Je, jeshi la Israel lina nguvu ya kupigana na maadui wengi kwa wakati mmoja?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Katika wiki chache zilizopita, Jeshi la Ulinzi la Israel limekuwa likifanya mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati.
    • Author, Fernando Paul
    • Nafasi, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Orodha ya pande zinazopigana na Israeli ni ndefu: Hamas huko Gaza, Hezbollah huko Lebanon, Wahouthi huko Yemen, Waislam wa Shia huko Iraqi , Syria, na Iran.

Katika wiki moja iliyopita, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilianzisha mashambulizi ya ardhini dhidi ya Lebanon, huku yakishambulia kwa mabomu maeneo mbalimbali nchini Yemen na kuendelea na mashambulizi yake ambayo tayari yameendelea huko Gaza.

Iran, mshirika na muungaji mkono wa kundi lenye silaha la Hamas, Hezbollah, Houthis na makundi mengine ya Shia walilipiza kisasi kwa makombora yaliyolenga miji ya Israel ya Jerusalem na Tel Aviv. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikuwa amesema kwamba jibu mwafaka litatolewa.

"Iran italipa gharama kubwa," alionya.

Tarehe 7 Oktoba 2023, shambulio la kushtukiza la kundi la wapiganaji la Hamas kwenye maeneo ya Israeli liliua karibu watu 1,200. Akijibu Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu alianzisha mashambulizi akisisitiza lengo lake la kuunda "utaratibu mpya" katika Mashariki ya Kati.

Matokeo yake , zaidi ya watu elfu 41 walikufa huko Gaza. Na nchini Lebanon, idadi tayari imezidi 2,000, maafisa wanasema.

Haya yote sasa ni matukio hatari zaidi katika historia ya hivi karibuni ya Mashariki ya Kati, anasema mwandishi wa usalama wa BBC Frank Gardner.

Lakini swali linalojitokeza kutokana na migogoro hii ni jinsi gani inawezekana kwa Israel kuwa katika vita dhidi ya mashirika mengi kwa wakati mmoja? Je, Israeli ina nguvu za kijeshi kufanya hivyo?

"Mashambulizi ya hivi punde yanaonyesha jinsi huduma za kijasusi za Israel na vikosi vya kijeshi zilivyo na uwezo, lakini pia zina kikomo. Kwa kuwa mashirika mengi yanapigana, itakuwa vigumu zaidi kwa Israel kuchukua hatua za kupambana," Shaun Sheikh, mtaalam wa ulinzi wa makombora na mwanachama wa Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa, aliiambia BBC Mundo.

Pia unaweza kusoma

Nguvu ya kijeshi ya Israeli ikoje?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Jeshi la Israel linajulikana duniani kote kwa teknolojia ya hali ya juu na uwezo wake wa hali ya juu.

Lakini data inahitaji kuzingatiwa na kuchambuliwa ili kujua hali yake halisi.

Kufikia 2019, Israeli imetenga dola za Kimarekani milioni 20,000 kila mwaka kwa jeshi, kulingana na data ya Benki ya Dunia kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati (IISS).

Kulingana na data ya hivi punde zaidi ya Benki ya Dunia, Iran imetenga takriban dola bilioni 7 za Marekani kwa matumizi yake ya kijeshi mwaka wa 2022. Israel inatumia mara mbili zaidi ya hiyo.

Hii inaipa Israeli fursa kubwa katika mzozo wowote na kuifanya kununua au kutenegeneza vifaa vya kijeshi vya kisasa.

Israel inatumia katika sekta yake ya ulinzi mara mbili zaidi ya Iran kama asilimia ya jumla ya pato la taifa (GDP).

Kulingana na takwimu za hivi punde kutoka Benki ya Dunia, Israel inatenga asilimia 4.5 ya Pato la Taifa kwa sekta ya ulinzi. Iran inachangia asilimia 2.6, Lebanon asilimia 3.4 na Syria asilimia 4.1 ya pato la taifa.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Moja ya nguvu muhimu za kijeshi za Israeli ni jeshi lake la anga

Kulingana na data kutoka kwa Taasisi ya Mafunzo ya Kimkakati ya Kimataifa, Israeli ina ndege za kivita 340 ambazo ziko katika hali ya kusubiri.

Hizi zitakuwa faida kubwa kwa mashambulizi ya anga ya Israel, anasema Aidan Shamir, mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati cha Begin-Sadad katika Chuo Kikuu cha Israel cha Bar Ilan.

"Kwa msaada wa jeshi lake la anga, Israel inaweza kulipua sehemu yoyote ya Mashariki ya Kati," aliambia BBC Mundo.

Israel ina ndege za kivita za F-15, ndege za siri za hali ya juu za F-35 na helikopta za mashambulizi ya haraka.

Aidha jeshi la Israel lina magari ya kivita, vifaru, mizinga, meli za kivita na ndege zisizo na rubani.

"Nadhani jeshi la Israel ni mojawapo ya vikosi vya kisasa vya kijeshi. Nchi ina uzoefu mkubwa, hasa baada ya vita dhidi ya Hamas huko Gaza," anasema Aidan Shamir.

Hasa, Mossad ya Israel, shirika la kijasusi linaloaminika kuhusika na mlipuko wa pager na walkie-talkies nchini Lebanon mwezi Septemba, lina nguvu nchini humo.

Kwa upande mwingine, mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga kama Iron Dome na David Sling ina jukumu muhimu katika ulinzi wa Israeli. Mifumo hii imezuia mashambulizi mbalimbali, kama vile shambulio la anga la Oktoba 1 dhidi ya Israel na Iran. Mifumo hii ya makombora ina uwezo wa kukatiza na kuharibu makombora ya adui.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Iron Dome ni mfumo wa ulinzi unaoweza kuzuia na kuharibu roketi zilizorushwa dhidi ya Israeli

Vikosi vya ardhini vya Israeli

Wataalamu waliozungumza na BBC Mundo walisema Israel ilikuwa na nguvu kubwa zaidi kuliko Hamas, Hezbollah au Houthis nchini Yemen.

"Vikosi vya Israel vina uwezo zaidi kuliko vikosi vingine vyovyote vilivyo na silaha kwa pamoja," anasema Shawn Shaikh wa CSIS.

Lakini anasema kuwa tatizo kuu la Israel litakuwa "kupigana na Iran huku ikipigana na mashirika mengine."

"Ni vigumu sana. Moja ya mambo ambayo Israel inaelekea kushindwa ni mfumo wao maarufu wa Iron Dome, kwa sababu hauwezi kuilinda Israel dhidi ya makombora yanayorushwa kutoka maeneo tofauti kwa wakati mmoja," alisema.

"Sababu ni kwamba sensa kwenye mfumo huu haziwezi kufuatilia mwelekeo fulani. Kwa mfano, ikiwa sensa inaelekeza kuelekea Lebanon kaskazini mwa Israel, haiwezi kufuatilia Iran mashariki au Yemen kusini", alisema.

Aidan Shamir anaeleza kuwa ugumu mwingine unaoweza kukabili Israel katika kukabiliana na migogoro katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati unahusiana na vikosi vyake vya ardhini.

Kulingana na Taasisi ya Mafunzo ya Kimkakati ya Kimataifa, Israel ina takriban wanajeshi 178,000 walio kazini, na wanajeshi 4,60,000 wa ziada wakiwa katika hali ya kusubiri. (Huduma ya kijeshi ni ya lazima kwa mtu yeyote zaidi ya miaka 18 katika Israeli)

Lakini Iran ina zaidi ya wanajeshi 600,000 na zaidi ya 300,000 wako tayari. Hezbollah inaaminika kuwa na wanajeshi kati ya 50,000 na 100,000, huku Hamas ikiwa na kati ya 20,000 na 30,000.

Shamir anasema tatizo kubwa la nchi hiyo ni ukosefu wa wanajeshi katika jeshi la Israel.

"Karibu asilimia 70 ya wanajeshi wake si wataalamu. Kwa hiyo, wanaweza kufanya kazi za kijeshi kwa muda mfupi tu. Hii inafanya baadhi ya misheni kuwa ndefu na ngumu," anasema.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa na Rais wa Marekani Joe Biden

Msaada wa Marekani

Jambo kuu la kuzingatia wakati wa kuchambua uwezo wa kijeshi wa Israel ni uungwaji mkono mkubwa wa nchi hiyo kutoka kwa Marekani.

Kulingana na ripoti ya hivi majuzi ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), 69% ya silaha zinazoagizwa kutoka Israel zinatoka Amerika ya Kaskazini.

Kufikia mwisho wa 2023, Marekani ilikuwa imewasilisha maelfu ya vifaa vya vilipuzi kwa Israeli, kulingana na data ya shirika hilo.

Kabla ya vita hivi, Marekani iliipa Israel dola bilioni 3.3 kwa mwaka katika ufadhili wa kijeshi. Serikali ya nchi hiyo ilitangaza nyongeza ya dola milioni 500 za ufadhili wa ulinzi wa makombora.

Mnamo mwaka wa 2022, ilitoa dola bilioni 1 za ziada ili kuboresha mfumo wa kuzuia makombora wa Iron Dome.

"Israel inategemea sana usaidizi wa Marekani. Ndege, vilipuzi na vifaa mbalimbali vya teknolojia huja Israel kutoka Marekani," anaeleza Aidan Shamir.

Anasema uungwaji mkono wa Marekani ni muhimu kwa Israel kuendelea na mashambulizi yake katika nyanja tofauti.

"Baraza la Umoja wa Mataifa linasema kuwa Israel lazima ikomeshe mara moja mashambulizi yake au ikabiliane na vikwazo vya kimataifa. Bila ya kuungwa mkono na Marekani, ambayo ina mamlaka ya kura ya turufu, inaweza kuwa hali ngumu kwa Israel," anasema Aidan Shamir.

Shaun Sheik anaripoti kwamba inaonekana kama utawala wa Marekani unaoongozwa na Joe Biden utaendelea kuunga mkono mashambulizi ya Israel katika Mashariki ya Kati.

"Utawala wa Biden umesema mara nyingi kwamba unataka kusitishwa kwa mapigano huko Gaza, lakini umechukua hatua kidogo sana kufanikisha hilo," anabainisha.

"Hayuko tayari kuacha kutoa msaada wa silaha na kifedha kwa Israel". Kwa hiyo ikiwa itaendelea kuongezeka, nadhani Marekani itaendelea kuiunga mkono Israel kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Nchi nyingine pia ni wafuasi wakubwa wa Israel.

Kwa mfano, kulingana na data ya SIPRI, Ujerumani ni ya pili kwa uuzaji mkubwa wa silaha (30%) kwa Israeli. Kufikia Novemba mwaka jana, mauzo ya silaha ya Ujerumani kwa Israel yalifikia jumla ya dola za Marekani milioni 326. Hii ni mara 10 zaidi ya mwaka 2022.

Kulingana na data ya SIPRI, Italia inashika nafasi ya tatu (0.9%) kati ya nchi zinazosambaza silaha kwa Israeli.

Nchi kama vile Ufaransa, Uingereza, Uholanzi, Canada na Australia pia husambaza silaha kwa Israel.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwanamke na mtoto wanatembea katika mji wa Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Zaidi ya silaha ...

Weledi wa mambo wanasema kuwa, kuchambua uwezo wa kijeshi wa Israel kunahitaji kutilia maanani mambo mengine zaidi ya idadi ya silaha, ndege, vifaru na wapiganaji ilionao.

"Tunajua kwamba Israel ina nguvu zaidi kuliko maadui zake na kwamba inaweza kuendeleza vita kwa muda mrefu. Lakini tunahitaji kuhesabu ni muda gani vita vinaweza kudumishwa sio tu na hifadhi ya silaha za nchi," Shamir alisema.

"Bei ambayo Israel inapaswa kulipa katika suala la uchumi, jamii na sifa ya kimataifa ni kubwa sana na nchi inapaswa kuchukua hatua ipasavyo," alisema.

Licha ya uwezo mkubwa wa kijeshi wa Israel, ukubwa wake katika Mashariki ya Kati unaweza kuwa hasara kwa Israel, anasema mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati cha Begin-Saad.

"Katika eneo kubwa linaloitwa Mashariki ya Kati, nchi ya Syria ni Israel. Kuna watu wengi wanaoishi huko," alisema.

"Kwa hiyo kama tutashinda nchi adui katika vita moja, mbili au 10, haileti tofauti. Israel haiwezi kuzishinda kabisa", anasema.

Kwa mfano, Iran ni nchi kubwa zaidi kuliko Israel. Inafaa kumbuka kuwa idadi ya watu wake (karibu milioni 89) ni mara nyingi zaidi ya Israeli (karibu milioni 10).

"Kwa kuleta usitishaji vita huko Gaza, majeruhi yasiyo ya lazima yangeepukwa. Ingeruhusu Hezbollah na Iran kurudi nyuma kutoka kwa vita na kupata ushindi wa kidiplomasia kwao," anasema mtaalamu wa ulinzi wa makombora Shawn Shaikh.

Hata hivyo, kwa kuangalia siku zijazo, wataalamu wote wawili wanakubali kwamba hakuna upande unaotaka "vita kamili" katika kanda kwa sababu ya vigingi vya juu vinavyohusika katika mzozo huo.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla