Moja kwa moja, Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei ameuawa, televisheni ya serikali imesema

Awali, Trump alithibitisha kuwa Khamenei amefariki kupitia akaunti yake kwenye mtandao wa Truth Social.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Mariam mjahid, Ambia Hirsi & Asha Juma

  1. Mrithi wa Khamenei hakutajwa kwenye tangazo la kifo chake

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Taarifa kutoka Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, vyombo kadhaa vya habari vya serikali nchini Iran vimethibitisha kifo cha Ayatollah Khamenei.

    Rais wa Marekani Donald Trump saa chache zilizopita alisema Kiongozi Mkuu huyo aliuawa wakati wa shambulio la pamoja na Israel katika maeneo kadhaa kote Iran.

    Katika taarifa hiyo, haikutajwa ni jinsi gani Khamenei mwenye umri wa miaka 86 alivyofariki, au ni nani anayeweza kuchukua nafasi ya kiongozi.

    Jamaa wa Khamenei pia wameuawa katika mashambulizi hayo

    Hapo awali, vyombo vya habari vya serikali vilisema kwamba binti wa Khamenei, mkwewe na mjukuu wake pia waliuawa katika mashambulizi hayo.

    Kulingana na Shirika la Habari la Fars, ambalo lina uhusiano na Kikosi cha Revolutionary Guard, kuna ripoti kwamba mmoja wa mabinti wa Khamenei ameuawa pia.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Habari za hivi punde, Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei ameuawa, televisheni ya serikali imesema

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Televisheni ya taifa ya Iran imethibitisha kuwa Ayatollah Ali Khamenei ameuawa.

    Siku arobaini za maombolezo zatangazwa nchini Iran

    Katika hotuba ya machozi, mtangazaji wa televisheni ya serikali ametangaza kifo cha Khamenei na kusema nchi itaingia katika siku 40 za maombolezo.

    Jamaa za Khamenei pia waliuawa katika mashambullizi hayo.

    Kulingana na Shirika la Habari la Fars ambalo lina mafungamano na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kuna ripoti kwamba binti mmoja wa Khamenei ameuawa pia.

    Soma zaidi:

  3. CBS yasema maafisa 40 wa Iran wauawa katika shambulizi

    Chanzo cha habari cha kijasusi na chanzo cha kijeshi kimeambia mshirika wa vyombo vya habari wa BBC, CBS News, kwamba takriban maafisa 40 wa Iran wameuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Haijulikani wazi kama maafisa hao walikuwa katika eneo moja au tofauti.

    Walidai kwamba kiongozi mkuu wa Iran, Ali Khamenei, alikuwa miongoni mwa waliofariki, pamoja na kamanda wa Kikosi cha Revolutionary na waziri wa ulinzi.

    Iran bado haijathibitisha ripoti zilizoenea kuhusu kifo cha Khamenei.

  4. UAE yalaani shambulio la Iran

    Umoja wa Falme za Kiarabu umelaani mashambulizi ya Iran dhidi ya eneo lake, ukiita ni "ukiukaji wa uhuru wa kitaifa na sheria za kimataifa".

    Katika chapisho kwenye mtandao wa X, UAE inaita hatua ya kulipiza kisasi ya Iran kuwa kuongeza hatari na "kitendo cha uwoga" kinachotishia usalama wa raia na kudhoofisha utulivu.

    Wizara yake ya ulinzi inasema iko " katika tahadhari ya juu" na tayari kukabiliana na vitisho vyovyote.

    Inaongeza kuwa vikosi vyake vya ulinzi vimezuia makombora 137 ya balestiki na ndege zisizo na rubani 209 zilizorushwa kuelekea nchini.

    Kumi na nne kati ya ndege zisizo na rubani zilizoanguka ndani ya maeneo na maji ya nchi hiyo zilisababisha "uharibifu fulani", inasema.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Ziara ya Rubio kwenda Israel yafutwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio hatasafiri tena kwenda Israel siku ya Jumatatu "kutokana na hali ilivyo kwa sasa", ofisi yake imesema.

    Wizara ya mambo ya nje ilisema jana Rubio alikuwa amepangiwa kwenda Israel kujadili mada mbalimbali, ikiwemo Iran.

    "Kutokana na hali ilivyo kwa sasa, Waziri Rubio hatasafiri tena kwenda Israeli mnamo Machi 2," msemaji anasema.

  6. Habari za hivi punde, Trump asema Kiongozi Mkuu wa Iran amekufa

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Khamenei, mmoja wa watu waovu zaidi katika Historia, amekufa," Rais wa Marekani Donald Trump ameandika kwenye Truth Social.

    'Haki si kwa watu wa Iran pekee, bali kwa Wamarekani wote Bora' - Trump

    Katika akaunti yake kwenye mtandao wa Truth Social, Rais wa Marekani Donald Trump ameandika.

    "Hii si haki kwa watu wa Iran pekee, bali kwa Wamarekani wote Bora," amesema.

    "Hakufanikiwa kukwepa Majasusi wetu na Mifumo yetu ya Ufuatiliaji ya Kisasa, na, kwa ushirikiano wa karibu na Israeli, hakukuwa ambalo yeye, au viongozi wengine awaliouawa pamoja naye, wangeweza kufanya."

    "Hii ndiyo fursa kubwa zaidi kwa watu wa Iran kuirudisha Nchi yao," ameongeza.

    Awali, Rais Donald Trump wa Marekani alizungumza na NBC News kwa njia ya simu - na wamemuuliza kuhusu ripoti kwamba kiongozi mkuu wa Iran ameuawa na mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel.

    "Nimezungumza na watu wengi, tunahisi huu ni ukweli," Inaripotiwa Trump amemwambia mtangazaji wa Marekani.

    "Idadi kubwa ya viongozi wao pia wameuawa," aliongeza, akirudia kile alichoambia ABC News.

    Pia aliambia NBC News kwamba operesheni ya Marekani nchini Iran "tayari imefanikiwa".

    Trump asema 'viongozi wengi wa Iran wameuawa

    Awali, Rais Trump alizungumza na ABC News na kusema kwamba mashambulizi ya Marekani "tayari yamesababisha uharibifu mkubwa" na kuwa viongozi "wengi" wa Iran wameuawa.

    "Hatujui yote, lakini mengi yanajulikana," Trump amesema katika mahojiano ya simu. Rais pia ameongeza kuwa Marekani "ina maono mema" juu kundi lijalo la viongozi wa Iran.

    Alipoulizwa kuhusu ni nani atakayechukua nafasi ya Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei, Trump kisha ameiambia NBC: "Sijui, lakini wakati fulani watanipigia simu kuuliza ni nani ningependa."

    "Ninakuwa na mzaha kidogo ninaposema hivyo," Trump ameongeza:

    Trump alipoulizwa ikiwa ana 'uhakika' kiongozi mkuu wa Iran ameuawa

    Rachel Scott, mwandishi mkuu wa habari za kisiasa katika shirika la ABC News, amesema Donald Trump amemwambia tu kwamba "anaamini" kiongozi mkuu wa Iran amekufa.

    Alipoulizwa kama ana "uhakika", Trump inasemekana alisema: "Sitaki kusema chochote kwa uhakika hadi nitakapoona kwa maco yangu lakini tunaamini amekufa."

    "Na viongozi wao wengi wameuawa. Sio tu kutoka kwenye eneo moja bali pia kutoka kwenye maeneo mengine mawili ambayo pia tumeshambulia. Tulikuwa na taarifa nyingi za ujasusi hivyo basi, tunaamini viongozi wengi wameuawa."

    Soma zaidi:

  7. Ripoti ambazo hazijathibitishwa zasema kuwa kiongozi mkuu wa Iran "ameuawa

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Kufuatia Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu kusema "kuna dalili zinazoongezeka" zinazoonyesha kuwa kiongozi mkuu wa Iran "ameuawa"’, tunaona ripoti ambazo hazijathibitishwa kwamba ameuawa na mashambulizi ya Marekani na Israeli.

    Shirika la habari la Reuters, limemnukuu afisa mkuu wa Israeli, na kusema kuwa mwili wa Ayatollah Ali Khamenei umepatikana.

    Axios, imenukuu chanzo, na kusema balozi wa Israeli nchini Marekani Yechiel Leiter amewafahamisha maafisa wa Marekani kwamba Khamenei aliuawa katika shambulio lililofanyika kwenye makazi yake huko Tehran.

    Na vyanzo vingi vya Israeli, ikiwa ni pamoja na News 12 na Times of Israel, vinanukuu maafisa wa Israeli pia wakidai kwamba kiongozi huyo mkuu amefariki.

  8. Dalili zinaonyesha kuwa kiongozi mkuu wa Iran 'ameuawa' - Netanyahu

    .

    Chanzo cha picha, GPO

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amezungumzia shambulizi dhidi ya eneo la Iran la kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ambalo tuliliripoti mapema.

    ‘Kuna dalili zinazoongezeka zinazoonyesha kuwa "dikteta huyu" "ameuawa"’, Netanyahu amesema.

    Katika hotuba yake, Netanyahu amewaambia Wairan kuwa mashambulizi hayo yatawasaidia "kujiondoa katika udhalimu" na kuongeza kuwa wana "fursa moja tu" ya kupindua utawala wa Iran.

    "Nendeni mitaani kwa wingi mumalize kazi hii," Netanyahu amesema.

    Ni "wakati muafaka wa kuungana pamoja kwa ajili ya misheni ya kihistoria", Netanyahu ameongeza.

    Amemalizia hotuba yake kwa kuwataka raia wa Israeli kusikiliza ushauri wa usalama kutoka kwa Kamandi ya Nchi baada ya kupendekeza kwamba operesheni dhidi ya Iran itaendelea "kadiri itakavyohitajika".

    Soma zaidi:

  9. Mashambulizi mapya yaripotiwa Iran huku nayo ikifanya mashambulizi ya kulipiza kisasi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mtu mmoja ameiambia BBC Persian kwamba mlipuko mpya umesikika magharibi mwa Tehran.

    Shirika la habari la AFP linaripoti kwamba waandishi wake wamesikia "mfululizo wa milipuko mipya" katika mji mkuu. Hapo awali shirika hilo lilisema shirika la habari la Iran Fars lilikuwa likiripoti kwamba vitongoji viwili katika mji wa Bushehr kusini mwa Iran - kuliko kiwanda cha nguvu za nyuklia - "vililengwa na makombora".

    Shirika la Habari la Jamhuri ya Kiislamu (IRNA) linaloendeshwa na serikali ya Iran pia linaripoti kuhusu milipuko mipya mjini Tehran.

    Ingawa chanzo hakijajulikana mara moja, hii inakuja baada ya Marekani na Israel kuanzisha mashambulizi ya pamoja dhidi ya Iran mapema hii leo, na kusababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka Iran dhidi ya maeneo lengwa kote Mashariki ya Kati.

    Jeshi la Anga la Israeli pia limechapisha kwenye mtandao wa X, likisema "limeanzisha shambulio lingine la anga na linashambulia maeneo ya kurusha makombora na mifumo ya ulinzi katikati mwa Iran".

    Soma zaidi:

  10. Kuanzia Dubai hadi Doha, Iran yafanya mashambulizi Mashariki ya Kati

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Baada ya mashambulizi ya Marekani na Israeli dhidi ya Iran, hatua ya kulipiza kisasi ya Iran imeshuhudiwa kote Mashariki ya Kati - hasa katika maeneo yenye kambi za kijeshi za Marekani, au ambayo ni washirika wa Marekani:

    • Huko Dubai, UAE, mlipuko umeshuhudiwa katika hoteli ya Fairmont The Palm. Mamlaka ya Dubai imesema watu wanne wamejeruhiwa baada ya "jengo la eneo la Palm Jumeirah" kushambuliwa
    • Wizara ya ulinzi ya UAE pia ilisema imezuia wimbi jipya la makombora na ndege zisizo na rubani za Iran, baada ya kusema hapo awali kwamba nchi hiyo imekabiliwa na "shambulizi baya linalohusisha makombora ya Iran".
    • Huko Doha, Qatar, milipuko imeonekana kulenga kambi ya jeshi la anga ya al Udeid, kambi kubwa zaidi ya kijeshi ya Marekani katika eneo hilo.
    • Kambi ya Jeshi la Wanamaji la Marekani huko Bahrain " imeshambuliwa kwa kombora", kulingana na taarifa iliyonukuliwa na Shirika la Habari la Bahrain linaloendeshwa na serikali.
    • Milipuko ilisikika nchini Kuwait, na shirika la habari la eneo hilo Kuna, lilisema kwamba ndege isiyo na rubani iliyolenga uwanja wa ndege wa kimataifa ilisababisha "majeraha madogo kwa wafanyakazi kadhaa" huku uharibifu "mdogo" ukitokea kwenye kituo cha uwanja wa ndege.
    • Reuters imeripoti kwamba ulinzi wa anga wa Marekani ulidungua ndege isiyo na rubani juu ya kambi ya kijeshi ya Marekani karibu na Erbil, Iraq
    • Jordan - ambayo inapakana na Israeli - inasema kwamba vikosi vyake vya kijeshi vilidungua makombora mawili ya masafa marefu na kwamba vifusi vilianguka katika maeneo mbalimbali
    • Israel pia imeripoti wimbi la makombora ya Iran, huku ving'ora vikilia kote nchini. Jeshi la Israel linasema Iran inataka "kuwatisha raia na kuharibu maeneo yaliyo jirani"

    Soma zaidi:

  11. Waziri wa mambo ya nje wa Iran asema kiongozi mkuu yuko hai

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi amezungumza moja kwa moja na shirika la NBC News huku mtandao ukiendelea kuminywa kwa raia wengi nchini Iran.

    Araghchi anasema kwamba Iran "huenda imepoteza kamanda mmoja au wawili" lakini pia ameongeza kuwa kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, "yuko hai" kulingana na kile anachofahamu.

    Vyombo vya habari vya Iran hadi sasa vimekanusha kwamba maafisa na makamanda kadhaa wa Iran wameuawa, akiwemo rais na kamanda mkuu wa Jeshi.

    Araghchi amesema kwamba kipaumbele kwa Iran ni kupunguza mvutano na iko tayari kwa mazungumzo, mradi tu Marekani na Israel zisitishe mashambulizi yao.

    Huku akisema kwamba hakuna mawasiliano yoyote "hivi sasa", Araghchi ameongeza kwamba "ikiwa Wamarekani wanataka kuzungumza na sisi, wanajua jinsi wanavyoweza kuwasiliana na mimi".

    Iran na Marekani zimekuwa zikishiriki katika mazungumzo mapya ya nyuklia, huku duru ya hivi karibuni ikifanyika siku mbili zilizopita. Araghchi pia amethibitisha kwamba Iran inashambulia kambi za Marekani katika eneo hilo, lakini anaielezea kama kitendo cha "kujilinda".

  12. Habari ya wakati huu msomaji wetu. Leo tunaendelea na matangazo yetu maalum mubashara kukujuza kila kinachoendelea kuhusu mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Mimi ni Asha Juma. Karibu.

  13. Jeshi la Israel lasema limekamilisha "shambulio kubwa" dhidi ya Iran

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Jeshi la Israel lilitangaza kuwa limekamilisha "shambulio kubwa" dhidi ya utawala wa Iran.

    Taarifa ya jeshi ilisema: "Moja ya mashambulizi haya yalifanywa kwenye mfumo wa ulinzi wa anga wa juu (SA-65) huko Kermanshah magharibi mwa Iran."

    Taarifa hiyo iliendelea kusema: "Mashambulizi haya yalifanywa kwa lengo la kuanzisha na kuimarisha uhuru wa vitendo wa Jeshi la Anga la Israel juu ya anga ya Iran, ili kudhoofisha uwezo wa Walinzi wa Mapinduzi na vitisho dhidi ya eneo la ndani la Taifa la Israel."

    Soma zaidi:

  14. 'Vigogo kadhaa' wa utawala wa Iran wameuawa - Jeshi la Israel

    Afisa wa jeshi la Israel anasema "maafisa kadhaa wenye ushawishi" wa utawala wa Iran "wameuawa" katika shambulioyala leo.

    Afisa huyo anasema maeneo matatu ambapomaafisa wa serikali ya Iran walikuwa wamekusanyika yalishambuliwa kwa wakati mmoja wakati wa operesheni hiyo.

    Shambulio hilo lilipangwa "kwa muda wa miezi kadhaa", na ujasusi kubaini "fursa ya kuchukua hatua" wakati "maafisa wakuu wa serikali wangekutana".

    Wanaongeza kuwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limekuwa kifanya kazi "kwa ushirikiano wa karibu" na Jeshi la Marekani ili kupanga orodha "ya thamani" ya shabaha.

    "IDF iko tayari kushambulia Iran tena ikilazimika kufanya hivyo," wanasema.

  15. Waziri Mkuu wa Uingereza: Ndege zetu za kivita ziko angani kulinda watu wetu, maslahi na washirika wetu

    f

    Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, amesema katika hotuba ya televisheni kuwa ndege za kivita za nchi hiyo “ziko angani leo kama sehemu ya operesheni ya pamoja ya ulinzi wa kikanda ili kulinda watu wetu, maslahi yetu na washirika wetu.”

    Katika tamko lake la kwanza hadharani kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yaliyosababisha Tehran kurusha makombora kuelekea nchi mbalimbali katika eneo hilo, Starmer alisema hatua ya Uingereza “inaendana na sheria za kimataifa.”

    Kauli hiyo ilitolewa baada ya Starmer kuongoza kikao cha dharura cha mawaziri wakuu na maafisa waandamizi wa serikali, kinachojulikana kama kikao cha Cobra, kujadili maendeleo yanayoendelea na kuongezeka kwa mzozo katika Mashariki ya Kati.

    Soma Pia:

  16. Waandamanaji wakusanyika nje ya ubalozi wa Iran London kuunga mkono mashambulizi ya Marekani na Israel

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Katika eneo la katikati mwa London, umati wa watu na misafara ya pikipiki walikusanyika nje ya ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuonyesha uungwaji mkono wao kwa mashambulizi ya Marekani na Israel.

    Waandamanaji hao, wakiwa wamebeba picha za Reza Pahlavi, walikuwa wakipiga kelele za kauli mbiu kama “Iran idumu, Israel idumu.”

    Mwandishi wa habari wa BBC News, Winnie O’Dowd, aliyekuwepo katika mkusanyiko huo, amesema kuwa mapema alasiri kwa saa za eneo hilo, kundi la watu na msafara wa waendesha pikipiki walikusanyika nje ya ubalozi wa Iran kusherehekea na kucheza. Mlio wa pikipiki na kauli mbiu za “Iran idumu, Israel idumu” zilisikika kutoka kwa Wairani waliokuwa na shauku, wakiwa wamebeba picha za Reza Pahlavi, mwana wa Shah wa mwisho wa Iran.

    Kwa mujibu wa mwandishi huyo wa BBC, Davoud Pahlavi, binamu wa aliyekuwa mrithi wa ufalme, alikuwa miongoni mwa waliokuwapo katika sherehe hizo. Umati uliokuwepo ulionekana kwa kiasi kikubwa kumuunga mkono Pahlavi.

    Baadhi ya waliohudhuria walikuwa wakinywa kinywaji cha kienyeji cha Iran kiitwacho sagi, aina ya pombe inayotengenezwa kwa zabibu nyeusi au nyeupe za Shiraz.

    Wengine walionekana kuwa na wasiwasi kuhusu ndugu na jamaa zao ambao hawakuweza kuwasiliana nao tangu jioni ya siku iliyotangulia.

    Unaweza kusoma;

  17. Watu wanne wajeruhiwa katika shambulio lililofanywa Dubai

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Dubai imesema “tukio limetokea katika jengo lililopo eneo la Palm Jumeirah.”

    Kwa mujibu wa ofisi hiyo, vikosi vya uokoaji vilitumwa mara moja katika eneo la tukio na moto uliotokana na tukio hilo sasa “umedhibitiwa.” Watu wanne wamejeruhiwa na wamepelekwa hospitalini kwa matibabu.

    Taarifa hiyo inafuatia ripoti ya awali ya shahidi wa tukio, iliyosambazwa pamoja na picha inayoonyesha moshi katika eneo hilo, baada ya vyombo vya habari vya serikali ya Iran kudai kuwa shambulio lilikuwa limeanzishwa dhidi ya Dubai.

    Haijabainika wazi Iran inalenga nini hasa, ingawa kuna uwepo wa kijeshi wa United States katika nchi hiyo.

    Palm Jumeirah ni visiwa bandia vinavyojulikana kwa hoteli za kifahari na makazi ya hali ya juu.

    Soma zaidi:

  18. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana baadaye leo

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umeitishwa baadaye Jumamosi mjini New York.

    Mkutano huo umeombwa na Bahrain, Colombia, China, Russia na Ufaransa.

    Hii inakuja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kulaani "hatua ya kijeshi ya leo katika Mashariki ya Kati".

    Katika taarifa yake, amesema kuwa vitendo hivyo vinadhoofisha amani na usalama wa kimataifa na kutoa wito wa "kusitishwa mara moja kwa uhasama".

  19. Mwili wa mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wazikwa Pugu, Tanzania

    f

    Mwili wa Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, umezikwa katika Kituo cha Hija cha Pugu, jijini Dar es salaam, Tanzania.

    Kardinali Pengo alizikwa ndani ya kanisa dogo lililopo katika kituo hicho, katika ibada iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali, waumini na wananchi mbalimbali.

    Akizungumza wakati wa mazishi hayo, Makamu wa Rais wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi, alisema miongoni mwa mambo aliyokuwa akiyachukia Kardinali Pengo ni migogoro na mifarakano ya kisiasa, akisisitiza umuhimu wa kudumisha upendo, mshikamano na umoja wa kitaifa.

    Polycarp Kardinali Pengo aliyefariki usiku wa Alhamis Februari, 19, 2026, kama ilivyotangazwa na Askofu Mkuu wa Dar es Salaam Thaddaeus Ruwa'ichi kuwa Pengo alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete akiwa na umri wa takribani miaka 82.

    Alifahamika kwa tabia ya upole na kuzungumza taratibu hata pale alipozungumzia masuala nyeti na mazito ya kiimani au kuikosoa mifumo ya uongozi wa kisiasa, serikali na viongozi wake.

    Hata alipochokozwa alijibu kwa upole. Wakati mmoja, Askofu Josephat Gwajima wa kanisa la Ufufuo na Uzima alimtolea maneno makali, lakini Pengo alipoulizwa na chombo kimoja cha habari alijibu kuwa hamfahamu huyo askofu.

    Soma zaidi:

  20. Watu sita wafariki dunia baada ya helikopta kuanguka nchini Kenya

    f

    Chanzo cha picha, facebook

    Watu sita wamefariki dunia baada ya helikopta kuanguka na kulipuka kwa moto katika eneo la Chepkiep, Kaunti Ndogo ya Mosop, Kaunti ya Nandi, Jumamosi, Februari 28, 2026.

    Kulingana na mkuu wa polisi katika Kaunti hiyo Samuel Mukuusi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

    Hata hivyo utambulisho wa wahasiriwa wa ajali hiyi iliyitokea alasiri bado haujabainika.

    Kwa mujibu wa taarifa za awali, helikopta hiyo ilikuwa na abiria sita wakati ilipoanguka.

    Katika picha na video zilizoonekana na BBC, wakazi wanaonekana wakikimbilia eneo la tukio kusaidia katika juhudi za kuwaokoa manusura wowote.

    Kwa sasa, taarifa kutoka Nandi zinaeleza kuwa nambari ya usajili wa helikopta hiyo ni 5Y-DSB, inayomilikiwa na kampuni yenye makao yake katika Uwanja wa Ndege wa Wilson, Nairobi.

    Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa kufuatilia safari za ndege wa Flightradar24, chombo hicho ni aina ya Airbus Helicopters H125.

    Mamlaka imepata simu ya mkononi na SIM card mali ya Mhe. Johana Ng'eno, Mbunge wa Jimbo la Emurua Dikir, Ikiwa kwenye eneo la ajali.

    Vifaa sawia vya Amos Kipngetich Rotich, afisa wa Huduma ya Misitu nchini (KFS), pia vimepatikana.

    Vitambulisho vya abiria wengine wanne waliosalia bado havijathibitishwa.

    Tunafuatilia taarifa hii kwa kina ili kukufahimisha zaidi.