'Kila kitu kilikwama': Kuzimwa kwa intaneti kulivyowaathiri Waganda

- Author, Sammy Awami
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Kampala
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Wakala wa fedha kwa simu Mirembe Tracy analalamika kwamba biashara yake katika mji mkuu wa Uganda wenye shughuli nyingi Kampala ililemazwa wakati serikali ilipofunga mtandao wakati wa uchaguzi mkuu uliokuwa na ushindani mkali wiki iliyopita.
"Huduma ya kutoa fedha ilikatizwa," anaiambia BBC, akiongeza kuwa anapata karibu mapato yake yote kutoka kwa ada ya huduma hiyo.
Bila hivyo, hapati mapato yoyote.
"Ninaweza kupata hadi shilingi 450,000 [za Uganda] au $130 kwa siku. Fedha hizo ndizo ninazotumia kulipa kodi. Nilipata hasara kubwa," anasema.
Kwa siku mbili hakuweza kufanya lolote ila kukaa nyumbani - aliweza tu kuuza airtime, ambayo anasema "haitozi ada ya huduma".
Mamlaka ya mawasiliano nchini Uganda iliamuru kufungwa kwa nchi nzima ili "kuhakikisha amani, kulinda utulivu wa kitaifa na kuzuia matumizi mabaya ya majukwaa ya mawasiliano wakati wa zoezi nyeti la kitaifa".
Upinzani ulisema ni hatua ya kuficha ulaghai wa wapiga kura na kuwazuia mawakala wake kushiriki matokeo kutoka kwa vituo vya kupigia kura.
Kukatizwa kwa hudama ya intanetia kulivuga maisha.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
Biashara za mtandaoni ambazo zinategemea malipo kupitia simu ziliathirika pakubwa, baadhi zilisitisha shughuli na zingine zikirejelea wakirejelea miamala ya pesa taslimu.
Kampala ni maarufu kwa uchukuzi wa boda boda (pikipiki) zinazopatikana kila mahali, huku waendeshaji wengi wakipata mapato yao kupitia programu ya SafeBoda
Mwanzilishi mwenza wa SafeBoda aliviambia vyombo vya habari vya ndani kwamba seva nzima ya jukwaa ilikuwa iliathirika baada ya mtandao kuzimwa, na wahudumu wengi walilazimika kuondoka barabarani na biashara zingine ambazo zinategemea huduma hiyo kukosa mapato yao.
Namukwaya Olivia, ambaye anauza mavazi ya kitamaduni na kutegemea sana mtandao wa Instagram, TikTok na WhatsApp kufikia wateja, anasema hakujifungua biashara wakati wa kipindi hicho.
Anaiambia BBC kwamba wateja wake wengi huomba picha kabla ya kuamua wanunue nini.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Hatukuweza kutuma picha, kuwasiliana na wateja wala kuwasilisha bidhaa kwa kwao ,"mwanabiashara huyo anasema.
Anaongeza kuwa athari ya kuzima kwa intaneti ilikuwa bayana, na ilifanya iwe vigumu kufidia gharama za kimsingi.
"Hatukuweza kulipa kodi katika kipindi hicho," anasema. "Hata sasa, mambo hayajakaa sawa kwa sababu wateja bado wanatatizika kutufikia mtandaoni."
Mwanahabari Ngabo Amon anasema simu yake ya mkononi, chombo cha kazi kwake, haikuwa na manufaa kwa kiasi kikubwa.
"Una simu na huwezi kufanya lolote na huna la kufanya, anasema.
Hakuweza tena kutafiti, kufuatilia matukio ya uchaguzi au kutuma taarifa kwenye chumba chake cha habari.
Anasema maisha ya kila siku yalibadilika yani kila kilikwama.
Baadhi ya watu walirejelea kutazama televisheni ili kujishughulisha, ama kutazama moja kwa moja, au kununua filamu za zamani zilizopakuliwa kutoka kwa maduka.
"Watu walinunua walichoweza kumudu, walirudi nyumbani na kuangaliana tu, kwa sababu hawakuwa na budi," Ngabo anasema.
Vijana pia hawakusazwa hasa ukizingatia vile wanavyopenda kufuatilia mambo mengi mitandaoni.
Ronnie Mwesigwa, 20, anasema alishindwa kuwasiliana na marafiki zake na hakuwa na fursa ya kupata burudani mtandaoni.
"Sikuweza kuwasiliana na mtu yeyote, na hata michezo ya kubahatisha ilipotea," anasema. "Haikuwa hali nzuri."
Ili kupitisha wakati wake, mchezaji aligeukia maudhui ambayo tayari yamehifadhiwa kwenye simu yake, akitazama tu.
"Sikuwa na lingine la kufanya."
Ngabo anasema hali hiyo iliwahangaisha sana waandishi wa habari waliokuwa wakifuatiliauchaguzi huo, kwani kukatika kwa umeme kuliwafanya kushindwe kupata taswira halisi ya kile kilichokuwa kikiendelea katika vituo vya kupigia kura.
"Unazungumzia watu kufanya fujo, mvutano wa mitaani, lakini watazamaji wanaona tu picha yako na kusikia sauti yako, na hii haimridhishi mwanahabari au mtazamaji," anasema.
Rais Yoweri Museveni, 81, alishinda uchaguzi huo kwa kishindo na kuongeza muda wa utawala wake wa miaka 40 na ameushutumu upinzani kwa kutaka kubadili matokeo kupitia ghasia.
Mpinzani wake wa karibu Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, anashikilia kuwa matokeo hayo ni "feki".
Kulingana na ripoti ya ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika (AU), "kuzimwa kwa mtandao kumeathiri ufikiaji wa habari, uhuru wa kujumuika [na] kuvuruga shughuli za kiuchumi".
Pia inabainisha kuwa hatua hiyo "imeibua hali kutoaminiana" katika mchakato wa uchaguzi.
Ngabo anasema kuwa hali ilikuwa mbaya zaidi katika maeneo ya vijijini. Kwa kutokuwa na mtandao, baadhi ya waandishi wa habari walilazimika kusafirisha video zao hadi kwenye vituo vyao vyao vya habari.
Anatoa mfano wa video, zilizorekodiwa mapema asubuhi ya uchaguzi kusafirishwa kwa basi kutoka eneo la kijijini, kufika Kampala jioni.
"Kufikia wakati huo, matokeo tayari yanajadiliwa na kujumlishwa na hakuna anayevutiwa na picha hizo ," anasema.
Caroline Mutai, mwandishi wa habari mwenye makao yake nchini Kenya ambaye alikwenda Uganda kuripoti uchaguzi huo, anasema kuzimwa kwa intaneti wakati wa uchaguzi "karibu kunipatie msogo wa mawazo".
Anaeleza matatizo aliyokumbana nayo akijaribu kuwasilishwa taarifa alizokusanya katika chumba chake cha habari, akipoteza muda mwingi kutafuta maeneo yenye intaneti, lakini akazuiwa au kufukuzwa.
Kuzimwa kwa intaneti pia kulimtenganisha na familia yake hasa ikizingatiwa hali ya usalama ilivyokuwa tete kipindi hicho.
"Baada ya kuhangaika kufanya kazi katika mazingira, unataka kuzungumza na watu walio karibu nawe," anasema. "Lakini huwezi kuwafikia, na hiyo inafanya hali kuwa ngumu zaidi."

Kwa wanafunzi, kukatika kwa umeme kumetatiza mawasiliano na shughuli za masomo.
Aaron Benitez, mwanafunzi wa mwaka wa mwisho wa shule, anasema hakuweza kuwasiliana na familia yake katika kipindi hicho.
"Nilihitaji kujua hali ya familia yangu na kile kilichokuwa kikiendelea nchini," anasema. "Lakini sikuweza kuungana nao hata kidogo."
Mafunzo ya mtandaoni pia yalisitishwa. Walimu hawakuweza kufunzamasomo yote ya mitandaoni iliahairishwa.
"Bwana wetu hakuweza kutuma maelezo kwenye WhatsApp," mwanafunzi huyo anasema. "Kwa kawaida tunasoma mtandaoni, wakati mwingine kwenye Zoom, lakini wakati huo kila kitu kilisimama."
Anaongeza kuwa ufikiaji unasalia kuwa wa polepole na sio wa kutegemewa, licha ya uchaguzi kumalizika.
"Imerudi, lakini imedhibitiwa. huwezi kufanya baadhi ya vitu na hii inaathiri masomo yetu."
Serikali ilirejesha muunganisho wa intaneti baada ya Museveni kutangazwa mshindi wa uchaguzi siku ya Jumamosi.
Baadhi ya majukwa, hasa mitandao ya kijamii bado yamedhibitiwa, hali inayowafanya vijana wengi kutumia njia mbadala ya kuwasiliana kupitia mtandao wa wa VPN (virtual private network), ambao unaficha mahali mtu alipo mtandaoni.
Kwa wengi, kuzimwa kwa intaneti ilikuwa usumbufu wa muda lakini ni ukumbusho dhahiri wa jinsi ulimwengu wa kidijitali unavyoathiri maisha yao ya kila siku.















