Je, Marekani na Israel zinataka kubadilisha utawala wa Iran?

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images
Rais wa Marekani anaonekana kuwa ameafikia malengo yake katika hatua ya kwanza ya vita vinavyoendelea Iran, vilivyoanza tarehe 28 mwezi Februari haswa baada ya kumuua kiongozi mkuu wa Iran Ali Khamenei.
Akiingia madarakani kwa awamu ya pili, rais wa Marekani Donald Trump, alisema anataka kudumisha amani, ila ameishambulia Iran kwa mara ya pili sasa.
Kwa sasa akiwa ameungana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kiongozi huyo wa Marekani ameanzisha vita vya kikanda na sio nchini Iran pekee.
Licha ya kuendelea kushambuliwa, baraza la wataalam nchini Iran, lazima limchague mrithi wa Ali Khamenei. Ila wale ambao wanataka kuipindua serikali hiyo na kubadilisha mfumo wa utawala, wanaiona kifo cha Khamenei kama nafasi nzuri ya kufanya mabadiliko hayo kwa usaidizi wa mamlaka za kigeni.
Professa Javadi Ali, mhadhiri katika chuo kikuu cha Michigan,na mtaalam wa masuala ya ulinzi, aliambia BBC Persia kuwa "inaonekana lengo kuu la Trump ilikuwa kumuondoa kiongozi mkuu wa Iran na viongozi wakuu wa kijeshi, na walitarajia huenda kifo chake kikasababisha maandamano makubwa." Anaongezea kuwa "serikali ya Iran imesema bado inaudhabiti kamili wa utawala huo na hakuna dalili kuwa majeshi ya Iran yameanza kugawanyika."
"Wakati wenu wa uhuru umefika" Trump aliwaambia raia wa Iran katika hotuba yake siku ya Jumamosi baada ya kuishambulia Iran.
Trump aliwataka watu kukaa majumbani mwao na kusema kuwa "Tukimalizana na oparesheni yetu, serikali itakuwa yenu muitawale wenyewe, na hii ni fursa ya kipekee ambayo imejitokeza."
Katika hotuba yake, Trump hakusema kuwa anapania kubadilisha mfumo wa utawala wa Iran.
Katika miaka ya hapo nyuma, Trump alikuwa akikashifu majaribio ya kuleta mabadiliko ya uongozi katika mataifa ya Mashariki ya Kati na kusema ukosefu wa uongozi dhabiti umesababisha kukuwa kwa makundi ya kigaidi eneo hilo na kuahidi kuwa akirejea madarakani "nitamaliza vita vya kiholela."
Lakini swali ni, Trump anamaanisha nini akisema anawaletea raia wa Iran uhuru? Je inamaanisha mabadiliko katika mfumo wa utawala, au itakuwa kama Venezuela?
"Si vita vya kubadilisha utawala"
Siku ya Jumatatu, siku ya tatu ya vita vya Iran,wizara ya ulinzi , White House, na wizara ya mambo ya kigeni nchini Marekani, walikuwa wanajaribu kujibu maswali kuhusu malengo yao ya vita hivyo pamoja na maswali mengine kuhusu uhalali wa vita hivyo.
Katika taarifa zao, viongozi wa Marekani walijikita sana katika kufafanua malengo yao ya kijeshi na kisiasa haswa katika utawala wa Iran siku za mbeleni.
Katika hotuba yake kuhusu malengo yao baada ya kuishambulia Iran, Trump alisema oparesheni hiyo ni ya kuondoa tishio la Iran kwa usalama wao kwa kuharibu vituo vyao vya wanajeshi wa maji, makombora, na silaha za nyuklia. Alisema si vita vya kubadili utawala ila "utawala tayari umebadilika"
Pete Hegseth, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alitumia neno "utawala wa zamani" akijibu maswali ya wanahabari.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa waziri wa ulinzi wa Marekani amesema hawabadilishi utawala wa Iran, katika upande mwingine wa Atlantiki, waziri mkuu wa uingereza alitoa onyo kuhusu kutumia mashambulizi ya angani kuleta mabadiliko ya utawala Iran.
Mafunzo waliyoyapata baada ya vita vya Iraq, "ni lazima tuwe na mipango dhabiti ya kuafikia malengo yetu," alisema Keir Starmer
Professa Robert Pip mhadhiri katika chuo kikuu cha Chicago na mtaalam wa masuala ya usalama anasema " katika miaka mingi ya vita, mashambulio ya angani yamefanikiwa pakubwa kuwaua viongozi, ila historia inaonyesha kuwa hakuna mashambulio ya angani yaliyochochea kubadilika kwa mfumo wa uongozi"
Pip anasema anaamini kuwa utawala huanguka baada ya majeshi yaliyo karibu na kiongozi wanaacha kumuunga mkono.
Uongozi mbadala kutoka nje au ndani ya nchi
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa mojawapo ya chaguo zilizo wazi kwa Marekani na Israel ni kuharibu na kulemaza kiini cha serikali, kisha kuunda mazingira yatakayoruhusu nguvu za ndani ya nchi kuchukua usimamizi wa taifa hilo.
Kulingana na Professa Javed Ali, anasema bado kuna sintofahamu na bado Washington na Tel Aviv hawajafanya uamuzi wao.
"Watatafuta chaguo ambalo halitakuwa na pingamizi kwao na kufanya kama Venezuela, au watachagua kuipindua kabisa serikali hiyo na kutafuta kiongozi mbadala"
Shirika la habari la Reuters, limetaja maafisa watatu wa Marekani, ambao wanasema wanauwezo wa kuipindua serikali hiyo ya kiislamu.
Shirika hilo linasema huenda jeshi la mapinduzi ya kiislamu la Iran la IRGC, likajisalimisha.
Bado hakuna dalili kutoka Marekani kuwa wamempta kiongozi mbadala nje ya Iran.
Katika taarifa ya pamoja kati ya Rais wa Marekani na Kansela wa Ujerumani, Trump alijibu swali la mwanahabari akikisia kuwa huenda akamuunga mkono mwanamfalme Reza Pahlavi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Siku ya Jumanne, utawala wa Trump ulifanya kikao na bunge la Congress, ambapo viongozi kadhaa wa Democrat walikashifu vikali mipango ya Trump kuishambulia Iran.
Trump alisema oparesheni hiyo huenda ikadumu kwa takriban wiki nne au tano.
"Oparesheni hiyo huenda ikachukua muda lakini haitachukua miaka"
Ujasusi wa Marekani na Israel wamekuwa wakifuatilia kwa karibu mashambulio ya Iran, na kutathmini jinsi ya kuendeleza vita hivyo, na hatari ya kutanua vita hivyo.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula












