Silaha za kivita zilizofichwa: Je, Iran ilitumaje silaha kupitia Syria ili kukabiliana na Israel?

Chanzo cha picha, RT
Oktoba 1, 2024. Video isiyo ya kawaida inasambaa katika mtandao wa vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.
Ni uwanja wa ndege wa kimataifa wa Syria ambao uligeuka kuwa kambi kubwa ya kijeshi ya Urusi tangu mwaka 2015.
Katika matukio yaliyorekodiwa na kamera, ndege ya Boeing inaonekana ikitua, ambapo nembo ya shirika la ndege la Iran pia inaonekana.
Wafanyakazi wanatoa idadi kubwa ya mizigo kutoka ndani ya ndege, ambapo wanaonekana watu wakiwa wamevalia mavazi ya kijeshi yenye alama ya askari wa Jeshi la Urusi.
Mizigo iliyojaa mablanketi ya kijani yanaonekana mbele ya kamera.
Siku chache baadaye, shirika lisilo la kiserikali (NGO) nchini Syria linatangaza kwamba Urusi imepeleka msaada kwa wahamiaji.
Blanketi za kuzuia milipuko
Lakini siku mbili baadaye, simulizi mpya inatokeza, ikiripotiwa na vyombo vingi vya habari vya Kiarabu na Magharibi.
Mnamo Oktoba 3, inaripotiwa kuwa Jeshi la Anga la Israeli lililenga kambi ya kijeshi ya Urusi ya Hmeimim nchini Syria.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa kivita, picha zilizotolewa baada ya shambulizi zilionyesha wazi si tu moto bali pia milipuko ya pili.
"Kila mtu anajua kwamba mablanketi haya yanalipuka vizuri," vyanzo vinavyofahamika na hali ya kambi ya Urusi huko Hmeymim viliambia BBC, vikizungumza kwa sharti la kutotajwa majina.

Alipoulizwa ikiwa Iran ilikuwa ikituma silaha au kitu kinachofanana na hicho kupitia vikosi vya Urusi, alijibu, "Unatarajia majibu gani? Mablanketi yalilipuka kwa namna iliyoleta uharibifu mkubwa kiasi kwamba kambi ilikuwa imeharibiwa kabisa."
Izingatiwe kwamba Urusi na Iran zinapoteza ushawishi wao nchini Syria baada ya kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad, nchi ambayo ni muhimu sana kwao katika eneo la Mashariki ya Kati.
Katika ripoti hii, BBC inachunguza usafirishaji wa siri wa silaha kupitia Syria wakati wa utawala wa Bashar al-Assad na ushirikiano kati ya Iran na Urusi kuhusu jambo hili.
Mashirika ya ndege ya Iran ya Fars Qeshm na Jeshi la Iran
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Shirika la ndege la Fars Qeshm la Iran linafanya kazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Imam Khomeini. "Shirika hili linaonekana kuwa ya kibinafsi, lakini kwa ukweli linamilikiwa na IRGC, Jeshi la Mapinduzi la Iran," alisema mtaalamu wa anga, akizungumza kwa sharti la kutotajwa majina.
Anaongeza kuwa kampuni nyingi nchini Iran ambazo zinahesabiwa kama za kibinafsi, kwa hakika zinamilikiwa na serikali.
"Kawaida, shughuli za Kampuni ya Ndege ya Fars Qeshm hufanywa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Imam Khomeini huko Tehran na vifaa vyote vya kijeshi vinatumwa au kupokelewa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mehrabad huko Tehran.
Hakuna usafirishaji wa kimataifa unaweza kufanyika kutoka Urusi au nchi nyingine kupitia Mehrabad, wala mablanketi wala msaada wa kibinadamu, ni usafirishaji wa kijeshi wa Iran pekee."
Mnamo 2018, Fox News iliripoti kwa mara ya kwanza kuhusu uwezekano wa ushiriki wa kampuni ya Fars Qeshm Airlines katika madai ya kupeleka silaha kwa wapiganaji wa Hezbollah nchini Lebanon.
Mtandao huo uliripoti, kwa kutaja vyanzo vya upelelezi kutoka Magharibi, kwamba Iran ilikuwa ikitumia njia zisizo za kawaida.
Kwa mfano, moja ya ndege za Fars Qeshm zinazotoka Tehran hadi Damascus ilichukua njia isiyo ya kawaida kupitia kaskazini mwa Lebanon.
Ripoti za upelelezi zilionyesha kwamba ndege hiyo ilikuwa inabeba vipengele vya silaha. Ndege nyingine, iliyopangwa kuruka moja kwa moja kutoka Tehran hadi Beirut, pia ilichukua njia isiyo ya kawaida upande wa kaskazini mwa Syria.
Kama Fox News ilivyoripoti, Shirika la Ndege la Fars Qeshm, ambalo lina uhusiano na Jeshi la Mapinduzi, lilifungwa mnamo 2013 lakini lilianza tena kazi mnamo 2017. Mtandao wa kituo hicho uliripoti kwamba shirika hilo linatumika kwa magendo ya silaha na kwamba wawakilishi wa IRGC wanafanya kazi katika shirik ahilo.
Uhusiano kati ya Shirika la Ndege la Fars Qeshm na Walinzi wa Mapinduzi umevuta hisia za waangalizi wa Magharibi.
Mnamo mwaka wa 2019, ndege mbili za mizigo za kampuni hiyo ziliwekwa kwenye orodha ya vikwazo vya Marekani.
Fars Qeshm ina ndege mbili za mizigo, moja ambayo haijasafiri kwa miaka mitatu iliyopita.
Ndege nyingine - iliyobeba misaada ya kibinadamu - iliruka hadi mji wa Latakia nchini Syria mara nne mwaka wa 2024.
Safari yake ya mwisho ilikuwa Oktoba 13.
"Kesi ya kampuni ya Fars Qeshm sio ya kipekee," mtaalamu wa Mashariki ya Kati Nikita Samgin aliambia BBC katika mahojiano. "Kampuni nyingi za Iran ziko chini ya vikwazo vya Magharibi, na nyingi zimekuwa zikitumika katika masuala ya kijeshi kwa namna moja au nyingine."
"Ina maana kwamba Urusi iliruhusu Wairani kutumia kambi yake ya anga kwa sababu vinginevyo Israeli ingeweza kuwashambulia kila wakati," Samgin alisema.
Kulingana na yeye, Iran pia ilikuwa na njia ya kupitishia vifaa ardhini ambayo Israeli ilishambulia mara kwa mara, lakini shehena nyingi zilienda Syria na Lebanon na hazikupitishwa kupitia vituo vya Urusi.
Anasema kwamba kama Iran mara kwa mara inatumia kituo cha Hmeimim kama njia ya kusafirisha mizigo, ilikuwa ni kwa ajili ya "mambo yasiyo na umuhimu" na kwamba njia ya kupitisha vifaa nchi kavu na uwezekano wa usafiri wa baharini ulikuwa muhimu zaidi. "Iran sasa imepoteza karibu kila kitu," Samgin alisema.
Ndege za siri
Mbali na viwanja vikuu vya ndege vya Iran, ndege hiyo, Boeing 747-281F yenye namba ya usajili EP-FAB, inayomilikiwa na kampuni ya Fars Qeshm, pia imefanya safari mara kadhaa kwenda Afrika, ikiwemo Eritrea (ambako ilitua ikiwa na kipima-mwelekeo chake) na Port Sudan.
Eritrea imetawaliwa kidikteta na Isaias Afwerki kwa zaidi ya miaka 30, na Sudan imetawala na baraza la kijeshi la mpito linaloongozwa na Abdel Fattah Abdelrahman al-Burhan tangu mapinduzi ya 2019.
Nchi hizi mbili zina makubaliano ya usambazaji wa silaha na Urusi. Mnamo 2017, karibu nusu ya silaha zote zilizokuwa zikiletwa Khartoum zilikuwa zikitoka Urusi, na makubaliano yalitiwa saini kuanzisha kambi kwenye Bahari ya Shamu kwa meli za Urusi, ikiwa ni pamoja na zile zinazotumia nishati ya nyuklia.
Mwanzo wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, Eritrea ilipiga kura dhidi ya azimio la Umoja wa Mataifa linalokemea uvamizi na kumega Majimbo ya Donetsk na Luhansk. Sudan haikujiunga na azimio hilo.
"Tuligundua uwepo wa ndege kadhaa za Iran katika uwanja wa ndege wa Hmeimim mwanzoni mwa mwaka wa 2023, na ndege hizi zilifahamika kubeba silaha kote kwenye eneo hilo," alisema Sarit Zahavi, aliyekuwa kamanda mstaafu wa jeshi la Israeli, mtaalamu wa upelelezi wa kijeshi na sasa mwasisi na mkuu wa kituo cha utafiti cha Israeli Alma, aliiambia BBC.

Chanzo cha picha, Morteza Nikoubazl_NurPhoto via Getty Images
"Israeli ilishambulia viwanja vingine vya ndege nchini Syria, ikiwemo Damascus na Aleppo, hivyo ndege hizi hazingeweza kutua huko, hivyo walitafuta njia mbadala," alisema Zahawi.
Aliongeza kuwa, Kituo cha Alma kiligundua kutua kwa ndege za Iran katika uwanja wa ndege wa Hmeimim mwaka wa 2023, na kwamba Wa-Iran wanaweza kutumia kambi hiyo kusafirisha silaha, na kwamba Warusi wangeweza kutoa ulinzi usio wa moja kwa moja.
"Alipoona ndege zisizo na rubani za Iran nchini Ukraine, mara moja alijiuliza Urusi ingelipa vipi. Kitu cha kwanza kilichokuja akilini mwangu ni kwamba makubaliano haya yalifanywa kupitia Syria."
Mkuu wa Kituo cha Alma aliongeza kuwa "Iran kimsingi ilitumaini kupata aina fulani ya kinga (kutoka kwa mashambulizi ya Israeli) kwa kushirikiana na Warusi kwenye kambi hiyo, tumaini ambalo mwishowe halikutimia."
Zahawi hajui ikiwa Urusi pia ililazimika kulinda ndege za Iran dhidi ya mashambulizi ya Israeli chini ya masharti ya makubaliano. Anasema, "Israeli haina haja ya kushambulia Urusi nchini Syria."
"Walikuwa wakichukua hatua kwa muda kuhakikisha kwamba Warusi hawadhuriki na mashambulizi ya Israeli dhidi ya Syria."
Ameongeza kuwa, jeshi la Israeli na vikosi vya Urusi vina njia maalum ya mawasiliano, na ukweli kwamba Warusi hawajapata madhara yoyote katika mashambulizi ya Israeli hadi sasa inaonyesha kuwa njia hii ya mawasiliano inafanya kazi ipasavyo.
Zahawi hakuweza kufafanua ni asilimia ngapi ya usafirishaji wa silaha za Iran zilihamishwa kupitia Hmeimim, lakini njia hii haikuwa chaguo pekee.
Iran pia ilituma silaha kupitia mpaka wa Syria-Lebanon. Mwanzoni mwa Oktoba, jeshi la Israeli lilitangaza kwamba liliharibu handaki iliyokuwa na urefu wa kilomita tatu na nusu kwenye mpaka wa Syria-Lebanon ambayo walisema ilikuwa inatumiwa kusafirisha silaha kwenda kwa Hezbollah.
Zahawi alisema, "Ushirikiano wa Iran na Urusi katika sekta ya usambazaji wa silaha sio jambo jipya, lakini kilichojitokeza ni kwamba sasa Urusi inanunua silaha kutoka Iran." Anaamini kuwa nchi hizo mbili zimekaribiana zaidi kutokana na matatizo ya kifedha.
Iran, Urusi, China, Korea Kaskazini, Syria, na Venezuela (nchi zilizoathiriwa na vikwazo) hufanya biashara kati yao na wamekuwa wakijaribu kuunda mifumo mbadala ya kiuchumi ili kuepuka vikwazo.
Iran na wawakilishi wake, kama Hezbollah wa Lebanon, walisaidia utawala wa Assad wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria. Utawala wa Assad ulikuwa mmoja wa wahusika muhimu katika "eneo la upinzani" lililoanzishwa chini ya udhamini wa Iran.
Hezbollah ilikuwa mshirika muhimu wa jeshi la Syria na ilifanya kazi kwa karibu na vikosi vya Urusi nchini Syria, lakini msimamo wa kundi hilo ulidhoofika sana mwaka jana na lilipata hasara kubwa nchini Lebanon kutokana na mashambulizi ya Israeli. Udhaifu wa Hezbollah unachukuliwa kuwa moja ya sababu za kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad.
"Sehemu kubwa ya silaha ambazo zilikuwa mikononi mwa serikali ya Syria sasa zimeharibiwa," anasema Nikita Samgin.
Baada ya kuanguka kwa utawala wa Assad, Israeli pia ililenga maghala ya silaha ya Syria.
Maafisa wa Israeli wamesema kuwa waliharibu asilimia 80 ya silaha za Syria.
Kwa msaada wa Ilya Barabanov. Serikali ya Urusi imeongeza Anastasia Lotarieva na Ilya Barabanov kwenye orodha ya 'maafisa wa kigeni'. BBC inapinga uamuzi huu mahakamani.















