Watu wanane wafungwa jela Tanzania kwa kudai kupotea kwa nyeti zao

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu wanane nchini Tanzania wamehukumiwa kwenda jela kwa kifungo cha kati ya miezi tano na sita kutokana na kusambaza taarifa zinazodaiwa kuwa za uongo za nyeti zao kupotea baada ya kushikwa bega.
Kati yao wawili walihukumiwa mkoani Shinyanga, wawili katika mkoa wa Rukwa, mmoja Geita na watatu walikamatwa, kushtakiwa na kupata hukumu mkoani Mbeya.
Taarifa mbali mbali za Jeshi la Polisi nchini Tanzania zinaeleza kuwa mahakama nchini humo zimehukumu watu hao kwa kutenda kosa la kudai kuibiwa nyeti, suala ambalo polisi wanasema si kweli na lilichochea wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwashambulia watu wasiokuwa na hatia.
Kwa mujibu wa taarifa hizo za polisi katika kipindi cha wiki moja watu zaidi ya 100 kote nchini walikamatwa, wengine wanashikiliwa huku baadhi wakisubiri kufikishwa mahakamani kwa tuhuma kujibu tuhuma kama hizo.
Hata hivyo polisi wamesema hawatasita kuchukua hatua pale watakapopata taarifa, huku wakieleza kuwa hatua zote zinachukuliwa kwa kufuata taratibu za kisheria ikiwemo kupata taarifa ya wataalamu wa afya pale inapobidi.
Mwishoni mwa juma lililopita kuliibuka taarifa katika maeneo mbalimbali nchini humo zikidai kuwa kuna watu wanapomshika mwanaume bega, basi maeneo yake nyeti yanapotea.
Hata hivyo mamlaka nchini humu zilikanusha taarifa hizo zikidai ni upotoshaji.
Taharuki na vifo
Msemaji wa jeshi la polisi David Misime alitoa taarifa ya jumla kuhusu kadhia ya matukio hayo Jumamosi Aprili 4 akitoa onyo kali kwa watu waliokuwa wakisambaza taarifa hizo ambazo zimekua zikizua taharuki kwenye maeneo yote ambapo uvumi huo ulilipuka.
"Tunasisitiza kuwa taarifa hizi hazina ukweli wowote. Uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa wanaodai kupoteza sehemu zao za siri walipokagulia walikutwa wakiwa kawaida kabisa," alieleza Misime.
Mpaka kufikia Aprili 4, watu watano walikuwa wameripotiwa kufariki na wengine kadaa kujeruhiwa baada ya kushambuliwa na makundi ya watu waliowatuhumu kuwa ni wezi wa nyeti. Watu wote watano waliuawa katika mkoa wa Songwe ambapo uvumi huo ulipoanzia kabla ya kusambaa mpaka mkoani Mbeya, Dodoma, Dar Es Salaam na Zanzibar.
"Wananchi wanapaswa kuwa watulivu na kutojihusisha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi ambavyo vinaweza kuhatarisha maisha ya watu wasio na hatia," Misime alisisitiza kwenye taarifa yake.












