Tetesi za Soka Ulaya Alhamisi: Aston Villa inamtaka Loftus-Cheek

.

Chanzo cha picha, Reuters

Muda wa kusoma: Dakika 3

Kiungo wa AC Milan na England Ruben Loftus-Cheek, 29, analengwa na Aston Villa, ambayo inataka kuimarisha safu yake ya kati baada ya mchezaji wa kimataifa wa Ufaransa Boubacar Kamara, 26, kupata jeraha baya la goti. (Telegraph - usajili unahitajika)

Loftus-Cheek pia ametolewa kwa Manchester United, na mazungumzo ya awali yamefanyika. (Talksport)

Villa imemuulizia mshambuliaji wa Fenerbahce Youssef En-Nesyri katika muda wa saa 24 zilizopita, lakini mchezaji huyo wa Morocco, 28, ataamua mustakabali wake hivi karibuni huku Napoli na Juventus pia zikimtaka. (Fabrizio Romano)

Tottenham iko tayari kutoa pauni milioni 25 kumsajili winga wa West Ham Mholanzi Crysencio Summerville, 24. (Mail)

Liverpool inavutiwa na beki wa Tottenham na Uholanzi Micky van de Ven, 24, ambaye bado hajasaini mkataba mpya na Spurs. (Mail - usajili unahitajika)

Manchester United inataka kusalia na kiungo wa Ureno Bruno Fernandes, 31, kwa mwaka mwingine na wangependa kujua msimamo wake kabla ya Kombe la Dunia msimu huu. (ESPN)

Nottingham Forest itamruhusu beki wa Brazil Cuiabano, 22, kuondoka kwa mkopo mwezi huu, huku beki wa pembeni wa Liverpool, 29, Ugiriki, Kostas Tsimikas, ambaye kwa sasa yuko kwa mkopo Roma,akiwa miongoni mwa wanaolengwa. (Athletic - usajili unahitajika)

Bruno Fernandes

Chanzo cha picha, Getty Images

Ombi la Forest kumsajili mlinzi wa Napoli Mathias Olivera limekataliwa, lakini bado ipo kwenye mazungumzo na mchezaji huyo wa kimataifa wa Uruguay, 28. (Tuttomercatoweb - kwa Kiitaliano)

Celta Vigo wamewasilisha ombi rasmi kwa Wolves kumsajili kwa mkopo Fer Lopez, 21, na itagharamia mshahara wote wa kiungo huyo mshambuliaji wa Uhispania aliye na umri wa chini ya miaka 21. (Sky Sports)

Real Madrid inafikiria kumsajili kiungo wa kati wa Ureno Ruben Neves, 28, ambaye yuko tayari kuhama Al-Hilal, huku Manchester United pia wakimnyatia nahodha huyo wa zamani wa Wolves. (AS - kwa Kihispania)

Ruben Neves (kulia)

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ruben Neves (kulia) alijiunga na Al-Hilal kutoka Wolves

Mchezaji wa Chelsea na England Cole Palmer, 23, yuko tayari kurejea Manchester kujiunga na Manchester United, ingawa mchezaji huyo wa zamani wa Manchester City ana mkataba Stamford Bridge hadi 2033. (Express)

Barcelona inataka kumsajili nahodha wa Manchester City, Bernardo Silva, 31, kwa uhamisho wa bure wakati mkataba wa kiungo huyo wa kati wa Ureno utakapokamilika mwishoni mwa msimu. (Nacional - kwa Kihispania)

Schalke inadaiwa kukubali masharti ya kumsajili mshambuliaji wa Bosnia-Herzegovina Edin Dzeko, 39, ambaye alijiunga na Fiorentina mwezi Julai. (Sky Sport - kwa Kijerumani)