Je, Israel inahofia nini katika mazungumzo ya nyuklia ya Marekani na Iran?

.

Chanzo cha picha, AP

Muda wa kusoma: Dakika 5

Marekani na Iran zinatazamiwa kufanya mazungumzo kuanzia Jumamosi ijayo (Aprili 19) ili kuafikia makubaliano mapya kuhusu mpango tata wa nyuklia wa Iran.

Mwaka 2018, Donald Trump aliiondoa Marekani kutoka kwa makubaliano ya hapo awali ya nyuklia kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani na kuweka tena vikwazo vya kiuchumi kwa nchi hizo, hatua ilioikasirisha Iran.

Trump ameonya kuwa hatua za kijeshi zitachukuliwa iwapo mazungumzo haya hayatafanikiwa.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Pia unaweza kusoma

Kwa nini Iran hairuhusiwi kuwa na silaha za nyuklia?

Iran inasema mipango yake ya nyuklia ni kwa madhumuni ya kiraia pekee.

Nchi hiyo inasema haitengenezi silaha za nyuklia, lakini nchi nyingi na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), shirika linalosimamia nyuklia duniani, hazijashawishika.

Wakati vifaa vya siri vya nyuklia vilipogunduliwa nchini Iran mwaka 2002, mashaka yaliibuka juu ya nia ya nchi hiyo.

Kwa kufanya hivyo, Iran ilikiuka Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia (NPT), mkataba ambao nchi nyingi duniani, ikiwemo Iran, zimetia saini.

Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia unaruhusu nchi kote ulimwenguni kutumia teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni yasiyo ya kijeshi kama vile dawa, kilimo na nishati. Hata hivyo, mkataba huo hauruhusu uundaji wa silaha za nyuklia.

Je, mpango wa nyuklia wa Iran umeendelea vipi?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tangu Marekani ilipojitoa katika mapatano ya sasa ya nyuklia, yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA), mwaka 2018, Iran imevunja ahadi kuu za kulipiza kisasi uamuzi wa kuviwekea tena vikwazo.

Iran imeweka maelfu ya vinu vya kisasa vya kurutubisha madini ya uranium, ambavyo vimepigwa marufuku na Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja.

"Silaha za nyuklia zinahitaji urani iliyorutubishwa kwa asilimia 90. Chini ya Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja, Iran iliruhusiwa kumiliki kilo 300 pekee za uranium iliyorutubishwa hadi 3.67%. Hii inatosha kwa nishati ya nyuklia ya jumla na madhumuni ya utafiti, kiasi hiki hakitoshi kuzalisha silaha za nyuklia."

Lakini mwezi Machi 2025, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki liliripoti kwamba Iran ilikuwa na takriban kilo 275 za uranium iliyorutubishwa hadi 60%. Ikiwa Iran ingerutubisha uranium hata zaidi, hiyo kinadharia ingetosha kutengeneza takriban nusu dazeni ya silaha.

Kwa nini Marekani ilijiondoa kwenye mkataba wa nyuklia?

Tangu mwaka 2010, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, na Marekani zimeiwekea Iran vikwazo vikali vya kiuchumi kutokana na tuhuma kwamba inatumia mpango wake wa nyuklia kutengeneza bomu la nyuklia.

Vikwazo hivi vya kiuchumi viliizuia Iran kuuza mafuta kwenye masoko ya kimataifa. Pia walizuia mali ya kigeni ya dola bilioni 100 nchini humo. Hii ilisababisha mdororo mkubwa wa kiuchumi kwa Iran. Thamani ya sarafu ya Irani ilishuka hadi chini kabisa, na kusababisha mfumuko wa bei kuongezeka.

Mwaka 2015, Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani (Marekani, China, Ufaransa, Russia, Ujerumani na Uingereza) yalifikia makubaliano yaliyoitwa Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA) baada ya mazungumzo ya miaka mingi.

Pamoja na vikwazo vilivyowekwa kwa mpango wa nyuklia wa Iran, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ulipewa ufikiaji wa vifaa vyote vya nyuklia vya Iran na kukagua maeneo yanayotiliwa shaka.

Kwa upande wao, walikubali kuondoa vikwazo vya kiuchumi kwa Iran. Makubaliano ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji yalibuniwa kudumu kwa miaka 15, ambapo vikwazo vingeisha muda wake.

Wakati Donald Trump alipoingia madarakani mwaka 2018, aliiondoa Marekani, ambayo ilikuwa nguzo muhimu ya makubaliano hayo, kutoka kwa makubaliano hayo.

Ameyataja mapatano hayo kuwa mabaya kwa sababu si ya kudumu na wala hayakushughulikia masuala mengine ikiwemo mpango wa makombora ya balistiki ya Iran.

Trump alirejesha vikwazo vya Marekani kama sehemu ya kampeni ya "shinikizo la juu" ili kuilazimisha Iran kufanya mazungumzo ya makubaliano mapya na ya kina.

Washirika wa Marekani, kama Israeli, hawakupenda mpango huo, kwa hivyo Trump alisitisha makubaliano ya nyuklia ya Iran.

Israel ilionya kuwa Iran bado inaendeleza mpango wa siri wa silaha na kwamba Iran itatumia mabilioni ya dola itakazopokea kutokana na kuondolewa vikwazo ili kuimarisha operesheni zake za kijeshi.

Marekani inataka nini?

.

Chanzo cha picha, Reuters / Getty Images

Tangazo la Trump la mazungumzo na Iran liliishangaza Israel. Kwa muda mrefu amesema atafuata mpango "bora" kuliko Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja. Hata hivyo, Iran hadi sasa imekataa kufanya mazungumzo ya makubaliano hayo.

Trump alikuwa ameonya hapo awali kwamba Iran ingeshambuliwa kwa bomu ikiwa haitakubali makubaliano mapya.

Mshauri wa usalama wa taifa wa Trump, Mike Waltz, amesema anataka "kusambaratisha kabisa" mpango wa nyuklia wa Iran. Amebainisha kuwa, urutubishaji wa nyuklia wa Iran unapaswa kuzingatiwa kuwa ni mpango wa mkakati wa makombora.

Wakati Donald Trump amesema kutakuwa na "mazungumzo ya moja kwa moja", Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi alisema mazungumzo ya Oman hayatakuwa ya moja kwa moja.

Amesema Iran iko tayari kuzungumza na Marekani, lakini Trump lazima kwanza aihakikishie kwamba hatua za kijeshi hazitachukuliwa.

Je, hofu kuu ya Israeli ni ipi?

Baada ya tangazo hilo la Trump, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema kuwa ni makubaliano tu ya Iran kuachana kabisa na mpango wake wa silaha za nyuklia ndiyo yatakubalika.

"Tutaingia, chini ya uangalizi na usimamizi wa Marekani, kulipua vinu vya nyuklia na kuharibu vifaa vyote," aliongeza.

Wasiwasi mkubwa wa Israel ni kwamba Trump atakubali maafikiano bila ya Iran kujisalimisha kikamilifu, hatua ambayo anaweza kuyaonyesha kuwa ni ushindi wa kidiplomasia.

Israel, ambayo haijatia saini Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia (NPT), inaaminika kumiliki silaha za nyuklia, madai ambayo Israel haidhibitishi wala kukanusha.

Israel inaamini kuwa Iran yenye silaha za nyuklia ambayo haikubali uwepo wa Israel itakuwa tishio kubwa kwa Israel.

Je, Marekani na Israel zinaweza kuishambulia Iran?

Marekani na Israel zina uwezo wa kijeshi kushambulia miundombinu ya nyuklia ya Iran, lakini operesheni kama hiyo itakuwa ngumu na ya hatari, na matokeo yake hayana uhakika.

Maeneo makuu ya nyuklia yamezikwa chini ya ardhi na yanaweza kufikiwa tu kwa kuyalipua kwa mabomu yenye nguvu sana. Ingawa Marekani inamiliki mabomu haya, Israel haijulikani kuwa nayo.

Iran hakika itajilinda yenyewe, ambapo ni pamoja na kushambulia mali ya Marekani katika eneo hilo na kurusha makombora kwa Israeli.

Ili kukabiliana na vitendo hivyo, Marekani italazimika kutumia kambi zake za kijeshi na meli za kubeba ndege za kivita katika Ghuba.

"Lakini ingawa nchi kama Qatar zina kambi kubwa ya anga ya Marekani, zinaweza zisiisaidie Marekani kushambulia Iran kwa kuhofia kulipizwa kisasi."

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi