'Balozi wa soka la Afrika' - Mane ni shujaa wa Senegal katika Afcon

Chanzo cha picha, Getty Images
Sadio Mane ni shujaa wa Senegal kwa mara nyingine, lakini mara hii ni kwa sababu tofauti kidogo.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Liverpool na Bayern Munich ameshinda taji lake la pili la Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) siku ya Jumapili, baada ya Teranga Lions kuishinda timu mwenyeji Morocco katika fainali iliyojaa utata.
Katika dakika za mwisho, kocha mkuu wa Senegal, Pape Thiaw, alijaribu kuwatoa wachezaji wake uwanjani baada ya Morocco kupewa penalti dakika ya 98 wakati mlinzi El Hadji Malick Diouf alipomwangusha Brahim Diaz.
Baada ya wachezaji wa Senegal kwenda kwenye chumba cha kubadilishia nguo, Mane alionekana akiingia kwenye chumba hicho na kisha kuwarudisha uwanjani, kwa msaada wa kipa Edouard Mendy.
Takriban dakika 16 baada ya penalti kutolewa, penalti ya Diaz aliyopiga katikati ya lango ilinaswa kwa urahisi na Mendy.
Sare ya 0-0 uliufanya mchezo huo kwenda hadi muda wa ziada. Ndipo Pape Gueye alipofunga bao la ushindi na Senegal kutwaa ubingwa.
Mane, ambaye amesema hii itakuwa Afcon yake ya mwisho, anaondoka kama kiongozi wa timu - baada ya kukabidhiwa kitambaa cha unahodha na wachezaji wenzake kabla ya kombe hilo kutolewa.
Wadau wa soka wanasemaje?

Chanzo cha picha, Getty Images
"Ingekuwa sio sawa kususia mchezo huu kwa sababu mwamuzi ametoa penalti. Nadhani hilo lingekuwa jambo baya zaidi kwa soka la Afrika. Bora kupoteza kuliko aina hii ya tukio kutokea kwenye soka letu," amesema Mane.
"Ni jambo baya. Soka halipaswi kusimama hata kwa dakika kumi. Tunapaswa kukubali kwamba tulisimama lakini jambo zuri ni kwamba tulirudi na tukacheza na kilichotokea kikatokea."
Mshambuliaji wa zamani wa Nigeria Daniel Amokachi ameiambia BBC World Service: "Mane alifanya kazi ya ziada kuirejesha timu yake na amefanikiwa."
"Ni balozi wa soka. Tunajua yukoje akiwa nje ya uwanja na anajua mpira wa miguu ni nini."
Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Morocco, Hassan Kachloul, amesema "mpira wa miguu wa Afrika na mpira wa miguu wa dunia ulikuwa unaharibika" hadi Mane alipoingilia kati.
'Hadithi ya Mane’
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Maisha ya Mane yalianzia Bambali. Kusini magharibi mwa Senegal ambapo alianza kucheza mpira wa miguu kwenye mitaa yenye udongo na viwanja vya mchanga.
Akiwa na umri wa miaka 13, aliitazama Liverpool dhidi ya AC Milan katika fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2005.
Tangu wakati huo ametwaa kombe hilo la Ligi Kuu England akiwa na Reds, na pia kushinda mataji mawili ya Afcon akiwa na Teranga Lions.
Mane alifunga penalti ya ushindi dhidi ya Misri katika fainali ya 2021 na kusema "ni siku bora zaidi maishani mwangu na kombe bora zaidi maishani mwangu."
Kufuatia ushindi huo, ili kutambua mafanikio yake, uwanja wa mpira katika mji wa Sedhiou ulipewa jina lake. Ni chini ya kilomita 20 kutoka mji alikozaliwa.
Sasa akiwa bingwa mara mbili na umri wa miaka 33, Mane amehitimisha maisha yake ya soka katika Afcon kwa kiwango cha juu zaidi.
Lakini Gueye anasema kikosi hicho kinalenga kumshawishi Mane ambaye anaitwa “gwiji wa Senegal,” kubadili mawazo yake kuhusu hii kuwa fainali yake ya mwisho ya Afcon na kubaki na timu hiyo kwa angalau mashindano ya 2027 nchini Kenya, Tanzania na Uganda.
"Tutajaribu kuwa naye kwa muda mrefu zaidi, kwa sababu bado ana uwezo wa kuendelea kucheza," mchezaji huyo wa Villarreal mwenye umri wa miaka 26 ameiambia BBC Afrique.
"Nimesikia alichosema na tutaona atakachoamua kufanya. Lakini tunamtaka abaki nasi kwa miaka mingi zaidi."
Mane mnyenyekevu

Chanzo cha picha, Getty Images
Mane, ambaye sasa anacheza katika ligi ya Saudi Arabia na Al-Nassr, ana kabati la makombe lakini hajawahi kusahau asili yake.
Alivutia mioyo ya wengi kwa kutoa misaada huko Bambali, ametoa pesa za kujenga hospitali na shule, kuchangia ujenzi wa misikiti na kutoa fedha za kusaidia mapambano dhidi ya janga la virusi vya korona.
Pia alituma jezi 300 za Liverpool katika mji wake wa nyumbani kabla ya klabu hiyo ya Anfield kucheza katika fainali ya Ligi ya Mabingwa ya 2018, ambapo Real Madrid ilishinda 3-1.
"Sadio anapokuja hapa, anakuwaa mnyenyekevu sana, sawa na watu wa Bambali," anasema Fode Boucar Dahaba, rais wa ligi ya kikanda, aliiambia BBC Sport Africa ilipotembelea kijiji hicho miaka michache iliyopita.
Wanafamilia wanamtaja kama mtu "anayefanya kazi kwa ajili ya kila mtu" na "Muislamu mzuri."
Hilo lilidhihirika wakati akicheza ligi kuu ya Uingereza, aliposaidia kusafisha vyoo katika msikiti mmoja huko Toxteth baada ya ushindi mmoja wa Liverpool.
"Alitaka ibaki kuwa siri na hakufanya hivyo kwa ajili ya kuonekana," alisema Abu Usamah Al-Tahabi, imamu katika Msikiti wa Al Rahma.
"Si mtu anayeendekeza umaarufu. Hana kiburi."
Mchango wake kwa Senegal

Chanzo cha picha, Gettty IMAGES
Bao lake la dakika ya 78 dhidi ya Misri, lilitosha kuwapeleka Teranga Lions kwenye fainali hii ya Afcon.
Mane amecheza zaidi ya mechi 120 na ndiye mfungaji bora wa nchi yake akiwa na mabao 53. Atacheza Kombe la Dunia baadaye mwaka huu. Ingawa alikosa kushiriki mashindano hayo huko Qatar 2022 kutokana na jeraha.
Mane ana tabia ya unyenyekevu na si nahodha wa Senegal, lakini anapozungumza, wachezaji wenzake humsikiliza.
"Ana uzoefu wa mechi kubwa, kwa hivyo pia anajua jinsi ya kututuliza. Anatuambia tuwe watulivu, hata baada ya kufunga au tukiruhusu bao," anasema Pepe Gueye.
Mane alishinda mechi nyingi za kimataifa chini ya Aliou Cisse, aliyekuwa meneja wa timu hiyo ya Afrika Magharibi kuanzia 2015 hadi 2024, na kocha wa sasa Pape Thiaw anataka Mane abaki.
"Nadhani alifanya uamuzi kwa kukurupuka na nchi haikubaliani naye, na mimi kama kocha wa timu ya taifa sikubaliani na uamuzi huo hata kidogo," amesema Thiaw.
"Tungependa kuwa naye kwa muda mrefu kadiri iwezekanavyo."














