Uvamizi wa Lebanon: Je! Jeshi la Lebanon liko wapi wakati Israel inavamia?
- Author, Carine Torbey
- Nafasi, BBC News
- Akiripoti kutoka, Beirut
- Muda wa kusoma: Dakika 5

Chanzo cha picha, Getty Images
Mgogoro wa sasa kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hezbollah unatokana na mambo mawili makubwa, ambayo yamedumu kwa zaidi ya miongo minne.
Israel inasema inataka kuisambaratisha Hezbollah kwani ni tishio kwake, huku Hezbollah ikiendelea kushambulia maeneo ya Israel katika juhudi za kuliangamiza taifa la Israel.
Kwa muda wa miezi 11 iliyopita, mashambulizi ya kila siku mpakani mwa nchi hizo mbili yameongeza mvutano huo wa muda mrefu.
Israel sasa imefanya uvamizi nchini Lebanon kwa mara ya kwanza tangu 2006. Wengi wanauliza; jeshi la Lebanon liko wapi wakati haya yote yakitokea, na linafanya nini kuzuia mzozo mkubwa zaidi!
Nani anailinda Lebanon?

Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la Lebanon halijashiriki katika mapigano ya Israel na Hezbollah – kundi ambalo linatajwa kuwa la kigaidi na Marekani, Uingereza na nchi nyingine za Ulaya na Kiarabu. Kinadharia, ni kazi ya jeshi kupambana na adui wa taifa na Israel ni adui rasmi wa Lebanon. Lakini jeshi la Lebanon linakosa zana na silaha zinazohitajika kwa makabiliano hayo.
Jeshi la Israel lina vifaa vya kutosha na linaungwa mkono na madola ya Magharibi – kifedha, kidiplomasia na katika suala la silaha.
Vilevile, kuna imani iliyoenea inayoungwa mkono na kauli kutoka kwa maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa zamani, wakiishutumu Marekani kwa kuzuia serikali ya Lebanon kupata silaha za kisasa ambazo zinaweza kuwa tishio kwa Israel.
Mgogoro mkubwa wa kiuchumi - uliochochewa na mlipuko mbaya wa ghala la mbolea huko Beirut 2020 - umefanya mambo kuwa mabaya zaidi kwa jeshi la Lebanon. Ukosefu wa fedha umeathiri wafanyakazi wake na mahitaji yake ya kimsingi ya kiutendaji, kama vile mafuta.

Chanzo cha picha, Getty Images
Michango kwa jeshi la Lebanon
La kushangaza zaidi, Marekani, ambayo inachukuliwa na Hezbollah kama adui yake mkubwa, ndiyo mfadhili mkuu wa jeshi la Lebanon. Washington imechangia mishahara midogo ya wanajeshi wa Lebanon.
Na misaada yake ni magari, vifaa na silaha za kawaida na sio msaada mkubwa ukilinganisha na misaada inayotoa kwa Israel.
Lakini baadhi ya wachunguzi wa mambo wanaeleza kuwa udhaifu wa jeshi la Lebanon dhidi ya Israel ni sawa na udhaifu wa majeshi mengine katika eneo hilo.
"Si jeshi la Lebanon wala jeshi lolote la nchi ya Kiarabu lenye uwezo wa kukabiliana na Israel," anasema Jenerali Mounir Shehade, mratibu wa zamani wa serikali ya Lebanon katika Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (Unifil).
"Njia pekee ya kupambana na Israel ni kupitia vita vya kuvizia, kama inavyotokea Gaza."

Chanzo cha picha, Getty Images
Khalil El Helou, jenerali mstaafu katika jeshi la Lebanon anasema "jukumu la jeshi la Lebanon ni kudumisha utulivu wa ndani, na leo hii hali ya ndani ni tete.
Kuhamishwa kwa wafuasi nusu milioni wa Hezbollah kwenda maeneo ambayo hayaungi mkono Hezbollah kunaweza kuleta msuguano ambao unaweza kuibua machafuko na pengine vita vya wenyewe kwa wenyewe," anasema.
Kufuatia kuuawa kwa kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah na Israel, jeshi la Lebanon lilisambaa kwa wingi katika maeneo mengi yanayoonekana kuwa "nyeti" ambapo kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kutokea mvutano kati ya makundi tofauti nchini humo.
Pia ilitoa taarifa Jumapili iliyopita ikiwataka "raia kudumisha umoja wa kitaifa," ikisisitiza kuwa inaendelea kuchukua hatua za kulinda amani ya raia nchini humo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi liko kwenye mgogoro na Israel?
Je, jeshi la Lebanon lina husika katika uhasama uliopo? Jawabu ni hapana.
Lakini jeshi hilo lipo kusini na kwa idadi kubwa. Hivi karibuni jeshi lilitangaza kuwa mwanajeshi wa Lebanon aliuawa na ndege isiyo na rubani ya Israel ambayo ililenga pikipiki iliyokuwa ikipita kwenye kituo cha ukaguzi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah








