Putin ameanza Vita vya tatu vya Dunia na lazima akomeshwe - Zelensky

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anaendelea kutuma ujumbe mkali.
Tulipokutana wikendi hii katika makao makuu ya serikali huko Kyiv, alisema kwamba mbali na kushindwa, Ukraine itamaliza vita ikiwa imeshinda.
Alikuwa kinyume kabisa na kulipa gharama ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyodaiwa na Rais Vladimir Putin.
Zelensky aliniambia, Putin tayari ameanza Vita vya Tatu vya Dunia, na jibu pekee lilikuwa shinikizo kubwa la kijeshi na kiuchumi ili kumlazimisha arudi nyuma.
"Ninaamini kwamba Putin tayari ameanza. Swali ni ni eneo gani ataweza kuliteka na jinsi ya kumzuia... Urusi inataka kulazimisha ulimwengu njia tofauti ya maisha na kubadilisha maisha ambayo watu wamejichagulia wenyewe."
Vipi kuhusu ombi la Urusi kwa Ukraine kukabidhi 20% ya eneo la mashariki la Donetsk ambalo bado inamiliki, safu ya miji ambayo Ukraine inaita "miji ya ngome", pamoja na ardhi zaidi katika maeneo ya kusini ya Kherson na Zaporizhzhia? Je, hilo si ombi linalofaa ikiwa litasababisha kusitisha mapigano?
"Ninaona hili tofauti. Silitazami kama ardhi tu. Ninaliona kama kutelekezwa, kudhoofisha misimamo yetu, kuwaacha mamia ya maelfu ya watu wetu wanaoishi huko. Hivi ndivyo ninavyoliona. Na nina uhakika kwamba 'kujiondoa' huku kutagawanya jamii yetu."
Lakini je, si bei nzuri kulipa ikiwa hilo litamridhisha Putin? Je, unafikiri litamridhisha?
"Labda litamridhisha kwa muda... anahitaji kusimamishwa... lakini mara tu atakapopona, washirika wetu wa Ulaya wanasema inaweza kuchukua miaka mitatu hadi mitano. Kwa maoni yangu, angeweza kupona katika muda usiozidi miaka michache. Angeenda wapi baadaye? Hatujui, lakini kwamba angependa kuendelea [vita] ni ukweli."
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Nilikutana na Volodymyr Zelensky katika chumba cha mikutano ndani ya eneo la serikali linalolindwa sana katika sehemu ya katikati ya Kyiv. Katika mahojiano hayo alizungumza zaidi kwa Kiukreni.
Unaweza kuhisi uzito wa uongozi anaoubeba Zelensky kutokana na umakini wa walinzi wake wa usalama.
Kumtembelea kiongozi yeyote wa taifa kunahitaji ukaguzi mkali. Lakini kuingia katika majengo ya rais mjini Kyiv kunapeleka mchakato huo katika kiwango ambacho mara chache nimewahi kushuhudia.
Hili halishangazi katika nchi iliyo vitani, yenye rais ambaye tayari amelengwa na Urusi.
Licha ya hayo yote, mtu huyu aliyeanza kama mburudishaji, aliyeshinda toleo la Ukraine la kipindi cha Strictly Come Dancing mwaka 2006, na kucheza nafasi ya rais wa Ukraine asiyetarajiwa katika tamthilia ya vichekesho ya televisheni kabla ya kuwa rais halisi wa Ukraine, anaonekana kuwa na ustahimilivu mkubwa ajabu.
Rais wa Marekani Donald Trump alisema kabla ya mazungumzo ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano mjini Geneva kwamba "Ukraine ni bora ifike kwenye meza ya mazungumzo haraka."
Anaendelea kuweka shinikizo zaidi kwa Ukraine kuliko kwa Urusi.
Wanadiplomasia wa Magharibi wameashiria tangu majira ya joto yaliyopita kwamba Trump anakubaliana na Vladimir Putin kuwa makubaliano ya kusalimisha baadhi ya maeneo ya Ukraine kwa Urusi ndiyo ufunguo wa kusitisha mapigano ambayo Trump anataka, ikiwezekana kabla ya majira ya joto yajayo.
Wachambuzi wengi nje ya Ikulu ya Marekani pia wanaona kuwa Ukraine haiwezi kushinda vita na, bila kufanya makubaliano na Moscow, inaweza kushindwa.
Nilimuuliza Zelensky kama Trump na wengine walikuwa na hoja.
"Uko wapi sasa?" Zelensky aliuliza kujibu. "Leo uko Kyiv, uko katika mji mkuu wa nchi yetu, uko Ukraine. Ninashukuru sana kwa hili. Tutashindwa? Bila shaka hapana, kwa sababu tunapigania uhuru wa Ukraine."

Chanzo cha picha, Fred Scott/BBC
Volodymyr Zelensky mara nyingi amesema kwamba Ukraine inaweza kushinda, lakini ushindi utakuwa na sura gani?
Alisema kwamba ushindi unamaanisha kurejesha maisha ya kawaida kwa Waukraine na kukomesha mauaji. Lakini mtazamo mpana wa ushindi alioueleza ulihusu zaidi tishio la kimataifa ambalo anasema linatoka kwa Vladimir Putin.
"Naamini kwamba kumsimamisha Putin leo na kumzuia kuiteka Ukraine ni ushindi kwa dunia nzima. Kwa sababu Putin hatasimama Ukraine tu."
Je, unasema ushindi si kurejesha ardhi yote, sivyo?
"Tutaifanya. Hilo liko wazi kabisa. Ni suala la muda tu. Kufanya hivyo leo kungekuwa na maana ya kupoteza idadi kubwa sana ya watu, mamilioni ya watu, kwa sababu jeshi la Urusi ni kubwa, na tunaelewa gharama ya hatua kama hizo. Usingekuwa na watu wa kutosha, ungekuwa ukiwapoteza. Na ardhi bila watu ina maana gani? Kwa kweli, si kitu."
"Pia hatuna silaha za kutosha. Hilo halitegemei sisi pekee, bali pia washirika wetu. Kwa sasa hilo haliwezekani, lakini kurejea katika mipaka ya haki ya mwaka 1991 [mwaka ambao Ukraine ilitangaza uhuru wake, uliosababisha kuanguka kwa umoja wa Sovieti] bila shaka si ushindi tu, bali ni haki.
Ushindi wa Ukraine ni kuhifadhi uhuru wetu, na ushindi wa haki kwa dunia nzima ni kurejeshwa kwa ardhi yetu yote."
Mwaka mmoja uliopita, Zelensky alitembelea White House na kupokea mapokezi ambayo mwanadiplomasia mmoja mkuu wa Magharibi aliyaita "shambulio la kidiplomasia lililopangwa mapema hadharani" kutoka kwa Donald Trump na Makamu wake wa Rais JD Vance.
Mabishano yao, mbele ya vyombo vya habari vya dunia, yalitazamwa na mamilioni ya watu duniani.
Trump, aliyekuwa ameapishwa hivi karibuni kwa mara ya pili kuwa rais, alikuwa akituma ishara kali zaidi kwamba kipindi cha uungwaji mkono ambacho Zelensky na Ukraine walitegemea kutoka kwa Joe Biden kilikuwa kimekwisha.
Wanachama wa NATO tayari walikuwa wameonywa na utawala mpya. Vance alikuwa ametoka tu kurejea kutoka Ulaya Magharibi, akivunja matarajio kuhusu nguvu ya ushirikiano wa kuvuka Atlantiki.
Tangu wakati huo, inaripotiwa kwamba Zelensky, akishauriwa na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Uingereza Jonathan Powell miongoni mwa wengine, ameepuka makabiliano ya hadharani na Trump.
Rais wa Marekani amesitisha karibu usafirishaji wote wa misaada ya kijeshi kwa Ukraine. Hata hivyo, Marekani bado inatoa taarifa muhimu za kijasusi, na nchi za Ulaya zinatumia mabilioni ya fedha kununua silaha kutoka kwa Marekani ili kuzipa Ukraine.

Chanzo cha picha, Reuters
Nilimuuliza rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kuhusu kauli za Donald Trump ambazo mara nyingi zinapingana, nikikumbusha kwamba miongoni mwa madai yasiyo ya kweli aliyoyatoa ni tuhuma kwamba Zelensky ni dikteta aliyeanzisha vita, madai yanayofanana kabisa na yale ya Vladimir Putin.
Zelensky alicheka.
"Mimi si dikteta, na sikuanzisha vita, ndivyo ilivyo."
Lakini je, unaweza kumwamini Trump? Kama utapata dhamana ya usalama kutoka kwake, nilimuuliza, je, atatimiza ahadi yake? Baada ya yote, ni mtu anayebadili mawazo mara kwa mara.
"Sio Rais Trump tu, tunazungumzia Marekani. Sisi sote tunakuwa marais kwa muda maalum wa uongozi. Tunataka dhamana kwa miaka 30, kwa mfano. Tabaka la kisiasa litabadilika, viongozi watabadilika."
Alimaanisha kwamba dhamana za usalama kutoka Marekani zinahitaji kuidhinishwa na Bunge la Congress huko Washington DC ili ziwe thabiti kabisa.
"Zitapigiwa kura katika Bunge kwa sababu fulani. Sio marais tu. Bunge linahitajika. Kwa sababu marais hubadilika, lakini taasisi hubaki."
Kwa maneno mengine, Donald Trump anaweza kuwa asiyeaminika, lakini hatakuwa madarakani milele.
Zelensky alisema dhamana hizo za usalama zitahitajika kwanza kabla hajazingatia shinikizo lingine la Marekani, kwamba Ukraine ifanye uchaguzi mkuu ifikapo majira ya joto, jambo linalorudia hoja nyingine ya Urusi kwamba Zelensky si rais halali.
Trump hajawahi kudai uchaguzi ufanyike Urusi, ambako Putin alikua kiongozi kwa mara ya kwanza siku ya mwisho ya karne ya 20.
Zelensky alisema bado hajaamua kama atagombea tena, wakati wowote uchaguzi utakapofanyika: "Naweza kugombea au nisigombee."
Uchaguzi ulipaswa kufanyika mwaka 2024, lakini haukuweza kufanyika chini ya sheria ya kijeshi iliyowekwa baada ya uvamizi mkubwa wa Urusi.
Zelensky alisema kufanya uchaguzi uliocheleweshwa kunawezekana kiufundi kama wangekuwa na muda wa kubadilisha sheria ili kuruhusu kufanyika kwake.
Lakini alisisitiza kwamba anahitaji dhamana za usalama kwa Ukraine kwanza.
Aliendelea kueleza changamoto nyingi zinazoweza kutokea katika kufanya uchaguzi wakati mamilioni ya Waukraine wako nje ya nchi kama wakimbizi na sehemu kubwa ya nchi iko chini ya udhibiti wa Urusi, hadi nikaona kwamba kwa kweli alikuwa anapinga wazo hilo.
"Kama hili ni sharti la kumaliza vita, basi tufanye hivyo. Nilisema, 'kwa kweli, mnaendelea kuibua suala la uchaguzi'. Niliwaambia washirika, 'mnahitaji kuamua jambo moja: mnataka kuniondoa au mnataka kufanya uchaguzi? Kama mnataka kufanya uchaguzi (hata kama hamko tayari kuniambia wazi hata sasa), basi fanyeni uchaguzi huo kwa uaminifu. Ufanyeni kwa njia ambayo watu wa Ukraine watautambua kwanza. Na ninyi wenyewe lazima mtambue kwamba huo ni uchaguzi halali.''
Volodymyr Zelensky ana wapinzani na wakosoaji wakali hapa Ukraine.
Serikali yake ilikumbwa na kashfa ya ufisadi msimu wa vuli uliopita ambayo ilisababisha kuondoka kwa mshauri wake wa karibu zaidi.
Lakini Zelensky, akiwa na timu mpya, bado ana kiwango cha juu cha uungwaji mkono ambacho viongozi wengi wa Ulaya Magharibi wanaweza kuota tu.
Wakati mwingine amewakasirisha washirika wake kwa madai ya mara kwa mara ya kuhitaji vifaa zaidi na bora. Mojawapo ya tuhuma alizoelekezewa mwaka mmoja uliopita na Donald Trump pamoja na JD Vance ilikuwa kwamba hakuwa akionesha shukrani za kutosha.
Baada ya yote aliyosema, nilimuuliza kama tunapaswa kujiandaa kwa vita virefu zaidi nchini Ukraine.
"Hapana, hapana, hapana, ni njia mbili zinazokwenda sambamba… unacheza mchezo wa chess na viongozi wengi, si na Urusi tu. Hakuna njia moja sahihi. Lazima uchague hatua nyingi zinazokwenda sambamba, mwelekeo mbalimbali kwa wakati mmoja. Na mojawapo ya njia hizi, nafikiri, italeta mafanikio. Kwetu sisi, mafanikio ni kumsimamisha Vladimir Putin."
Lakini Vladimir Putin hatamaliza vita hivi, sivyo? Isipokuwa awe chini ya shinikizo kubwa sana, na haonekani kuwa hivyo.
"Ndiyo na hapana. Tutaona. Ndiyo na hapana. Hataki, lakini kutotaka hakumaanishi hatofanya. Mungu awabariki. Mungu awabariki, tutafanikiwa. Asante."
Baada ya hayo, alipiga picha, akapeana mikono na timu ya BBC, na akaondoka.















