Man United yaporomoka miongoni mwa vilabu tajiri zaidi duniani

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 3

Orodha mpya ya vilabu tajiri zaidi duniani imetangazwa, na Manchester United haipo tena kileleni!

Manchester United iliyoshikilia nafasi ya pili mwaka jana kwa utajiri, na kushikilia nafasi mbili za kwanza kwa zaidi ya miaka 15, mwaka huu imeshuka hadi nafasi ya 8.

Licha ya kuongeza kipato cha jumla kwa asilimia 40, uongozi wa Sir Jim Ratcliff na kampuni ya Ineos umeshuhudia timu hiyo kuporomoka kwa kiwango cha chini zaidi katika historia ya mapato .Hili halijawahi kutokea .

Ijapokuwa mapato ya Manchester United yaliongezeka hadi pauni milioni 692, timu hiyo iliyomaliza nafasi ya 15 msimu uliopita wa ligi kuu ya Uingereza pamoja na kushuka kwa asilimia 45 ya mapato ya matangazo ya mechi zao ndio vyanzo vikuu vya kudidimia kwao.

Kwa mara ya kwanza Man United wameshindwa na Liverpool, Manchester City na Arsenal katika orodha ya timu zinazoingiza fedha nyingi England. Kwa sasa Liverpool iko kidedea kwenye mapato nchini England baada ya kushinda ligi msimu uliopita.

Miamba wa soka wa Uhispania Real Madrid wameendelea kuongoza orodha hiyo wakiandikisha mapato ya pauni bilioni 1.013 ikiwa milioni 203 ni mapato ya ada za kutazama mechi uwanjani, milioni 292 mapato ya ada za matangazo ya mechi na milioni 518 ni mapato ya matangazo ya biashara.

Barcelona wa Uhipania ni wa pili, wakipanda kutoka nafasi ya 6 mwaka jana baada ya kujiingizia pauni milioni 851.

Nafasi ya tatu kwa utajiri ni klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani wakijipatia pauni milioni 751.

Timu ya nne ni PSG ya Ufaransa ikiwa na pauni milioni 730.

Timu ya kwanza kutoka nchi ya England iko katika nafasi ya tano ya orodha hiyo, ambayo ni Liverpool walio na pauni milioni 729.

Wamefuatwa kwa karibu na Manchester City katika nafasi ya sita, wakiwa na pauni milioni 723. City nao pia wameshuka kwa kiwango kikubwa mwaka huu, kutoka nafasi ya 2 msimu uliopita .

Arsenal hawakusonga mbele wala kurudi nyuma, wamesalia katika nafasi ya saba baada ya kuvuna mapato ya pauni milioni 717.

Manchester United wameorodheshwa katika nafasi ya 8 kutoka nafasi ya pili mwaka jana, baada ya kujipatia kipato cha pauni milioni 692.

Nafasi ya tisa ni Tottenham Hotspur ya England waliojipatia pauni milioni 587 mwaka huu.

Anayefunga orordha hiyo mwaka huu ni Chelsea wa England ambao wamejikusanyia jumla ya pauni milioni 510.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rodrigo na Vinicius Jr wakisherehekea ushindi wa goli

Je, Sababu ya United kushuka ni ipi?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hii ni mara ya kwanza kwa United kutoka kwenye orodha ya timu tano zinazoingiza fedha nyingi kwa muda wa miaka 29.

Na ikizingatiwa kuwa United itacheza mechi 20 tu msimu huu katika uwanja wa Old Trafford kufuatia kuondolewa kwenye michuano ya Carabao na pia kombe la FA,na isitoshe hawakushiriki katika michunao ya klabu bingwa ulaya basi ni dhahiri shahiri kwamba,hakutakuwa na maajabu mwaka ujao,mapato yao yanatarajiwa kuendelea kushuka kwa pauni milioni 85 au hata zaidi na hizi ni za matangazo ya mechi tu hujapiga hesabu ya fedha kutoka kushiriki michuano hiyo.

Katika muda wa 15 iliyopita Manchesetr United ilitia fora dunia na kuzitetemesha timu nyingine kwenye orodha ya vilabu tajiri kwa kuwa walikuwa wakiingiza kuingiza fedha kwa njia nyingi kutokana na makali yao uwanjani na nguvu ya biashara nje ya uwanja ila sasa kudorora kwa matokeo yao kumeanza kukausha njia zao za kuingiza fedha.

Wachambuzi hata hivyo wanasema ,United bado inasalia kuwa klabu yenye hadhi na jina kubwa zaidi duniani, ila iwapo haitaimarisha kikosi chao na kuanza kuandikisha matokeo mazuri na kushinda mataji, basi hali yao ya kifedha itazidi kuwa mbaya.

Kwenye mchezo wa kandanda ,ushindi ama utawala wa jana haujalishi,cha muhimu ni timu kujipnanga kwa matokeo ya leo?Hapo ndipo mfereji wa mapato unapomiminika.