Je, Israel itajibu vipi, na Iran itafanya nini wakati huo?

.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Israel imeapa kulipiza kisasi, baada ya Iran kurusha makombora 180 siku ya Jumanne
    • Author, Frank Gardner
    • Nafasi, Mwandishi wa Habari za Usalama, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Mashariki ya Kati kwa mara nyingine tena iko ukingoni mwa vita vikali na vya uharibifu kati ya wahusika wakuu wawili ambao wamekuwa wakikabiliana kwa muda mrefu wa miaka 45 iliyopita. Hii sasa ni moja ya wakati hatari zaidi kwa eneo zima.

Iran ambayo ilikuja kuwa Jamhuri ya Kiislamu baada ya kupinduliwa utawala wa Shah mwaka 1979, kwa muda mrefu imekuwa ikiapa kuliangamiza taifa la Israel inaloliita “Utawala wa Kizayuni”. Israel inashutumu Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) kwa kueneza ghasia katika eneo la Mashariki ya Kati kupitia washirika wake, maoni ambayo yanashirikiwa na serikali kadhaa za Kiarabu.

Israel iko tayari kulipiza kisasi dhidi ya Iran kwa kosa la Jumanne la makombora ya balistiki, ambayo baadhi yake yalipenya ngome za anga za Israel.

Iran inasema hiyo ilikuwa ni kujibu mauaji mawili ya Israel - ya kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah huko Beirut na kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh huko Tehran.

Kwa hivyo nini kitatokea baadaye?

Israel na mshirika wake wa karibu, Marekani, wameapa kuiadhibu Iran kwa kurusha makombora 180 huko Israel. "Iran," anasema Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, "italipa gharama kubwa."

Kujizuia ambako washirika wa Israeli walihimiza juu yake mara ya mwisho kulikuwa na msuguano kama huu mnamo Aprili lakini kumezimwa zaidi wakati huu. Na kwa kuzingatia dhamira ya Israel ya kuwakabili maadui zake wote mara moja - huko Lebanon, Gaza, Yemen na Syria - serikali ya Netanyahu inaonekana kutokuwa na hali ya kujizuia.

Wapangaji wa Israeli sasa watakuwa wakijadili sio ikiwa na wakati wa kuishambulia Iran, lakini kwa makali au nguvu kiasi gani.

Maelezo ya video, Tazama: Ilivyokuwa kutoka juu Iran ikirusha msururu wa makombora kuelekea Israel
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakisaidiwa na ujasusi wa satelaiti wa Marekani na Mossad (shirika la kijasusi la Israel ng'ambo) maajenti walioko ardhini nchini Iran, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lina malengo mengi ya kuchagua. Hizi zinaweza kugawanywa kwa jumla katika vikundi vitatu:

Jeshi la kawaida - Lengo la mapema na dhahiri litakuwa vituo ambavyo Iran ilirusha makombora hayo ya balistiki. Kwa hivyo hiyo inamaanisha maeneo yakuzindua mashambulizi, vituo vya usimamizi na udhibiti wa operesheni, matangi ya kujaza mafuta na vyumba vya kuhifadhia silaha. Inaweza kwenda mbali zaidi na kushambulia kambi za IRGC pamoja na ulinzi wa anga na betri zingine za makombora. Inaweza hata kujaribu kuwaua watu muhimu wanaohusika katika mpango wa makombora ya balistiki ya Iran.

Kiuchumi - Hii itajumuisha mali ya taifa ya Iran iliyo hatarini zaidi - mitambo yake ya mafuta ya petroli, uzalishaji wake wa kawi na mali zake zinazohusiana na usafiri wa meli. Hii, hata hivyo, itakuwa hatua isiyopendwa na watu wengi nchini Iran kwani itaishia kuumiza maisha ya watu wa kawaida zaidi kuliko shambulio lolote dhidi ya jeshi.

Nyuklia - Hii ndio kubwa kwa Israeli. Ni ukweli unaojulikana, uliotambuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la uangalizi wa nyuklia, IAEA, kwamba Iran inarutubisha uranium zaidi ya 20% inayohitajika kwa nguvu za nyuklia za matumizi ya kiraia. Israel, na wengine, wanashuku Iran kwa kujaribu kufikia "hatua ya upeo" ambapo iko ndani ya muda mfupi sana wa kuweza kutengeneza bomu la nyuklia. Maeneo kwenye orodha inayowezekana ya kulengwa na Israeli ni pamoja na Parchin, kitovu cha mpango wa nyuklia wa kijeshi wa Iran, vinu vya utafiti huko Tehran, Bonab na Ramsar, na vile vile vituo kuu huko Bushehr, Natanz, Isfahan na Ferdow.

Sehemu kubwa ya hesabu zao itahusisha kujaribu kukisia jibu la Iran na jinsi ya kulipunguza. Msimamo wa Iran ni kwamba baada ya kurusha makombora hayo kwa kile inachosema yalikuwa malengo ya jeshi la Israeli mnamo Jumanne upizaji huo sasa sasa umefanyika . Lakini inaonya kwamba ikiwa Israeli italipiza kisasi itajibu pia.

"Huu ni mwanzo tu wa uwezo wetu," Rais wa Iran Masoud Pezeshkian alisema. IRGC imesisitiza ujumbe huo kwa kusema: "Iwapo utawala wa Kizayuni utajibu oparesheni za Iran, utakabiliwa na mashambulizi makali."

Iran haiwezi kuishinda Israel kijeshi. Kikosi chake cha anga ni cha zamani na kimepungua makali na uwezo, ulinzi wake wa anga ni mbaya na imelazimika kukabiliana na vikwazo vya nchi za Magharibi kwa miaka mingi.

Lakini bado ina idadi kubwa ya makombora ya balestiki na mengine pamoja na droni zilizojaa vilipuzi na wanamgambo wengi washirika karibu na Mashariki ya Kati. Milipuko yake inayofuata ya makombora inaweza kulenga maeneo ya makazi ya Israeli, badala ya kambi za kijeshi. Shambulio la wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran kwenye vituo vya mafuta vya Saudi Arabia mnamo 2019 lilionyesha jinsi majirani zake walivyo hatarini kushambuliwa.

Jeshi la Wanamaji la IRGC, ambalo linahudumu katika Ghuba, lina safu kubwa za boti ndogo za makombora ya haraka ambayo inaweza, kuyatumia kusakama ulinzi wa meli ya kivita ya 5th Fleet ya Marekani katika shambulio la pamoja. Ikiwa itapata maagizo ya kufanya hivyo, inaweza kujaribu kutega mabomu katika Mlango-Bahari wa Hormuz, na kutatiza mtiririko wa hadi asilimia 20 ya mauzo ya mafuta ya kila siku duniani, jambo ambalo litakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa dunia.

Na kisha kuna kambi zote za kijeshi za Marekani, zilizo juu na chini upande wa Ghuba ya Uarabuni, kutoka Kuwait hadi Oman. Iran imetoa onyo kwamba iwapo itashambuliwa haitaijibu Israel tu, italenga nchi yoyote ambayo inaona kuwa inaunga mkono mashambulizi hayo.

Haya basi, ni baadhi tu ya matukio ambayo wapangaji wa mipango ya ulinzi huko Tel Aviv na Washington sasa watazingatia.

Iran missile range

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Seif Abdalla