Kwanini Wakurdi wanataka kujiunga na vita vya Marekani dhidi ya Iran?

Mwanajeshi akiwa amejihami na bunduki.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Kwa siku ya sita sasa, Israel na Marekani bado wanaishambulia Iran.

Je, kuna uwezekano wa wanajeshi wa kigeni kuingia Iran na kupigana? Labda. Ila wanajeshi hao hawatakuwa wa Marekani.

Kundi la upinzani la Kikurdi la Iran, wenye makazi yao kaskazini mwa Iraq, wameiambia BBC kuwa wanamipango ya kuvuka mpaka na kuingia Iran, ila wanapinga madai kuwa wapiganaji wake tayari wameingia Iran.

"Tumekuwa tukijiandaa kwa miaka 47 tangu kuundwa kwa jamhuri ya kiislamu." Alisema Hana Yazdanpana kutoka chama cha Kurdistan Freedom Party, ambacho kinadai kuwa na kikosi kikubwa cha Wakurdi.

Ila alisistiza kuwa hakuna mpiganaji yeyote aliyevuka mpaka.

Yazdanpana alisema kuwa makundi sita ya upinzani ambayo yaliungana hivi karibuni, wanashirikiana kisiasa na kijeshi "hakuna anayefanya kazi pekee yake" alituelezea. "Tutajua iwapo ndugu zetu wameanza safari"

Yazdanpana anatuambia kuwa, haoni uwezekano wa wapiganaji hao kuingia Iran wiki hii, kwani lazima wapewe ishara ya kufanya hivyo na Marekani.

"Hatuwezi kwenda iwapo anga juu yetu bado ni hatari na tunahitaji maghala ya silaha kuharibiwa, au bure tutakuwa tunaenda kuuawa, kwani utawala huo hauna huruma na sisi silaha pekee tuliyonayo ni bunduki aina ya AK 47."

Aidha anaongezea kuwa Marekani inafaa kupiga marufuku usafiri wa anga ili kuwalinda wapiganaji wa Kikurdi.

"Tumewauliza wafanye hivi mara nyingi na hata kutuma barua pepe. Tunahitaji hilo kufanyika haraka"

Ikulu ya White House imepinga ripoti kuwa rais wa Marekani Donald Trump anawapa silaha Wakurdi, wengi wao ambao awali walipewa mafunzo na jeshi la Marekani ili kupigana na kundi la kigaidi la Islamic State nchini Iraq.

Uwezakano wa kundi la Kikurdi kuingia Iran ukiwepo, Tehran imezidisha mashambulizi dhidi yao kwa kutumia makombora.

Uharibifu uliosababishwa na shambulizi la Iran dhidi ya kundi la Kikurdi, Kaskazini mwa Iraq.

Chanzo cha picha, Matthew Goddard/BBC

Baadhi ya makundi yameondoa vikosi vyao katika kambi zao na kuvihamisha ili kujaribu kuvilinda dhidi ya mashambulizi.

Kujiunga katika mapambano dhidi ya utawala wa Iran ni hatari kubwa, na haijulikani ni nini ambacho Trump atawapa kama malipo.

Wakurdi, ambao ni kundi la nne kwa ukubwa wa kikabila katika Mashariki ya Kati, wametawanyika kati ya Iran, Iraq, Syria na Uturuki. Wana historia ndefu ya kuteswa na kusalitiwa.

Wakurdi wanamsemo unaosema, "hatuna marafiki isipokuwa milima."

Je, Marekani inaweza kuaminika kutimiza ahadi zozote itakazotoa?

Wakurdi wengi nchini Syria ambao walishirikiana na Marekani katika vita dhidi ya IS walikasirishwa hivi karibuni wakati Trump alipoegemea upande wa serikali ya mpito ya Damascus dhidi yao.

Lakini baadhi ya viongozi wakuu wa Wakurdi wa Iran wana mtazamo tofauti.

Mustafa Mauludi, naibu rais wa Kurdistan Democratic Party of Iran (KDPI),Iraq Kaskazini.

Chanzo cha picha, Matthew Goddard/BBC

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Vita hivi vilianzishwa na Marekani na Israel kwa ajili ya maslahi yao wenyewe," alisema Mustafa Mauludi, makamu wa rais wa Kurdistan Democratic Party of Iran (KDPI). "Lakini wanalenga vituo vya Islamic Revolution Guard Corps (IRGC), na hili litakuwa zuri kwetu na litatusaidia kuingia Iran."

Akiwa na umri wa miaka 67, amekuwa akisubiri katika sehemu kubwa ya maisha yake kuanguka kwa utawala wa Kiislamu wa Iran.

Akiwa amevaa nguo ya kiasili ya Wakurdi, alisimulia historia ya familia yake yenye maumivu. Binamu yake mmoja aliuawa na utawala wa kiislamu akiwa na umri wa miaka 13 na mwingine bado yuko gerezani baada ya miaka 31 kwa tuhuma za kushirikiana na upinzani. Alisema 60% ya familia yake waliwahi kushikiliwa na kudhulumiwa kwa sababu ya shughuli zake za kisiasa.

Mauludi tayari ana picha akilini mwake ya jinsi atarajea katika taifa lake.

"Wakati nitakapofika katika kijiji cha kwanza," alituambia, "nitasema kwa sauti kubwa nimekuwa nikiwapigania nyinyi, nyinyi ni watu wangu, na sasa nitawapigania zaidi." Anaamini atakuwepo katika sherehe ya sikukuu ya mwaka mpya ya Wakurdi, Nowruz, inayofanyika tarehe 21 mwezi Machi.

Idadi ya Wakurdi ni takriban 10% ya idadi ya watu wa Iran, inayokadiriwa kuwa milioni 90. Viongozi hao wanaitaka jamii ya kimataifa kumuunga mkono Trump, na pia kuwaunga wao mkono.

"Sisi ndicho kikundi kilicho jipanga kisiasa zaidi nchini Iran," alisema Abdullah Mohtadi, katibu mkuu wa Komala Party of Iranian Kurdistan. "Na hatutaruhusu kupoteza fursa hii ya mabadiliko."

Aidha amekakatishwa tamaa na msimamo wa Uingereza kuhusu kutojihusisha na vita hivi.

"Nashangazwa kuwa Uingereza ndiyo nchi pekee barani Ulaya ambayo haijaisajili IRGC kama shirika la kigaidi," alisema Mohtadi.

Wapiganaji wa Kikurdi kutoka chama cha Kurdistan Democratic Party of Iran (KDPI), Iraq Kaskazini

Chanzo cha picha, Matthew Goddard/BBC

Ni vigumu kujua idadi kamili ya wapiganaji Wakikurdi.

Kulingana na mwanahabari mmoja wa Kikurdi alituambia kuwa "wanaweza kuwa maelfu ikiwemo walioko Iran. Wanataka kuwa sehemu ya mabadiliko, licha ya historia yao bado wako na matumaini."

Baadhi ya Wakurdi wa Iran wanaoishi Iraq, wanasema ni wakati wa kuwajibika bila ahadi za Marekani au hata wakiungwa mkono na Marekani.

Hii inaiweka Iraq katika njia panda, wakihofia kuingizwa katika vita ambavyo hawakuwa wanataka kuhusishwa navyo.

Serikali ya Baghdad imesema haitaruhusu makundi hayo kuvuka mpaka wa Iran au kutekeleza ugaidi wakiwa katika ardhi ya Iraq.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula