Kwa nini rais wa Iran ameomba msamaha?

Pezeshkian wearing a suit looks ahead.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian
    • Author, Amir Azimi
    • Nafasi, BBC Persian
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amewashangaza waangalizi wengi kwa kuomba msamaha majirani wa Iran kwa mashambulizi ya hivi karibuni dhidi yao, wakati wa hotuba aliyoitoa Jumamosi asubuhi kama sehemu ya uongozi wa mpito wa nchi hiyo.

Msamaha kati ya nchi ni nadra sana, hasa wakati wa migogoro inayoendelea, na maneno yake walikuwa wazi. Viongozi kwa kawaida huonyesha "majuto" au hujitenga na uwajibikaji.

Badala yake, Pezeshkian alikiri moja kwa moja kwamba nchi jirani zilikuwa zimelengwa na akasema wanajeshi wa Iran sasa wameombwa kuacha kuwashambulia isipokuwa mashambulizi dhidi ya Iran yawe yanatoka katika eneo lao.

"Naona ni muhimu kuomba msamaha kwa nchi jirani zilizoshambuliwa," alisema. "Hatuna nia ya kuvamia nchi jirani."

Hilo pekee linaibua swali la kwanza: je, huu ulikuwa ni msamaha wa kweli, na kwa nini sasa?

Uwezekano mmoja ni kwamba uongozi wa mpito unajaribu kudhibiti athari zinazoongezeka za matokeo ya mashambulizi yao kikanda.

Baadhi ya nchi katika eneo hilo zimekumbwa na mapigano baada ya mashambulizi yaliyoanzishwa na Marekani na Israel Jumamosi tarehe 28 Februari.

Pezeshkian alisema mashambulizi haya yalifanywa chini ya maagizo ya kufanya hivyo "kwa hiari yao na kuchagua maeneo lengwa yao wenyewe" baada ya wimbi la awali la mashambulizi kuua makamanda wakuu wa Iran na kuvuruga miundo ya amri kuu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwitikio wa ndani pia unaonyesha mvutano huo. Baadhi ya watu wenye msimamo mkali tayari wamekosoa matamshi ya Pezeshkian kama udhaifu.

Kipindi cha sasa cha kisiasa nchini Iran si cha kawaida: baadhi ya watu wenye msimamo mkali wenye nguvu zaidi katika ngazi ya juu ya mfumo wameuawa, lakini maafisa wengi wa ngazi za chini na makamanda bado wanatilia shaka sana sauti yoyote ya upatanishi.

Kwao, kuomba msamaha kwa serikali za kigeni kuna hatari ya kuonekana kama kujisalimisha wakati wa mgogoro wa kitaifa.

Nje ya Iran, mwitikio huo umechochewa na simulizi tofauti sana. Donald Trump alidai haraka kwenye mtandao wa Truth Social kwamba Iran "iliomba msamaha na kujisalimisha" kwa majirani zake, akisema kwamba hatua hiyo ilithibitisha shinikizo la kijeshi la Marekani na Israeli lilikuwa likifanya kazi.

Lugha hiyo pia inaonyesha jinsi Washington inavyoweza kutafsiri ishara za Tehran. Trump amesisitiza mara kwa mara kwamba matokeo pekee yanayokubalika ni "kujisalimisha kabisa" kwa Iran.

Hilo linaleta utata wa kidiplomasia.

Kihistoria, mara chache nchi hukubali kujisalimisha bila masharti chini ya mashambulizi ya anga pekee, bila kujali jinsi mashambulizi ya mabomu yalivyo makali. Bila vikosi vya ardhini, kulazimisha matokeo kama hayo ni vigumu sana.

Kwa hivyo, kutafsiri msamaha wa Pezeshkian kama aina ya kujisalimisha kunaweza kutumika kama daraja la kisiasa kwa Washington: njia ya kudai kupiga hatua bila kuachana rasmi na hitaji la kujisalimisha.

Kwa Pezeshkian na baraza la uongozi la mpito, hesabu inaweza kuwa tofauti.

Kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano sasa kunaweza kuleta utulivu kabla ya kiongozi mpya wa kudumu kuibuka.

Kama mtu anayefuata kutawala mfumo wa kisiasa wa Iran atakuwa kiongozi wa kidini mwenye msimamo mkali, matarajio ya diplomasia yatakuwa finyu zaidi.

Uwezekano huo unaibua swali lingine la kimkakati: je, Pezeshkian anajiweka kama mtu anayeweza kuingia kwenye meza ya mazungumzo, aina ya kiongozi anayefanya kazi kwa vitendo ambaye serikali za Magharibi zinaweza kupendelea kujihusisha naye?

Katika hotuba yake, alijaribu kusawazisha ukaidi na uwazi, akikataa kujisalimisha huku akiashiria kujizuia kuelekea mataifa jirani.

Wakati huo huo, mvutano kuhusu uongozi wa baadaye wa Iran tayari umeanza kujitokeza.

Watu mbalimbali wa kisiasa na kidini, pamoja na makamanda ndani ya IRGC na vikosi vya usalama, wanaweza kuona mgogoro wa sasa kama fursa ya kuimarisha msimamo wao.

Baadhi wanataka Kundi la Wataalamu kuchukua hatua haraka ili kuchagua kiongozi anayefuata.

Ikiwa Pezeshkian atashindwa kuleta utulivu au kudhibiti vikosi vya jeshi, wapinzani wanaweza kusema kwamba msimamo mkali zaidi unahitaji kuchukuliwa.

Kwa sasa, mtihani mkubwa uko nje ya mipaka ya Iran.

Hadi kufikia sasa, nchi nyingi jirani zimejibu kwa tahadhari au zimekaa kimya, zikisubiri kuona kama msamaha huo utakuwa na matokeo yanyaoonekana.

Israeli, ambayo inaona mzozo huu kama fursa adimu ya kudhoofisha kile inachokiona kama tishio la muda mrefu la Iran, huenda isielekee sana kutafsiri ujumbe huo kama hatua ya nia njema na kweli kuelekea kupunguza mgogoro huo.

Tafsiri hiyo inaweza kuwa ya makusudi.

Msamaha wa Pezeshkian unaacha fursa ya tafsiri kadhaa: jaribio la kweli la kutuliza mgogoro wa kikanda, hatua ya kimkakati ya kupoteza muda ili uongozi wa mpito wa Iran ujiweke sawa, au ishara ya mwanzo wa mabadiliko ya kisiasa ndani ya Tehran yenyewe.

Katika mgogoro wenye kujumuisha mvutano wa ndani wa madaraka na vile vile vita vya nje, inaweza kuwa yote matatu kwa wakati mmoja.

Imetafsiriwa na Asha Juma