Nani kumrithi Khamenei kama kiongozi mkuu wa Iran?

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei aliuawa katika shambulio la anga lililotekelezwa na ndege za kivita za Marekani na Israel katika makazi yake Tehran mnamo Februari 28.
Khamenei, aliyekuwa na umri wa miaka 86, amekuwa kiongozi mkuu wa Iran tangu 1989, alipomrithi mwanzilishi wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu, Ayatollah Ruhollah Khomeini.
Kabla ya hapo, alihudumu kama rais mara mbili, kuanzia 1981 hadi 1989.
Kufuatia kifo chake, serikali ilitangaza siku 40 za maombolezo ya kitaifa na siku saba za mapumziko, huku nchi hiyo ikiendelea kuwa vitani na Marekani na Israeli.
Maendeleo haya yamefufua mijadala kuhusu mrithi wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu - si tu baada ya kifo cha Khamenei, bali pia miongoni mwa baadhi ya vitisho vikubwa zaidi ambavyo utawala huo umekabiliana navyo tangu 1979, ikiwa ni pamoja na maandamano mabaya ya mwezi Januari, ambapo maelfu waliuawa, na hofu inayoongezeka ya mabadiliko ya utawala unaoungwa mkono na Marekani.
Katiba ya Iran inasemaje kuhusu mrithi wake?
Kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Iran, kiongozi anayefuata huchaguliwa na Baraza la Wataalamu (Assembly of Experts – AE), kundi la maulamaa wakuu 88 wanaochaguliwa kila baada ya miaka nane kupitia uchaguzi wa kitaifa.
Uchaguzi huo husimamiwa na Baraza la Walinzi (Guardian Council), ambalo ni chombo kinachopima na kuhakiki (kuchuja) wagombea wote kabla hawajaruhusiwa kushiriki.
Wale walio watiifu kwa kiongozi mkuu walishinda viti vyote katika uchaguzi wa 2024, huku viti vinne vilivyoachwa wazi na vifo vya wanachama - akiwemo Ebrahim Raisi - vitajazwa katika uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Mei 2026.
Kifungu cha 111 cha katiba kinasema kwamba baraza la mpito la watu watatu litachukua majukumu ya kiongozi mkuu hadi kiongozi mpya ateuliwe.
Baraza la uongozi wa mpito litakuwa na Rais Massoud Pezeshkian, Jaji Mkuu Gholamhossein Mohseni Ejei, na mwanasheria mmoja kutoka Baraza la Faragha.
Mjumbe wa tatu anateuliwa na Baraza Kuu, Kamati Kuu ya Upatanishi, inayoongozwa na Sadeq Amoli Larijani, ambaye wanachama wake wanateuliwa na kiongozi mkuu.
Mnamo Machi 1, Alireza Arafi - kasisi wa kihafidhina ambaye anaweza kuwa mgombea wa kuchukua nafasi ya kiongozi huyo wa kiroho - aliteuliwa kuwa mjumbe wa tatu wa baraza la uongozi wa mpito.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ali Larijani, katibu mwenye ushawishi mkubwa wa Baraza Kuu la Usalama wa Kitaifa na kaka mkubwa wa Sadeq Larijani, aliiambia televisheni ya serikali kwamba baraza hilo litafunguliwa Machi 1. Baadaye siku hiyo, Rais Pezeshkian alithibitisha kwamba baraza hilo limeanza kazi yake.
Ingawa AE inapaswa kumteua kiongozi mpya "haraka iwezekanavyo," hakuna tarehe ya mwisho iliyoainishwa kisheria. Ikiwa mgombea hatashinda wingi wa theluthi mbili, baraza la mpito linaweza, kwa nadharia, kutawala kwa muda usiojulikana.
Ingawa wanachama wake wote ni waaminifu kwa Khamenei, uwepo wa rais mtetezi wa mageuzi, kama Pezeshkian, unaweza kuleta mabadiliko madogo wakati wa nyakati ngumu.
Hatimaye, uamuzi wa Baraza la Wataalamu (AE) kuhusu kiongozi mkuu anayefuata utahitaji uratibu na Kikosi chenye nguvu cha jeshi la Kiislamu (IRGC) na mzunguko na ofisi ya ndani ya Khamenei.
Ingawa makamanda kadhaa wakuu wameuawa pamoja na Khamenei, maafisa wakuu wa IRGC ambao wanabaki katika nafasi zao wanaaminika bado wana ushawishi mkubwa kwani nchi iko vitani na ushawishi wake unaongezeka.
Mrithi yeyote bado atahitaji idhini ya vikosi hivi na vyombo vya usalama.
Kamati ndogo ya wanachama watatu ya AE inaripotiwa kufanya kazi kwenye orodha ya "siri kuu" ya wagombea watarajiwa, lakini usiri unaozunguka majadiliano yao umechochea uvumi.

Chanzo cha picha, KHAMENEI.IR
Ni nani wagombea wengine?
Wagombea kadhaa kutoka vyama vya kihafidhina na vya wastani wameondolewa katika kinyang'anyiro cha uongozi katika miaka ya hivi karibuni.
Miongoni mwao alikuwa aliyekuwa mkuu wa idara ya mahakama Sadeq Amoli Larijani na rais wa zamani Hassan Rouhani.
Baadhi ya wanachama wa AE pia wanachukuliwa kuwa wagombea, akiwemo Arafi, ambaye matarajio yake yanaonekana kuongezeka baada ya kuteuliwa katika baraza la uongozi la muda.
Kiongozi huyo wa kidini mwenye umri wa miaka 66, ambaye ana historia ndefu ya kushika nyadhifa alizoteuliwa na Khamenei, ni mkurugenzi wa taasisi zote za eimu ya kidini nchini humo, nafasi ya juu zaidi ya kidini nchini Iran.
Mwaka 2019, Khamenei alimteua katika Baraza la Walinzi (Guardian Council).
Baada ya uchaguzi wa Machi 2024, Arafi alipata nafasi muhimu katika AE, akawa makamu mwenyekiti wa pili.
Baadhi ya wanachama wa kihafidhina na wenye misimamo mikali wa AE, kama vile Naibu Mwenyekiti wa Kwanza Hashem Hosseini Boushehri, Mohsen Araki na Mohammad Mehdi Mirbaqeri, wanaripotiwa kuwa kwenye orodha ya wanaoweza kuchukua nafasi hiyo.
Hassan Khomeini, mjukuu wa Ayatollah Ruhollah Khomeini, ni mgombea anayependwa na makundi ya mageuzi na ya wastani.
Asili yake ya kidini na urithi wa familia ni mambo muhimu, lakini uzoefu wake mdogo wa kisiasa na uwepo wa wapinzani wenye nguvu unapunguza nafasi zake.
Aliwahi hata kuzuiwa kugombea katika uchaguzi wa AE wa mwaka 2016. Mustakabali wake unategemea mabadiliko ya mazingira ya kisiasa na iwapo watu wenye nguvu nchini Iran wanaweza kufikia mwafaka.














