kumuadhibu yule mtakayemtia hatiani.

Watanzania hawaandamani barabarani kama ambavyo labda Wakenya wanafanya kuonesha hawajafurahishwa na kitu lakini kupitia michango hii wanaziambia mamlaka kwamba hawakubaliani na sheria kandamizi zinazominya uhuru wa watu kujieleza, anaongeza Massawe.

Wiki moja iliyopita, Japhet Matarra pia aliachiwa baada ya michango iliyofanyika kupitia mitandao ya kijamii. Lakini Matarra hakuwa na bahati sana. Wakati anatoka jela tayari alikuwa ametumikia kifungo chake kwa mwaka mzima baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya kimtandao.

Mwaka 2023 Matarra alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya shilingi milioni 7 baada ya kuchapisha katika mtandao wake wa kijamii kile alichokiita makadirio ya utajiri wa marais wa Tanzania. Mwishoni mwa mwezi June, taarifa zake ziliibuka mitandaoni, na ndipo watu mbalimbali walipomchangia kiasi kamili cha faini alichotakiwa kulipa ili kuachiwa huru

“Kweli nilikuwa nimekata tamaa, lakini kwa sababu Mungu yupo, lilitokea tukio la tofauti sana. Niendeleze shukrani zangu kwa ndugu zangu wa Twitter” Matarra aliwaambia waandishi wa Habari

Pia unaweza kusoma
.

Chanzo cha picha, Mwanachi

Maelezo ya picha, Shadrack Chaula

Ukusanyaji wa michango

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ukusanyaji wa michango kwa njia ya mitandao si mipya. Hutokea wakati watu wanapohitaji msaada wa matibabu na mahitaji mengine. Lakini vinara wa ukusanyaji wa michango ya aina hii wanasema uchangiaji wa fedha kwa watu waliotiwa hatiani kupitia sheria zinazodaiwa kuwa kandamizi wanafanya hivyo si kwa minajili ya masuala ya kijami bali kupinga baadhi sheria na kukosoa utendaji wa mamlaka.

Machi 2021, Mfanyabiashara Yericko Nyerere alikwepa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kukutwa na hatia kufuatia kuchapisha kile mahakama ilichokiita kuwa maneno ya uchochezi katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook. Watumiaji wa mitandao walichangisha kiasi cha shilingi milioni 5 na kusaidia kuachiwa huru kwa Yericko Nyerere.

Mwaka mmoja kabla (Machi 2020), Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake nane waliachiwa huru baada ya kulipa faini ya shilingi milioni 350, ambazo zilipatikana kupitia uchangishaji uliofanyika katika mitandao ya kijamii

“Hii ni namna tu ya wananchi kueleza hisia zao” anasema Godlisten Malissa, mtumiaji wa mitandao na mmoja wa wachangishaji wakubwa wa michango kwa wahitaji.

Malissa anasema mamlaka inabidi isikilize kwa makini kile wachangiaji wa faini hizi wanachokisema kupitia utayari wa kuja pamoja na kumsaidia mwananchi anayeonekana kuonewa na mamlaka.

Teknolojia imebadilisha namna michango hii inafanyika, lakini jamii za ukanda huu wa Afrika Mashariki, dhana ya wananchi wa hali ya chini kuja pamoja na kukwamuana katika shida ya namna moja au nyingine si geni, inafahamika kama Harambee.

Hata hivyo, wanazuoni wamekuwa wakikosoa namna dhana hii imebinuliwa na sasa kufanyika si kijamii tena, na katika ngazi ya mitaa na vijiji. Wanasema imegeuka kuwa mbinu ya kukusanya fedha za ujenzi wa majengo na miundombinu mingine kama nyumba za ibada, shule au madaraja, ambapo wenye nacho hasa wanasiasa na wafanyabiashara wanapata fursa ya kusimika ushawishi wao.

“Harambee imegeuka kuwa nyenzo ya maendeleo ya huduma za kijamii” anaandika Peter M. Ngau, kutoka Chuo Kikuu cha California, Marekani. “Kwa wakulima wengi, juhudi za kuja pamoja sasa zinalenga shule, vituo vya afya, barabara, na makanisa badala ya maendeleo ya mashamba au biashara.”

Katika dhana ya Harambee, jitihada za kusaidiana zilikua za hiari kwa asili, ambapo jamii zilijitolea ardhi, walilima pamoja, au walimsaidia mwanajamii kuhamisha familia yake au kurekebisha nyumba yake. Koo kutoka kijiji kimoja au viwili, vilikutana kufanya mojawapo ya shughuli hizo, zikibadilishana kutoka kaya moja hadi nyingine na kutoka kijiji kimoja hadi kingine. Maamuzi yalifanywa kwa njia isiyo rasmi kupitia majadiliano na wanachama wote wa kila kundi wakiwa wamekaa pamoja.

Wakati michango hii inayolenga kuwakomboa watu kutoka mikono ya kisheria si kama michango mingine ya kusaidia shughuli za kijamii kama kilimo, biashara, msiba au harusi, watetezi wa haki za binaadamu wasema njia pekee ya kuitikia ujumbe unaotumwa na michango hii ni kwa mamlaka kuachana na sheria kandamizi zinazoadhibu haki ya wananchi kujieleza.