Tunachojua kuhusu shambulio la kombora la Iran dhidi ya Israel

Iran imerusha mamia ya makombora kuelekea Israel, huku baadhi ikipiga maeneo ya Israel.
Hilo ni shambulio la pili kufanywa na Iran mwaka huu, baada ya kurusha mamia ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel mwezi Aprili.
Maafisa wa jeshi la Israel walisema mashambulizi yanaonekana kumalizika na hakuna tishio tena kutoka kwa Iran "kwa sasa" lakini bado haijafahamika ni kiasi gani cha uharibifu uliosababishwa.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameonya kuhusu "matokeo" baada ya shambulio hilo.
Hivi ndivyo tunavyojua hadi sasa.
Je, shambulio la Iran lilikuwa na ukubwa gani?
Iran ilirusha takribani makombora 180 kuelekea Israel, jeshi la Israel lilisema. Hilo lingelifanya kuwa shambulizi kubwa kidogo kuliko mashambulizi ya Aprili, ambayo yalishuhudia takribani makombora 110 ya balistiki na makombora 30 ya baharini yakirushwa kuelekea Israel.
Picha za video zilizobebwa na TV ya Israel zilionekana kuonesha baadhi ya makombora yakiruka juu ya eneo la Tel Aviv muda mfupi kabla ya 19:45 saa za ndani (16:45 GMT).
Makombora mengi yaliangushwa na mifumo ya ulinzi ya anga ya Israel, afisa wa usalama wa Israel alisema, huku mwandishi wa BBC mjini Jerusalem akisema baadhi ya kambi za kijeshi zilipigwa, pia migahawa na shule zilipigwa.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) lilisema kuwa asilimia 90 ya makombora yalifikia maeneo yao, likisema makombora ya hypersonic yametumiwa kwa mara ya kwanza. Duru za IRGC zilisema kuwa kambi tatu za kijeshi za Israel zililengwa.
Mamlaka ya ulinzi wa kiraia ya Palestina katika mji unaokaliwa wa Ukingo wa Magharibi wa Jeriko ilisema mtu mmoja alikufa wakati wa shambulio la kombora la Iran.
Kulingana na shirika la habari la AFP, ambalo lilizungumza na gavana wa jiji Hussein Hamayel, mwathiriwa aliuawa na vifusi vya roketi vilivyoanguka.
Maafisa wa Israel hawajaripoti majeraha yoyote mabaya kutokana na mashambulizi ya anga ya Jumanne, lakini madaktari wa Israel walisema watu wawili wamejeruhiwa kidogo na milipuko.
Kwa nini Iran ilishambulia Israel?
IRGC imesema mashambulizi hayo yalitokana na mauaji ya Israel dhidi ya mmoja wa makamanda wake wakuu na viongozi wa wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran katika eneo hilo.
Ilieleza mauaji ya mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah na kamanda wa IRGC Abbas Nilferoshan katika mji mkuu wa Lebanon Beirut tarehe 27 Septemba.
Pia ilirejelea mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh huko Tehran mwezi Julai. Ingawa Israel haijakiri kuhusika na kifo cha Haniyeh, inaaminika kuwa ilihusika.
Afisa mkuu wa Iran aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei, ndiye aliyetoa agizo la shambulio la kombora la Jumanne.
Iran haitambui haki ya Israel kuwepo na inataka kutokomezwa. Imetumia miaka mingi kuunga mkono mashirika ya kijeshi yanayopinga Israel.
Israel inaamini kuwa Iran ni tishio lililopo na imetumia miaka mingi kuendesha operesheni za siri dhidi ya Tehran.
Je, makombora yalizuiwa na Iron Dome?
Israel ina mfumo wa kisasa zaidi wa ulinzi wa anga, unaojulikana zaidi ambao ni Iron Dome. Imeundwa kuzuia roketi za masafa mafupi za aina zinazorushwa na Hamas na Hezbollah.
Ingawa ilitumiwa kujilinda dhidi ya shambulio la mwisho la Iran mwezi Aprili, vipengele vingine vya mifumo ya ulinzi ya "layered" ya nchi huenda ilifanya kazi kubwa Jumanne.
Washirika wa Israeli wamesemaje?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Rais wa Marekani Joe Biden alithibitisha uungaji mkono wa Marekani kwa Israel baada ya shambulio hilo la kombora, na kulitaja kuwa "lililoshindwa na lisilofaa".
Alikuwa ameamuru vikosi vyake katika eneo hilo "kusaidia ulinzi wa Israel" na kuangusha makombora ya Iran.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin pia alithibitisha uvamizi akilaani "kitendo hiki cha uchokozi cha Iran".
BBC pia imethibitisha picha za video zinazoonesha makombora yakitegwa katika mji mkuu wa Jordan wa Amman. Nchi hiyo pia ilidungua idadi kadhaa ya makombora wakati wa shambulio la mwisho la Iran mwezi Aprili.
BBC inaelewa kuwa ndege za kivita za Uingereza zilihusika katika kuisaidia Israel siku ya Jumanne, kama ilivyokuwa mwezi Aprili.
Waziri wa Ulinzi John Healey alisema vikosi vya Uingereza "vimetekeleza sehemu yao katika majaribio ya kuzuia kuongezeka zaidi" Jumanne jioni, bila kutoa maelezo zaidi.
Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer alisema Uingereza ilisimama na Israel na kutambua "haki yake ya kujilinda".
Ufaransa na Japan ziliongeza sauti zao kulaani mashambulizi ya Iran na pia kutoa wito kwa pande zote kuepuka kuongezeka zaidi.
Nini kitatokea baadaye?
Netanyahu alisema Iran imefanya "kosa kubwa" na "italipa".
"Tuna mipango, na tutafanya kazi mahali na wakati tutakaoamua," alisema msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel Daniel Haggari.
IRGC ya Iran ilisema jibu la Tehran litakuwa "la kuponda na kuharibu zaidi" ikiwa Israeli italipiza kisasi.
Wakati huo huo, jeshi la Israel lilifanya mashambulizi mapya ya anga mjini Beirut dhidi ya shabaha za Hezbollah usiku kucha baada ya kuwaonya wakazi kuondoka katika vitongoji vya kusini mwa mji huo ambako kundi hilo lipo.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












