Waziri wa Ulinzi wa Israel: 'Iran itajipata ikiwa kama Gaza na Lebanon'

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant aliionya Iran kuwa "ikiwa Jamhuri ya Kiislamu inataka kuidhuru Israel, huenda ikaathirika sawa na Gaza au Beirut." Kwa upande mwingine, kamanda wa Jeshi la Wanamaji la IRGC anasema, "Tumeandaa mazingira ya kukabiliana na adui wetu."
Akizungumzia shambulio la hivi karibuni la makombora dhidi ya Israel, Bwana Gallant amesema Iran ililenga vituo viwili vya jeshi la anga la Israel, lakini "Wairani hawakuharibu zana zetu za jeshi la anga, hakuna ndege iliyoharibiwa, na hakuna kikosi cha anga kilicholemazwa."
"Yeyote anayefikiria kujaribu kutudhuru kutatuzuia kuchukua hatua anapaswa kuangalia kile ambacho tumefanikiwa huko Gaza na Beirut."
Katika siku zilizopita, baada ya shambulio la pili la moja kwa moja dhidi ya Israeli, ambalo Iran iliita kama kulipiza kisasi, hali ya wasiwasi wa vita kuzuka imeongezeka.
Waziri Mkuu wa Israel amelitaja shambulizi la hivi majuzi la IRGC "moja ya mashambulio makubwa zaidi ya makombora ya balestiki katika historia" na kusema kuwa Iran italipa gharama yake.
Iran inasema kuwa shambulio la pili la moja kwa moja dhidi ya Israel lilikuwa ni kujibu mauaji ya Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas mjini Tehran, na mauaji ya Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hezbollah nchini Lebanon, na Brigedia Jenerali Abbas Nilfroushan, mmoja wa makamanda wakuu wa Jeshi la Quds la IRGC huko Dahiya, Beirut
Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la IRGC: Tumeandaa mipango tofauti kwa Netanyahu kucheza na moto
Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran IRGC amesema kwamba mipango tofauti imeandaliwa kwa ajili ya Netanyahu kucheza na moto.
Alireza Tangsiri alikiambia kituo cha habari cha Iran cha lugha ya Kiarabu, Al-Alam Sedav-Sima kwamba anaonya "maadui" ikiwa wanataka "kucheza na moto" katika eneo hilo, watachukuliwa hatua "madhubuti". Wakati huo huo, Bw. Tangsiri alisema kwamba ikiwa "maslahi yetu ya kitaifa na Kiislamu hayataathiriwa, hatutaonyesha hisia yoyote."
Kamanda huyo wa Jeshi la Wanamaji la IRGC alisisitiza kwamba kikosi hicho kinajitayarisha kwa hali yoyote: "Moja ya kesi hizi ni Netanyahu kucheza na moto na kuwasha moto wake, na hata tumeandaa mafunzo tofauti kwa hilo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa mafuta wa Iran nje ya nchi; Je, miundombinu ya mafuta ya Iran iko hatarini?
Waziri wa Mafuta wa Iran Hassan Paknejad alizuru kisiwa cha Kharg kutembelea vituo vya mafuta na kukutana na kamanda wa kitengo cha 4 cha jeshi la Wanamaji la IRGC.
Katika mkutano huo, waziri wa mafuta wa Iran alimsifu Mohammad Hossein Bargah kwa "kudumisha usalama wa majukwaa ya Pars Kusini".

Chanzo cha picha, Fararu
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kitengo cha nne cha Jeshi la Wanamaji la IRGC (Tharullah) linawajibika kwa ulinzi na usalama wa eneo muhimu, ikiwa ni pamoja na majukwaa ya mafuta ya Pars Kusini na vifaa vya pwani.
Kisiwa cha Kharg ndicho kituo kikuu cha mauzo ya mafuta nchini Iran na wakati wa vita vya miaka minane vya Iran na Iraq, kililengwa mara kwa mara na Jeshi la Wanahewa la Iraq.
Frank Gardner, mwandishi wa masuala ya usalama wa BBC, anasema kuwa ulipuaji wa bomu mjini Kharg utakuwa mgumu, kwa sababu ndege za Israel zitalazimika kupita katika anga ya nchi za Kiarabu au kupitia rasi nzima ya Arabia, jambo zitahitaji kujazwa mafuta.
Safari ya bwana Paknejad katika kisiwa cha Kharg imefanyika huku kukiwa na uvumi kuhusu uwezekano wa Israel kushambulia vituo vya mafuta vya Iran.
Ali Fadavi, Naibu Amiri Jeshi Mkuu wa IRGC alionya siku mbili zilizopita kwamba iwapo Israel "itafanya makosa, tutalenga vyanzo vyote vya nishati, mitambo ya nishati, na mitambo yote ya kusafisha na gesi ya utawala huu."
"Iran ni nchi kubwa na ina vituo vingi vya kiuchumi, wakati Israel ina mitambo mitatu ya kuzalisha umeme na mitambo kadhaa ya kusafisha mafuta. "Tunaweza kulenga haya yote kwa wakati moja."
Bw. Fadavi alikuwa miongoni mwa waliokuwepo katika chumba cha vita wakati Iran iliposhambulia Israel wiki jana
Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Yusuf Jumah












