Israel yaishambulia Beirut, kuwataka watu zaidi kuondoka kusini mwa Lebanon
Israel inadai kuyashambulia "makao makuu ya kijasusi ya Hezbollah" mjini Beirut.
Muhtasari
- Iran yazishutumu nchi za G7 kwa 'upendeleo'
- Tazama: Moshi ukifuka Beirut kufuatia mashambulizi mapya ya Israel
- Rais wa Sudan Kusini amfuta kazi mkuu wake wa ujasusi
- Emirates yasitisha safari zake kuelekea Iran, Iraq na Jordan
- Watu 20 wafariki baada ya feri kuzama katika ziwa DR Congo
- Uingereza kuikabidhi Mauritius visiwa vya Chagos
- Israel yasema iliwaua viongozi watatu wakuu wa Hamas mjini Gaza
- Shambulio la Israel Gaza liliua watu 22 likilenga mwanachama mmoja wa Hamas-BBC yaambiwa
- CIA inawasaka wahudumu wapya Korea Kaskazini, Iran na China
- Mwanamuziki nguli wa nyimbo za Injili Afrika Kusini Solly Moholo afariki dunia
- Video: Tazama kupatwa kwa jua Amerika ya kusini
- Rwanda kuanza majaribio ya chanjo ya ugonjwa wa virusi vya Marburg
- Israel na Lebanon: Israel yafanya shambulio la kwanza katikati mwa mji mkuu Beirut
- Takriban watu sita wameuawa katika shambulizi la anga la Israel katikati mwa Beirut
- Mamlaka Tanzania zaifungia Mwananchi kuchapisha habari mtandaoni kwa 'ukiukaji wa kanuni'
- Urusi yafanya mashambulizi ya mabomu ya Shahid na kamikaze katika maeneo tofauti ya Ukraine
- Biden: Marekani haiungi mkono shambulio la Israeli kwenye maeneo ya nyuklia ya Iran
Moja kwa moja
Na Ambia Hirsi & Dinah Gahamanyi
Iran yazishutumu nchi za G7 kwa 'upendeleo'

Chanzo cha picha, Reuters
Wizara ya mambo ya nje ya Iran imezishutumu nchi za G7 kwa "upendeleo na kutowajibika" kutokana na jinsi yalivyolaani mashambulizi yake yamakombora dhidi ya Israel.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Esmaeil Baghaei aliashiria "jukumu la nchi za G7, hususan Marekani, kwa kuchochea vurugu katika eneo la Asia Magharibi" kwa kuipatia silaha na kuiunga mkono Israel.
Siku ya Jumatano, viongozi wa G7 - Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani - katika taarifa ya pamoja walishutumu mashambulizi ya Tehran na kuelezea "wasiwasi wao" kuhusu mgogoro huo.
Huku hayo yakijiri Rais wa Marekani Joe Biden amepuuzilia madai kwamba Israel inapanga kufanya mashambulizi dhidi ya Iran.
Alipoulizwa na waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani iwapo Marekani itairuhusu Israel kujibu mashambulizi ya Jumanne ya Iran, Biden alisema: "Kwanza kabisa, 'hatuiruhusu' Israel, tunaishauri Israel. Na hakuna kitakachofanyika leo."
Kufuatia mashambulizi makubwa ya makombora yaliyofanywa na Iran, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alionya kwamba Iran italipa "kosa hilo kubwa".
Soma pia:
Tazama: Moshi ukifuka Beirut kufuatia mashambulizi mapya ya Israel
Maelezo ya video, Israel yaishambulia Beirut, kuwataka watu kuondoka kusini mwa Lebanon Israel inasema imeyashambulia "makao makuu ya kijasusi ya Hezbollah" mjini Beirut.
Katika taarifa, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema kuwa mashambulizi hayo "yaliwalenga wapiganaji wa kundi hilo", vituo vya usalama "vya kukusanya taarifa za kijasusi".
IDF pia ilidai makao hayo makuu yanaelekeza "shughuli za kijasusi za Hezbollah" na kuratibu "taarifa za kijasusi".
Rais wa Sudan Kusini amfuta kazi mkuu wake wa ujasusi

Chanzo cha picha, Eye Radio
Maelezo ya picha, Chini ya uongozi wa Jenerali Akol Koor Kuc, NSS imekuwa na sifa ya kutisha Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amemfuta kazi mkuu wake wa ujasusui wa muda mrefu Jenerali Akol Koor Kuc.
Alikua mkuu wa Huduma za Usalama wa Kitaifa (NSS) zilizoogopwa baada ya uhuru mnamo 2011 na akaendelea katika vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe vilivyofuata.
Hakuna sababu iliyotolewa katika amri ya rais iliyotangaza kuondolewa kwake, ambayo ilisomwa kwenye runinga ya kitaifa Jumatano usiku - lakini amefanywa kuwa gavana wa jimbo la nyumbani la rais la Warrup, ambako ukosefu wa usalama umekithiri.
Wachambuzi wanasema huenda ikaashiria mzozo wa madaraka miongoni mwa wandani wa Kiir - huku baadhi ya watu wakiamini Jenerali Kuc anaandaliwa kuchukua madaraka kutoka kwa rais huyo mwenye umri wa miaka 73.
Haijulikani jasusi huyo wa zamani ana umri wa miaka mingapi - lakini anaaminika kuwa na umri wa kati ya miaka 50 au 60.
Mabadiliko katika idara ya ujasusu yanakuja wiki kadhaa baada ya uchaguzi uliotarajiwa kufanyika Desemba, kuahirishwa kwa miaka miwili.
Emirates yasitisha safari zake kuelekea Iran, Iraq na Jordan
Shirika la ndege la Emirates limetangaza kuahirisha safari zake kutoka Dubai hadi Iraq, Iran na Jordan kwa siku tatu kutokana na "machafuko ya kikanda".
"Wateja wanaopitia Dubai kuelekea Iraq, Iran na Jordan hawatakubaliwa kusafiri katika maeneo yao ya asili hadi ilani nyingine itakapotolewa," ilisema taarifa.
Wiki iliyopita Emirates iliahirisha safari za ndege kati ya Dubai na Beirut hadi tarehe 8 Oktoba.
Takriban watu 20 wafariki baada ya feri kuzama katika ziwa DR Congo

Chanzo cha picha, reu
Maelezo ya picha, Watu wamekusanyika ufuoni katafuta habari za wapendwa wao Takriban miili 20 imeopolewa kutoka Ziwa Kivu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, baada ya feri kuzama umbali wa mita mia chache tu kutoka ilipokuwa inaelekea.
Boti hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka mji wa Minova huko Kivu Kusini na kuzama ilipokuwa ikiwasili kwenye ufuo wa Goma siku ya Alhamisi asubuhi.
Video inayosambaa mtandaoni inaonyesha mashua ikiinamia upande mmoja na kisha kuzama.
Bado haijulikani ni watu wangapi walikuwa ndani ya chombo hicho, lakini manusura kadhaa waliambia shirika la habari la Reuters kuwa huenda ilikuwa imebeba takribani watu 200.
Reuters ilinukuu mamlaka ya uhamiaji ya eneo hilo ikisema takriban wanaume 45 na wanawake 35 walisajiliwa kama abiria, lakini umri wao haujathibitishwa.
Mwanaharakati wa eneo hilo, Aaron Ashuza, ambaye yuko ufukweni, aliambia BBC kwamba aliona miili ikitolewa nje ya mto na kusema waliojeruhiwa wamepelekwa hospitalini.
Takriban watoto wawili walifariki baada ya kupelekwa hospitalini baada ya ajali hiyo, kulingana na AFP.
Ajali kama hizo ni za kawaida katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako boti mara nyingi huwa na abiria wengi ambao hawapewi jaketi za usalama na mara nyingi hawawezi kuogelea.

Uingereza kuikabidhi Mauritius visiwa vya Chagos

Chanzo cha picha, Alamy
Uingereza imetangaza mpango wa kuachia mamlaka ya kundi la visiwa muhimu vya kimkakati katika Bahari ya Hindi baada ya zaidi ya nusu karne.
Mpango huo - uliofikiwa baada ya mazungumzo ya miaka mingi - utashuhudia Uingereza ikikabidhi Visiwa vya Chagos kwa Mauritius katika hatua ya kihistoria.
Hii ni pamoja na eneo la kitropiki la Diego Garcia, linalotumiwa na serikali ya Marekani kama kituo cha kijeshi cha meli zake za jeshi la wanamaji na ndege za masafa marefu.
Tangazo hilo, lililotolewa katika taarifa ya pamoja ya Mawaziri Wakuu wa Uingereza na Mauritius siku ya Alhamisi, linahitimisha miongo kadhaa ya mazungumzo ya mara kwa mara kati ya nchi hizo mbili kuhusu visiwa hivyo.
Jeshi la Marekani na Uingereza litasalia Diego Garcia - jambo muhimu linalowezesha mpango huo kuendelea huku ushindani wa kijiografia katika eneo kati ya nchi za Magharibi, India na China ukiendelea.
Mkataba huo bado haujakamilishwa lakini pande zote mbili zimeapa kufikia hilo haraka iwezekanavyo.
Viongozi watatu wa Hamas waliuawa miezi kadhaa iliyopita - IDF

Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limetangaza kwamba, miezi mitatu iliyopita, liliua viongozi watatu wakuu wa Hamas huko Gaza.
Miongoni mwao ni Rawhi Mushtaha, aliyetambuliwa na IDF kama mkuu wa serikali ya Hamas, pamoja na Sameh al-Siraj na Sami Oudeh, ambao walisimamia masuala ya usalama katika Hamas.
IDF inasema walikuwa wamejificha katika boma la chinichini kaskazini mwa Gaza na waliuawa kupitia mashambulizi ya angani.
Israel inasema Hamas haikutangaza vifo hivyo "ili kuzuia kupotea kwa ari na utendaji kazi wa mawakala wao wa ujasusi".
Katika taarifa yake, IDF ilisema Rawhi Mushtaha alikuwa "mmoja wa watendaji wakuu wa Hamas na alikuwa na mamlaka ya za moja kwa moja katika uaamuzi unaohusiana utendakazi wa vikosi vya Hamas".
Vifo vilivyotangazwa Alhamisi vinaongeza orodha ya viongozi mashuhuri wa Hamas waliouawa mwaka jana, tangu shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba na vita vilivyofuata huko Gaza.
Mwezi Agosti, jeshi la Israel lilisema lilimpiga risasi kiongozi wa Hamas Wissam Khazem, wakati wa operesheni kubwa katika Ukingo wa Magharibi.
Unaweza pia kusoma:
Shambulio la Israel Gaza liliua watu 22 likilenga mwanachama mmoja wa Hamas-BBC yaambiwa

Maelezo ya picha, Amal anasema yeye na watoto wengine katika makazi yake huamka na kwenda kulala wakiwa na hofu Onyo: Taarifa hii ina maelezo ambayo baadhi ya watu wanaweza kukasirishwa nayo
Shambulio la anga la Israel lililoua watoto wengi katika shule ya zamani siku kumi na mbili zilizopita lilikuwa likilenga mtu mmoja,mwanachama wa Hamas, BBC imeambiwa.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema "kituo cha udhibiti" cha Hamas kilikuwa kimepachikwa ndani ya boma katika mji wa Gaza, ambacho kililengwa katika "shambulio lenye usahihi" mnamo 21 Septemba.
Liliua watu 22, wakiwemo watoto 13 na wanawake sita, kulingana na wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas.
Shule hiyo, iliyofungwa wakati wa vita, ilikuwa na makazi ya watu waliohamishwa, wizara ya afya ilisema.
Msichana mmoja mdogo, Amal, aliiambia BBC kuwa alikuwa ndani ya jengo la shule ilipogongwa na kuona miili "ikiwa imesambaratika".
"Tumefanya nini kama watoto? Tunaamka na kwenda kulala kwa hofu," alisema. “Angalau zilinde shule; hatuna shule wala nyumba - tunaenda wapi?"
Vyanzo vya habari vimeiambia BBC kwamba mmoja wa waliouawa ni mwanachama wa Hamas, ikimaanisha kuwa raia wengi walikufa kutokana na mtu mmoja kulengwa.
Huda Alhadad alipoteza watoto wawili - mtoto wa kiume Muhammad, 13, na binti Hanan, 12. "Nilikuwa nikitoka kwenye barabara wakati kombora lilipoanguka. Nilikuja na kumkuta mume wangu akipiga kelele akisema, 'Watoto wangu, watoto wangu, watoto wangu,'' aliambia BBC.
“Nikamuuliza, 'Wako wapi?' Niliwatafuta na kuwakuta chini ya vifusi.”
Katika siku kumi na mbili baada ya shambulio la anga, angalau mashambulio mengine manane mabaya yalifanyika huko Gaza kwenye majengo ya shule zinakoishi familia zilizohamishwa - shambulio la hivi karibuni zaidi katika safu ya mashambulio kwenye majengo kama hayo, ambayo yanatoa usalama mdogo.
Unicef imesema zaidi ya 50% ya shule zinazotumiwa kama makazi huko Gaza ziliathiriwa moja kwa moja wakati wa vita vya sasa, na "matokeo mabaya kwa watoto na familia".
Katika kila shambulio la hivi punde, IDF ilitoa taarifa kwa umma ikisema shule za zamani zilikuwa na magaidi wa Hamas au vituo "chini ya udhibiti" wa Hamas.
CIA inataka kuwasajili wahudumu wapya Korea Kaskazini, Iran na China

Chanzo cha picha, CIA/Facebook
Shirika la Ujasusi la Marekani limezindua mpango mpya wa kuwaajiri watoa habari nchini China, Iran na Korea Kaskazini.
Shirika hilo lilichapisha jumbe kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii katika lugha ya Mandarin, Farsi na Korea siku ya Jumatano, likiwaelekeza watumiaji jinsi ya kuwasiliana nalo kwa usalama.
Juhudi hizi za hivi punde zinafuatia kampeni ya kuwasajili Warusi kufuatia uvamizi wa Ukraine, ambao CIA inasema ulifanikiwa.
"Tunataka kuhakikisha watu binafsi katika tawala zingine za kimabavu wanajua kuwa tuko wazi kwa biashara," msemaji wa CIA alisema katika taarifa.
Ujumbe wa ajira - ambao uliwekwa kwenye majukwaa kama vile X, Facebook, YouTube, Instagram, Telegram na LinkedIn- ziliomba majina ya watu binafsi, maeneo na maelezo kuhusu mawasiliano.
Maagizo ya kina yaliwashauri watumiaji kuwasiliana na CIA kupitia tovuti yake rasmi kwa kutumia Mitandao ya Kibinafsi (VPNs) inayoaminika au kivinjari kisichojulikana kinachojulikana kama mtandao wa Tor, ambao mara nyingi hutumiwa kufikia tovuti kisiri.
Mwanamuziki nguli wa nyimbo za Injili Afrika Kusini Solly Moholo afariki dunia

Chanzo cha picha, Solly Moholo/Facebook
Msanii mkongwe wa nyimbo za Injili kutoka Afrika Kusini, Solomon Molokoane, almaarufu Solly Moholo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 65, wasimamizi wake wametangaza.
Mwanamuziki huyo aliyeshinda tuzo alikuwa amelazwa hospitalini kwa wiki kadhaa baada ya kuugua akiwa katika ziara ya muziki nchini Botswana mwezi uliopita.
Alipata umaarufu mwanzoni mwa miaka ya 2000 na kuwa jina maarufu katika muziki wa injili wa kitamaduni wa Afrika Kusini.
Wasimamizi wake walisema atakumbukwa sana kwa "muziki wa uponyaji aliotupa kwa miaka mingi".
Mwezi uliopita, timu ya Moholo ilisema alipatwa na kiharusi na kwamba viungo kadhaa mhuhimi wilini mwake vimeacha kufanya kazi.
Familia yake ilitoa ombi la umma la kuchangisha fedha za gharamia matibabu yake.
“Ni kwa masikitiko makubwa tunawataarifu kwa niaba ya familia ya Molokoane, kwamba gwiji wetu mpendwa ‘Solly Moholo’ amefariki dunia,” uongozi wake ulisema.
"Alifariki tarehe 2 Oktoba 2024 akiwa hospitalini."
Video: Tazama kupatwa kwa jua Amerika ya kusini
Maelezo ya video, Tazama: kupatwa kwa kujua Amerika Kusini Kupatwa kwa jua kulionekana kutoka Kisiwa cha Pasaka, Chile na Buenos Aires, Argentina tarehe 2 Oktoba.
Kupatwa kwa jua hutokea wakati mwezi unapotoa kivuli kwenye Dunia na katika kupatwa kwa jumla, mduara mzima wa Jua unazibwa.
Kupatwa kwa jua kwa mwaka hutofautiana kwa sababu Jua mara nyengine huonekana kama pete ya kuvutia huku kitovu kikiwa kimezuiwa na Mwezi.
Rwanda kuanza majaribio ya chanjo ya ugonjwa wa virusi vya Marburg

Chanzo cha picha, Getty Images
Rwanda iko tayari kuanza majaribio ya chanjo na matibabu ya kutibu ugonjwa wa Marburg, Yvan Butera, waziri msaidizi wa afya alisema siku ya Alhamisi, huku taifa hilo la Afrika Mashariki likipambana na mlipuko wake wa kwanza wa homa hay ya virusi ambayo imewaua watu11.
Ugonjwa huo ulithibitishwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwa Septemba, na watu 36 wameripotiwa kupata maradhi hayo hadi sasa, data ya wizara ya afya inaonyesha.
"Hii ni sehemu ya juhudi zetu za kusaidia watu kupona haraka kwa kutumia chanjo na dawa zilizotengenezwa mahsusi kupambana na mlipuko huu, kwa sasa katika awamu ya mwisho ya utafiti," waziri, Sabin Nsanzimana, aliiambia Reuters.
"Tunashirikiana na makampuni ya dawa yaliyotengeneza dawa hizi, pamoja na Shirika la Afya Ulimwenguni ili kuharakisha mchakato huo kupitia ushirikiano wa kimataifa."
Alisema serikali inazungumza na makampuni yaliyoko Marekani na Ulaya.
Wizara hiyo ilikuwa ikifuatilia watu 410 ambao walikuwa wamewasiliana na wale walioambukizwa, aliongeza, huku i wengine watano waliopimwa wakibainika kuwa hawana, lakini walisubiri matokeo ya vipimo zaidi.
Homa ya virusi Marburg hivyo husababisha kuvuja damu, na miongoni mwa dalili zake ni maumivu makali ya kichwa hadi kutapika, maumivu ya misuli na tumbo, na unaweza kuua baadhi ya wagonjwa, wizara imesema.
Israel na Lebanon: Israel yafanya shambulio la kwanza katikati mwa mji mkuu Beirut

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Jengo la ghorofa katika kitongoji cha Bachoura ambalo lilipigwa katika shambulio la anga la Israel Mlipuko mkubwa ulisikika wakati Israel iliposhambulia Beirut usiku wa manane.
Jengo lililopigwa lilikuwa katika kitongoji cha Bachoura, karibu na bunge la Lebanon, likiwa ni shambulio la kwanza la anga la Israeli kupiga kitovu cha mji mkuu katika mzozo huu.
Picha za tukio hilo zilionyesha jengo la ghorofa lililoharibika sana, ghorofa ya kwanza ikiwa imeharibiwa kidogo.
Dahieh, ngome ya Hezbollah kusini mwa Beirut, pia ilishambuliwa. Jeshi la Israel lilitoa maagizo mapya kwa wakazi kuyahama maeneo kadhaa ya wilaya hiyo, likisema litalenga vituo na maslahi ya Hezbollah katika siku zijazo.
Kusini mwa nchi hiyo, kulikuwa na ishara kwamba Israel ilikuwa ikijiandaa kupanua uvamizi wake wa ardhini, huku wanajeshi zaidi wakitumwa kwenye mpaka hapo jana.
Unaweza pia kusoma:
Takriban watu sita wameuawa katika shambulizi la anga la Israel katikati mwa Beirut

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Mfumo wa ulinzi wa anga wa Iron Dome wa Israeli unazuia makombora yaliyorushwa kutoka kusini mwa Lebanon juu ya Galilaya, kaskazini mwa Israeli, siku ya Jumatano. Maafisa wa Lebanon wamesema watu wasiopungua sita wameuawa huku Israel ikipanga kuendelea na mashambulizi yake ya anga.
Jeshi la Israel limekuwa likiwaonya wakazi wanaoishi kusini mwa Lebanon, karibu na mpaka wa Israel, wasirudi nyumbani.
Israel ilianza uvamizi wa ardhini wiki hii, na kutangaza kifo cha wanajeshi wanane wa Israel ndani ya Lebanon hapo jana.
Jana usiku waandishi wa BBC walisikia milipuko mikubwa mjini Beirut huku mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya mji huo yakiendelea. Milipuko pia ilisikika kupitia Dahieh, ngome ya Hezbollah katika vitongoji vya kusini.
Wakati hayo yakijiri sauti za ving'ora kaskazini mwa Israel zinasikika huku milio ya roketi ikiendelea kutoka Lebanon.
Zaidi ya makombora 240 yalirushwa kutoka kusini mwa Lebanon kuelekea kaskazini mwa Israeli siku nzima ya Jumatano, kulingana na Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF).
Na ufyatuaji wa roketi unaonekana kuendelea, huku ving'ora vya tahadhari katika angalau maeneo manne kaskazini mwa Israel vikisikika Alhamisi asubuhi, IDF imesema kwenye Telegram.
king'ora cha hivi punde zaidi kilikuwa Galilee Panhandle, karibu na mpaka wa Lebanon.
Unaweza pia kusoma:
Mamlaka Tanzania zaifungia Mwananchi kuchapisha habari mtandaoni kwa 'ukiukaji wa kanuni'

Chanzo cha picha, MCL
Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) imesitisha kwa muda huduma za maudhui ya mtandaoni za Mwananchi Communication Limited (ML) kwa 'ukiukaji wa kanuni'
Katika tangazo lake kwa umma TCRA imesema imesitisha leseni ya huduma za maudhui ya mtandaoni dhidi ya kampuni ya habari ya MCL nchini humo, kwa ukiukaji wa kanuni ya mwaka 2020.
TCRA imesema tarehe 01 Oktoba 2024, MCL ilichapisha maudhui mjongeo na sauti (audio-visual kwenye mitandao yake ya kijami, maudhui yaliyozuiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 16 ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020.
''Maudhui hayo yameleta tafsiri hasi kwa taifa, jambo ambalo linaathiri na kuharibu umoja, amani na mshikamano wa taifa’’, imeeleza taarifa ya TCRA , iliyotumwa kwenye mitandao yake ya kijamii:
Ruka Instagram ujumbeRuhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya njeMkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa Instagram ujumbe
''Umma unaarifiwa kuwa, kufuatia kuchapishwa kwa maudhui yaliyokatazwa na yanayopingana na sheria, TCRA imesitisha kwa muda leseni za huduma za maudhui mtandano za Mwananchi Communication Limited (The Citizen, Mwananchi Digital, Mwananchi na Mwanaspoti) tangu tarehe ya kutolewa taarifa hii, wakati masuala mengine ya kiusimamizi yanafanyiwa kazi,’’ limehitimisha tangazo hilo.
Mwananchi Communication Limited imesemaje?
Kufuatia kuondolewa kwa leseni hiyo, MCL imetangaza kuondoa maudhui yake ya michoro kwenye mitandao yake ya kijami.
Kupitia gazeti lake la lugha ta Kiingereza The Citizen, kampuni hiyo imesema: ‘’Tumeamua kuondoa michoro iliyoshirikishwa Oktoba 1, 2024 kwenye mitandao ya kijamii (X na Instagram), kwa kuwa ilionyesha matukio yaliyoibua hofu kuhusu usalama wa watu binafsi nchini Tanzania.’’
''Uamuzi wetu wa kuondoa katuni unatokana na kusababisha tafsiri mbaya ambayo ni kinyume na nia yetu’’, taarifa hiyo iliongeza.
Maudhui yaliyoiweka MCL lawamani ni ya katuni ambayo ilikuwa ikionesha raia wa nchi hiyo wakilalama kwenye runinga juu ya matukio ya watu kutekwa na kuuawa nchini humo. Katuni hiyo ilikuwa ikimuonesha mtu ambaye alikuwa akitizama runinga ambaye wengi wametafsiri kuwa ni Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan.
Matukio ya watu kutekwa, kupotezwa na kuuawa katika mazingira ya kutatanisha yamezua gumzo katika miezi ya hivi karibuni nchini Tanzania.
Unaweza pia kusoma:
Urusi yafanya mashambulizi ya mabomu ya Shahid na kamikaze katika maeneo tofauti ya Ukraine

Chanzo cha picha, State Emergency Service of Ukraine
Jeshi la Urusi limetumia ndege zisizo na rubani za kamikaze na shahid katika maeneo ya kaskazini na kusini mwa Ukraine usiku kucha.
Jeshi la Anga la Ukraine linaripoti kuwa mabomu ya "shahid" yalirushwa katika maeneo tofauti juu ya mikoa ya Sumy, Poltava, Cherkasy, Kherson na Nikolaev.
Kituo cha ufuatiliaji wa vita nchini Ukraine kimeripoti kuwa kuwa tayari kuna ndege zisizokuwa na rubani hamsini zilizorushwa na jeshi la Urusi katika anga ya nchi hiyo.
Matangazo ya tahadhari ya mashambulizi ya angani yametangazwa karibu eneo lote la mashariki mwa Ukraine kufuatia mashambulizi hayo.
Mashambulizi ya mabomu katika mji wa KharkovWakati hayo yakijiri meya wa Kharkov na vyombo vya habari vya Ukraine wameripoti kuwa jeshi la Urusi limeupiga mji huo kwa mabomu ya glide
"Mlipuko ulitokea katika eneo hilo. Kharkov inashambuliwa na adui wa KABs. Uwe mwangalifu. Mashambulio ya mara kwa mara yanawezekana," Meya wa Kharkov Igor Terekhov aliandika kwenye kituo chake cha Telegram.
Kwa mujibu wa Terekhov, shambulizi hilo lililenga wilaya za Shevchenkivsky na Kievsky za Kharkov, na habari kuhusu athari za mashambulizi hayo bado hazijatolewa.
Kituo cha Telegram cha mkuu wa utawala wa mkoa wa Kharkiv, Oleg Sinegubov, kimeandika kwamba, kulingana na data za awali, "kuna uharibifu wa miundombinu ya raia"
Vita vya Ukraine: Mengi zaidi
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
Biden: Marekani haiungi mkono shambulio la Israeli kwenye maeneo ya nyuklia ya Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Joe Biden amesema kuwa haungi mkono shambulio katika maeneo ya nyuklia ya Iran kufuatia mashambulizi ya makombora ya masafa ya Iran dhidi ya Israel na kuitaka Israel kuchukua hatua " sawia" dhidi ya adui yake mkuu wa kikanda.
Kauli za Biden siku ya Jumatano zilikuja siku moja baada ya Iran kurusha makombora zaidi ya 180 ya masafa marefu dhidi ya Israeli siku ya Jumanne, katika hatua ambayo Biden aliitaja kuwa "isiyofaa."
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliapa kuwa Iran italipa gharama ya shambulio hilo.
Biden aliwaambia waandishi wa habari kabla ya kupanda ndege ya raias,b Air Force One, "Tutajadiliana na Waisraeli watafanya nini, lakini sisi sote (nchi za G7) tunakubali kwamba wana haki ya kujibu, lakini lazima iwe kwa uwiano."
Katika miezi ya mwisho ya muhula wake, Biden anakabiliwa na ukosoaji mkali ndani na nje ya nchi kutokana na uungwaji mkono mkubwa wa kijeshi wa Marekani kwa Israel, ukosoaji uleule anaokabiliana nao naibu wake, Kamla Harris, mgombea urais wa Chama cha democrat.
Unaweza pia kusoma:
karibu tena leo Alhamisi tarehe 03.010.2024 kwa matangazo haya ya mubashara, tukikuletea habari za kikanda na kimataifa. Shukran kwa kujiunga nasi.


