Iran haiwezi kuishinda Marekani kijeshi: Je, inatumia mbinu gani kujiokoa?

j

Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images

Maelezo ya picha, Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), kikosi kikuu ndani ya jeshi la Iran, hudhibiti programu za makombora na ndege zisizo na rubani na huongoza shughuli muhimu za kikanda.
    • Author, Luis Barrucho
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Marekani na Israel zinadai mashambulizi yao ya pamoja dhidi ya Iran yanayoendelea kudhoofisha kwa kiasi kikubwa uwezo wa kijeshi wa nchi hiyo.

"Ulinzi wao wa anga, jeshi lao la anga, jeshi lao la wanamaji, na viongozi wao – vyote vimetoweka," Rais wa Marekani Donald Trump aliandika kwenye Truth Social siku ya Jumanne, Machi 3.

Iran ililipiza kisasi kwa kuanzisha mashambulizi dhidi ya Israel na nchi za Mashariki ya Kati zinazohifadhi kambi za kijeshi za Marekani.

Mkakati wa Iran

Dkt. HA Hellyer, mtaalamu wa usalama wa Mashariki ya Kati katika Taasisi ya Fikra tunduizi huko Uingereza RUSI (Royal United Service Institute), anasema mbinu ya sasa ya kijeshi ya Iran hailengi kuishinda Marekani au Israeli "katika vita vya kawaida," bali ni kuufanya mgogoro huu "uwe mrefu, uliotawanyika kikanda, na wenye gharama kubwa kiuchumi."

"Iran haiwezi kushinda kwa njia ya kawaida, lakini mkakati wake ni kuhakikisha kwamba ushindi wa wengine unakuja kwa gharama kubwa na usio na uhakika," anaelezea.

Nicole Grajewski, mhadhiri katika Kituo cha Masomo ya Kimataifa (CERI) cha Sciences Po, anasema:

Anaelezea mkakati wa Iran kuwa ni mbinu ya kijeshi iliyoundwa kumchosha adui kwa rasilimali zake na kusababisha hasara endelevu hadi uwezo wake wa mapigano utakapopungua.

Pia kuna mwelekeo wa kisaikolojia.

"Wakati wa Vita vya Siku Kumi na Mbili [vya Israel na Iran mwaka jana], Iran ilizidisha mashambulizi katika maeneo ya kiraia," anaelezea Nicole Grajewski. "Hii inasababisha hofu na kiwewe cha kisaikolojia miongoni mwa wakazi."

Makombora na ndege zisizo na rubani kwa ujumla huchukuliwa kuwa uti wa mgongo wa ulinzi wa Iran.

Israel inakadiria kwamba Iran ilikuwa na makombora yapatayo 2,500 hadi Februari 2026, yakiwa ya masafa mafupi (hadi kilomita 1,000) na masafa ya kati (km 1,000 hadi 3,000).

Makombora na Droni

k

Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images

Maelezo ya picha, Inaaminika Iran ina silaha nyingi zaidi za makombora ya masafa marefu katika Mashariki ya Kati.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Jenerali Dan Caine, kamanda wa vikosi vya Marekani, anasema makombora ya Iran yamepungua kwa 86% tangu siku ya kwanza ya mapigano, Jumamosi, Februari 28. Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) pia iliripoti kupungua zaidi kwa 23% Jumanne, Machi 4.

Licha ya haya, Hellyer anaamini Iran ina uwezo mkubwa wa kushambulia "miundombinu ya Israel, kambi za Marekani na washirika wa Ghuba, huku ikitatiza mtiririko wa nishati ya mafuta duniani yanayopita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz".

"Usumbufu huo unaweza kuwa na athari kubwa za kiuchumi duniani," anasema.

Takriban 20% ya mafuta duniani hupitia njia hii nyembamba, ambayo sasa imefungwa na Iran, na imeapa kushambulia meli yoyote inayojaribu kupita.

Ingawa Iran inaweza kukabiliwa na uhaba wa makombora, Grajewski anasema uwezo wake wa ndege zisizo na rubani bado ni mkubwa.

Inakadiriwa kwamba nchi hiyo ilizalisha maelfu ya ndege zisizo na rubani za Shahed kabla ya vita. Ndege hizi zisizo na rubani hutumikia kimkakati zaidi "kudhoofisha mifumo ya ulinzi wa anga polepole" kwa kuwalazimisha wapinzani kutumia makombora ya gharama kubwa ya kuzizuia.

Hata hivyo, Marekani inadai kwamba kurusha ndege zisizo na rubani za Iran kumepungua kwa 73% tangu kuanza kwa mzozo huo. Taasisi ya Masomo ya Usalama wa Kitaifa (INSS), yenye makao yake makuu Tel Aviv, inaripoti kwamba Marekani na Israeli zimefanya mashambulizi zaidi ya 2,000, huku Iran ikirusha makombora 571 na ndege zisizo na rubani 1,391, ambazo nyingi zimedunguliwa.

Kulingana na wataalamu, kudumisha kasi hii ya mapigano kutakuwa vigumu zaidi kwa pande zote mbili kadri mzozo unavyoendelea.

Mgogoro wa muda mrefu

k

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Iran ina takriban wanajeshi 610,000, kulingana na wataalamu katika Taasisi ya Kimataifa ya Masomo ya Mikakati (IISS).

Iran pia ina mojawapo ya vikosi vikubwa zaidi vya kijeshi Mashariki ya Kati.

Kulingana na makadirio katika ripoti ya "Kijeshi 2025" ya Taasisi ya Kimataifa ya Masomo ya Kimkakati (IISS), ina takriban wanajeshi 610,000 wanaofanya kazi.

350,000 katika jeshi la kawaida. 190,000 ndani ya Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ambacho husimamia programu za makombora na ndege zisizo na rubani pamoja na shughuli nyingi za kikanda.

Iran pia inategemea mtandao wa washirika wa kikanda - wakiwemo waasi wa Houthi nchini Yemen, vikundi vyenye silaha nchini Iraq, Hezbollah nchini Lebanon na Hamas wa Gaza.

Lakini Mhimili huu wa Upinzani umepata hasara kubwa katika wimbi la mapigano yaliyoenea katika eneo hilo baada ya shambulio la Hamas kutoka Gaza Oktoba 2023.

Licha ya changamoto hizo, Iran ina uzoefu katika migogoro ya muda mrefu, anasema Grajewski.

Ustahimilivu wake ulianza tangu Vita vya Iran-Iraq, ambapo miji yake ililengwa mara kwa mara licha ya udhaifua wake katika sialaha.

Lakini uendelevu wa mkakati wa Iran unaweza kutegemea mshikamano wa ndani wa nchi hiyo.

"Kila kitu kinategemea uwezo wa wanasiasa na wasomi wa usalama kubaki wamoja dhidi ya migawanyiko," anaelezea Grajewski. "Migawanyiko hii inaweza kusababisha kuongezeka kwa machafuko katika ngazi ya kijeshi."

Kuutanua mgogoro

Grajewski anasema Uturuki ilisema kwamba ulinzi wa anga wa NATO uliharibu kombora la Iran siku ya Jumatano ambalo lilikuwa linaelekea anga yake.

Uturuki, jirani wa Iran, ambayo ilijaribu kupatanisha kati ya Marekani na Iran kabla ya kuanza kwa mzozo imeonya "pande zote kujiepusha na hatua yoyote ambayo inaweza kusababisha kuongezeka zaidi kwa mzozo."

Lakini lengo pana la Iran ni kufanya mzozo upanuke na kufika kwa majirani zake kiasi kwamba "wanaweza kuweka shinikizo kwa Marekani, au angalau kujaribu kuwafanya watamani suluhu ya mazungumzo au kukomesha vita," anaelezea Grajewski.

"Kwa sasa, sijui kama mkakati huu utazaa matunda, lakini inaonekana kwamba hii ndiyo kamari ambayo Iran inaicheza kwa sasa," anaongeza.

Hata hivyo, kamari hii inaweza kusababisha matokeo mabaya. Hellyer anasema mataifa ya Ghuba "yanaweza kuamua kwamba, ingawa mwanzoni yalipinga vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Iran, usalama wao wenyewe sasa unatishiwa na kisasi cha Iran. Kwa hivyo itakuwa busara zaidi kuunga mkono kampeni ya Marekani ili kukomesha tishio linalosababishwa na Iran."

"Sidhani kama nchi za Ghuba zimefika huko sasa," anaongeza, "lakini naamini muda si mrefu watafikia maamuzi hayo."